SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA MIA ISHIRINI NA NNE
Muda huohuo baada ya ile simu toka kwa Songelael gari tano za Polisi zikiwa na Polisi zaidi ya arobaini zilikuwa njiani kuelekea porini Ngome. Gari za polisi zilitembezwa kwa kasi sana huku zikiwa na Askari waliojipanga kivita, na silaha mzitomzito, walikuwa tayari kwa lolote, walikuwa na uhakika na wanachoenda kukifanya baada ya kuhakikishiwa na askari imara wa kike, inspekta Jasmine, kuwa wanakoenda ndio kwenye jibu la wahalifu wote wanaoisumbua Kilwa. Inspekta Jasmine mwenyewe alikuwa juu ya pikipiki kubwa aina ya Kawasaki, naye akielekea porini Ngome kwenda kuumaliza mchezo.
Kule ndani ya kambi sasa, Mpelelezi Daniel Mwaseba walikuwa wanatazamana macho kwa macho na Moja wa toka kundi la Six killers.
Kukutana ghafla na Mateka wao akiwa huru kulimfanya Moja asite kidogo, alibabaika kwakuwa hakujua Daniel katokaje katika chumba cha kifo, pia alibabaika kwa kuwa hakujua amfate yupi? amfate yule mtu aliyekuwa kule juu ya ukuta wa kambi yao ama aanze kupambana na huyu aliyepo mbele yake, Daniel Mwaseba. Kusitasita kwa Moja ilikuwa faida kubwa sana kwa Daniel Mwaseba. Baada moja alipata wazo la kutoa bastola yake iliyokuwa kotini, aliamua kuanza kummaliza Daniel Mwaseba kwa risasi, lakini alikuwa amechelewa sana........ Daniel aliruka sarakasi kwa kasi toka pale alipokuwa amesimama na kwenda kumvaa Moja kwa nguvu. Bastola ya Moja ilirudi tena ndani ya koti bila kupenda.
Kule juu ya ukuta alikokuwa Dokta Yusha, alikuwa anashuhudia kila kitu. Sasa Dokta Yusha alikuwa anatafuta namna ya kudumbukia ndani kutokea kule juu ya ukuta.
Baada ya kuvamiwa kwa nguvu na Daniel Mwaseba, Moja aliyumba kidogo kisha akasimama imara tayari kwa kupambana na Daniel Mwaseba. Ilhali sasa wote wakiwa mikono mitupu.
Kabla hawajaanza hata kurushiana ngumi, Tatu wa Six Killers alitoka nje ya ile nyumba ya bluu, akiwa na bastola mkononi.
Tayari kwa kuuwa!
Balaa!
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA