SIMULIZI: BALAA
Mwandishi: HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA MIA NA KUMI NA NNE
Maswali mengi sana yalipita katika kichwa cha mpelelezi Daniel Mwaseba. Lakini maswali yote hakuwa na majibu yake kabisa, pamoja na kutopata majibu ya maswali yake lakini Daniel hakuacha kujiuliza maswali ingawa alijua hakukuwa na wa kumjibu . Lakini alijiuliza.....
"Je kiti hiki kimekuja kwa bahati mbaya au makusudi katika kambi ya watu hawa hatari?" Daniel Mwaseba alijiuliza kimoyomoyo huku akikiangalia kile kiti.
Bahati mbaya kwa maana kundi lile hatari labda walikiiba kiti kile toka mikononi kwa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Justus Bitesigile, au Waziri mkuu alikuwa na dhamira tangu mwanzoni, dhamira ya kuwaletea kiti kile kundi hatari la Six Killers. Kwa dhamira hii wanayoifanya watu hawa. Daniel Mwaseba akajua umakini mkubwa zaidi unahitajika katika kutatua mkasa huu mzito! Mkasa wenye sura ya usaliti, mkasa wenye sura ya usiri mkubwa sana. Mkasa wenye nia mbaya kwa nchi ya Tanzania.
Hisia kuwa kuna viongozi wakubwa toka serikalini pia wanahusika katika mkasa huu mzito zikatamalaki katika kichwa cha Daniel Mwaseba. Uwepo wa kiti kile mahali pale ulidhihirisha hilo.
"Wakubwa, kwa dhamira ipi sasa? Iweje viongozi wa nchi wauwe wananchi wao?, kosa la wananchi ni lipi? Wananchi ndio waliowachagua hao viongozi, kwa hiyo moja kwa moja viongozi wana dhima ya kuwalinda wananchi, kuwahudumia wananchi, Kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za kijamii" Daniel Mwaseba aliendelea kujiuliza mwenyewe na kujielezea mwenyewe. Tena sasa sio kimoyomoyo tena, alikuwa anaongea kwa sauti ndogondogo...ya kunong'ona.
"Sasa kwa mfano wananchi wote wakiuwawa na kundi hatari la Six Killers, tena kuuwawa kikatili na kwa makusudi watawaongoza kina nani hao viongozi waliopo katika mpango huu?"
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA