RIWAYA: Anga ya Washenzi na Gilbert Evarist Mushi

Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.

Msimu Wa Nne
Sehemu ya 07&08
Majira ya Saa nane usiku ndani ya nyumba ya Dokta Yusha kulikuwa na kikao kizito. Kikao hiki kilihudhuriwa na watu watano. Wawili wa kike ambao ni Cara na Elizabeth Neville. Huku watatu wa kiume ni Dokta Yusha, Gilbert Mwaitika wakiwa pamoja na Mwanasheria Mlevi.

"Hali halisi ndio hiyo ndugu zangu, mchana nikiwa nazungumza naye aliniambia atanipigia maana kuna jambo ameliona na halielewi hivyo nikakata simu" Gilbert Mwaitika alisema.

"Panapopambazuka asubuhi na mapema inabidi niongozane na Elizabeth Neville katika jengo la Uchumi maana hii waleti imeshatupa jibu juu ya muhusika wa mauaji ya Mawazoo. Alama ya Damu iliyoonekana kwenye kitambulisho inaonekana ni ya Mawazoo. Ahsante Dokta kwa kutusaidia katika utambuzi wa hili. Tanzania inazidi kukua katika teknolojia kila kukicha, kwani miaka ya nyuma ilikuwa ni ngumu kugundua damu ni ya nani hadi uchukue na damu ya mhusika kisha uzipime zote.

"Kingine ni kuhusu yule mtoto wa Henry. Ni ngumu sana kumtoa ile kill plug aliyowekewa katika ubongo wake. Nilichofanya ni kumficha kule chini ya ardhi pasipo na mtandao ili asiweze kuuwawa kirahisi. Hii nyumba kwa kweli Dokta uliitengeneza kiutaaalam sana. Hata mtu akikutafuta katika mtandao kama upo kule chini huwezi patikana katu. Na ndipo tulipomhifadhia pia Festus baada ya kubaini pia anacho kifaa karibu na moyo wake kinachoonyesha ni wapi alipo. Inabidi pia tujitahidi kutafuta namna ya kuondoa kifaa hicho maana nilipokifwatilia kupitia mtandao, taarifa zinaonyesha ni kifaa ambacho kina uwezo pia wa kuondoa uhai wa mtu kama atapandikiziwa katika kiungo chochote kilicho ndani ya mwili kama vile figo, moyo, ini, na kadhalika. Maana huwa kinapasuka. Ili kipasuke kinahitaji muunganiko wa kimtandao kutoka kwa mpandikizaji na kifaa hicho. Kama tungechelewa kujua haya naamini Festus angekuwa ni marehemu sasa hivi." Cara alieleza vizuri na kwa urefu zaidi.
Waliendelea kuzungumza pamoja, lakini Elizabeth Neville alikuwa ni kama vile hayupo pale, hakuwa akielewa kinachozungumziwa pale. Kichwani alikuwa amebeba neno moja tu. Daniel

Ni Asubuhi na mapema ndani ya mji wa Moshi. Jua lilichomoza mapema mno na lilikuwa ni kali pia. Asubuhi hii iliwakuta Mwanasheria Mlevi pamoja na Elizabeth Neville nje ya jengo la Uchumi Plaza. Walizama ndani ya viunga vya uchumi na kuangaza macho huku na kule. Mara wakasikia wakiitwa na mlinzi mmoja.

"Mnahitaji kwenda wapi? Mmewahi sana maana ofisi nyingi huwa zinafunguliwa saa mbili asubuhi, na sasa ndio kwanza saa moja kasoro" Mlinzi alieleza. Alikuwa amebeba bastola yake mkononi, katika mfuko wa shati yake ya sare kulikuwa na nembo ya K4A Security ambayo ni kampuni binafsi ya ulinzi na usalama.

"Tuna shida na Exaud Kimbori. Sisi ni maofisa kutoka jeshi la polisi, vitambulisho vyetu ni hivi. Habari yako Mr." Mwanasheria Mlevi akasema na kutoa salamu.

"Ohoo..! Salama kabisa kamanda. Bila shaka mnamuulizia yule meneja wa hili tawi la NMB bank hapa Uchumi." Mlinzi yule akasema, wakatingisha vichwa vyao kwa pamoja kuafiki ni huyohuyo wanayemuulizia.

"Kama ni yeye basi tangu jana alipotoka hapa majira ya saa sita mchana hajarejea hadi sasa. Labda muwasiliane nae kwa njia ya simu" Mlinzi akasema

"Unaweza kunisaidia kunielekeza anaishi mtaa gani hapa mjini ndugu yangu?" Mwanasheria akasema kwa sauti ya chini kidogo huku akimsogelea kwa karibu zaidi mlinzi yule.

"Si unajua lakini ni mwiko katika kazi?" Mlinzi akadokeza.

"Nalijua hilo ndio maana naomba unisaidie ndugu yangu. Tutalindana hivyohivyo si unajua tena?" Mwanasheria akasema huku akimpatia mkono wake mlinzi yule, na kumbe katika mkono alishika noti moja ya Shilingi Elfu kumi ya kitanzania. Mlinzi yule akatoa maelekezo ni wapi bwana Exaud anaishi, ilikuwa sio mbali sana na pale. Si hivyo tu, na nambari yake ya simu walipewa na mlinzi yule.
Baada ya kutoka pale wakamtafuta Cara kwenye simu na kumpata. Elizabeth ndiye aliyepiga.

"Cara tusaidie jambo moja sasa hivi, Mwanasheria kuna simu anaipiga hivi sasa, tafadhali ifuatilie huyo anayepigiwa yupo wapi kwa wakati huu."

Mwanasheria akapiga nambari ile aliyopatiwa, kwa bahati nzuri ilikuwa ikiita. Iliita hadi ikakata. Akapiga mara ya pili, safari hii ikapokelewa.

"Haloo.. Unazungumza na Joseph Urio, bila shaka ninazungumza na Exaud Kimbori Meneja wa NMB katika tawi dogo lililopo hapa Uchumi Plaza" Mwanasheria alikuwa akiongea.

"Bila shaka ni mimi. Karibu nikusaidie" Sauti ikasikika simuni ikisema. Mwanasheria akatabasamu baada ya kusikia. Akaitazama saa yake ya mkononi na kisha akamtazama Elizabeth Neville. Elizabeth naye hapohapo akamcheki Cara. Baada ya sekunde tano hivi Elizabeth Neville akampa Mwanasheria ishara ya kuendelea kuzungumza kupoteza muda ili Cara afanikiwe kule alipo. Mwanasheria bila kusita akafanya hivyo.

"Kuna swala la kibiashara ningependa kujadiliana nawe, ni kuhusiana na kazi yako pia katika maswala ya kibenki. Tafadhali nijuze ni wakati gani tunaweza kuonana hapa ofisini kwako au sehemu nyingine tuzungumze." Mwanasheria akasema.

"Samahani kwa hilo. Kwa sasa nipo Mkoani Tanga kikazi tangu jana, hivyo naomba nitafute kesho kutwa." Meneja Exaud alisema na kisha simu kukatwa. Mwanasheria alimtazama Elizabeth Neville huku akiduwaa. Elizabeth Neville alikuwa akitabasamu kwa mbali, na kwa mbali alionyesha huzuni pia.

"Cara anasema mnara unasoma PANAMA Hotel. Bila shaka ile anuani aliyotupatia yule mlinzi ilikuwa sahihi. Twende Panama Hotel sasa hivi" akasema Elizabeth Neville, haraka wakageuza gari na kuelekea barabara ya kuelekea soko la vyakula Mbuyuni. Mbele kidogo wakakunja kulia barabara inayowapeleka moja kwa moja Panama Hotel.
Dakika mbili tu mbele walifika mbele ya Jengo la Panama Hotel. Lilikuwa ni jengo la ghorofa nane kwenda juu. Walishuka kwenye gari, wakajitazama kama wapo sawa, wakaingia ndani kuelekea mapokezi.
Pale mapokezi walikutana na Dada mmoja mnene. Baada ya salamu wakagundua dada yule ni mchaga kutokana na lafudhi yake.

"Naam Karibuni sana Panama Hotel" Dada yuke akawakaribisha tena kwa ukarimu.

"Ahsante sana Dada. Sisi ni maofisa wa polisi, kuna mtu wetu yupo hapa hivyo tumekuja kumchukua. Vitambulisho vyetu ni hivi unaweza kuvitazama." Elizabeth Neville akasema huku akimpatia dada yule wa mapokezi kitambulisho chake. Mwanasheria naye akatoa chake na kumwonyesha asome huku akiangaza macho yake kuelekea kwenye ngazi za kupandishia juu.
Dada yule pia akaonyeshwa kitambulisho cha Exaud Kimbori. Macho ya dada huyo yalionyesha ni kweli alikuwa akimfahamu mtu huyo, lakini kabla hajasema kitu ikasikika sauti ya mtu akijikohoza nyuma yao.

"Hey Lady. Natoka, naomba mtu yoyote akija kuniulizia hapa mwambie sijaonekana hapa tangu jana, pia nitaarifu." Mtu yule akasema, na kumbe mtu huyo alikuwa ni Exaud Kimbori.

Naam, hatimaye Exaud Kimbori kajileta kiulaini mbele ya wapelelezi. Nini kitajiri? Watafanikiwa kumkomboa Daniel Mwaseba? Leo Jioni tutafunga ukurasa wa msimu wa nne. Usikose saa kumi na moja jioni hapahapa. Cha kufanya ni like na kukoment pia alika marafiki zako waufollow ukurasa huu.

Msimu wa tano wa Riwaya yetu ya Anga ya Washenzi unapatikana kwa Tshs 700 tu. Lipa kwenda M pesa namba 0765824715 au TigoPesa namba 0678824073 kisha njoo whatsapp kwa namba 0621249611 nikutumie.

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 
Gilbert Evarist Mushi anakusimulia Anga ya Washenzi.
Hii ni Sehemu ya 08

Songa Nayo....
Palepale Mwanasheria akageuka kwa kasi kumuelekea Exaud na kukionyesha kitambulisho chake...
"Bwana Exaud Kimbori upo chini ya ulinzi kuanzia hivi sasa. Naitwa Songelael Ntenga, ni afisa wa Jeshi la polisi, ukiwa mtaratibu nami nitakuwa mtaratibu kwako.
Ni wazi Exaud hakutegemea lile. Alishagundua hilo mapema baada ya kupigiwa simu ile hivyo alikuwa katika harakati za kutaka kuondoka pale.
Mwanasheria na Elizabeth Neville walifanikiwa kuondoka na Exaud na walipanga kumpeleka katika ile nyumba iliyopo stesheni ya treni.

Asubuhi hiyo Gilbert Mwaitika alikuwa pamoja na Cara wakifuatilia baadhi ya taarifa kutoka mitandao mbalimbali. Moja ya jambo ambalo walikuwa wakilifuatilia ni juu ya taarifa za Daktari mmoja ambaye waliamini anao uwezo wa kuwasaidia katika kuondoa kile kifaa kilichowekwa katika kichwa cha mtoto wa Henry na kile kilichowekwa katika moyo wa Festus. Daktari huyu alikuwa anaitwa Dokta Kalita.

"Dokta Kalita aliwahi kuwa mganga mkuu wa serikali katika nyakati tofauti, pia aliwahi kuwa dokta wa ikulu ya rais. Kwa sasa hana kazi baada ya kuomba kupumzika. Inasemekana anayo maabara yake iliyopo huko Igumbilo Iringa. Dokta huyu tukiweza kumpata anaweza kutusaidia." Cara akasema huku akimtazama Gilbert Mwaitika. Wote wakatazamana kwa sekunde tatu ndipo wakayakwepesha macho yao kwa haraka.

"Wazo lako Gilbert. Unafikiri tutampataje?" Aliuliza Cara
Gilbert akaachia pumzi ndefu akionekana kama kutafakari jambo.
"Kuna mtu nafahamiana naye huko Iringa, tumtumie huyo labda. Kipindi nikiwa polisi wa kawaida nilikuwa nina urafiki naye sana."
Gilbert alichukua simu yake na kuitafuta namba ya Richard. Anamkumbuka Richard Mpwepwa, walikuwa pamoja miaka mitano iliyopita katika mkasa mmoja mzito uitwao BIASHARA YA WATOTO, mkasa ulioandikwa katika majarida mbalimbali na mwandishi Gilbert Evarist Mushi. Anakumbuka katika mkasa huo alishirikiana vyema na Richard kuwadhibiti watu wote waliokuwa wakifanya biashara haramu ya kuteka watoto na kuwauza katika nchi za Marekani na Canada. Aliiona nambari ya Richard, akaipiga. Simu yake ilionekana kuita kwa muda mrefu hadi kukata.

"Vipi, hapatikani?" Aliuliza Cara wakati anamtazama Gilbert kwa kukosa matumaini.

"Inaita tu. Ngoja nipige tena" Gilbert akasema na kujaribu tena. Safari hii ikapokelewa kwa haraka.

"Gilbert Mwaitika huyooo. Yaani leo ndio unanikumbuka rafiki yangu?" Sauti ya Richard ilisikika simuni

"Richard habari za miaka? Nimekukumbuka leo rafiki yangu, bila shaka upo Iringa" Gilbert Mwaitika alisema

"Ni msaada wangu unauhitaji ndio maana umenikumbuka Gilbert? Hahahaha.. Nipo Iringa lakini. Kuna ishu naifwatilia inaniumiza kichwa tangu jana mchana. Niambie lakini kwema?"

"Ni kwema kiasi rafiki yangu. Nilikuwa nina shida na Daktari mmoja hivi anaishi huko Iringa. Naomba unisaidie jinsi ya kumpata ikiwezekana leoleo apande ndege aje huku Moshi." Gilbert akaeleza.

"Mmmh. Niambie lakini, japo nimebanwa sana na majukumu rafiki yangu. Ni Dokta gani huyo na anaishi wapi? Nipe anuani yake Gilbert."

"Anaitwa Dokta Kalita. Igumbilo ndio yalipo makazi yake kwa sasa. Inasemekana Dokta huyu ni.. " Gilbert alishindwa kuendelea baada ya Richard kumkatisha.

"Unamzungumzia Dokta Kalita ambaye aliwahi kuwa mganga mkuu wa serikali?" Richard aliingilia kati.

"Huyo huyo Richard. Unamfahamu?" Gilbert akauliza. Wakati huo Cara alikuwa akijaribu kumtafuta Henry katika simu.

"Gilbert. Nasikitika sana kukueleza hutoweza kumpata Dokta Kalita" Sauti ya Richard ilisikika ikisema kinyonge.

"Kwanini haitawezekana Richard? Nieleze tafadhali Richard unanipa mashaka. Nakutegemea rafiki yangu maana hakuna awezaye kunisaidia zaidi ya daktari huyu." Gilbert alionekana kutaka kujua.

"Ni hivi Gilbert. Jana majira ya mchana kituoni kwetu tulipokea taarifa ya uvamizi katika maabara ya Dokta Kalita, jambo la kushangaza ni kwamba wavamizi waliondoka na Dokta bila kuchukua kitu chochote kile. Jalada hili nilipewa mimi na mkuu wangu wa kituo, nimejaribu kufanya kila namna lakini nimekosa kabisa mwangaza." Maneno ya Richard yalimwacha Gilbert kinywa wazi. Hakujua aseme nini, alichoka akili na nguvu.

"Mungu wangu...! Ngoja nitakupigia baadae kidogo Richard, lakini ni lazima tumpate maana ni yeye tu." alisema Gilbert Mwaitika.

"Kuna nini Gilbert? Imeshindikana?" Cara alihoji baada ya kumwona Gilbert akikosa matumaini.

"Dokta Kalita ametekwa na watu wasiojulikana toka jana. Ni lazima tumtafute haraka iwezekanavyo. Halafu kwanza nimegundua kitu. Dokta Kalita kama alishawahi kufanya kazi Ikulu ya Rais basi ni lazima anayo chipu ya kuonyesha popote alipo. Mfanyakazi yeyote ambaye hufanya ndani ya ikulu ya rais tena katika kitengo kikubwa kama kile huwa ni lazima kupandikizwa chipu kwani watu kama hao ni rahisi kukimbia na taarifa nyeti ama kutekwa. Sidhani kama Dokta Kalita hana hiyo chipu. Tufanye mpango wa kupata taarifa za ni wapi alipo" Gilbert alifufua matumaini ya kumpata Dokta.

"Halafu kweli. Yaani sikuwa hata na wazo hilo. Sasa hapa ni lazima tumtumie Elizabeth Neville ili awasiliane na Chifu amweleze hili, maana sio rahisi kama unavyodhani. Ngoja nimpigie Elizabeth Neville"
Cara akasema huku akitafuta namba ya Elizabeth Neville. Aliipata na kuipiga. Baada ya sekunde nne ilianza kuita. Hatimaye ikapokelewa.

"Elizabeth habari za huko?. Kuna swala nahitaji utusaidie, uko wapi kwa sasa?..... Ohoo kumbe, mmepata chochote?... Hongereni. Sasa ni hivi, tulikuwa tukitafuta Dokta anayeweza kutusaidia kwenye lile swala, tumempata lakini kwa bahati mbaya haijulikani alipo na ni lazima tumpate. Kwa vile anayo chipu basi tunaomba utusaidie kuongea na Chifu Abdallah Ntenga ili tuweze kujua ni wapi alipo."
Cara alikuwa akiongea na Elizabeth Neville. Walikuwa wakipambana kujua ni wapi alipo Dokta Kalita aweze kuwasaidia. Hivyohivyo kwa Mwanasheria Mlevi na Elizabeth walikuwa wakimtafuta Daniel Mwaseba. Lakini Dokta Kalita alionekana ndani ya treni akimuuguza Daniel Mwaseba ambaye hana fahamu. Hawakujua hilo.
Hawakujua.

Huu ni Mwisho wa Msimu wa Nne wa Anga ya Washenzi. Mwandishi wako ni mimi Gilbert Evarist Mushi. Msimu wa Tano unakwenda kutupa majibu ya kila swali. Usikose
Ni kwa Tshs 700 tu utakwenda kuusoma msimu wa tano ambao ni wa mwisho. Lipia kwenda M pesa namba 0765824715 au TigoPesa namba 0678824073 kisha njoo whatsapp nikutumie. Kumbuka kunichangia tshs 700 na sio kulalamika. Kama huna whatsapp nicheki inbox nikuelekeze utaipataje hapahapa Facebook.
Ahsanteni sana. Tujiandae na riwaya mpya iitwayo MAITI 15 TU NITAFURAHI TENA.

2023

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 

Riwaya ya kipelelezi: Maiti 15 tu nitafurahi tena
 
Back
Top Bottom