Richa ndiye wa kulaumiwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,009
Baada ya kushinda alitakiwa awasiliane na washiriki wa nyuma ili kupata maoni yao kuhusiana na mashindano hayo. Angeweza kuwatafuta mmoja mmoja au kuwaita wote kwa kikao ili akakusanya maoni ya nini cha kufanya katika mashindano hayo.

Aliona umuhimu wa kufanya sherehe na wahindi wenzie ili kusheherekea ushindi wake, lakini hakuona umuhimu wa kukaa na washiriki waliopita ili kukusanya maoni yao na kuyafanyia kazi, sasa analalama hawakuja kumpokea! :confused:

Warembo kumtenga Richa noma

Khadija Kalili
Tanzania Daima

SALAAM aleikum wapenzi wasomaji wa safu ya Busati, ni matarajio yangu kwamba kila mmoja wetu hajambo na mambo ya kila mmoja ni safi.

Leo wapenzi wasomaji nitazungumzia juu ya mrembo wetu wa taifa, yaani Miss Tanzania 2007 Richa Adhia, hivyo hapa nitazungumzia namna alivyoyapokea matokeo ya kushiriki kwake katika shindano la Miss World kwa ujumla.

Awali ya yote, mara tu mrembo huyu alipotwaa taji hili yalisemwa mengi huku wengi wakimpinga na kusema kwamba hawamkubali, huku kila mmoja akitoa sababu zake.

Katika hali ya kawaida, mimi binafsi huwa naheshimu sana mawazo ya mtu na kamwe huwa simpingi, kwa kuwa huwa nasikiliza hoja kwanza.

Nasema hivi kwa kuwa wapo baadhi ya watu ambao siku zote wao huwa ni mashabiki na wanazi katika mambo mbalimbali, yaani ilimradi tu aonekane na kusikika kachangia kwa kusema jambo fulani mbele ya watu.

Siku zote watu kama hawa si watu wa kuwasikiliza, vivyo hivyo katika masuala ya urembo watu wengi tumekuwa tukijadili hili ama lile ilhali kwamba wengi wetu bado hatujafahamu nini kigezo kikuu cha kuwa Miss World.

Jambo hili limekuwa likinibangua kichwa binafsi, hasa pale nilipohesabu miaka mitatu mfululizo shindano la kumsaka mrembo wa dunia limekuwa likifanyika Sanya, China huku Wachina wakishuhudia warembo wa kigeni wakinyakua taji na kurudi makwao.

Hivyo basi, mwaka huu zamu imekuwa kwa Wachina, ambapo wametwaa taji nyumbani kwao na si kwamba labda wametwaa kwa upendeleo, la hasha!

Wamefanya jitihada binafsi na kama ingelikuwa kuna kubebana basi wangebebwa kwa miaka yote ambayo wamekuwa wakiandaa, ilionekana dhahiri kwamba mrembo wao alistahili.

Naweza kusema kwamba China walijiandaa na kuweka mikakati ndiyo mana wamefanikiwa kulibakisha taji hilo nyumbani kwao ambapo haikuwahi kutokea kabla.

Vivyo hivyo naweza kusema kwamba hili liwe fundisho kwa nchi zote mbazo hupata nafasi ya kushiriki katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia kwa kuweka mikakati ya kutwaa taji kwani huleta sifa kwa nchi husika.

Hivi sasa China iko juu, licha ya kwamba tayari ilikwisha kuendelea, hivyo hawakubweteka na maendeleo waliyoyapata, ndiyo mana hivi sasa katika kila kona ya dunia Wachina wapo wakiendelea na mambo yao ya kutafuta maendeleo.

Sasa iweje leo sisi tunashindwa kutafuta njia mbadala na kuendeleza majungu na chuki kwa mrembo, hasa pale anapovurunda, tujiulize nini chanzo na nani wanahusika.

Kadhalika Watanzania tusidhani kutwaa taji la mrembo wa dunia ni lele mama, kwa kuwaandaa warembo kwa muda wa mwezi mmoja tu pale wanapokuwa katika kambi ya Miss Tanzania halafu wanakwenda ughaibuni, huku tuliobaki nyumbani tukitazamia maajabu yatokee.

Tunachotakiwa sasa ni kupenya nyuma ya pazia jeusi ambalo warembo wengi ambao waliwahi kushiriki wamekuwa wakilalama kwa kusema kwamba kuna mambo mengi katika shindano la Miss World, tofauti na jinsi ambavyo wamekuwa wakifikiria.

Hivyo basi, sasa tutafute ufumbuzi wa makosa na kasoro wanazokutana nazo warembo wanapokwenda kushiriki kama hamasa ya kufunua kombe, badala ya kulifunika ili mwanaharamu apite.

Itakuwa faraja kubwa siku Mtanzania atakapong’ara kwenye jukwaa lile lililosheheni mabinti warembo wenye vimo na sura nzuri za kuvutia.

Tuachane na dhana potofu ya kuwaita warembo wetu wanaoboronga kuwa ni vichwa vya wendawazimu, na kama wao ni wendawzimu, basi ikumbukwe kuwa wendawazimu watakuwa wengi, kuanzia majaji hadi waandaaji, kitu ambacho si sahihi na hakipendezi.

Kadhalika wakati umefika sasa Kamati ya Miss Tanzania ikae na kuunda mikakati mipya ambayo itasaidia kuwapata warembo wenye sifa zote.

Hakuna ubishi kwamba kila mtu ambaye ni mdau wa masuala ya urembo aliangalia namna shindano la mwaka huu lilivyosheheni warembo wenye sifa kutoka kila kona ya dunia huku kila mmoja akionekana kuchanua kama waridi.

Katika hatua nyingine, warembo wetu wameonyesha kuwa ni wenye fikra fupi, hasa baada ya kumsusa mwenzao kwa kuacha kwenda kumpokea uwanja wa ndege, hata kama hakufanikiwa kupata taji wala nafasi yoyote, lazima hilo lilaaniwe.

Nasema lilaaniwe na kukomeshwa, kwani linapanda mbegu mbaya miongoni mwa warembo wa kizazi kijacho, kwani hadi hapo utaona namna warembo wetu wanavyochangia kuipaka matope fani hii.

Warembo hapo hamjengi na mmeonyesha jinsi gani mlivyo watovu wa nidhamu, hasa ukizingatia nidhamu ni sifa moja kuu katika urembo, Jambo la msingi tulilotarajia ni kuona warembo walioshinda katika nafasi mbalimbali katika miaka yote wakiwa pamoja uwanjani kumpokea mwenzao, lakini haikuwa hivyo, kwani mrembo huyo alipokewa na kamati ambayo imesheheni kina baba pekee.

Labda hawakuwa na taarifa kama mwenzao anarudi na kumwandalia mapokezi, si lazima yawe makubwa, lakini japo angewakuta wachache mngempa faraja.

Miss World mwaka huu ni Zi Lin Zhang, ambapo mrembo kutoka Angola Micael Reis, alishika nafasi ya pili, aliyefuatiwa na Carolina Moran Gordillo kutoka Mexico.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Miss World, Julia Morley, amesema kwamba mrembo atakayetwaa taji la Miss World atatembelea nchi zote zilizokuwa na washiriki, ikiwemo Tanzania, ambapo atatumia ziara yake kuhamasisha jamii kujikinga na ukimwi.

Warembo wengine ambao waliwahi kushiriki katika shindano la dunia na kushindwa kufurukuta ni: Aina Maeda (1994), Emily Adolph (1995), Shose Senare (1996), Saida Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999), Jacqueline Ntuyabaliwe (2000), Happiness Magese (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta (2004), na Nancy Sumari, ambaye ndiye mrembo pekee aliyeweza kuitangaza nchi kwa kuwa mrembo bora barani Afrika ‘Miss World Afrika’ 2005; na mwaka jana Tanzania iliwakilishwa na Wema Sepetu.
 
Back
Top Bottom