Nimeisoma Rasimu ya Katiba
Inayopendekezwa, nimeisoma yote, ni bahati
mbaya inapigiwa upatu kwamba imebeba
mambo ya wananchi, mambo ya wakulima,
wafugaji, wavuvi, vijana na kadharika. Jamani
hayo ni hadaa, msingi wa muundo
umebadilishwa, Tanganyika imevalishwa koti
jipya la Muungano, ambalo tusipokuwa
makini itaendelea kuishi nalo muda mrefu
zaidi.
Kigezo cha kukataa serikali 3 hakina
hoja zenye mashiko, wanasema Hati ya
Makubaliano ilisema serikali 2 hivyo hatuwezi
badili, huu ni uongo, mbona Hati ilisema
mambo ya Muungano ni 11, mbona wao
wameweka 14, uhalali wa kubadili mambo ya
Muungano kama Hati haibadiliki wanaupata
wapi.? Hii ni double standard. hati
haikujieleza kwamba kwa baadhi ya maeneo
mwiko kubadili na ruksa kwa mengine, Amka
ee Mtanzania.
Unasema katika Sura ya Pili unaanzisha Tume
ya Mipango ya Taifa ilhali ukijua Zanzibar
wana Tume ya Mipango pia, nashangaa sana.
Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inasema
Kutakuwa na Dira, Ohoo, kutakuwa tena,
nilidhani inapaswa itamkwe, na kwa asili ya
"Programmatic Constitutions" Dira inakuwa
ni ujumla wa Lengo Kuu la Katiba Pamoja na
Malengo Mahususi kama ilivyokuwa kwenye
Rasimu.
Wamefuta kumwajibisha Mbunge, wamefuta
ukomo, wamefuta mbunge asiwe waziri,
wamefanya ugombea binafsi kuwa mgumu
zaidi, wamevuruga Tume ya Uhusiano na
Uratibu, wao wamesema Tume hii ni kwa
Mambo ya Muungano, hili ni kosa kubwa la
kisanifu (design), Mambo ya Muungano
yanasimamiwa, yasiyo ya Muuungano
yanaratibiwa.
Wameweka Baraza la Vijana,
vijana wenzangu hii ni hadaa, walio wengi ni
wanawake mbona lao hawakuliweka,
ninazingatia haki hapa, wanataka
kuwahamasisha kwa mambo ambayo katika
utalaamu na uandishi wa Katiba hayapo,
yamewekwa ili msahau yale waliyofuta.
Wamerudisha wakuu wa Mikoa, wananchi
mlisema sana juu ya uwepo wa wakuu wa
mikoa na wilaya.. kwa namna walivyo rudi
sitashangaa wakiendelea kuwa makada wa
vyama vya siasa. Haya maoni ya kuwaweka
wakuu wa mikoa katika namna hii wameyatoa
wapi.? Maoni hayo mimi sikuyaona Tume ya
Katiba kipindi chote nilichokuwepo.
Vyanzo vya mapato ni vile vile kwa serikali ya
muungano (Katiba ya 1977) na wakadhani
mwarobaini ni kurejesha Tume ya Pamoja ya
Fedha ambayo haikuwahi kufanyiwa kazi
(kuna sababu kubwa zaidi kuliko kuwa na
Tume ya Pamoja ya Fedha), Bahati mbaya
Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa imelikosa
hili.
Rasimu ya Katiba inayopendekezwa inasema
Makamu wa Rais Watatu, Makamu wa Kwanza
(Muungano), Makamu wa Pili (Rais wa
Zanzibar) na Makamu wa Tatu (Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano)... Jamani
watanzania wenzangu, huu UTATU mbona
tunapewa kwa mgongo wa chupa, TATU
tunaziogopea nini.? Tume ya Pamoja ya Fedha
iliwaambia anzisheni akaunti ya pamoja ya
fedha, ikawa kigugumizi, leo kipi kitafanya
tuweze?
Mnasema Mahakama Kuu ya Zanzibar na
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano
zitakuwa na Mamlaka sawa (concurrent
jurisdiction), hata kwa jina hapo si
tunadanganyana.? Hakuna kitu kama
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano,
kwasababu ninyi mnajua haina Mamlaka
Zanzibar sasa kuiweka kwenye Muungano
kunani.?
NINAENDELEA NA UCHAMBUZI, KAMA
NILIVYOSEMA KAZI NDIO KWANZA IMEANZA.