Si nia yangu ya kuzungumzia tabia binafsi ya mtu, lakini linapokuja suala kubwa na la kitaifa kama hili la kuandika Sheria Mama ya Nchi, hivi ndiyo CCM ilikosa mtu mwenye mikono misafi ya kutuandikia Katiba Mpya? Nimeipitia katiba yake mpaka nimeona aibu kama mtanzania kwa sababu imeandikwa huku mtu akijitazama dhamira yake na kuweka vitu ambavyo havita mgusa kwa sababu tayari amesha "chafuka mikono"!
Kama Taifa tujitazame, hivi Chenge anaweza kutuandikia Katiba ya Nchi....Kweli? HAPANA tumepotea! Vifungu vingi vinamuajibisha moja kwa moja mwananchi na inaelekeza sheria nyingine zitatungwa kumuwajibisha mwananchi. Haitofautiani na Katiba hii ya sasa, ambayo madaraka aliyopewa mwananchi ni kupiga kura kumchagua kiongozi kisha akae mita 200, asisogelee hata sanduku la kura mpaka baada ya miaka mitano!
Katiba ya Sitta na mwandishi wake Chenge, inatoa madaraka makubwa kwa viongozi na watendaji wa umma na wasiwajibishwe moja kwa moja na wananchi kwa mujibu wa katiba hii. Kama mwananchi tumenyimwa nguvu ya kikatiba ya kumuwajibisha kiongozi au mtumishi wa umma, basi wananchi tutaendelea na tabia ya "KULALAMIKA" kama awali, kwa maana hatuna nguvu ya kikatiba ya kutenda! Na tukisema "tutende", virungu, maji ya kuwasha na risasi zitatuangukia.
Hii ni Katiba iliyoandikwa na Viongozi kwa wananchi na si Katiba iliyotungwa toka maoni ya wananchi kwa viongozi. Tumerudi miaka 50 nyuma!