Raia waendelea kufia mikononi mwa polisi, tukimbilie wapi IGP Wambura?

Shahed kamikaze

JF-Expert Member
Jul 4, 2016
575
959

Watatu wafia mikononi mwa Polisi K’njaro, Dodoma​

SATURDAY SEPTEMBER 17 2022​



wafiaapiic

Summary

  • Matukio ya watu kufa wakiwa mikononi mwa Polisi, yameendelea kushika kasi kufuatia vifo vilivyotokea katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma hivi karibuni, huku jeshi hilo mkoani Kilimanjaro likithibitisha kutokea kwa mauaji hayo.
K’njaro/Dodoma. Matukio ya watu kufa wakiwa mikononi mwa Polisi, yameendelea kushika kasi kufuatia vifo vilivyotokea katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma hivi karibuni, huku jeshi hilo mkoani Kilimanjaro likithibitisha kutokea kwa mauaji hayo.

Miongoni mwa matukio hayo ni lile la Septemba 8, mwaka huu, ambapo mkazi wa kijiji cha Kirongo Chini wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, Ulirki Sabas(47) alidaiwa kupigwa na polisi wa kituo cha Usseri na kusababisha kifo chake kwa madai ya kulala na mwanafunzi.

Tukio jingine lilimhusisha mkazi wa Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi mkoani hapa, Nicholaus Mushi (27) aliyedaiwa kujinyonga Septemba 13 kwa kutumia tambara la dekio akiwa mahabusu katika kituo kikuu cha Polisi mjini Moshi alikokuwa akishikiliwa kwa madai ya kuiba simu ya mkononi na kompyuta mpakato.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema wanaendelea kuchunguza vifo hivyo, kikiwamo kifo cha mwananchi anayedaiwa kupigwa na askari.

Akizungumzia tukio la Mushi kujinyonga akiwa mahabusu, dada wa marehemu Nicholaus, Angella Mushi alisema kifo cha ndugu yake kimewaacha na maswali mengi kwa kuwa maelezo waliyoyapata polisi kuhusiana na kifo hicho, yana utata.

“Mtu yuko mahabusu, tunaambiwa amejinyonga na dekio, tunajiuliza hilo dekio limetoka wapi mahabusu? Lilikuwa gumu kiasi gani?

“Tunaambiwa kabla ya kujinyonga alijikata kwenye koromeo na wembe na wakampeleka hospitali, sasa swali la kujiuluza ni kwamba aliwezaje kuingia mahabusu akiwa na wembe?” alihoji.

Katika tukio la mwananchi kudaiwa kupigwa na kufia polisi, familia ya Ulirki ambayo inadai ndugu yao aliuawa kwa kipigo ndani ya kituo cha polisi, wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mauaji ya ndugu yao ili haki itendeke.

Mke wa marehemu, Prisila Kavishe, alisema Septemba 8 alipompelekea mume wake chai alimkuta akiwa buheri wa afya, ambapo muda mfupi baadaye askari walimtaka aondoke kituoni hapo kwa kuwa walimwambia atapelekwa mahakamani.

Alidai muda mfupi baada ya kuondoka, alipigiwa simu na jirani yake kuwa hali ya mume wake ni mbaya na alipofika kituoni alimkuta amelala chini akiwa ameumizwa ambapo sehemu ya utosini kulikuwa na uvimbe mkubwa, jicho moja likiwa limejeruhiwa, mdomo ukiwa umevimba, huku akivuja damu puani na mdomoni.

“Tunajua Rais wetu ni mtu anayependa haki na hapendi kuona mtu anaonewa. Sisi ni familia ambayo hatuna uwezo hivyo tunaomba msaada wa Serikali na mama yetu Samia Suluhu Hassan aingilie kati jambo hili ambalo limetuumiza familia,” alisema.

Hata hivyo, jana Kamanda Maigwa aliagiza mwili wa marehemu kuondolewa katika hospitali ya Huruma wilayani Rombo ulikokuwa umehifadhiwa na kupelekwa hospitali ya KCMC Moshi kwa ajili ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi mkubwa.

Akizungumza mjomba wa marehemu, Deusdedith Massawe ambaye alishiriki kwenye shughuli ya upasuaji wa mwili wa ndugu yake KCMC, alisema baada ya mwili kuchunguzwa daktari aliwaeleza kuwa sehemu ya kichwani (kwenye fuvu) kulikuwa na jeraha kubwa lililosababisha kifo chake.

Mwili wa mwanaume huyo ulizikwa jana katika kijiji cha Kirongo Chini, wilayani humo jambo ambalo limelaaniwa vikali na baadhi ya viongozi wa CCM wakisema haki haikutendeka.

Taarifa mpya zinadai kuwa mwanaume huyo baada ya kupigwa na kujeruhiwa, polisi hao walijaribu kumpeleka gereza la Ibukoni na kituo cha polisi mkuu ambapo alikataliwa kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Hata hivyo, kamanda,alisema jana wamefanya postmortem (uchunguzi wa kifo) na majibu yanatolewa na daktari.

Adaiwa kujinyonga Dodoma
Utata kama huo umejitokeza jijini Dodoma, ambapo fundi ujenzi, Gaston Moshi amedaiwa kujinyonga katika kituo cha Polisi cha Bonanza.

Mwili wa fundi huyo upo katika hospitali ya Rufaa ya General na unatarajiwa kuzikwa leo na Serikali kutokana na ndugu zake kutojulikana.

Hata hivyo, kumekuwa na sintofahamu jinsi ambavyo kifo chake kimetokea huku baadhi wakidai walikuwa wakigombania mwanamke na askari wa kituo cha Bonanza ambaye alienda kumkamata katika eneo lake la kazi.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,Martin Otieno alisema atafutwe baadaye kwani alikuwa akimsindikiza Makamu wa Rais Dk Philip Mpango uwanja wa ndege. Alipotafutwa kwa mara ya pili alisema yupo katika kikao na Mkuu wa Mkoa na kwamba akitoka angempigia mwandishi. Hakufanya hivyo mpaka gazeti linakwenda mtamboni.

Undani tukio la dodoma
Fundi mwenzake, Abdul Khamis alisema Jumatano ya Septemba 7 mwaka huu, askari ajulikanaye kwa jina la moja la Samweli alifika katika eneo lao la kazi eneo la Zuzu katika kiwanda cha mabati cha Ando, akiwa na gari lenye namba za usajili T497 DMS na kumuulizia marehemu.

Alisema alipofika alitaka kuingia moja kwa moja na gari hiyo, lakini mlinzi aliyekuwepo alimkataza akimtaka aandikishe kwanza jina.

Alisema alipofika alimkamata na kumfunga pingu na kuondoka naye bila ya wao kujua wanaelekea wapi.
“Tulipomuuliza yule askari shida ni nini alisema kuna dada amekwenda kituoni na kudai Gaston amempokonya simu yake, hatukuhoji sana tukajua yataenda kuisha,” alisema.

Khamis alisema baada ya kukamatwa Gaston hakuonekana kazini kwa siku tatu hivyo ilivyofika Jumapili ikabidi waanze kumtafuta. Alisema walienda mpaka katika kituo cha polisi cha Bonanza lakini hawakumkuta na walipomuulizia waliambiwa wasubiri watapewa majibu.

“Ilibidi tumpigie simu tena afande Samweli na alifika kituoni alitueleza kuwa marehemu alijinyonga kwa kutumia shati kituoni hapo na mwili wake wameupeleka mochwari katika hospitali ya Rufaa ya General,” alisema.

Alisema walipoenda hopitalini hapo walikuta ni kweli mwili wa Khamis upo na maelezo waliyopewa ni kwamba utazikwa leo.

Chanzo: Mwananchi
 
Hao ndiyo PT. Raia huenda kujiuia kwao. Ni ling'ombe tu ndilo linaloweza kukubliana na habari zao za kubumba hizi.
 
Back
Top Bottom