Shule ya umma anayosoma Pauline Wahuna, iliyoko katika Kaunti ya Kajiado, kusini mwa Kenya, inaweza kutoonekana kwa urahisi, lakini imekuwa kituo kinachoshamiri cha kuendeleza kizazi kijacho cha waandishi wa Msimbo (coding).
Mwaka 2024, Pauline Wahura, mwenye umri wa miaka 15 anayesoma Daraja la 9, alijiandikisha katika program ya Msimbo shuleni hapo. Program hiyo inaungwa mkono na CODEMAO, jukwaa la elimu la mtandaoni la nchini China, kwa kushirikiana na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Kutokana na utashi na mapenzi yake, Wahura sasa anatumia muda wake mwingi akiwa na kompyuta kibao (tablet) mkononi, akizama kwa kina katika dunia ya msimbo ambayo ina uwezo wa kuchochea uvumbuzi wa kipekee.
Mapenzi ya Wahura katika mambo ya msimbo kwa sehemu yaliyotakana na nia yake mwenyewe lakini pia na kuungwa mkono na mama yake, ndugu zake na walimu, ambao walisisitiza fursa yake katika kubadili maisha yake ya baadaye.
Wahura anasema kando ya uzinduzi wa awamu ya pili ya mkutano wa vijana kuhusu msimbo nchini Kenya ulioandaliwa na CODEMAO na UNESCO hivi karibuni jijini Nairobi, kwamba anachotaka ni kufahamu zaidi kuhusu michezo ya kwenye kompyuta na jinsi inavyotengenezwa, pamoja na michoro, na ndio sababu kuu ya kuingia katika dunia ya msimbo.
Kutokana na juhudi zake, Wahura amejitokeza kama mmoja wa wanafunzi bora wanne kitaifa waliochaguliwa kushiriki ziara ya mafunzo mjini Shenzhen, kituo maarufu cha teknolojia kusini mashariki mwa China, ambayo yanatarajiwa kuanza tarehe 9 hadi 16 mwezi Julai. Katika ziara hiyo ya wiki moja, Wahura na wanafunzi wenzake watatu pamoja na mwalimu wao, watatembelea kampuni za teknolojia, kutafiti utamaduni wa Kichina, na kujifunza kuhusu maendeleo mapya katika mambo ya msimbo na Akili Mnemba (AI).
Jadiel Korir, ambaye pia ana umri wa miaka 15 na anasoma Daraja la 9, anasema alianza kuvutiwa na msimbo mwaka mmoja uliopita, alipomwona binamu yake ambaye ni mtaalamu wa usalama wa mtandaoni. Anasema msimbo unaweza kumsaidia kufanya uvumbuzi unaoweza kubadili jamii, akisema ana hamu sana ya kujifunza zaidi kuhusu AI atakapokuwa nchini China.
Collins Okwoyo, mwenye umri wa miaka 16 na anayesoma Daraja la 9, tayari amewavutia sana walimu na wanafunzi wenzake kutokana na shauku yake inayoongezeka kwenye mambo ya msimbo. Anasema anatarajia ziara yake ya mafunzo nchini China itamsaidia kupanua uwezo wake kwenye dunia ya msimbo na akili bandia, huku akishiriki katika mabadilishano ya kitamaduni na kujifunza zaidi kuhusu China.
Faith Wanjiru, ambaye ni Mwalimu wa shule sekondari anasema, pendekezo la msimbo kwa vijana la CODEMAO na UNESCO limewawezesha vijana kuwa na vifaa vinavyosaidia ujuzi wa kidijitali na kuamsha moyo wao wa uvumbuzi. Pia amesema, utaalamu katika msimbo na akili bandia umeboresha utafiti, kufanya mafunzo kuwa na maingiliano zaidi na ya kufurahisha, na pia unasaidia kutengeneza kizazi cha viongozi wa kiteknolojia nchini Kenya.
James Njogu, kaimu katibu mkuu na ofisa mkuu mwandamizi wa Tume ya Kenya katika UNESCO anasema, kuwawezesha vijana kwa ujuzi wa msimbo na akili bandia ni muhimu katika ujenzi wa uchumi jumuishi wa kidijitali. Anasema ufahamu wa kidijitali kati ya vijana ni msingi muhimu kwa kubadilisha siku za baadaye ambapo uvumbuzi unashamiri, nan i fursa ya ustawi inayopatikana kwa watu wote.