SEHEMU YA 178
Kwa mara ya pili, Tatiana alikuwa kipofu, hata alipopona kabisa, hakutaka kukaa nchini Marekani, alichokifanya ni kurudi nchini Tanzania tena kijijini Chibe, kule alipozaliwa ili kama kufa, basi alitaka kufa ndani ya nchi yake, tena katika kijiji alichozaliwa.
Kila Mtanzania alihuzunika, wengi walikuwa wakimlaumu Buffet na msichana wake Nikola kwa kile walichokifanya kwa msichana yule.Nyota kali ya mafanikio iliyokuwa ikiwaka, ilizimika ghafla.
Kila siku Tatiana alikuwa mtu wa kulia tu, aliyakumbuka maisha yake ya zamani, alitamani kurudi kule alipokuwa, aombe msamaha kwa kila kitu kilichotokea ili arekebishe maisha yake lakini hilo halikuweza kujirudia tena.
Mapenzi yalimchanganya, mapenzi hayohayo yalimfanya kuwa kipofu kwa mara nyingine tena. Peter hakutaka kumtenga Tatiana, akaamua kurudi kijijini kule kama ilivyokuwa zamani. Kipindi kile, alirudi akiwa na mapenzi ya dhati, alilia sana lakini katika kipindi hiki alirudia akiwa mtu tofauti kabisa, alimchukulia Tatiana kama msichana wa kawaida, kila kitu kilichopita kama mapenzi na ubaya aliotendewa, akaamua kuusahau, hakutaka kuupa tena nafasi.
Kila Tatiana alipokuwa akiisikia sauti ya Peter, alibaki akilia tu. Katika maisha yake yote hakuwahi kumuona mwanaume huyo, hakujua alifananaje, alipotabasamu uso wake ulikuwaje. Alikuwa kipofu ambaye mara kwa mara alikuwa akishinda chumbani kwake.
Kupitia fedha zake, akafungua biashara nyingi, akaendelea kuingiza fedha na kuwa mwanamke tajiri kuliko wote Afrika Mashariki. Alichokifanya ni kugawa asilimia ishirini ya utajiri wake kwa Peter kama msamaha kwa kila kitu kibaya alichomfanyia kwani aliamini kwamba mwanaume huyo alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
“Naomba unisamehe kwa kila kitu Peter, ni shetani tu aliyenifanya nikuumize,” alisema Tatiana huku akilia, machozi yalimbubujika mashavuni mwake.
“Usijali Tatiana! Mungu ni mwema, labda kutokuwa nawe kulikuwa na sababu, labda ningekuwa nawe hata hatua hii niliyofikia ya kumtumikia yeye nisingeifikia,” alisema Peter kwa sauti ya chini.