Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,742
- 40,874
Ukiona hawa wote, utadhani wako wote,
Wanalia panya wote, wasikika kotekote,
Kumbe lao si lolote, hawamaanishi wote,
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Paka afungwe kengele, analia panya yule,
Tujue akija pale, anaongeza na yule,
Tumkimbie paka yule, wanasema panya wale,
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Ulipoanza mkasa, leo nawasimulia,
Panya walifanya kosa, paka kumkumbatia,
Ni kosa la kisiasa, wakaja kulijutia,
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Paka aliwaambia, tena kwa kuwaapia,
Amebadili tabia, tabia ya kurukia,
Wao wakikubalia, kamwe hatowabugia!
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Panya wakafikiria, mwisho wakakubalia,
Paka mwana jumuiya, ya panya akaingia,
Vikao kahudhuria, vya panya wale mamia,
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Kila wanapokutana, kuna panya katoweka!
Ndipo wakaulizana, wameingiwa mashaka,
Kweli inawezekena, paka amekuwa paka!?
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Paka na akanenepa, huku panya wapungua!
Undugu waliompa, vipi watautumbua!
Ni vipi watamkwepa, bila ya kumshtua?
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
“Na tumfunge kengele”, wazo likakubaliwa!
Tukisikia kelele, anakuja tutajua!
Hatotushika milele, adui ameshakuwa!
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Tatizo wakatambua, panya wakafadhaika
Nani watamchagua, aende kwa uhakika,
Na kengele kuinua, kumfunga huyo paka,
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Wote wakaanza ruka, tena kuruka kimanga!
Wanamuogopa paka, yasijekuwa matanga!
Mabingwa wa kuropoka, midomo waliifunga!
Panya kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Akatokea mmoja, panya asiye na jina,
Akasema neno moja, neno lile alinena,
Yatosha mimi mmoja, kujitoa kiaina!
Panya kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
“Nitamfunga kengele”, na kumfunga huyo paka!
Utawala wake ule, utakoma kwa hakika!
Mwisho wake paka yule, umefika natamka!
Panya kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Akatoka panya yule, kwa mbinu za uhakika,
Yakimcheza machale, akilindwa na mahoka!
Kamkuta paka yule, ameshiba na kuchoka!
Panya kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Paka yule kasinzia, na ndoto zimenogea,
Shujaa kamvizia, huku ananyemelea,
Kaanza kumfungia, huku anamtegea,
Panya kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Mara panya kasikia, wapo wengine walia!
Paka wanamlilia, ati mwanajumuiya!
Ya wale panya mia, paka anaojilia!
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Waliomsema paka, wakaanza kutetea!
Ana haki za kipaka, vipi tunamuonea,
Amelala amechoka, vipi twamnyemelea!
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Paka afungwe kengele, au tumuache ale?
Tumtwange na gobole, tumtupe mbali kule?
Twende naye pole pole, paka huyu paka yule?
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Kwenye himaya ya panya, mfalme hawi paka!
Kuna neno ninaonya, kwa tungo niloandika,
Wakigawanyika panya, ndiyo furaha ya paka
Paka kufungwa kengele, siyo lao panya wote!
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)