Ota ndoto yako, usioteshwe ndoto ya mwingine

Ota ndoto yako, usioteshwe ndoto ya mwingine

Elius W Ndabila

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2019
Posts
339
Reaction score
678
Na Elius Ndabila

0768239284


Kuna mtu ukionana naye au ukimsikia unatamani umwambie unapotea, lakini hofu inakujia kuwa nikimwambia uhusiano wangu na yeye utakufa au anaweza kunidhuru.

Njoo nikwambie kitu; Hivi hujawahi kutana na mtu akakwambia kuwa mimi darasani kwetu ndiye nilikuwa na akili? Anakwambia yaani hata yule B munayemheshimu mimi darasani nilikuwa nikimuongoza kwenye masomo.

Mimi ndiye nilikuwa ninamfundisha. Ataendelea kukwambia mimi hata simu yake nikipiga atapokea. Atamalizia kwa kusema basi tu mimi sikuwa na bahati sikufaulu au atakwambia wazazi wangu walishindwa kunisomesha. Yaani anakwambia haya maneno akiwa yuko serious.

Hivi hujawahi kukutana na mtu anakwambia bila mimi yule asingekuwa na biashara ile anayofanya? Anasema mimi ndiye nilimshauri afungue duka. Au anakwambia mimi ndiye nilikuwa msimamizi wa lile duka, nilikuwa na uwezo wa kukaa na fedha zake zote kwa muda wote.

Anakwambia yaani bila mimi yule alikuwa masikini sana. Lakini jambo la kusikitisha utakuta mtu anayekupa simulizi hiyo maisha yake hayana mwelekeo, ila anajua siri zote za mafanikio ya B na huku akijinasibu kuwa yeye ndiye siri ya hayo mafanikio. Kimoyomoyo unasema, eeeee Mungu msaidie.

Ipo hivi, kwenye maisha kuna watu wanajua kusimulia mafanikio ya wengine huku wakijipa ufalume kwenye yale mafanikio kuwa ni wao walichangia.

Lakini huwa hawasemi kama wao ndio chanzo cha mafanikio ya hao watu kwa nini wao hadi leo hawajafanikiwa? Ndipo unapoweza kusema huyu mtu anaJIMWAMBAFAI na si chochote na si lolote.

Unapata wapi legality ya kusema umechangia mafanikio ya A wakati wewe miaka inaenda huna kinachofanana na unachotuaminisha kuwa umefanya kwa B?

Nimekuwa nikishuhudia hata kwenye siasa. Wapo watu atakusimulia siasa za tangu mwaka 1990. Atakwambia mwaka 1995 mimi na Y ndiye tulimfanya B ashinde nafasi hiyo. Atakwambia mwaka 2005 tulihama kambi tukaenda kwa C, tulipambana hadi akashinda.

Mwaka 2015 mimi niliamua kumuunga mkono E nilitembea usiku na mchana hadi E akashinda. Atakwambia mimi ni mwanasiasa niliyeiva na nimepikwa kwenye tanuru la UVCCM/ BAVICHA. Atakwambia siasa ya nchi hii mimi ninaijua.

Yaani anakwambia haya hata cheo cha ubalozi wa nyumba kumi hana ila anajisia kuvusha watu. Mwisho unakaa na kutafakari kuwa huyu mtu anaakili sawa sawa? Ni kweli kuwa amesaidia hawa watu kushinda au anajipa sifa zisizo zake?

Lakini unapata majibu ya aina mbili kuwa inawezekana anaJIMWAMBAFAI na si chochote na si lolote. Lakini jibu la pili unasema kama hili ni kweli basi amekosa mtu wa kumshauri.

Unatamani umwambie sasa achana na kazi ya kusaidia watu, nenda kasimame mwenyewe lakini unaogopa kumwambia kwa kuwa unajua atakasirika.

Mwisho niwashauri vijana ambao umri unafanana na wa kwangu, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Ubunge, Urais na Udiwani. Twendeni tukasimame wenyewe badala ya hizi simulizi kuwa bila mimi yule asingeshinda.

Twendeni tukajaribu ndoto zetu na tuache kuwaotea watu ndoto, tujiotee ndoto zetu. Tukijaribu tukishindwa tusikasirike twendeni tukaviunge vyama vyetu mkono kuhakikisha vinashinda.

Vyama vyetu vikishinda sasa ndipo unapata legality na legiticy ya kusema mimi nilijaribu nilishindwa, lakini kwa ushindi wa F nilisimama kuhakikisha anashinda. Huu ndo uhodari na Ushujaa.

Kukaa miaka 20 wewe kila mwaka unavusha watu ni ujinga, ni sawa na Baba anayemwambia mwanae mimi darasani nilikuwa na akili kuliko wote, ila B alifaulu kwa bahati na mimi ndiye nlikuwa ninamfundisha.

Mungu hawezi kukufanya wewe kuwa ndoto yaw engine bila kukupa ndoto yako. Tujiotee ndoto zetu kabla ya kuwaotea wengine. Mh Rais JOHN JOSEPH POMBE Magufuli asingekuwa Rais angesikiliza ndoto za Watanzania.

Watanzania walilazimishwa kuoteshwa ndoto na ndoto zao zikawaambia Rais ni Mh Membe au Mh Lowassa. Lakini Rais Magufuli pamoja na watanzania kulazimishwa kuoteshwa, yeye alisimamia ndoto yake.

Alikutana na changamoto nyingi wakati wa kutafuta wadhamini na alikutana na zomea zomea ya ya wafuasi waliolazimishwa kuwaotea watu ndoto lakini aliamua kusimama kidete juu ya ndoto yake.

Leo Dk. Magufuli ni Rais kwa kuwa alisimama na ndoto yake na waliokua wamelazimishwa kuoteshwa ndoto za watu wengine wamebaki na hadithi tu.
 
Back
Top Bottom