Operation Jicho la Paka na dakika za Mwisho(with Wolf rules )

Operation Jicho la Paka


Sehemu ya Tisa


Luteni kanali Mwinyi Kisoda komando mzoefu alikuwa ndani ya matatizo katika uwanja wa Vita huku akiwa hajui adui yupo upande gani

Alichoka!!!!

Luten kanali Mwinyi Kisoda alianza kukimbia kwa kasi kuelekea upande wa kusini ambako ndiko kikosi cha Koboko kilichoongozwa na Zaza kilikuwako na pia hata Alpha 01 na Alpha 06 walikuwa wameelekea huko.

Luten kanal Mwinyi Kisoda alikuwa anazidi kukaribia makadirio ya umbali aliohisi kikosi cha Koboko kilichoongozwa na Luten Zaza kilikuwako.

Upepo ulizidi kuvuma na kumfanya Luteni Kanali Mwinyi kisoda ashindwe walau kusikia uwepo wa watu kule alikokuwa akielekea.

Akiwa amefika usawa wa mita hamsini kama makadirio ya ruti ya mwanzo yalivyokuwa na alipofika usawa huo hakuona japo dalili ya uwepo wa mtu na eneo zima lilikuwa kimya kabisa.

“Alpha six, Alpha seven..”Luteni Kanali alijaribu kuita kwa kupitia vifaa vilivyokuwa masikioni mwa makomando wote lakini hakupata kuitikiwa na upande wowote.


Akiwa anazidi kupiga hatua kusonga mbele huku bunduki ikiwa mkononi tayari kwa lolote hapo akapata kuona jambo kwa mbele.

Mawani aliokuwa amevaa yakamsaidia kuona katikati ya kiza kile na kile alichokiona kwa mbele ndicho kilichomstua na kumfanya apunguze hatua za miguu yake kisha akaangaza kushoto na kulia na pasipo kufikiria zaidi akasogea hadi karibu na kile alichokiona na mara mwanga wa radi ukamlika na kumfanya atazame aina ya mkao wa kile alichokiona.

Mwili wa mtu ulikuwa umelala kifudifudi na kwa uzoefu wake mwili ule aliona haukuwa na uhai,akainama na kuutazama vyema mwili ule na hakuamini macho yake baada ya kuona ni mwili wa komando mwenzake komando aliekuwa na utambulisho wa Alpha 01.

Luteni Kanali Mwinyi kisoda akahamaki kwa hasira na uchungu,akamgeuza 01 na hapo akakutana na tundu kubwa la risasi usawa wa moyo na damu zilikuwa zinatiririka kumaanisha ya kuwa hakupigwa risasi muda mrefu na kwa makadirio yake alihisi ni dakika kumi zilizopita tangu kupigwa kwake.

Akilini mwake alijua kabisa silaha iliotumika ni silaha ya kudungulia tena yenye kiwambo cha kuzuia sauti.

Makomando watatu walikuwa tayari wameaga dunia huku akiwa hajui adui yupo upande gani na kubwa lililomuumiza ni kuona adui alijua usawa waliokuwa wao na ilionekana amejiandaa mapema kuwapokea.

“tumesalitiwa”alijisemea Luteni kanali mwinyi kisoda.

Akapitisha kiganja chake juu ya uso wa komando yule ili kumfumba macho kisha akajipiga kifuani kama ishara ya kujipa moyo na kuahidi uzalendo mbele ya makomando waliotangulia mbele za haki.

Akiwa anataka kutoka pale alipokuwa mara akili yake ikahisi kuna mtu anamtazama kutoka pahali alipokuwa na hakutaka kujiuliza sana akaruka kwa kutanguliza bega chini kisha akasimama kwa kupiga goti na kujirusha tena kwa kunyooka kama nyoka na kujifutika kwenye kichaka cha majani marefu yaliokuwa kando ya mwili wa komando alielala chini bila uhai.

Akiwa anapata adha ya kulala juu ya nyasi zenye maji ya mvua macho yake yakaelekea kule alikohisi anatazamwa,ilikuwa ni juu ya mti mrefu wenye kiambaza kwa juu,na hapo akaona kweli kulikuwa na kirundo cha majani,lakini pale alipokiona kile kirundo hakukuwa na uwezekano wa kuweza kuwa na tawi la kubeba kirundo kile cha majani.

Luteni Kanali Mwinyi Kisoda alikuwa ni mzoefu wa uwanja wa vita na si ukomando tu uliompa uzoefu huo,aliupata uzoefu huo sehemu nyingi alizowahi kushiriki vita kama Sudan,Congo na hata wakati mmoja huko Syria aliokoenda kwenye mpango wa kuhakikisha Marekani haifanikiwi kuteka ama kutawala vita ile na alikuwako huko kwa ombi maalumu la Rais wa Urusi ambae amewahi kuwa mwalimu wa weledi wa Luteni kanal Mwinyi kisoda,hivyo kwa uzoefu huo wa harakati za vita na namna walivyokuwa wamesalitiwa alijua kabisa kirundo kile kimehifadhi mtu na mtu yule ni mdunguaji.

Luteni kanali Mwinyi kisoda aliiweka sawa bunduki yake ya kisasa na akaikoki vyema akakiweka sawa kiona mbali kilichokuwa kwenye bunduki ile kisha akaweka kidole chake kwenye kifyatulio na kisha akaachia risasi moja na ikaenda pale pale alipokusudia na kweli akaona kivuli cha mtu kikishuka chini kwa kasi na hapo akajua tayari amepunguza mmoja ya adui zake.

Licha ya kumpiga risasi mdunguaji yule hakutaka kufanya haraka ya kutoka pale alipokuwa maana aliamini kabisa wadunguaji huwa hawako peke yao huwa kuna mtu maalumu wa kusoma mwelekeo wa kile wanachokilenga ili kurahisisha kazi yao.


Na ndivyo ilikuwa bada ya kuona mwenzie kadondoka chini yaezekana hakujua kilichomwangusha,msoma masafa alitikisika kutoka pale alipokuwa kwa lengo la kushuka chini,hilo hakutimiza risasi ya kutoka kwenye bunduki ya Luteni kanali Mwinyi Kisoda ililenga kichwa na kumshusha chini kwa mwenzie na Mwinyi hakutaka kujua kilichoendelea kutoka kule chini ya mti walipo adui zake.

Akataka kusimama ili atoke alipokuwa hapo akili yake ikakumbuka jambo


Wakati anasimama anaachia risasi ya pili alisikia mlio wa bunduki yake kuashiria risasi zimeisha au la basi risasi zilikuwa zimekwama kwenye chemba.

Akataka kuhakikisha akaikoki tena lakini mara hii mlio ukawa tofauti na mwanzo kuashiria risasi zilizopo hazitoshi kukaa ndani ya chemba ya bunduki ile.

Mwinyi akapagawa,kwa haraka akachomoa magazine ili ahakikishe,na alipoitoa akashangaa kuona risasi zipo zimejaa bado na akanyofoa risasi moja akaitikisa kwa nguvu karibu na sikio lake,mara akatokwa na msonyo wa fadhaa,kwa uzoefu wake alitambua ya kuwa risasi walizobeba ama magazine walizobeba zilikuwa ni za mpira au plastic kwa lugha rahisi na aina ya silaha waliobeba risasi ile haiwezi kupita chemba maana spring muzzle haiwezi kuhimili wepesi wa kasi ya kutoka kwake.

Luteni kanali akarudi tena kutazama risasi zingine ndani ya magazine ile na bado ilionesha vilevile,.

Akili yake iliona maigizo waliofanyiwa bila wao kujua,na alijiambia kabisa ya kuwa trap imeanzia ndani ya kambi yao kwa kupewa silaha na risasi za mazoezi.

Lakini jambo kubwa kukuuliza kwanini risasi mbili za mwanzo zilikuwa risasi kamili?! Hilo hakupata jibu na akaona kuendelea kukaa ndani ya kichaka cha nyasi hakutaweza kumsaidia na hapo akajaribu kutambaa tena kuelekea ilipo maiti ya komando mwenzie na alipoifikia akaishia kuchukua bunduki iliokuwa imedondoka pembenI kidogo na akaikoki na yenyewe ikatoa mlio uleule wa risasi kukwama chemba.

Mwinyi jasho likamtoka licha ya kuwa na baridi kali na matone ya maji kutoka kwenye miti na majani aliolalia.

“tulishindwaje kutambua hili mapema”alijiambia lakini bado akaishia kukubali ya kuwa aliewasaliti alitumia akili nyingi sana.

Akasimama kwa umakini wa hali ya juu na akazitupa chini bunduki zile na katika miguu yake huwa anapenda kuchomeka bastola zake mbili ambazo huwa hategemei kuzichukua kwenye gala la jeshi hizi ni zake na hutembea nazo popote aendapo.

Akaziweka vyema mkononi kisha akaanza kupiga hatua ndefu kusonga mbele kujaribu bahati yake ya kuwatafuta makomando wengine waliopotezana.

Akiwa amekimbia umbali wa kama mita mia mbili hivi mara akaona tena mbele yake kuna mti mrefu na juu yake kuna kitu kinabembea,akapunguza kasi ya miguu yake,na akajipa utimamu wa akili kisha akarekebisha mawani yake vyema maana yalianza kupunguza uwezo wa kuona kizani na hapo hakutaka kuamini ni komando mwingine tena alikuwa ameuwa na kuninginizwa juu ya kichwa chini miguu juu.

“yamefanyika saa ngapi mambo haya jamani”alijisemea kwa hamaniko Luteni kanali Mwinyi Kisoda huku akizidi kukaribia eneo lile la mti mrefu.

Akiwa amebakiza hatua chache kufikia maiti ile inayobembea,akapata kuona kama kivuli cha mtu kikipita kwa kasi mbele yake na kuishia kwenye kichaka cha majani marefu kisha kikatulia.

Kwa uchungu na hasira alizokuwa nazo, akaona hana muda wa kusumbuana na mpuuzi yule, akapiga hesabu za haraka na kuona umbali wa kichaka kile na yeye ni kama hatua sita tu,akaona atachelewa kukimbia kwa kasi ya upepo akapaa kwenda juu kisha akafanya simasoti kavu hewani na alipotua chini akakutana na mlio wa kukokiwa bunduki ya masafa watalamu wanaita gaflerifle,na hapo macho yake yakapata kukutana na kivuli cheusi ti kikiwa na bomba refu mbele,nae hakutaka kuremba akalishika bomba lile na kulivuta kwa nguvu kumwelekea na likaja na kivuli chake kisha kwa kutumia armhit kama wacheza mieleka akakikutaniza na mkono kikaenda chini,

Alikuwa ni mtu!!!


Mtu yule aliepigwa pigo lile na kudondoka chini akataka kujinyanyua lakini bareta moja kutoka mkononi mwa Luteni kanali Mwinyi Kisoda ilikuwa imefanya kazi yake na kuondoka na uhai wa mtu yule.

Baada ya kuhakikisha muasi yule ameaga dunia Mwinyi akazidi kusogea mbele na katika kutazama kwake akaona kuna pahali mbele yake kuna majengo kama mawili hivi na kulikuwa na taa zinawaka.

Akayasogelea majengo yale na kabla hata hajayafikia akapata kuona miili kadhaa ya makomando wenzie wa kikosi namba 309Unit wakiwa wamelala chini na pua zake zikanusa harufu ya baruti ya risasi katika eneo lile na hapo akapata kujua ya kuwa yalitokea mapambano ya anakwaana.

Akiwa bado amesimama huku tayari akiwa na idadi ya makomando nane kupoteza maisha,mara umeme ukakatika gafla katika majengo yale na kukawa na kiza sehemu yote.

Hakutaka kuwa mzembe akachoropoka pale alipokuwa na kusonga mbele zaidi kuyakaribia majengo yale huku akiwa makini na kila hatua aliokuwa akipiga.

Milango ya majengo yale ilikuwa wazi.

Hakujali wala hakuwaza kuwa hiyo inaweza kuwa ni mtego,yeye akasonga mbele na kuyaingia majengo yale.

Ndani ya jengo la kwanza hakukuta kitu kabisa wala kuwako dalili za kuwapo na kitu,akaachana nalo akapiga hatua kuzama jengo la pili.

Ni wakati akiingia tu mara umeme ukarudi gafla na hapo akajibanza nyuma ya mlango na kupitia mwanya mdogo uliokuwa katikati ya maungio ya mlango akatazama nje kwa tuo na hakuona kitu,kisha akageuka ili apate kuona vyema ndani ya jengo lile,macho yake hayakuamini

Alimwona Kapteni Zaza akiwa yupo juu ya meza huku risasi kadhaa zikiwa zimekaa kifuani kwake na pia chini ya meza kulikuwa na maiti nyingine nne za makomando wa kitanzania zikiwa zimelala katikati ya dimbwi la damu na kwa haraka alijua ya kuwa kifo kiliwakuta muda mfupi uliopita.

Luteni kanali Mwinyi Kisoda hakutaka kuamini macho yake japo ndivyo ilikuwa ya kuwa sasa makomando wote kumi na tatu wamepoteza maisha na amebaki peke yake na hajui walau adui yake yupo upande gani,japo aliamini kabisa hadi wakati huo adui anamuona au anajua uelekeo alipo.

Mwinyi Kisoda aliisogelea miili ile na hapo akapata kuona risasi zimetoboa hadi fulana ya kuzui risasi na kisha kuwadhuru na kuwaua kabisa.

Akaitazama fulana yake na hapo akili yake ikamwambia ya kuwa yaeza kuwa walipewa fulana feki za kuzuia risasi na kisha akajiwazia ya kuwa huo ulikuwa ni mchezo waliochezewa tangu wakiwa nyumbani Tanzania.

“kwanini wametufanyia hivi!!”akajiwazia Luteni kanali Mwinyi Kisoda huku akigeuka nyuma ili atoke ndani ya jengo lile,mara akasikia hatua za mtu zikinyata kusogelea jengo lile na yeye akawahi kuruka juu na kuipiga taa ikavunjika na pale ndani kukawa giza.


Itaendelea
 
Back
Top Bottom