Nitakufa Mara Ya Pili

Nitakufa Mara Ya Pili

60--Helena alinikanda mwili nzima huku maumivu ya majeraha nikiyasikia kila yalipoguswa na maji. Nilishangaa jinsi Helena alivyojitolea kunisaidia kwa kunikanda.

Baada ya kumalizaa nilivaa nguo zangu na kunisindikiza hadi nyumbani, tulipokaribia kufika tulisimama na Helena alinipatia kipande cha ngozi kama alichonipa Sabina. “Shija nakuomba ngozi hii usiitupe, hakikisha muda wote unakuwa nayo, iweke pembeni wakati wa kuoga tu, zaidi ya hapo hakikisha ipo mwilini mwako.

Nakwambia hivyo kwa kujua kipindi hiki ni kibaya kuliko chochote kilichotokea. Sasa hivi wachawi hawana pingamizi lolote watafanya watakavyo , hivyo hii ngozi ndiyo kinga yako kipindi hiki cha kujiandaa na mtihani, ukimaliza tu nakuomba uende mjini kwa mjomba wako.”

“Nimekuelewa Helena, nashukuru sijui bila wewe leo ningekuwa katika hali gani, kwani muda huu ni saa ngapi?” Nilipokea kipande cha ngozi na kuuliza.” “Inakimbilia saa nane za usiku.” “Mungu wangu! Sijui nyumbani wamenitafuta sana.”

“Lazima watakuwa wamekutafuta .” “Sijui nitawajibu nini, lakini nimekumbuka nitawaeleza kuwa nililala kwa rafiki yangu kwa ajili ya kujisomea.” “Na haya makovu?” “Mmh, hapo sasa sijui nitawadanganya vipi?”
“Sasa, sikiliza wakikuuliza waeleze mlikwenda kucheza mpira wakati wa kurudi aliangukia shimoni ndipo rafiki zako walipokusindikiza , mlipofika usiku ulikuwa mkubwa uliingia chumbani kwako kulala.”

“Mmh! Sidhani kama watanielewa .” “Basi kapumzike usiku mkubwa, nina imani bado wanakutafuta mwisho watakuja kwako usiogope hawawezi kukuona.” “Nashukuru Helena.” “Nilitaka kusahau nakuomba usiwaeleze chochote wazazi wako.” “Nitafanya hivyo .”

Niliagana na Helena kwa kuingia ndani kulala, wasiwasi wangu mkubwa nilijiuliza nitaweza kulala kwa kuhofia maumivu ya mwili. Lakini haikuwa hivyo , nilipogusa ubavu tu usingizi mzito ukanichukua. Nilishtuka siku ya pili pale nilipoamshwa na sauti ya baba.

Niliamka kwa kuhofia maumivu, sehemu kubwa ya mwili ulikuwa na maumivu madogo, kasoro kwenye goti kulikuwa na maumivu makali yaliyonifanya nitembee kwa kuchechemea. Baba aliponiona alishtuka. “Vipi tena?” “Ajali baba.” “Ya nini na imetokea saa ngapi?” “Nilidondokea kwenye shimo wakati wa kurudi nyumbani, kutokana na giza sikuweza kuliona na kupoteza fahamu kwa muda.”

“Mungu wangu! Lakini mchezo wa kutembea usiku umeuanza lini Shija?” “Imetokea tu baba, roho haikunipa kulala kule kwa kuwa sikuaga.” “Siku ya pili hata kama hukuaga, lala hukohuko mpaka asubuhi usitembee usiku ni mbaya sana, ona sasa yaliyokukuta , unafikiri ungekufa nani angejua?” “Samahani baba, nimekuelewa.”

“Na umerudi saa ngapi?” “Sikujua ni muda gani ila ulikuwa usiku sana.” “Ona sasa, sisi tulifikiri utalala kwa rafiki zako kujisomea, kumbe umekumbwa na masahibu mazito.” “Ni kweli nilitaka kulala, lakini sikuaga niliamua kurudi japo usiku.” Mama naye alikuja kunijulia hali na kuniasa kwamba nisitembee usiku,
nilimkubalia huku bado nikificha siri moyoni mwangu.

Sikuweza kwenda shule kutokana na jeraha la goti lililokuwa likiniuma sana. Ilibidi nitafutiwe mti wa kutembelea. Baada ya wazazi kuondoka nilibakia peke yangu nyumbani, kutokana na kuhisi uchovu, nilirudi chumbani na kujilaza. Niliwaza mengi kutokana na kupoteza mfuko wangu wa shule na kiatu kimoja.

Kiatu hakikuniuma sana japo hali yetu ya kujikongoja ilinikatisha tamaa kukipata haraka. Kilichoniuma sana ni ‘counter book’ zangu zilizokuwa na ‘notice’ nyingi nilizotumia kujisomea kila nilipopata muda. Nikiwa katika lindi la mawazo, sauti ya Helena alinizindua.

“Shija...Shija.” “Helena.” “Abee,” Helena aliitikia huku akisukuma mlango. “Vipi Shija, umeamkaje?” “Sijambo ila jeraha la kwenye goti ndilo linanisumbua.” “Hebu,” niliusogeza mguu karibu yake.

Nilipojaribu kujinyanyua na kutembea maumivu yalinifanya nishike ukuta. “Basi Shija, pole eeh.” “Asante.” “Vipi wazazi wako umewambiaje?” “Nimewadanganya wameniamini.” “Ooh, afadhari,” Helena alishusha pumzi ndefu. “Vipi mbona hivyo ?” Nilimuuliza baada ya kushusha pumzi kama ameshusha mzigo mzito.

“Nilikosa usingizi juu ya maswali ya wazazi wako, nilijua wangekubana lazima ungesema ukweli.” “Helena, mpaka mzee Manoni anafariki nimebaki na siri nyingi ambazo wazazi wangu hawazijui, kama wangezijua, baba yangu angemkata mapanga mama yako.” “Ooh, asante Shija kwa kuficha siri hizo.”

“Helena huu mguu ni wa kawaida au wa kichawi?” “Wa kawaida, wachawi hawakuwahi kukugusa, ila kuna dawa nitakuletea itakusaidia, ambayo hutumiwa na wachawi wanapopata majeraha kwenye kazi zao na wakiumia hupona kwa muda mfupi.”

“Nitashukuru, Helena nataka kusoma, nikikaa nyumbani nitapitwa na vitu vingi hata couter book zangu na kiatu kimoja vimepotea.” “Ooh kweli nilisahau, nilitaka kukuuliza jana kuhusu kiatu na mfuko wa madaftari.” “Kiatu sijui nilivuka wakati gani, ila mfuko wa madaftari niliutupa wakati nakimbia baada ya kuuona mzigo.”

“Basi hebu niachie hiyo kazi nitakutafutia nina imani kuwa asubuhi hii hakuna aliyeviokota .” “Vipi usiku hukutoka?” Nilimuuliza. “Shija hayo si muhimu kama kutafuta vitu vyako vya shule.” “Sawa.” Baada ya mazungumzo Helena aliondoka huku nikiamini ni vigumu kuvipata vitu vile.

Nilijilaza kitandani kumsubiri, kutokana na uchovu usingizi ulinipitia, nilishtushwa tena na sauti ya Helena. “Shija umelala?” “Si unajua uchovu vipi za huko?” “Nzuri vitu vyako nimevipata, wala sikupata shida kuviona,” Helena alisema huku akiwa ameshikilia mfuko wa madafutari na kiatu. “Ha! Siamini umevipata wapi?” “Ulipoviangushia”

Kilichonishangaza kilikuwa ni mfuko wangu wa madaftari, ulikuwa mkavu pamoja tofauti na mvua ilivyonyesha . “Helena mbona mfuko unaonesha kama hakukuwepo na mvua jana. “Shija mbinu za kichawi huziwezi, hakukuwa na mvua yoyote zaidi ya kiini macho.”


Baada ya kifo cha mzee Manoni wachawi wametangaza vita nzito na Shija, Je, Helena ataweza kumvusha salama?

INAENDELEA.....
 
kama kawa lete story muuza ubuyu kazi anayo babu yake mzee manoni kafa
 
61--Wakati vishindo vikiendelea kuizunguka nyumba, nilijua kabisa nimezidiwa ujanja. Bado sikuamini kama kweli kipande cha ngozi kimepotea, nilirudia kutafuta katika mfuko wa kaputula. Jibu lilikuwa lile lile hakukuwa na kipande cha ngozi.

Nilijikuta nimetumia nguvu nyingi kutafuta, jasho lilinivuja kama nimemwagiwa maji, mapigo ya moyo yalikuwa juu kwa hofu. Nilishika kiuno kuwaza kipande cha ngozi nimekipotezea wapi. Nilifikiria kama ingekuwa mapema ningekwenda kwa Helena kuomba msaada lakini ulikuwa usiku mkubwa niliokatazwa na wazazi wangu kutembea muda huo.

Nilijiuliza nitafanya nini, kwani vishindo vilizidi kuisogelea nyumba yetu, nilitamani kupiga kelele kuomba msaada kwa wazazi wangu lakini nilichelewa. Ghafla upepo mkali ulivuma uliosababisha kibatari kuzimika. Haikuchukua muda, mvua kubwa iliteremka. Sauti kali ya mvua ilinifanya nisisikie chochote kilichokuwa kikiendelea nje.

Nilisimama wima huku nikitetemeka kwa kuamini ile haikuwa mvua ya kawaida bali ya kichawi ya kuja kunichukua. Nilimuomba Mungu aniokoe na balaa la wachawi , mvua ilinyesha kwa muda mrefu sana na ilipokatika nje kulikuwa kumepambazuka. Nilipoangalia nje ilionesha kweli kulikuwa na mvua kubwa iliyonyesha kiasi cha kuweka madimbwi.

Nilitoka nje na kwenda msalani na kukuta mlango wa chumba cha wazazi wangu bado umefungwa kuonesha kuwa bado hawajaamka. Nilijiuliza muda ule utakuwa ni saa ngapi? Nilirudi chumbani kwangu na kukaa kitandani huku nikikisikia kichwa kizito kutokana na kukesha kwa hofu ya wachawi .

Niliamua kujilaza kidogo kuvuta muda kutokana na kuhisi uchovu kila kona ya mwili. Wakati naanza kusinzia mlango uligongwa na kusikia sauti ya baba. “Shija amka kumekucha.” Nilitaka kuitikia lakini midomo ilikuwa mizito kutokana na usingizi ulionijaa kichwani, baba aliendelea kuniita. “Wee Shija, mvua zinakudanganya amka kumekucha.”

Nilijilazimisha kunyanyuka huku nikisikia kichwa kizito na kizunguzungu. Nilifungua mlango na kutoka nje. “Vipi mbona hivyo ?” “Kichwa kinaniuma.” “Nawe unasoma sana punguza kusoma, kama hukuelewa miaka yote minne utaelewa kwa hizi wiki mbili zilizobaki?” “Nitapunguza baba.”

“Sasa shule utakwenda?” “Lazima niende, muda uliobaki si wa kukosa hata kidogo.” Nilikwenda kuoga kuondoa uchovu, baada ya kuoga nilielekea zangu shule huku mwili ukiwa umechangamka kiasi lakini kichwa bado kilikuwa kizito kwa usingizi.

Nilipofika shule bado sikuwa nimechangamka kama nilivyozoeleka , hata darasani muda mwingi nilisinzia na nilipoulizwa, nilisingizia naumwa. Lakini nilijitahidi kusoma mpaka muda wa kuondoka, kama tulivyokubaliana siku ile ya Ijumaa tulitakiwa tusome pamoja, sikuweza kurudi nyumbani kwenda kwa mwanafunzi mwenzangu wa kike ambaye pia alikuwa mpenzi wangu tuliyepeana mikakati mingi, baada ya kumaliza elimu yetu ya chuo kikuu kama tukifika.

Kwa vile sikupata muda wa kulala, nilipofika kwa rafiki yangu alinielekeza chumba cha wageni ambako nilala kupunguza usingizi kabla kuanza kujisomea. Hakuwa tofauti na Sabina, alikuwa mdadisi mzuri sana na mtu mwenye uchungu wa kufika mbali. Pamoja na kuwa mpenzi wangu, wakati wa kujisomea tuliweka urafiki pembeni na kusoma kwa bidii.
Rusia alinishtua saa mbili usiku, wakati huo chakula cha usiku kilikuwa tayari, nilijumuika na familia yake kula chakula na baada ya chakula tulipumzika mpaka saa tatu na nusu, tuliingia kwenye chumba tunachokitumia kujisomea.

Tulijisomea huku nikimsaidia baadhi ya vitu ambavyo yeye vilimtatiza, ilipofika saa sita usiku,
kichwa kilianza kuniuma kwa mbali. Rusia aliniletea dawa ya kutuliza maumivu, nikameza. Kilitulia kidogo na kutufanya tuendelee kusoma lakini ilipofika saa nane usiku, maumivu yalirudi tena kwa kasi.

Rusia alinishauri tupumzike ili kesho tuendelee kusoma, alinisindikiza chumba cha wageni na kuniacha nikijilaza na yeye kwenda chumbani kwake . Nililala vizuri hadi asubuhi, kwa vile haikuwa siku ya shule, niliamua kurudi nyumbani kutokana na hali yangu nilivyoisikia .

Japo Rusia aliniomba anipeleke hospitali, nilimueleza ule ulikuwa ni usingizi tu wala si kitu chochote na baada ya muda, ningekuwa katika hali ya kawaida.

Niliagana na Rusia na kurudi zangu nyumbani tukiahidiana kuonana Jumapili ambapo tulipanga kusoma kuanzia saa nane hadi saa mbili usiku, kisha tungepumzika kwa ajili ya chakula na kuendelea tena saa nne hadi saa nane usiku.

Nilirudi hadi nyumbani ambako nilifika majira ya saa nne asubuhi, bado mwili ulikuwa na uchovu. Nilipanga nilale kidogo nikiamka nijisomee mpaka kiza kitakapoingia. Nilipoingia chumbani kwangu, kichwa kilinipasuka katikati ya utosi na kuhisi maumivu makubwa.

Nilishika mikono kichwani kama nitaweza kukizuia kisipasuke, nilijivuta mpaka kitandani na kujilaza huku maumivu ya kichwa yakizidi kuongezeka kama kuna mtu ananichokonoa na mti kwenye ubongo. Nilitaka kupiga kelele kuomba msaada lakini sauti haikutoka. Mlangoni niliwaona watu wakiingia wakiwa uchi, sikushangaa kwani nilijua wale ni wachawi . Mmoja alinifuata kitandani na kunilisha kitu ambacho kilinifanya niuone ulimi wangu mzito kama jiwe. “Jamani tufanyeni haraka, tusifanye tena kosa,”
alisema jamaa mmoja aliyeonekana kiongozi wao aliyekuwa amejifunga pembe ndogo mkono wa kushoto.

Walitoa kitu kama unga na kunipulizia kisha kuniondoa kitandani, baada ya muda kiliingizwa kitu sawa na urefu wangu ambacho nilikitambua ni kipande cha mgomba na kulazwa kitandani kwangu.

Baada ya kulazwa, ulitolewa unga kama niliopuliziwa na kupulizwa kwenye ule mgomba ambao uligeuka na kuwa mtu aliyeonekana amelala. Mtu mwenyewe nilikuwa mimi, vitu vile havikuwa vigeni kwangu niliamini tayari nimegeuzwa msukule.


Ni Kweli Shija kageuzwa msukule? Mtihani wa kumaliza kidato cha nne atafanya

INAENDELEA....
 
Very interesting,uhondo mwanzo mwisho.Endelea kutupiamo kaka.
 
62--Baada ya zoezi la kuugeuza mgomba kuwa na taswira yangu kumalizika, walinichukua na kunisimamisha nyuma ya mlango. Baada ya hapo waliondoka na kuniacha.

Baadaye niliisikia sauti ya Helena ikiniita kutokea nje, alipokosa jibu aliingia ndani lakini hakuniona. Nilimuona akinitafuta kitandani, lakini sikuwa na uwezo wa kutoa sauti kumwambia nipo nyuma ya mlango. Baada ya kunikosa ndani, alitoka huku akiendelea kuita kwa kuzunguka nyuma ya nyumba.

Nilimsikia akisema kwa sauti. “Atakuwa amekwenda wapi?” Baada ya muda nilisikia sauti ya kuondoka kwa Helena ambaye aliamini kabisa sipo nyumbani. Muda ulikatika huku hali ya ukimya ikitawala, juu ya kitanda mgomba wenye taswira yangu ulikuwa umelazwa na kufunikwa shuka.

Majira ya jioni niliwasikia wazazi wangu wakirudi kwa kuzisikia sauti zao. “Shija atakuwa amerudi au na leo anaendelea kusoma?” Sauti ya mama iliuliza.


“Mmh! Sijui lakini mlango wake unaonesha kama amerudi.” Ulipita muda huku wakizungumzia mambo ya shamba, giza liliendelea kuumeza mwanga na nuru ya mchana ilipotea. Niliusikia mlango ukifunguliwa na kuingia mtu aliyekuwa na kibatari mkononi ambaye nilimtambua kuwa ni baba.


“Shija...Shija,” aliniita lakini hakukuwa na jibu. Baba alisogea karibu na kitanda na kuanza kukitikisa kipande cha mgomba kilicholazwa bila kujua sikuwa mimi. “Shija...Shija,” aliendelea kuniita, lakini hapakuwa na jibu, nilijitahidi nifunue mdomo wangu kumueleza nipo nyuma yake lakini sikuweza.

Baba aliendelea kunitikisa huku akiniitaka kwa kuongeza sauti lakini sikuweza kuitika. Baba alionekana kuongeza nguvu ya kutikisa huku akiniita kwa sauti ya juu ambayo hata mama aliisikia. “Baba Shija vipi?” Mama aliuliza. “Usingizi gani huu, mtu namtikisa na kumuita kwa sauti lakini haamki.”


“Labda kachoka na masomo, muache apumzike si unajua mwanao amepanga kufanya vizuri kwenye mtihani wake?” “Mmh, hata hivyo hatuwezi kumuacha, alipotoka jana alfajiri hadi leo tumuache, lazima tumjulie hali yake.”


“Si ungemuacha mpaka chakula kitakapoiva .” “Mke wangu hata sielewi, leo roho yangu imekuwa na hamu ya kuzungumza na mwanangu.” “Haya muamshe,” mama alisema huku akitoka nje. Baba aliendelea kuutikisa ule mgomba bila kuonekana dalili zozote za kuamka.


Ndipo alipotoka na kurudi na maji ambayo aliumwagia ule mgomba aliodhania ni mimi, lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote . Nilimsikia akisema: “Usingizi gani wa namna hii, mpaka nammwagia maji bado tu haamki.”


Aliendelea tena kuutikisa kwa nguvu huku akiita. “Shija... usingizi gani huu?” “Baba Shija kwani kuna nini?” Mama alirudi tena ndani baada ya kuona baba katumia muda mrefu sana kuniamsha.


“Yaani haya ni maajabu, haijawahi kutokea kumuamsha Shija kwa kipindi kirefu hivi, nimemwagia maji kichwani lakini bado tu haoneshi kushtuka.” “Sasa ni usingizi huo? Hata kama angekesha anasoma, mtu umwagiwe maji bado uendelee kulala, hebu muamshe kwa kumnyanyua .” Baba alifuata maelekezo ya mama, aliunyanyua mgomba ambao ulionekana ni mimi kabisa.


Lakini hakuonesha dalili zozote za uhai, kulegea kwa ule mgomba ambao wazazi wangu waliamini ni mtu kuliwatisha. Katika kuuchunguza mwili ule waligundua haukuwa na uhai. “Mama Shija kuna usalama kweli hapa?” “Kwani vipi mume wangu?” “Hebu subiri,” baba bado hakuamini kama kweli nimekufa, alipima mapigo ya moyo ambayo niliamini kabisa yatakuwa yamesimama.


Haikuwa tofauti na siku kaka aliporudi, siku ya pili nikakuta amefariki kumbe tuliwekewa ‘danganya toto’. Baba alitoka nje, haukupita muda mama alirudi kutaka kupata uhakika.


Mama hakuwa na simile, aliangua kilio cha sauti ya juu kunililia. Haikuchukua hata dakika kumi majirani walifika kutaka kujua kuna nini, mama aliwaeleza kuwa sipo tena dunia. Hapo ndipo vilio vilipoongezeka kutokana na jinsi nilivyokuwa nikiishi na majirani. Nilisikia sauti za wanaume wakizungumza kuhusu kifo changu.


Kila mtu nilimsikia akisema lake, baada ya muda waliingia wanaume watatu ambao waliuweka vizuri mwili wa bandia na kuufunika shuka nyeupe. Nje vilio viliendelea kutawala, sauti ya mama ndiyo iliyokuwa juu kuliko wote waliokuwa wakilia. Moyo uliniuma jinsi watu walivyokuwa wakinililia kama nimekufa kumbe nipo nyuma ya mlango.


Walipotoka watu walioteuliwa kuitengeneza maiti, niliona ukuta ukipasuka na kuingia wachawi waliokuja asubuhi wakiwa na tunguri mkononi. Mmoja ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wao, alimimina unga mweusi kiganjani kwake , kisha aliinyunyizia ile maiti ya bandia kwa kuanzia kichwani mpaka miguuni.

Baada ya kumaliza, unga uliobakia alinisogelea na kunipulizia usoni kisha walitoweka . Waliponipulizia nilihisi kama mwili umekufa ganzi, nilitamani kulia lakini nilihisi machozi yamenikauka .


Nini kitaendelea? Ni kweli Shija ndio ameshakuwa msukule?

INAENDELEA....
 
63--Maandalizi ya mazishi yangu yaliendelea huku wazazi wangu wakionekana kupagawa sana. Nilimsikia akizungumza na watu waliomuuliza kuhusu mipango ya mazishi yangu. “Mzee mwenzetu pamoja na msiba kutokea ghafla una mpango gani?”
“Yaani mpaka sasa hivi sijajua nifanye nini, la muhimu ngoja akili itulie kwa vile ni haraka sana kusema tutazika lini.


Kwa vile tuna ndugu la muhimu kuwajulisha habari za msiba na pia shuleni kwake .” “Ni kweli, na kuhusu mwili wa marehemu tuupeleke hospitali au tutauhifadhi ndani?” “Hakuna haja ya kujipa usumbufu usio wa lazima, tutauhifadhi ndani tukiendelea na mipango ya mazishi.”


“Poleni sana, si alikuwa kidato cha nne?” “Ndiyo.” “Na wiki ijayo alikuwa anafanya mtihani?” “Mungu wangu! Kwa nini jamani hakumuacha mtoto afanye mtihani?” “Maamuzi ya Mungu hatuwezi kuyaingilia japo inauma,” baba alionesha ujasiri kuwajibu majirani.


Mara nilisikia baba akiitwa na mtu, sauti ya baba niliisikia kwa mbali sana, lakini sikusikia alikuwa akizungumza nini. Baada ya muda waliingia wanawake ambao walitoa vitu vyote na chumba kilibakia na kitanda tu, kama ilivyo katika misiba mingi ambapo chumba cha maiti hubakia na kitanda tu.

Walipomaliza kufanya usafi wa chumba, waliingia wanaume wanne na kitanda cha kamba ambacho hutumika kumlazia maiti.
Kitanda cha chuma kilitolewa na kuwekwa cha kamba, kisha mwili ulilazwa juu yake na kufunikwa shuka jeupe.


Baada ya matayarisho walitoka na kuuacha mwili wa bandia ukiwa umelazwa kitandani. Pamoja na roho kuniuma, lakini nilishuhudia vitu vingi ambavyo vinafanyika baada ya mtu kufa japo hapakuwa na msiba wa kweli. Muda ulikatika na usiku ukaingia.


Kina mama waliingia kulala na mwili wa marehemu wakiamini kabisa mwili uliolala kitandani ni wangu. Usiku wa manane, nje ya nyumba yetu kulikuwa na ngoma ya kichawi.


Baada ya muda, ukuta ulipasuka tena na wakaingia tena wachawi wakiwemo mama Helena na Sabina.


Mama Helena ndiye aliyekuwa kiongozi aliyeshikilia matunguli. Kitu kilichonitisha kilikuwa jinsi walivyowafanyia uchawi waliolala mle chumban. Baada ya kuwamwagia dawa kina mama wote walianza kuwapanda kama farasi na kuzunguka nao mle chumbani. Waliwafanya vile huku nje ngoma ikiendelea kuchezwa.


Mama Helena alinifuata na kunizomea na kunifanyia mzaha, sikuwa na la kufanya kwani nilikuwa kama mtu aliyefungwa nati ili nisitikisike. Ngoma ile iliendelea mpaka mapambazuko yalipokaribia, wakawalaza wale kina mama na kuwanyunyizia dawa kisha wakaondoka .


Alfajiri nilisikia sauti za kina baba wakizungumza nje kuonesha wamekwisha amka. Lakini kina mama bado waliendelea kuuchapa usingizi kama wamelala majumbani kwao na siyo msibani. Niliwasikia kina baba nje wakiulizana.


“Jamani wanawake hawajaamka?” “Ajabu! Au wamejisahau kama wamelala msibani?” Mara mlango uligongwa ukifuatiwa na sauti ambayo niliifahamu ni ya baba Godi, jirani yetu. “Kina mama kumekucha, mnajisahau kama mpo kwenu?”


Sauti ile iliwafanya kina mama washtuke na kuona kumepambazuka, mmoja alisema: “Ha! Jamani kulala gani huku?” Alisema huku akimtikisa mwenzake wa pembeni yake ambaye bado alikuwa akiendelea kuuchapa usingizi. Waliamshana na kushangaa kwa nini walijisahau kama wapo msibani. Kila aliyeamka alilalamika kuwa anahisi mwili umechoka sana.


“Jamani mbona mwili unaniuma,” alisema mmoja aliyekuwa akijinyoosha. “Mmh! Hii siyo kawaida, hata mimi mwili nahisi kama nilikuwa na kazi ya kumbeba mtu usiku kucha,” mama alisema huku akijinyoosha. “Jamani hata mimi,” kila mmoja alilalamika kuchoka mwili.


Walitoka nje ya chumba kufanya mipango ya kifungua kinywa na mambo mengine, chumbani nilibakia peke yangu na mwili bandia uliokuwa umelazwa kitandani. Majira ya mchana nilisikia watu wakilia nje, baada ya muda mke wa mjomba toka Mwanza aliingia chumbani. Mama alipomuona alimpokea kwa kilio, kukawa ni vilio mtindo mmoja.


Niliamini mtu ambaye alikuwa mbali ni mjomba, kama ameshafika mipango ya mazishi ingefanyika mara moja. Baada ya muda, kina mama walitolewa nje na wakaingia wanaume walioufanyia usafi mwili kabla ya kuuvisha sanda.


Kama nisingeshuhudia jinsi wachawi wanavyofanya viini macho, ningeamini kilicholazwa kitandani na kufanyiwa usafi kabla kuuvisha sanda ni mtu wa kweli. Kwa macho yangu niliona mambo mengi ya kichawi ambayo siyo rahisi mtu wa kawaida kuyaona.


Niliapa kuwa kama nitapona na kurudi tena kwenye uhalisia wangu, nitayatoa yote ya moyoni mwangu toka siku ya kwanza nilipokutana na mzee Manoni mpaka siku nitakapokuwa nimefikia. Nilijua wengi hawaamini uchawi, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wachawi wapo na ni watu wabaya ambao ni kiwazo kwa wengine.


Baada ya wale wanaume ambao wote niliwafahamu kuuosha mwili wa bandia, waliuvisha sanda na kuuandaa kwa ajili ya mazishi. Walipomaliza kazi yao ya maandalizi ya kuuandaa mwili, walitoka nje na baadaye aliingia kiongozi wa dini, Katekista Mathayo kuuombea mwili kabla ya kuingizwa kwenye jeneza. Baada ya maombi waliruhusiwa watu kuuingiza kwenye jeneza.


Nini hatma ya Shija baada ya hatua zote hizo?

INAENDELEA....
 
64--Waliingia wazee wawili na vijana wanne, walishirikiana kuuingiza mwili wa bandia kwenye jeneza. Baada ya zoezi lile lilibebwa jeneza na kutolewa nje, sikujua nini kinaendelea huko nje zaidi ya kusikia nyimbo za maombolezo zilizokuwa zikiimbwa na kina mama.


Ilifanywa sala ya kuombea maiti kisha niliwasikia wakiondoka kuelekea makaburini. Baada ya muda pakawa kimya kuonesha watu wote wameelekea makaburini kuuzika mgomba. Zilipita dakika tano, mara mlango ulifunguliwa na kuingia wachawi wanne wa kiume, walinibeba juu juu na kuelekea makaburini.


Tulikuwa wa kwanza kufika kabla wazikaji hawajafika , nilipandishwa kwenye mti uliokuwa karibu na kaburi lililochimbwa kwa ajili yangu. Eneo lote la makaburi kulikuwa na wachawi zaidi ya hamsini.


Sikujua wingi ule ulikuwa kwa ajili ya gani. Kwa mbali niliwaona watu waliobeba jeneza lenye mgomba wakisogea makaburini, baada ya muda walikusanyika . Jeneza lilipofika liliwekwa pembeni ya kaburi, nilishuhudia wazazi wangu hasa mama aliyeletwa akiwa ameshikiliwa na wanawake wenzake wakipita mbele karibu kabisa na jeneza.


Uso wa mama ulikuwa umemvimba na macho kuwa mekundu kwa kunililia bila kujua mwanaye sijafa nipo kwenye mti nikishuhudia yote. Baada ya kimya kifupi, Kiongozi Msaidizi wa Kanisa, Mathayo alianza kuliombea kaburi kabla ya kuingizwa mwili wa bandia kaburini.


Baada kulibariki kaburi, mchungaji aliruhusu mwili uingizwe kaburini. Nilishuhudia mwili bandia ukiteremshwa kaburini huku familia yangu hasa mama akilia mpaka kupoteza fahamu. Baba yangu mishipa ya kichwa ilimsimama, hakuweza kuzungumza zaidi ya kutokwa na machozi mfululizo.


Wadogo zangu kila mmoja alilia ajuavyo kutokana na jinsi walivyonipoteza kaka yao, majirani nao walipatwa na mshtuko. Hata rafiki yangu wa kike, Lusia alizirai. Kifo changu kilimchanganya kutokana na siku ya jana yake kuwa pamoja tukisoma mpaka usiku wa manane.


Alichanganyikiwa zaidi kutokana na ukaribu wetu na jinsi alivyonitegemea katika masomo. Si yeye tu, hata wanafunzi wenzangu hawakuamini hasa kutokana na kushirikiana nao katika mambo mengi ambapo nilikuwa msaada mkubwa katika mtihani wa mwisho. Kila mmoja alijua lazima nipasue tena kwa alama za juu kutokana na uelewa wangu.


Baada ya mwili kuingizwa kaburini, ndugu wachache ndiyo walioweza kwenda kuweka mchanga kwenye kaburi kabla ya mwili kuzikwa rasmi. Baba alikuwa ameiva macho na kuwa mekundu. Alijikaza kwa vile ni yeye ndiye alitakiwa kusimama kidete kuyaongoza mazishi yale.


Kama siyo hivyo naye alikuwa kwenye wakati mgumu, kila mara alifuta machozi kwa kitambaa cha mkononi na kufuta kamasi nyembamba zilizokuwa zikitoka bila kizuizi. Majirani wenye mioyo migumu waliweza kwenda kutia udongo kwenye kaburi, wadogo zangu walisaidiwa kufika kwa kushikiliwa.


Baada ya watu muhimu kumaliza kuweka udongo kwenye kaburi langu, waliruhusiwa wote wazike kwa kupokezana. Niliushuhudia mwili bandia ukifukiwa na huku kila mmoja akiwajibika kutupa mchanga ndani ya kaburi.


Wengi hawakuamini, wapo waliosema ni amri ya Mungu na wapo waliosema siyo bure kuna mkono wa mtu. Baada ya kuzika, kila mmoja aliweka shada la maua. Mama yangu ilibidi wambebe mpaka kwenye kaburi kutokana kushindwa kutembea, baba yangu aliangua kilio upya baada ya kupata uhakika kweli mwanaye nimefariki. Watu walimshika baba ambaye uvumilivu wa kujikaza kiume ulimwisha dakika za mwisho baada ya kuzikwa mwili wangu. Kilikuwa kilio kilichowaumiza wengi, kitendo cha baba yangu kulia kilifanya hata wenye mioyo migumu hasa wanawake kuungana na baba yangu kunililia kwa sauti ya juu. Mchungaji alifanya kazi ya ziada kuwakumbusha watu wote waliokuwepo makaburini kuwa isifike hatua ya watu kumkufuru Mungu pale tu misiba inapotokea katika familia zao. Aliwaeleza wanatakiwa kutambua kila neno aliloahidi Mungu lazima litimie kama mauti kwa mwanadamu.


“Ndugu zangu, najua kifo kinapotokea huwagusa watu hasa wahusika, lakini watu wengi tumesahau kuwa Muumba wetu aliahidi kila kiumbe kilichotokana na mavumbi kitarudi mavumbini. Kinapotokea kifo ni somo kwa sisi tuliobaki ili tujiandae kwa vile hatujui siku wala saa. “Ndugu zangu, kila mwanadamu anapaswa kutengeneza makazi yake ya kudumu yaliyo mazuri kwa kutenda mema.


Leo kijana wetu ameondoka tuliobaki tumejiandaa vipi? “Tusimkufuru Mungu kwa kuamini kuna imani za kishirikina, shetani hana mamlaka mbele ya Mungu. Hivyo basi tunatakiwa kumuombea kijana wetu Shija apumzike kwa amani katika makazi mazuri ya kudumu.


Bwana alitoa! Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. “Wafiwa mtegemeeni Bwana Yesu kwani ndiye mfariji mkuu, enendeni kwa amani ya Bwana. “ Baada ya mazishi yaliyowaliza wengi, niliwaona watu wakiondoka makaburini kurudi nyumbani kila mmoja akizungumza lake.


Nina imani mpaka hapa kila anayesoma mkasa huu amejua tafsiri ya mimi kufa mara ya pili. Nina imani umeona jinsi nilivyoona toka nilipoanza kupata misukosuko ya wachawi , kifo changu cha kichawi mpaka mwili wangu wa bandia kuzikwa .
INAENDELEA.....
 
mpaka naogopa sasa,kumbe ni hadithi tu,utadhani kweli
 
65--Baada ya watu wote kuondoka, walibakia wale wachawi makaburini, waliniteremsha na kunikalisha katikati ya kaburi lililozikwa mgomba na kuanza kucheza ngoma kunizunguka. Walicheza kwa furaha huku wakishangilia kuonesha wamefanikiwa walichokitaka .


Walicheza kwa muda mrefu bila kuchoka, sehemu ya makaburi yote ikawa vumbi mtindo mmoja. Katika watu walioonesha furaha ni mama Helena, alijirusha huku na huku na kila tulipokutanisha macho, alinizomea.


Kingine kilichonishangaza ni kumuona Helena naye yupo kwenye ngoma ile, alionekana akicheza kwa furaha kama hakuwa mtu aliyenisaidia nisipatwe na wachawi . Nilijiuliza furaha ile ameitoa wapi, kwa nini alisema atanisaidia mpaka hatua ya mwisho na siku ya mwisho amefurahia kukamatwa kwangu.


Nilijikuta nikipata wasiwasi na Helena na kukumbuka maneno ya Sabina kuwa Helena si mtu mzuri. Ilionesha wazi hata kuonesha ukaribu bado alikuwa na lake jambo la kuniteka kimawazo na mwisho wa siku kunitupia kwenye mikono wa wachawi kama siku ile.


Ngoma ya wachawi
makaburini ilikoma majira ya usiku giza lilipochukua nafasi kubwa. Baada ya kutosheka na ngoma yao, nilibebwa juu juu na kurudi nyumbani. Tulipofika nyumbani nilishangaa kurudishwa nyuma ya mlango.


Nilijiuliza wananirudisha nyumbani ili iweje, wakati tayari nyumbani wanajua nimekufa. Baada ya kunirudisha nyuma ya mlango waliondoka na kuniacha pale. Mazungumzo yote kuhusiana na kifo changu niliyasikia watu waliofika kuwapa pole wazazi wangu.


Wapo walioamini kazi ya Mungu lakini wapo ambao hawakukubali na kusema ule ulikuwa mkono wa mtu. Walisema kifo kile si bure hasa kutokana na kina mama waliolala na mwili wa bandia kuamka wakiwa wamechoka sana.


Kuna mmoja alisema kwa sauti ya juu kuwa msiba ule si bure kama wataangalia upande wa pili watagundua vitu vingi. Alitoa ushuhuda ulioungwa mkono na wengi kuhusu matukio kama yale. “Nataka kuwaambia kitu kimoja kuhusiana na hali iliyojitokeza siku ya jana, aminini msiamini kifo cha Shija ni cha utata kutokana na hali ya jana tuliyokutana nayo.


Nataka kuwaelezea ukweli, piteni chini juu mtaniambia kuna kitu, si bure.” “Mama Suzana, huenda kuna matukio yasiyo ya kawaida lakini kama kiongozi wa familia nitabakia na msimamo kuwa mwanangu amefariki kwa amri ya Mungu.”


Kauli ya baba iliuumiza moyo wangu na kuona yeye ni nani asiyeamini mambo ya kishirikina? Mbona alipoumwa alitumia mambo ya jadi? Nilimuunga mkono mama Suzana alikuwa ameona mbali. Lakini sikuwa na sauti ningeweza kuipaza ili baba yangu ajue mwanaye sijafa nipo hai, nahitaji nguvu za ziada kunirudisha duniani.


Mazungumzo yaliendelea huku baadhi ya watu wakimuunga mkono mama Suzana kwa wazazi wangu kuhangaika zaidi kupata ukweli wa kifo changu. Lakini msimamo wa baba ulibaki palepale. Baada ya mazungumzo, watu walitawanyika na kubakia majirani wa karibu.


Usiku wa siku ile kama kawaida, wachawi walikuja kunichukua na kunipeleka kwenye kilinge chao, walicheza ngoma mpaka ilipokaribia kupambazuka walinirudisha nyuma ya mlango, nilijiuliza maisha yangu yote yatakuwa pale nyuma ya mlango? Chakula changu kikuu kilikuwa uji ambao ulionesha kama ulichemshwa bila kuiva wala kuwekewa sukari.


Kutokana na njaa niliyokuwa nayo, sikuweza kukataa, nilikunywa hivyo hivyo , ilikuwa ajabu pamoja na uji ule kutokuwa mzuri, niliweza kushiba na kuendelea kusimama nyuma ya mlango bila kuchoka. Siku ya pili nilimsikia mama akizungumza kwa sauti: “Baba Misoji, una habari?” “Ipi?”
“Ya mama Suzana.” “Mama Suzana! Kafanya nini?”
“Mama Suzana amefariki dunia.” “Wewe!”

Baba alishtuka hata mimi ndani nilipatwa na mshtuko mkubwa, niliamini kabisa mdomo wake ndiyo uliomponza kutoboa siri za wachawi mbele za watu.


“Tatizo nini? Si jana jioni baada ya mazishi tumezungumza naye, ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu?” “Haswaa.” “Kipi kilichomsibu?” “Mumewe anasema kichwa tu.” “Mmh, mbona inatisha.” “Mimi, nina wasiwasi .” “Wa nini?” “Kauli yake aliyoitoa jana.”

”Ipi hiyo?” “Kuhusiana na wachawi .” “Sasa kauli yake na kifo chake vinahusiana vipi?” ”Baba Shija acha ubishi.” “Mke wangu ubishi wa nini?” “Nina wasiwasi huenda mdomo umemponza.” “Kumponza vipi?” “Mume wangu acha kujitoa akili, wachawi wanaweza kumtenda.”


“Kwa maana hiyo mama Suzana hakufa?” “Sijui, inawezekana, kifo gani hicho?” “Ina maana na Shija hajafariki?” “Inawezekana pia.” “Mke wangu umeanza kuingia katika imani za ajabu, ina maana baba au bibi yako walipokufa , nao hawakufa ?” “Walikufa.”


“Sasa kwa nini huyu mwanao na mama Suzana useme hawakufa ?” “Shija alikuwa mzima, tulimkuta amekufa bila kuumwa, mama Suzana kaumwa kichwa tu, kafa, huoni kuna kitu kimejificha hapo?” “Mke wangu sipendi kusikia tena upuuzi kama huo,” baba alikuja juu.


Nilibakia nikiumia moyoni kwa majibu ya baba kujifanya haamini ushirikina wakati anaamini mizimu. Kingine kilichoniumiza ni ubishi wa baba, jambo linaonekana lakini yeye alijifanya hajui kitu. Nilijikuta nikipata wazo huenda baba kanitoa kafara na yeye ni mshirika wa wachawi .


Je, ni kweli baba Shija ni mchawi?
INAENDELEA...
 
Unatupia kipande kingine au ndio mpaka kesho tulale
 
66--Baada ya siku saba nilitolewa nyuma ya mlango na kwenda kuwekwa katikati ya shamba kubwa ambalo sikuelewa pale ni wapi. Muda ule ilionesha kama majira ya alfajiri kutokana na giza cha kufifia na baridi kali.


Baada ya kuniacha pale, wachawi waliondoka na kuniacha peke yangu. Nilijiuliza pale ni wapi na kwa nini waniache sehemu ile peke yangu, nia yao ilikuwa nini kwangu? Kutokana na kuwa kifua wazi na kaptura pekee, baridi iliniingia mpaka kwenye mifupa.


Nilishindwa nifanye nini au niende wapi kwa vile shamba lile sikujua pale ni wapi. Haikupita muda, mvua kubwa ya mawe ikashuka. Sitasahau mateso mazito yaliyonipata kwa kunyeshewa na mvua ya mawe kwenye mwili uliokuwa mtupu.


Mawe ya kwenye mvua nayo yalinipiga na kusababisha maumivu makali. Shamba lilionekana la mihogo na mahindi yaliyokuwa marefu kiasi cha kushindwa kuona nipo sehemu gani. Nilijikunyata na kuanza kulia japo niliamini kilio changu kilikuwa sawa na samaki, machozi yalikwenda na maji.


Mvua ilikuwa kama ya kutumwa kwani iliendelea kwa muda mrefu bila kukatika, nilijikunja kwenye tuta moja ambalo kwa maajabu ya ulimwengu, liligeuka na kuwa tope tupu. Kwa mateso yale, niliamini kifo changu kilikuwa kimetimia.


Nilijikuta nikizama kwenye tope lile lililogeuka kuwa dimbwi, nilikumbuka maneno ya Helena kuwa, huenda ile mvua haikuwa ya kawaida ila ya kichawi. Niliamini yale ni mateso yaliyofanywa makusudi ili kunikomesha baada ya kunitafuta kwa muda mrefu bila mafanikio.


Nilimkumbuka Sabina, kama angekuwepo asingekubali niteseke kiasi kile, pia nilijilaumu kuwa karibu na Helena ambaye niliamini ndiye aliyefanikisha kukamatwa kwangu na wachawi . Moyoni bado nilikuwa na wasiwasi na kauli za baba yangu kukataa kwenda kwa wataalamu kuangalia sababu ya kifo changu cha utata.


Nilijikuta nikipoteza imani kwake kwa kumuona naye ni mhusika mkuu wa kifo changu kwa kuukataa ukweli. Nilikumbuka kauli moja ya Sabina kuwa kila mchawi hutoa mtu mmoja sehemu ya familia yake kama kafara ya kula nyama za wenzake.


Kingine kilichonifanya niwe na wasiwasi na baba yangu ni kutokana na ngoma ya wachawi iliyokuwa ikichezwa nje ya nyumba bila kutoka. Nilijikuta nikiamini huenda na yeye ni mhusika, sikuwa na imani naye hata kidogo. Lakini nilijiuliza mbona baba yangu sikuwahi kumuona kwenye ngoma zote za wachawi nilizowahi kuhudhuria? Au alikuwa akijificha.


Sikuwa na njia nyingine zaidi ya kumuachia Mungu. Tope lile lilianza kunimeza taratibu, nilijiuliza shimo lile limetoka wapi, wakati mwanzo kabla ya mvua kuanza kunyesha kulikuwa na tuta. Kila nilivyojitahidi kujitoa, tope lilinizidi nguvu na kuamua kutulia. Mvua ya mawe nayo iliendelea kunisulubu, usichukulie kama simulizi ya kusisimua bali mateso ya shetani motoni japo sijawahi kufika.


Nilijikuta nimezama mpaka tumboni na tope liliendelea kunimeza taratibu, jinsi mvua ilivyokuwa ikiendelea, ndivyo nilivyozidi kuzama chini. Sauti ya Helena ilinishtua. “Shija...Shija,” nilifumbua mdomo kuitika lakini sauti haikutoka.


“Shijaaaaa...Shijaaa upo wapi?” Ilionesha Helena hajui nilipo. Tope nalo liliendelea kunimeza taratibu, bahati nzuri aliniona na kusogea mpaka kwenye shimo la tope. Kilichonishangaza Helena alikuwa mtupu kama alivyozaliwa , kiunoni alikuwa amejifunga kitambaa cheusi kilichosokotwa kama kamba.


“Shijaaa, nipe mkono,” alisema kwa sauti ya juu. Nilimpa mkono ambao aliudaka na kunivuta juu, ajabu hakusumbuka sana, aliponishika tu, alinitoa kwenye tope. Nilijiuliza Helena ana nguvu gani za kuweza kunichomoa kwenye tope kwa urahisi namna ile. Baada ya kutoka kwenye tope likiwa limenienea mwili mzima, Helena alinikumbatia huku akilia.


“Jamani Shija pole,” nilishangaa kumuona akitokwa na machozi ambayo nayo yalikwenda na maji ya mvua. Nilifumbua mdomo ili nimjibu sauti haikutoka, Helena alichanganyikiwa kwa kunipapasa kila kona ya mwili kama ndiyo siku ya kwanza kuniona. Ilikuwa ajabu, pamoja na kuwa mtupu mbele yangu hakushtuka zaidi ya kuniangalia huku akibubujikwa na machozi.


“Pole Shija,” niliitikia asante lakini sauti haikutoka. Helena baada ya kuona sauti haitoki, alielekeza nipanue mdomo, baada ya kufanya vile aliingiza vidole mdomoni kwangu kisha alinieleza. “Shija zungumza sasa.” “Helena,” nilimwita na sauti ilitoka. “Abee Shija, pole sana.”


“Asante” “Shija ngozi uliiweka wapi?” “Hata sijui.” “Shija kwa nini umekiuka masharti yangu?” “Helena hata sijui imepotea vipi” Nilimueleza jinsi ilivyopotea siku nilipokwenda kuoga mtoni. “Shija ulishindwa vipi kusubiri mpaka ufanye mtihani ndipo ufanye upuuzi wako?” “Samahani Helena.”


“Shija mbona hujipendi?” Nilikosa la kumjibu na kubakia kimya nimeinama chini. “Shija unanifanya nionekane mjinga mbele ya wachawi .” “Helena bahati mbaya.” “Haya bahati mbaya upo hapa, bora ningejua mapema kabla ya kujulikana umekufa.”


“Helena naweza kurudi tena duniani?” “Mmh! Sijui lakini nitajitahi japo uwezekano ni mdogo sana.” “Kwa hiyo nimeshakuwa msukule?” “Toka siku ulipojulikana umekufa lakini ndani ya siku saba kulikuwa na uwezekano wa kurudishwa duniani. Kwa sasa hakuna ujanja.” “Sasa utanisaidiaje?”



Je, Helena atamtoa Shija kwenye umsukule?

ITAENDELEA kesho.....
Mola Awavushe Salama!
 
mpaka naogopa sasa,kumbe ni hadithi tu,utadhani kweli

We ogopa ogopa tu utamuona mzee manoni hapo akikushughulikia, hivyo Kuwa makini! Nakushauri usisinzie hata kidogo mpaka kesho wasije wakakufuata usiku!

Sent from my BlackBerry 8520 using JamiiForums
 
Back
Top Bottom