Nitakufa Mara Ya Pili

Nitakufa Mara Ya Pili

50--“Shija... Shija,” aliniita jina langu hata kabla hajafika nyumbani.
“Vipi Sabina mbona hivyo ?” ujio wake ulinitisha. “Shija... Shija,” Sabina alisema huku akihema kwa kushika magoti, ilionesha amekimbia umbali mrefu.

“Sabina mbona sikuelewi, kuna nini?” “Mmh, wee acha! Baada ya vitisho vya baba yako kumetokea malumbano mazito, kidogo mwalimu mkuu ashikane na mama Helena ambaye alikuwa akishabikia ufukuzwe kabisa shule.

Lakini mwalimu mkuu amesema lazima ufanye mtihani wa mwisho. “Basi hapo ndipo kazi ilipoanza, baadhi ya wazazi wakitaka usimamishwe kwa wiki na wengine wakitaka ufukuzwe kabisa.”
“Sasa nini kilichoamuliwa?” “Mwalimu mkuu amesema lazima utafanya mtihani na ile adhabu ya kusimamishwa amesema ataitengua ili kesho uende shule.”

“Wazazi walisema nini?” “Mama Helena kamwambia mwalimu akikurudisha shule ataona cha moto labda sio yeye . ” “Mwalimu alisemaje?” “Alisema hatishiki na lolote.” “Iliishaje?” “Baada ya kugundua tupo mle ndani wakati wakiendelea kuzozana, walitutimua nje.

Baada ya kutoka nikaona nije huku, vipi baba yupo wapi?” “Amekwenda shamba.” “Amesemaje kuhusiana na hukumu kama ile ya kukukandamiza, wahusika hatupewi adhabu unapewa usiyehusika?” “Lakini Sabina wewe ndiye aliyeitoa siri yetu polisi.” “Shija polisi wanatisha, baada ya kunibana sana na maswali niliogopa kuitoa siri yetu na kuamua kusema vile.”

“Mmh, kweli ulijitahidi kuunda uongo.” “Sasa Shija kama wakikuzuia kufanya mtihani utafanya nini?” “Sina jinsi, itanibidi niende mjini kwa anko nikarudie shule.”
Tukiwa katikati ya mazungumzo, sauti ya hodi ilitushtua, tulipoangalia sote tulishtuka baada ya kumuona mwalimu mkuu akiwa katika mlango wa kuingilia nyumbani.

Sote tuliingiwa na woga baada ya mwalimu mkuu kutukuta pamoja wakati nikiwa bado na tuhuma za kuwa wapenzi na Sabina. Nilimuona Sabina uso umemshuka kama mchawi aliyekamatwa mchana akiloga. “Karibu mwalimu,” nilijikaza kiume kumkaribisha lakini mwili kwa hofu haukuwa wangu, niliamini kabisa mwalimu mkuu alishapata ushahidi na kilichobakia ni hukumu.

Woga niliokuwa nao niliamini hata kule kunitetea kwake lazima atabadili uamuzi wake kwa kuamini kilichosemwa juu yangu.
Nikiwa bado sijiamini, Sabina vidole vilikuwa mdomoni, mwalimu mkuu aliuliza. “Shija baba yako yupo wapi?” “Yupo shamba.” “Unaweza kunipeleka?” “Ndiyo mwalimu.” “Basi nipeleke.”

Niliongozana na mwalimu kuelekea shamba, Sabina aliyekuwa amekosa raha toka mwalimu mkuu afike pale. Niliongozana na mwalimu hadi shambani, wazazi wangu walipomuona waliacha kulima. “Karibu mwalimu.” “Asante.” “Una taarifa gani tena naona umeongozana na mwanafunzi wako?”
“Mmh, kuna mtafaruku umetokea ambao ndiyo ulionifanya nitengue uamuzi wa kumsimamisha Shija.“

“Mh, baada ya kuutengua ikawaje?” “Japo nimepata vikwazo vingi toka kwa baadhi ya wazazi baada ya kuitengua adhabu waliyoitaka . Wapo walionitolea maneno ya vitisho kuwa sitakuwa na umri mrefu. Lazima nitakufa.” “Ni nani?” “Mama Helena huyo.”

“Ina maana uchawi wake anafikiri utafanya kazi kwa kila mtu? Tunajua yule mama ni mchawi lakini sisi tunamtegemea sana Mungu.” “Basi mguu huu ni kuja kukutaarifu kwamba kesho mwanao aje shule kama kawaida, nitapambana na yoyote atakayetaka kukwamisha maendeleo ya Shija.” “Nashukuru sana mwalimu.”

Baba na mama walimpa mkono wa shukrani mwalimu kwa uamuzi wake wa busara. Baada ya taarifa ile iliyorudisha furaha moyoni mwangu, nilirudi na mwalimu ambaye alinieleza nizingatie masomo na kuachana na mapenzi. Nilijua alisema vile baada ya kuniona na Sabina nyumbani, mtu niliyekuwa natuhumiwa naye kuwa ni wapenzi.

Baada ya kuachana na mwalimu nilirudi nyumbani. Ilikuwa ajabu kwani baada ya kufika nyumbani, hata sijakaa Sabina aliingia. “Shija vipi mwalimu alikuwa akisemaje?” Nilimueleza yote yaliyosemwa , uso wa Sabina ulijenga tabasamu la matumaini. “Ooh, afadhali umerudi shule, Shija nikuambie kitu?” “Niambie.”

“Nilipanga kama wewe usingefanya mtihani na mimi nisingefanya.”
“Kwa nini?” “Shija siwezi kufanya mtihani wakati mimi ndiye chanzo cha yote, ningeweza kumzuia hata Helena lakini kwa vile kichwani hakuna kitu ningemwacha afanye.” Siku hiyo nilishinda na Sabina kutwa nzima, jioni tuliagana ili tukutane shuleni kesho yake.


INAENDELEA...
 
51--Siku ya pili nilikwenda shuleni na kusoma kama kawaida bila kutokea tatizo lolote zaidi ya wanafunzi wa kike kunitania shemeji kwa ajili ya uzushi uliojaa shule kuwa ugomvi wa Sabina na Helena ulitokana na mambo ya mapenzi.

Japo sikupenda maneno yale lakini kwa upande wa pili nilishukuru Mungu siri iliyo kati yetu ilibakia kwetu watatu. Sabina alikuwa msichana wa ajabu wala hakuona aibu kuwa na mimi karibu muda mwingi alinisogelea kutaka kujua baadhi ya masomo yaliyokuwa yakimsumbua.

Na kweli alikuwa makini sana na masomo tofauti na nilivyomfikiria kipindi kile labda matatizo yale yangemchanganya . Nilikumbuka ahadi aliniyonieleza siku moja kuwa atahakikisha atakuwa mmoja wa wanafunzi watakao ungana nami kwenda kidato cha kwanza.

Katika maisha yake yote aliuchukia sana uchawi. Alinieleza ni shinikizo la wajumbe wa baraza la wachawi kutaka kila mwanachana lazima amtoe mtoto wake mmoja atakayefundishwa uchawi ili wakizeeka wapate warithi.

Ilikuwa tofauti na Helena ambaye alionesha wazi kuwa katika chama wa wachawi kwake ilikuwa furaha ambayo ilionesha aliitamani muda mrefu. Nami nilimpa moyo kuwa azidi kumuomba Mungu ipo siku atasikiliza kilio chake na kuachana na kazi ile chafu. Na hata nilipokuwa namfundisha alionesha kweli mwanzo alikuwa akicheza na muda ule alikuwa ameamua kusoma.

Mawazo ya wengi juu ya ukaribu wetu uliwachanganya hata mwalimu mkuu ni kubadilika kiuwezo kwa Sabina kuweza kuwa mshindani na si mshiriki darasani. Siku zote katika kila kitu kuna washindani ambao kila siku huitafuta namba moja au kuwa katika namba nzuri zitakazo msaidia kuonekana anaweza.

Lakini kuna wengine wapo kama wapo kutokuelewa kwao hakuwaumizi kichwa na kuamini maisha si darasani popote wanaweza kuishi hata bila elimu. Hao siku zote wamekuwa washiriki na si washindani. Lakini toka nilipokuwa karibu na Sabina hiyo ilibadilika hata mwalimu alinisifia kwa hilo.

Siku ya tatu baada ya kurudi shule asubuhi tukiwa katika usafi baada ya kuhesabu namba, iligongwa kengele kutuashiria tunaitwa. Ilikuwa ajabu kupigwa kengele asubuhi kama ile. Wanafunzi wote tulikusanyika ili kusikia wito ule ulikuwa wa nini.

Baada ya kukusanyika mwalimu mkuu msaidizi akiwa na walimu wenzake ambao wote nyuso zao zilionesha kuna jambo fulani kutokana na kila mmoja kushikilia kitambaa mkononi na kufuta machozi kwa muda. Nilijiuliza machozi ya walimu yalimaanisha kitu gani ambacho si cha kawaida.

Baada ya kujadiliana walimu, mwalimu mkuu msaidizi alisema kwa sauti ya juu. “Ndugu wanafunzi kumetokea tatizo zito hapa shuleni kwetu, si jambo la kawaida kuwaiteni muda huu lakini imebidi kufanya hivi ili tuwaelezeni kilichotokea alfajiri ya leo.

Mwalimu mkuu wakati akitoka kuoga alianguka na kupoteza maisha.” Kauli ile ilinishtuka kwa kumsikia lakini sikumuelewa hata wanafunzi wenzangu walikuwa kama hawakumuelewa mwalimu mkuu msaidizi.

“Wanafunzi shule yetu imepata msiba mzito mwalimu mkuu hatunaye amefariki dunia alfajiri hii na mwili wake upo hospitali ya wilaya .” Kauli ile ilieleweka vizuri katika sikio la kila mmoja aliyekuwepo pale, kilio cha wanafunzi kilitawala shule huku walimu nao wakishindwa kujizuia kwa kuungana na wanafunzi kumlilia mwalimu mkuu.

Sabina alikuwa kama kapigwa butwaa hakulia bali macho yalimtoka pima, alinishika mkono na kunitoa kwenye kundi la wanafunzi waliokuwa wakilia kwa kujitupa chini kwa uchungu. Nikiwa bado nimepigwa na butwaa nisielewe kilichotokea. Tulipofika pembeni Sabina alinieleza kitu.

“Shija umeona?’ “Nini?” “Mama Helena alichomfanyia mwalimu mkuu kwa ajili ya kukurudisha shuleni?” “Sabina ina maana mwalimu mkuu hakufa?” “Sijajua mpaka nihudhurie kikao cha wachawi .” “Sasa kama kafa kwa ajili yangu unafikiri nitaweza kuendelea kusoma?”

“Kwa nini usisome kwa vile hakuna ushahidi na wewe kuwa na kosa zaidi ya chuki za watu. Sasa hivi utasoma tu labda afe mzee Manoni.”
“Una maana gani?” “Si kukuua au kukuchukua kwa uchawi, kwani siku hizi mambo ya vitisho usiku yanatokea?” “Hapana.” “Basi sasa hivi wanakuogopa kama ukoma ndiyo maana mama Helena alitaka ukose masomo ili iwe njia ya kukukomoa.”

“Shija tuondoke turudi nyumbani hali ya hapa haieleweki.” “Mmh, sasa hali hii itaendelea mpaka lini na kwa nini kwa hili mzee Manoni asilikemee?” “Hata mimi sijui, ila nataka kukueleza wachawi wote lao moja, ni ajabu kwako mzee Manoni amekuwa akikukingia kifua ni tofauti na kesi zote zilizowahi kufikishwa kwake .

Watu wengi wamechukuliwa misukule kutokana na chuki au hata kuuawa na kuliwa nyama kwa ajili ya ugomvi mdogo mtu akileta mashtaka yake anakubaliwa na kupewa msaada wa kumkomoa mtu.”

“Unafikiri ni kwa ajili gani mzee Manoni amekuwa akinitetea hivyo ?” “Mzee Manoni amekuwa akikutetea kwa sababu maalum, kuna siku nilisikia akisema kuwa shida yake kubwa ni kukurithisha mkoba wa kichawi.”

“Etiiii?” “ Shija ukweli ni huo hakuna njia iliyo salama kwako ya kukufanya uendelee kuwa salama hata baada ya mzee Manoni kufa zaidi ya kujiunga na chama cha wachawi .”

“Sabina una uhakika gani na hayo unayoyasema ?” “Shija huna njia ya salama kwa vile unajua siri nyingi za kichawi hivyo hawawezi kukuacha hivi hivi tu, lazima watakulazimisha uingie kwa nguvu la sivyo watakuua au kukugeuza msukule ili usitoe siri zao.”

“Sabina mbona unanichanganya, kwa hiyo kuna siku mzee Manoni atanieleza habari hizo?” “Hakuna salama yako lazima ujiunge na wachawi kama sisi, mimi sipendi kuwa mchawi lakini nipo kwa usalama wangu japo nafanya makosa mengi.

Cheo cha mama yangu ndicho kinachonilinda.” “Sasa unaniushauri nini?” Nilijikuta nachanganyikiwa . “Hebu kwanza tuondoke eneo la shule ili tuache kwanza mipango ya msiba wa mwalimu.


INAENDELEA...
 
52--Nina imani kabisa ilikuwa siku yangu ya kwanza kuhisi kama moyo ulitaka kupasuka na kupiga kelele ambazo niliamini kabisa ndizo zilizokuwa zikipunguza maumivu makali ya uchungu wa kumpoteza mwalimu aliyekuwa mtetezi wangu siku zote za uhai wake, nililia mpaka nikapoteza fahamu.

Niliposhtuka nilijikuta nimelala kwenye kitanda na mkononi nilikuwa naongezwa maji, pale palionesha ni hospitali. Nikiwa natafakari ilikuwaje, muuguzi alinisogelea na kuniuliza: “Unaendeleaje?’ “Sijambo kiasi.”

“Unakumbuka ulipatwa na nini?” Nilitulia kwa muda na kuvuta kumbukumbu lakini sikukumbuka, nilitikisa kichwa na kusema: “Sikumbuki.” “Unaitwa nani?” “Shija.” “Mara ya mwisho ulikuwa unafanya nini?”
Nilitulia tena kuvuta kumbukumbu taratibu nilikumbuka mara ya mwisho tulikuwa tukiuaga mwili wa mwalimu mkuu kabla ya kuusafirisha kwenda kwao kwa mazishi.

Kwa sauti ya chini nilimueleza: “Nakumbuka.” “Unakumbuka nini?” “Nilikuwa nauaga mwili wa mwalimu mkuu.” “Inaonekana peke yako ndiye uliyekuwa ukimpenda mwalimu wako.” “Kwa nini?” “Kutokana na maelezo, wakati unamuaga baada ya kuiona sura yake uliangua kilio kilichopelekea kupoteza fahamu kwa saa saba.”

“Mungu wangu!” “Ndiyo maana nilikuuliza ulikuwa ukimpenda sana.” “Tena sana, bado siamini mtu adondoke na kufa.” “Ni jambo la kawaida kitaalamu, kilichomuua mwalimu wenu ni shinikizo la damu na si kingine kama ninavyosikia labda kauawa kichawi.

Vipimo vilionesha baada ya kupatwa na mshtuko mishipa ya damu ilipasuka na kusababisha mauti yake.” “Hata hivyo , mwalimu mkuu alikuwa mtu muhimu sana maishani mwangu bila yeye leo hii nisingefika hapa.

Nitaendelea kumlilia siku zote za maisha yangu.” “Unamfahamu Sabina?” “Sabina! Sabina gani?” Nilishtuka kusikia jina la Sabina. “Unayesoma naye darasa moja.” “Kama huyo kwa nini nisimfahamu?” “Unamfahamu kivipi?” “Kama mwanafunzi mwenzangu.”

“Si zaidi ya hapo?” “Mbona unaniuliza hivyo ? Kuna nini?” “Sabina naye yupo hapa.” “Yupo hapa anafanya nini?” “Jana baada ya wewe kuanguka na kupoteza fahamu kutokana na maelezo ya mashuhuda walisema kuwa, alifikiri umekufa.

Alipatwa na mshtuko na kuanguka chini kitu kilichosababisha apoteze fahamu. Mliletwa kwa pamoja, lakini yeye aliwahi kuzinduka na alipozinduka aliendelea kukulilia huku akisema hakubali.” “Hakubali nini?’
“Hata sisi hatujui lakini baada ya kumueleza unaendelea vizuri alinyamaza na kuwa na hamu ya kukuona kwa kuamini tunamdanganya na ukweli ni kwamba umekufa.”
“Mungu wangu, mbona Sabina ana matatizo?” “Amkose mwalimu hata mpenzi lazima achanganyikiwe .” Sikumjibu muuguzi ambaye alikuwa mcheshi na mpole, alinijulisha wazazi wangu wapo nje.

Aliwaruhusu kuja kuniona huku mama akionekana kuchanganyikiwa sana. “Shija unaendeleaje baba?” “Sijambo mama.” “Pole sana mwanangu, najua ulikuwa ukimpenda sana mwalimu wako.” Baba aliongezea.

Muuguzi aliwaeleza ugonjwa wangu si mkubwa ila nitakuwepo pale hospitalini hadi siku ya pili kwa ajili ya uangalizi. Baada ya maelezo yale, muuguzi aliwaomba wazazi wangu anipatie tiba ili nipumzike.

Kwa vile chakula kilikuwa kimeletwa, nilikula kwanza kisha muuguzi alinidunga sindano na kuniomba kupumzika. Baada ya muuguzi na wazazi wangu kuondoka nilibakia na mawazo mengi. Ajabu sikumfikiria mwalimu mkuu aliyesababisha niwe pale zaidi ya kumfikiria Sabina.

Nilijiuliza Sabina ananipenda kiasi gani kufikia kutaka kufa kwa ajili yangu? Bado moyo wangu haukuwa na kitu ambacho ungeridhika kukitoa kwa Sabina ili kilingane na moyo wake ulivyojitoa kwangu. Niliamini kabisa kama Sabina angeanguka wakati wa kumuaga mwalimu mkuu.

Kwa upande wangu nisingeweza kufanya alivyofanya Sabina, kwangu lazima ningeona aibu kumlilia Sabina kwa vile tayari shuleni tulijukana kuwa ni wapenzi. Lakini nilijiapiza kumuonesha najali chochote alichokifanya na atakachokifanya .

Dawa nilizodungwa zilianza kufanya kazi, kichwa kilikuwa kizito na usingizi ulinichukua. Nilipozinduka nilikuwa kama nipo ndotoni, mkono ukinipapasa usoni, nilipofumbua macho kweli alikuwa Sabina. Aliponiona nimeamka alishtuka. “Aah!” “Vipi?” Nilimuuliza kwa sauti ya chini.
“Unaendeleaje?” “Mi sijambo sijui wewe ?” “Mimi mzima hadi nimekuja kukuona, basi ujue nipo fiti.”

“Nashukuru, hata mimi nipo fiti kama si muda ningeruhusiwa leo, lakini kesho mpaka saa nne nitaruhusiwa.”

“Hata mimi nilitaka kuruhusiwa nikaomba tutoke pamoja.” “Haya mama.” Siku ile muda wote tulikuwa pamoja mpaka usiku ulipoingia kila mtu alikwenda kulala kusubiri siku ya kesho yake kuruhusiwa.


Inaendelea....
 
53--Lakini wakati tukiwa hosptali tulipata taarifa ya kushangaza kuwa, maiti ya mwalimu mkuu iliyopelekwa Mochwari, usiku wa kuamkia siku ya pili ilikutwa nje ya chumba hicho cha kuhifadhia maiti.

Tukio hilo liliwafanya wauguzi na madaktari washtuke, hata hivyo habari hazikusambaa sana kwa sababu mganga alionya. Wengi waliamini nguvu za giza zilitumika na kwamba, mwalimu mkuu hakufa.

Nilijikuta nikiungana na kauli ya Sabina kwamba lazima mwalimu alikuwa amefichwa mahali akiwa hai na walichokuwa wakikiona watu ni kivuli chake tu. Lakini wakati baadhi ya watu waliamini hivyo , wapo waliosema ni habari za uongo na za kupotosha jamii wakiamini kuwa mwalimu mkuu alikufa sawa sawa na vifo vingine.

Nyumbani niliyaanza maisha mapya bila mtetezi wangu, nikiamini kwamba kwa kipindi kilichobaki nilitakiwa kuwa makini ili nifanye mitihani yangu ya mwisho bila tatizo la kiakili. Kama kawaida, niliendelea kuwa karibu na Sabina ambaye alionesha kunijali.

Katika uchunguzi wake wa kifo cha mwalimu alinieleza kuwa ni kweli alikufa pamoja na uchawi kutumika kumuondoa duniani lakini waliomuua ambao ni wachawi walishindwa kuchukua maiti ambapo alikuwa mzito kuliko kawaida kitu kilichowafanya waachane naye.

“Shija, mwalimu kweli alikufa na maiti yake ilipopelekwa hospitali, nia ya wachawi ilikuwa kumchukulia kule na kukiacha kivuli chake. Wachawi walifanikiwa kumtoa katika chumba cha kuhifadhia maiti, lakini walipofika nje wakati wanataka kumbeba ili waondoke nayo alikuwa mzito kama kajengewa chini.

“Wachawi walihangaika kumtoa pale chini na kutumia kila mbinu lakini mwili uliendelea kuwa mzito usiobebeka. Huwezi kuamini, kidogo alfajiri iwakute pale, ndipo walipoamua kuondoka. Na asubuhi mhudumu wa chumba cha maiti alishtuka kuona mwili wa mwalimu upo nje wakati mlango umefungwa.

“Ndipo alipoita watu ambao waliushangaa ule mwili, waliubeba na kuurudisha sehemu ulipohifadhiwa mwanzo.” “Sabina yote hayo ulikuwa unayajua mbona hukuniambia mapema?”
“Shija, nilikuwa sijui lolote,si unajua siku hizi sina kinga ya safari za hatari, walikwenda peke yao na hata waliporudi walikaa kimya.

Siku tulipotoka hospitali nilimuuliza mama kuhusu taarifa zilizozagaa kwamba mwili wa mwalimu ulikutwa nje ya chumba cha kuhifadhia maiti. “Alinijibu ni kweli na kunipa mkasa huu ambao haukuwa mgeni kwangu kwani matukio kama yale tuliishakutana nayo mara nyingi.

Si ya maiti kugoma kubebwa tu bali wengine wakishazikwa , kaburi huwaka moto na kushindwa kuwachukua maiti hao. “Kwa nini inakuwa hivyo ?” “Mara nyingi watu wa aina hiyo huwa wamezindikwa , maiti hawaliwi nyama.”

“Sabina kama wamezindikwa kwa nini wanakufa ?” “Shija nataka nikueleze jambo moja huenda unalijua au hulijui, hakuna mwanadamu anayeweza kumuua mwanadamu mwenzake ila kwa ruksa ya Mungu.” “Sabina ni Mungu gani anayeruhusu mtu amuue mwenzake?” “Shija hata mimi nilitatizika nilipoelezwa hivyo na mwanzo nilijua binadamu anaweza kumuua binadamu mwenzake.

Nafikiri kuna siku nilikueleza msukule huwa anakufa?” “Ndiyo nakumbuka.” “Basi katika maisha ya mwanadamu kila kiumbe kina siku yake ya kufa, ila unaweza kufanikiwa kumuua kupitia siku yake na hapo unapata dhambi ya kuua, lakini hata usingemgusa angekufa.”

“Kwa hiyo mwalimu amekufa au ameuawa?” “Kifo cha mwalimu mkuu mhusika ni mama Helena na washirika wake na baada ya kufa walitaka kumla nyama lakini wameshindwa .”
“Sasa wamepata faida gani?” “Hakuna faida! Ni roho mbaya tu isiyo na huruma.” Maneno ya Sabina yaliniongezea hofu moyoni na kuamini kama mama Helena amefanikiwa kumuua mwalimu hatashindwa kuniulia baba yangu mzazi.

Wasiwasi mkubwa ulitokana na siku ya kikao ambapo aliwatishia wajumbe na mwalimu mkuu ambaye baadaye alijirudi, kitu kilichosababisha kifo chake. Wasiwasi wangu ulizidi na kuamini kuwa kinga niliyopewa na mzee Manoni ili wachawi wasiniguse nilikuwa nayo peke yangu.

Kwa wazazi wangu bado nilikuwa na wasiwasi maana kama kweli mwalimu mkuu ambaye ilisemekana alikuwa na kinga ya mwili lakini mwisho wa siku alipatikana na wakamuondoa duniani sembuse wao, hasa baba ambaye siku zote haamini uchawi.

Lakini siku zilikatika, muda ukawadia tukafanya mitihani, nakumbuka siku hiyo Sabina alikuwa akisumbuliwa na kichwa hivyo hakuwa katika hali nzuri lakini alijitahidi japo kwa shida na kuacha baadhi ya maswali.

Nilimpa pole na kumpa moyo kwamba, kama maswali mengi alijibu vizuri yanaweza kumsaidia katika matokeo, alinishukuru na kuanza safari ya kurudi nyumbani. Njiani Sabina alishangaa kujiona yupo sawa, kichwa kikikuwa kimepoa: “Shija kichwa hiki si bure, subiri aliyesababisha kiniume, jasho litamtoka.”


INAENDLEA....
 
54--Ugonjwa wa Sabina ulinishtua na mimi, kichwa kupoa baada ya kutoka chumba cha mitihani! Niliwaza moyoni kuwa, aliyefanya vile lazima atakuwa Helena, hakukuwa na mtu mwingine na kama ni Helena vita yao itakuwaje? Wasiwasi wangu, Sabina angemfanyia kitu kibaya ambacho kingechukua muda mrefu kusahaulika akilini mwa watu.

“Shija nikifeli mtihani nakufa na mtu, waombe nisifeli.” “Sasa unamjua ni nani?” “Kuna mwingine zaidi ya mama Helena, mchawi asiye na haya.” “Lakini si ulisema anamuogopa mama yako?” “Ni kweli, ndiyo maana nashangaa.”

“Lakini....au malaria?” ”Shija acha kujitoa akili, malaria gani ya darasani tu?” “Hata mimi bado nipo njia panda.” “Shija kila dakika hasira zinapanda, nakuhakikishia mpaka kunakucha kuna jambo utalisikia.” “Jambo gani?” “Lile la mwanzo dogo, hili wataokota maiti.” “Sabina hupendi uchawi kwa nini unapenda kuua? Kwa nini usiwasamehe tu ili uweze kujipanga upya.

Maisha yako si kumuua Helena bali kujipanga kwa ajili ya hatima baada ya mitihani.” “Ni kweli Shija, lakini nimekuwa na hasira sana pale mtu anaponigeuka kwa kutumia ukaribu wetu.” “Sawa najua inauma, lakini wakati mwingine izuie nafsi yako kutenda mambo mabaya.”

“Sawa Shija nimekusikia, sitafanya niliyokusudia lakini nitamshikisha adabu.” “Sabina, mshukuru Mungu kwa kila jambo ili kuupa uhuru moyo wako.” “Shija, leo nashangaa kila unalolizungumza linaniingia na kupoa kama maji mtungini.” “Nashukuru Sabina kwa kunielewa.”

Niliagana na Sabina kila mmoja alielekea kwao. Nilipofika nyumbani nilijawa na mawazo juu ya kilichomtokea Sabina ndani ya chumba cha mitihani na baada ya kutoka.Nilijiuliza kama wachawi kwa wachawi wanachezeana mimi nitafanyaje?

Lakini ulinzi wa mzee Manoni ulinipa kichwa kufanya mambo yangu bila wasiwasi wala kutokewa na mauzauza usiku. Siku zote nililala vizuri na kuamka vizuri hakukuwa tena na vishindo, ngoma wala njozi za kutisha. Siku zilikatika huku wanafunzi wote tuliomaliza darasa la saba tukisubiri majibu kwa hamu kubwa.

Hatimaye siku ikafika matokeo yakatoka , shule yetu ilitoa wanafunzi kumi na nne, mimi nikiwa mmoja wa waliochaguliwa . Lakini kwa bahati mbaya Sabina hakuwemo. Kukosekana kwake kulimuumiza na kumfanya alie sana. Nilimbembeleza huku nikimueleza kuwa kuna maisha baada ya shule.

Ningeweza kusema labda wazazi wake wangeweza kumsomesha shule za kulipia, lakini haikuwa hivyo , maisha yetu ya kijijini tuliyajua wenyewe . Wacha kufeli hata waliofaulu wengine hushindwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na ukata.

Nilichaguliwa nijiunge na shule ya mjini ambayo ilichukua wanafunzi waliofanya vizuri. Kutoka tunapokaa mpaka mjini kwa baiskeli ni mwendo wa robo saa na saa moja kwa miguu. Nilifurahi kusoma shule ile kutokana na sifa zake za ufundishaji mzuri, tofauti na shule nyingi za kata, zilikuwa na walimu wachache.

Kuchaguliwa kwangu ilikuwa furaha kubwa kwa familia yangu hata Sabina naye alisema amefarijika. “Shija heri nimekosa mimi, ningeumia sana kama ungekosa wewe .”

“Sabina nashukuru lakini ndoto zangu hazikutimia.” “Ndoto zipi Shija?” “Nilitaka tufaulu wote na siku moja tuweze kukisaidia kijiji chetu.” “Shija, kijiji hiki hakitaendelea milele.” “Kwa nini?” “Na wachawi wa hapa utawaweka wapi?”

“Unataka kuniambia wachawi wa hapa hata maendeleo hawataki?” “Shija uchawi ni uharibifu, uchawi ni kikwazo , hivyo kila mtu atakayejifanya anajua kijijini hapa lazima afe.” “Unataka kuniambia Samuel aliyefungua duka mwaka juzi na kufa wiki moja baadaye aliuawa na wachawi ?” “Shija, Samuel hakufa, aligeuzwa msukule.” “Mh! Makubwa.”

Wakati tukizungumza, Sabina alionesha kuna kitu kinamsukasuka moyoni, nililigundua hilo na kumuuliza: “Sabina kuna kitu kinaonekana usoni kwako , una tatizo gani?” “Hakuna kitu Shija,” Sabina alinikatalia akiwa ameangalia chini. “Hapana Sabina kuna kitu, wewe si mgeni kwangu.”

“Shija sina jinsi, lazima niseme ukweli, ni kwamba matokeo haya yameniumiza sana baada ya kujua sababu ya kuumwa kwangu kichwa, ilikuwa vile ili nifeli.” “Ha! Kwa sababu gani Sabina?” “Shija, mwanzo nilijua labda Helena na mama yake kumbe siyo, yaani siamini aliyenifanyia sikutegemea hata siku moja.”


Inaendelea....
 
Wana JF niungeni mkono tupatiwe JUKWAA LA MAISHA,MIKASA na USHAURI
ili simulizi kama hizi za Majigo Mzizi Mkavu zisaidie kutujenga kimaisha.
 
Last edited by a moderator:
Ni kwel kabisa nahisi kama cku yangu inaenda vizur tokea jana Tetra
 
Last edited by a moderator:
55--“Nani aliyekufanyia mchezo huo?” “Mama.” “Mama! Unamaanisha mama yako?” ”Eeh.” ”Mama yako mzazi?” “Ndiyo.” “Sabina hebu acha utani,” niliamini Sabina alitaka kunirusha roho. “Shija naomba uamini ninachokisema hapa ndiyo ukweli wenyewe .”

“Sabina unajua tunazungumza jambo la muhimu, kwanini unaleta mzaha?” “Najua huwezi kuamini, siku zote kikulacho kinguoni mwako, amini aliyenifanyia mchezo ule mbaya ni mama yangu mzazi.” “Sasa alifanya ili iweje?”
“Kulikuwa na siri nzito ambayo mwanzo niliona aibu kuisema, lakini kutokana na umuhimu wako kwangu, sina budi kulianika mbele yako leo.”

“Eehe!” “Shija siku nilipotoka shuleni baada ya mtihani na hali iliyonitokea, nilikwenda kumueleza mama huku nikitangaza vita na familia ya kina Helena. Ajabu mama alipinga na kuniomba afanye mambo yake ili amtambue mbaya, jibu alilonipa lilinikatisha tamaa.”

“Alikueleza nini?” “Eti alinieleza sijalogwa na mtu ile hali ilinitokea kwa hofu ya mtihani na kuniomba niachane na familia ya mama Helena. Pia Shija naomba nikuombe samahani kwa kutokueleza mambo yaliyotokea siku za hivi karibuni. Baada ya mtihani familia ya mama Helena ilikutana na yetu kuondoa tofauti zilizotokea.
Niliwakubalia mdomoni lakini Helena niliapa kuwa adui yangu milele.” “Sabina nataka kukueleza adui wa leo ni rafiki wa kesho, kila mwanadamu ana upungufu wake hivyo si vizuri kumchukia mtu milele. Tumefundishwa kusamehe ili tusamehewe.”

“Ni kweli, hivi wewe upo tayari kumsamehe Helena?” Sabina aliniuliza akinikazia macho. “Nipo tayari, na nilikwishamsamehe muda mrefu.” “Shija wewe ni mtu gani usiyejihurumia, mtu alitaka kukutoa sadaka ukaliwe nyama leo hii unamsamehe?”
“Sabina adui wa leo ni rafiki wa kesho, kumbuka Helena huyo huyo ndiye aliyeshirikiana nasi kumtoa kaka yangu kwa kujitoa kwa hali na mali. Kama jana alikuwa rafiki, leo adui basi kesho atakuwa rafiki mwema zaidi.”

“Shija wewe kiumbe wa ajabu.” “Siyo wa ajabu siku zote ubaya ukilipwa jema, ubaya hukosa nafasi hivyo kumfanya aliyetenda ubaya ajidharau na kuiga tabia njema.” “Kwa hiyo unanishauri nimsamehe toka moyoni?” “Ndiyo maana yangu.” “Nitajitahidi kufanya hivyo .”

“Ulisema kuwa mama yako ndiye aliyekufanya uumwe kichwa wakati wa mtihani ili iweje?” “Nisifaulu ili niolewe.” “Wewe ulijuaje kama aliyefanya vile ni mama yako?”

“ Baada ya mtokeo ya darasa la saba, mama alikuwa akizungumza na mtu bila kujua mimi nipo ndani, nilimsikia akijisifia njia aliyotumia nifeli mtihani ili niolewe na baada ya matokeo, harusi iliandaliwa. Bwana anayetaka kunioa anatoka Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Shinyanga, tena ananioa kwa mahari ya ng’ombe 30.” “Ulijuaje?”

“Baada ya kusikia vile nilisubiri mgeni aondoke ndipo nilipomuangushia kilio mama, kwa kitendo chake cha kuniroga nisifanye mtihani ili niolewe.” “Mama alinieleza kufanya vile alikuwa na maana kubwa kwa vile nikiolewa nitakuwa nimejitoa kwenye mtandao wa kichawi na kunifanya niishi maisha ya amani.” “Wewe uliamua nini?”

“Sikuwa na jinsi kwa vile mtihani nimeshindwa na uwezo wa kunisomesha hakuna, wameamua niolewe ili kunitoa kwenye mtandao wa kichawi, wacha nikubali au ulikuwa unanishauri nini?” “Japo kitendo cha mama yako sikukipenda, nilipenda kukuona ukiwa sehemu ya maendeleo ya kijiji chetu.

Lakini hata walichokiamua si kibaya, kitakufanya uishi maisha ya amani.” Baada ya kuagana na Sabina nilirudi nyumbani nikiwa na mawazo mengi juu kitendo alichokifanya mama Sabina kwa mwanaye .

Nilijua sababu kubwa ya watu wa vijijini hawathamini elimu zaidi ya mali, wakiamini wakimuoza mtoto wa kike wanapata ngombe. Niliamini kabisa ng’ombe 30 ni mtaji mkubwa katika maisha ya kijijini.

Nilijua wingi wa ng’ombe katika mahari ya Sabina ulitokana na rangi yake ya weupe, katika Kabila la Wasukuma, wanawake weupe wana thamani kubwa katika mahari tofauti na wanawake weusi. Wiki moja kabla ya kuanza shule, Sabina aliolewa na kuhamia Bariadi na kuniacha mkiwa. Sikuwa na jinsi, nilijipanga kuanza masomo wa sekondari.


Inaendelea...
 
56--Namshukuru Mungu niliyaanza masomo yangu vizuri huku nguvu zangu zote nikizihamishia huko. Uwezo wangu kimasomo niliokuwa nao shule ya msingi niliuendeleza shule ya sekondari. Hali yangu ya maisha ilikuwa ya kawaida hakukuwa na vikwazo vyovyote vya awali wakati nikiwa shule ya msingi, mauzauza ya wachawi yalikoma.

Siku moja nikiwa natoka shule nilishtuka kukutana na Helena njiani, moyo wangu ulinilipuka na kujua si rahisi binti yule kuja kunitembelea kwaheri. Nilipomkaribia nilimpita bila kumsemesha, wazo la haraka lilikuwa baada ya kumpita nitimue mbio. “Shija,” sauti ya Helena iliniita na kuufanya moyo wangu unilipuke kwa hofu zaidi.

Sikumjibu nilikaza mwendo ili nitimue mbio lakini Helena aliendelea kuniita. “Shija, najua mimi ni adui yako mkubwa, pengine usingependa kuniona machoni mwako, ila nakuomba unisikilize kabla ya kuamua lolote lile juu yangu.” Maneno ya Helena yalinifanya nipunguze mwendo ili nimsikilize, nilisimama na yeye alikuja mbele yangu na kupiga magoti.

“Shija najua kiasi gani nimekufanyia mambo mabaya ambayo hatakiwi kufanya mtu mwenye ubinaadamu, nakubali nimekukosea. Nakuomba unisamehe kwa yote niliyofanya ya kutaka kukuondoa duniani, si mimi, kila nilichokifanya kilikuwa shinikizo la mama na washirika wenzake.
“Nililazimishwa na nilipokataa walinitishia kunitoa kafara, kwa kweli niliogopa na kutii amri yao.

Lakini naamini maisha yako ni marefu kwani kila hila imeshindikana na leo hii bado unaendelea kuishi. Shija wewe ni kiumbe wa ajabu ambaye sijawahi kumuona chini ya jua, pamoja na yote niliyokufanyia kwa kunijua bayana bado hukutaka kulipa kisasi kama Sabina.

“Sikuamini siku Sabina aliponieleza dhamira yake mbaya juu yangu, lakini ni wewe ndiye uliyeubadili moyo wake na hatimaye kuurudisha urafiki wetu.

Nimekuwa na wakati mgumu kusimama mbele yako kuomba msamaha kwa kuona aibu. “Huwezi kuamini leo ni siku ya tano nasimama maeneo haya kukusubiri kutaka kukuomba msamaha.
“Lakini kila nilipokuona ujasiri ulinipotea na kuamua kujificha nyuma ya mti na wewe kupita bila kujua kama nipo sehemu hii.

Shija nimejiuliza hali hii ya kukosa ujasiri wa kukueleza itaendelea mpaka lini, kama nina uwezo wa kwenda kumtoa mtu ndani mwake au kumfukua maiti kaburini kwa nini nilishindwa kusimama mbele yako?
“Lakini nimeamini kazi ile hujaa nguvu za kichawi na si mtu kamili, tofauti na mimi kusimama mbele yako bila nguvu za kichawi. Kweli uso wa mwanadamu umeombwa na aibu. Shija napiga magoti mbele yako kukuomba msamaha toka chini ya uvungu wa moyo wangu. “Nakuahidi alilolifanya Sabina ndilo nitakalo lifanya kuhakikisha unakuwa salama siku zote.

Najua sasa hivi upo salama sana baada ya adhabu aliyotoa mzee Manoni kwa wote waliotaka kukugeuza kitoweo. Ninavyokueleza mtoto wa kaka yangu mwezi jana ametolewa sadaka kama faini ya kile walichotaka kukufanyia .

“Shija nipo tayari kwa lolote utakalotaka kunifanya hata likiwa zaidi ya alilotaka kunifanya Sabina nipo tayari. “Nimekutendea mambo mabaya ambayo sikustahili kusimama mbele yako, lakini moyo unanisuta lazima nisimame ili unipe hukumu inayolingana na kosa langu.”

Maneno ya Helena yaliufanya moyo wangu usisimke na kujikuta nikitokwa na machozi, niliamini alichokisema kilitoka moyoni mwake na kuzidi kuamini kwamba adui wa jana ni rafiki ya leo.
Machozi yangu yalizidisha kilio cha Helena ambaye alijikuta akikaa chini bila kupenda huku akinishika miguu yangu.
“Shija najua roho inakuuma kila ukiniona mbele yako, unatamani kunirarua na kunila nyama.

Nakuomba uamini hili nisemalo, sisi wasichana wa kijijini tumekuwa tukilazimishwa kuingizwa kwenye uchawi bila kupenda kwa kisingizio cha kurithi mikoba ya wazazi wetu watakapozeeka .
“Tumekuwa tukifanyishwa mambo ambayo nafsi zetu hayazitaki, lakini siku zote ukiifanya kazi mbaya kwa muda mrefu hatimaye unajikuta umeingia na kuwa mshiriki kamili usiye na chembe ya huruma.

“Sabina kabadilika hivi karibuni baada ya kuzama katika penzi lako, lakini Sabina ndiye aliyeongoza kwenye mambo mazito hasa ya kufukua maiti za watoto, kutoa mimba za wanawake ambao hujiona wana mimba na mwisho wa siku huzaa vitu vya ajabu.

“Kweli nimeamini penzi kitovu cha uzembe, Sabina tangu kuwa na wewe amejikuta akikiuka miiko yote ya uchawi na kuwa tayari kwa lolote, kilichomsaidia Sabina ni uwezo mkubwa wa kichawi wa mama yake tofauti na mimi. Nataka nikueleza kitu kimoja, baada ya zoezi la kumtorosha kaka yako kushindikana, nilitakiwa nitolewe kafara ili niliwe nyama.

“Mama yangu aliwapigia magoti nisifanyiwe hivyo , walikubali kunisamehe lakini sharti kubwa nililopewa ni kuhakikisha nafanikisha kukuua au kukuchukua msukule.

Shija ile ilikuwa siri ambayo hata Sabina hakuijua, nina imani angeijua mapema nisingekusogelea. “Kwa ukaribu wetu Sabina alinipa siri kuwa ngozi ya kinga ya safari za hatari alikupa wewe ili kukukinga.

“Kwenye kamati ya uchawi alisema ameidondosha, kwa vile alikuwa akiaminika kwenye safari zote za kiuchawi, binafsi sikumuamini aliponiambia kuwa amekupa nilidhani amepoteza kweli. “Lakini kikwazo cha kukupata kilinifumbua macho na kufanya upelelezi na kuamini kumbe kweli. “Hapo ndipo nilipobahatika kukipata kipande cha ngozi na kuondoka nacho.

“Tukiwa na uhakika wa kukupata, lakini kwa maajabu makubwa, siku tulipokuja tulishangaa kutokukuta, nilijikuta nikichanganyikiwa na kujiuliza wewe ni kiumbe wa aina gani, nilianza kukata tamaa ya kukupata, ndipo nilipotumia njia ya kukutafuta mchana, bahati nzuri nilikukuta umelala ndani na kukulisha dawa za kichawi ili ufe.

“Shija, Sabina kweli aliapa kuyatetea maisha yako, aliweza kuyaokoa tena maisha yako kwa kukutapisha dawa za kichawi, niliamini kupitia ugonjwa wako, basi tungeweza kukupata na kweli tulikupata bado Sabina aliyaokoa tena maisha yako kwa kupeleka taarifa kwa mzee Manoni.

“Shija nakuomba kuanzia leo unione ni kiumbe kipya niliyemsafi mbele yako, nakuahidi kuyafanya yote aliyoyafanya Sabina au pengine mara mbili yake.” Baada ya kumsikiliza Helena na kuona kwamba mengi hayakuwa mageni kwangu zaidi ya kunifafanulia kwa kina, niliamini ni muda mwingine wa msamaha kuchukua nafasi yake.

Nilimshika mabegani na
kumnyanyua , nilimtazama, alikuwa akiaanza kuvimba macho kutokana na kilio. “Helena,” nilimwita kwa sauti ya chini. “Abee Shija.” “Nimekusamehe.” “Kweli Shija?” “Kweli.” “Au unanifurahisha tu?”

“Helena nilikusamehe tokea siku ya kwanza nilipojua dhamira yako, nina imani msamaha wangu ndiyo uliomfanya Mungu naye anilinde. Amini kweli nimekusamehe tumefundishwa kusamehe ili tusamehewe.” “Asante Shija, umenipa funzo maishani mwangu.” “Kwa hiyo umeachana na uchawi?” Nilimuuliza.


INAENDELEA.....
 
Nasubiri kujua namna gani mzee manoni nilishindwa kumrithisha mikoba yangu Shija, inaniuma kweli ndugu yangu Majigo!
Kwi kwi kwi kwi! JF bwana hadi raha!

Sent from my BlackBerry 8520 using JamiiForums
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom