"MPAKA sasa, bado nashindwa kuelewa, ni vigezo gani hasa vilivyotumiwa na Chadema, kuwapata wabunge wa viti maalumu, maana, baadhi ya wanawake walioteuliwa ninawazidi elimu, muda wa kujiunga na chama, michango katika chama na hata nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali."
Huyo ni Leticia Musori, aliyekuwa maarufu kwa jina la mama Bawacha. Alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Wanawake wa Chadema kabla ya kukihama chama hicho.
Musori anasema uamuzi wa kujiondoa Chadema unatokana na kuchoka kuimba wimbo aliouita wa zidumu fikra za Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye anasema amekuwa akiwadhibiti wanawake na kuwazuia kufanya maamuzi yoyote wenyewe bila kuwaingilia.
Anadai akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake, Mbowe alikuwa akishinikiza Katibu wa Baraza hilo kuwa na mamlaka ya kiutendaji zaidi yake licha ya kuwa ndiye aliyekuwa bosi wake kiuongozi.
Anadai kwamba hali hiyo ilikuwa ikilalamikiwa na wanawake wengi lakini hawakusikilizwa na badala yake anasema aliahidiwa kuwa suala lake litajadiliwa na Katibu Mkuu bila mafanikio.
Baada ya kuona danadana, yeye na wenzake waliipuuza na kuamua kuchapa kazi lakini uvumilivu wao uliwatumbukia nyongo baada ya wanawake wa umoja huo kuingiliwa katika mchakato wa kuwachagua wanawake wanaoona wanafaa kuwawakilisha bungeni na badala yake jukumu hilo likapelekwa kwa wataalamu. Anaamini kwamba huo ulikuwa ni ujanja wa wakubwa kutaka nafasi ya kuteua watu kwa maslahi yao.
Vigezo vya kuteuliwa
"Wametaja vigezo vyao vyote, nimeangalia mimi ninavyo. Kama ni muda wa kutumikia chama nimejiunga na Chadema tangu mwaka 2004, tena nimeanza katika ngazi ya chini ya uongozi mpaka nikafikia hatua ya kuaminika na wanawake wenzangu na kunipa nafasi ya uenyekiti wa Taifa. Nimekuwa diwani kwa miaka mitano, nimekuwa mweka hazina wa madiwani wote wa Chadema."
Mbali na uongozi ndani ya chama, anasema amekuwa katibu wa mitandao ya asasi zilizo za kiserikali katika Wilaya ya Tarime, Mwenyekiti wa Wanawake wa Kanisa Katoliki Jimbo la Ukonga, Mratibu wa Asasi ya Mkamilishano Trust Fund iliyokuwa na makao makuu yake Ujerumani na Mwenyekiti wa Tukamilishane Women Association.
Elimu
Ni mhitimu wa kidato cha nne aliyepata pia mafunzo ya uuguzi nchini Ujerumani kwa muda wa miaka minne katika ngazi ya stashahada.
"Naweza kuzungumza vyema lugha tatu, Kiswahili, Kiingereza na Kijerumani, najiuliza kati ya wabunge wote wa viti maalumu kwa nini waniache wakati wapo wabunge waliochaguliwa ambao nawazidi elimu, michango katika chama, uwezo na hata muda wa kukitumikia?" anasema.
Mchango katika Chama
"Nimetoa michango mingi ndani ya chama. Mwaka 2006 nililipia pango la ofisi ya chama kwa pesa zangu mwaka mzima. Nilitoa pesa zangu nikanunua kiwanja kwa ajili ya kujenga ofisi ya chama huko Tarime. Kiwanja hicho kilikuwa katika Kata ya Nyanungu. Sasa hivi hiyo kata imegawanywa na kipo katika Kata ya Ikiryo."
Anasema ingawa anaweza kuonekana kuwa na hasira baada ya kunyimwa ubunge, anaamini kuwa waliopo ndani ya Chadema ndiyo wanaojua ubovu wa viongozi na udhaifu walionao.
"Chadema imeendeleza uozo na udikteta katika kufanya maamuzi, bado kinaendeshwa kama kampuni ya wakubwa katika maamuzi mbalimbali. Hili la kuteua viti maalumu kwa misingi ya undugu, ubinafsi na mahusiano ya vigogo ni mfano tu wa malalamiko ya wanawake wengi" anasema.
Anasema kinachomkera ni kuwa uchaguzi halali wa baraza hilo ulivunjwa kwa makusudi na viongozi wa taifa wa chama hicho ili kutoa nafasi kwao kuingiza wanawake wanaowataka badala ya kuwaachia wenyewe wajiamulie na kujichagulia wawakilishi wanaowataka kama inavyoelekezwa katika kanuni za katiba ya baraza hilo.
Anasema katika uchaguzi wa wanawake wa baraza hilo uliofanyika PTA Temeke, alishika nafasi ya tano huku wabunge wote wa viti maalumu wa mwaka 2005-2010 wakiambulia kura mbili mpaka tano hali iliyokuwa ikiwazuia kuendelea kuwa wabunge.
Lakini anasema kwa nafasi yake na kwa wingi wa kura alizopata ameshindwa kuwa miongoni mwa wabunge 25 walioteuliwa jambo ambalo anasema mbali na kumshangaza na kumhuzunisha, limeonyesha kuwa chama hicho kina wenyewe.
Musori anasema uchaguzi wowote ni kipimo cha demokrasia siyo tu kwa serikali iliyopo madarakani, bali hata taasisi zote za kiraia pamoja na vyama vya siasa. Anasema Ndani ya Chadema demokrasia ni wimbo unaoimbwa kwa ajili ya watu wa nje na si wa ndani ya chama hicho.
Anatoa wito kwa Watanzania na wafuasi wa chama hicho kuacha ushabiki na kukitazama chama hicho kwa umakini mkubwa. "Ndugu zangu, mnaweza msinielewe, lakini iko siku mtaelewa, acheni ushabiki wa kisiasa, angalieni viini vyanzo vya vyama kabla ya kujiunga navyo," anasema.
Source: Gazeti Mwananchi Tuesday 30 November 2010.
Comment: This is loud and clear!...THOSE ARE TRUE COLOURS OF CHADEMA!