Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Nimechafuka na wino, sababu yako fulani,
Ili nipate maneno, nikukomeshe fatani,
Siyataki malumbano, hilo liweke kichwani,
Nimefanya kosa gani? mwenzangu sifiche neno.
Nimepata mnong'ono, waniteta mtaani,
Wayasaka mapambano, kwa uvumba na ubani,
Nakuuliza nonino, wapata faida gani?
Nimefanya kosa gani? mwenzangu sifiche neno.
Mswaki kwa yako meno, uchao niko kinywani,
Yangekuwa msumeno, ningeshakufa zamani,
Fungua yako mabano, nimefanya baya gani?
Nimefanya kosa gani, mwenzangu sifiche neno.
Wataka nini cha mno, ukitaje hadharani,
Nikupe pasi bishano, ipatikane amani,
Ni tayari hata chano, upate poa shetani,
Nimefanya kosa gani, mwenzangu sifiche neno.
Tamati nipe mgono, nielekee bwawani,
Usisahau ndoano, na ndoo ya wastani,
Niepushe mapigano, nisiitwe hayawani,
Nimefanya kosa gani, mwenzangu sifiche neno.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
call/whatspp 0622845394 Morogoro.