Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,286
Miyenu ninavyohema, kama nyumbu akimbizwa,
Mwili wangu wakutema, siko sawa naumizwa,
Ila nashindwa kusema, nachelea kupotezwa.
Moyoni ninatatizwa, nahisi siko salama.
Kila nikijitazama, najiona kama zwazwa,
Nilochagua kiama, mwepesi wa kuchukizwa,
Sasa nakumbuka zama, zile za kusikilizwa,
Moyoni ninatatizwa, nahisi siko salama.
Si usingizi zahama, naota ninagombezwa,
Kukicha nashika tama, nawazia kufukuzwa,
Nimefanya nini jama, uchao naelelezwa,
Moyoni ninatatizwa, nahisi siko salama.
Ikome hiyo mitama, na fimbo za kuchalazwa,
Sitaki kono la chuma, ninataka kuongozwa,
Nihimizwe kujituma, penye kosa kuelezwa,
Moyoni nina tatizwa, nahisi siko salama.
Kesho yetu sio njema, uhuru ukipuuzwa,
Linauma kwa mtima, kwa haki kukandamizwa,
Nilozoea 'tazama, bila hoja nakatazwa,
Moyoni ninatatizwa, nahisi siko salama.
Hapa mwisho kaditama, sorry uliyechukizwa
Haya yote nilosema, yanataka kuchunguzwa,
Likiwepo lenye jema, vizuri kutekelezwa,
Moyoni ninatatizwa, nahisi siko salama.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
whatspp/call 0622845394 Morogoro.