RAIS NIOMBE RADHI.

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,284
1464897120084.jpg


Rais niombe radhi, tena iwe hadharani,
Kauli yako yakuudhi, imekera si utani,
Leo nakupa waadhi, uandike ukutani,
Nasi tuna yetu hadhi, tulo feli darasani,
Mimi kunita kilaza, rais niombe radhi.

Nimeketi nimewaza, mkono uko kichwani,
Baba wanita kilaza, mwana atanita nani?
Nini hasa uliwaza, hebu nitoe gizani,
Hakika umenikwaza, moyoni sina amani,
Mimi kunita kilaza, rais niombe radhi.

Makosa yalotokea, ni sawa kusawazisha,
Kwa hilo hujakosea, tena nakupa motisha,
Ila ulikoendea, fahamu kwasikitisha,
Yaepuke mazoea, yasije kukutingisha,
Mimi kunita kilaza, rais niombe radhi.

Neno likiwa na meno, halifai asilani,
Lisiwe kama ndoano, likatunase kinywani
Ama liwe msumeno, kukata yetu amani,
Lataka liwe mfano, kutoka kwa Sulemani,
Mimi kunita kilaza, rais niombe radhi.

Kalamu naomba koma, sinitie gerezani,
Karatasi soma zama, hizi sio za zamani,
Wino ufanye hima, wangojea kitu gani?
Hapa sasa kaditama, penye kosa samahani,
Mimi kunita kilaza, rais niombe radhi.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
whatspp/call 0622845394 Morogoro.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom