SEHEMU YA 17
Sikumjibu kitu, niliendelea kumshika tu, nilijua hakuwa ametulia, kichwa chake kilichanganyikiwa na muda wote alikuwa akilia kwa uchungu. Niliumia zaidi, maneno yake yalinichoma, nikahisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wangu.
Nilishindwa kujitetea, niligundua kwamba huo haukuwa muda mzuri kwangu kumwambia Isabela ukweli kutokana na kile kilichokuwa kikiendelea. Alilia sana, nilibaki kimya, nikamsogeza na kumkumbatia, hakukuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya hicho.
Mimi: Naomba unisamehe Isabela mpenzi.....(nilimwambia kwa sauti ndogo karibu na sikio lake)
Isabela: Kwa nini umenifanyia hivi Denis, kwa nini umeniumiza hivi?
Mimi: Si lengo langu kukuumiza, naomba futa machozi mpenzi, nitakuelezea kila kitu, naomba tuondoke kwanza.....
Nikamtoa hapo ndani na kuelekea naye nje, huko, nikamuingiza ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea katika lodge moja iliyokuwa maeneo ya Kinondoni. Ndani ya gari, muda wote alikuwa mwenye huzuni tele, bado alikuwa akilia kwa kilio cha kwikwi, macho yake yalivimba mno.
Nilichanganyikiwa mno, kuna kipindi nilishika usukani, nikajisahau kutokana na mawazo mengi niliyokuwa nayo, ghafla, nikaliona gari letu likihama njia na kuelekea mtaroni, nilishtuka, kwa juhudi, nikalidhibiti, likarudi barabarani.
Hatukuchukua muda mrefu, tukafika katika lodge hiyo ambapo nikasimamisha gari na kuingia ndani huku tayari ikiwa ni saa moja usiku. Nikalipia chumba na kuingia, siku hiyo hatukuja humo kufanya ufuska, tulikwenda kwa kuwa nilitaka kuzungumza naye.
Mimi: Kwanza naomba unisamehe mpenzi... (nilimwambia mara baada ya kuingia ndani)
Isabela: Yule ni nani? (aliniuliza huku akiniangalia usoni)
Mimi: Anaitwa Salama.
Isabela: Ni nani yako? (aliniuliza swali jepesi ila lenye ugumu kujibika, nikashusha pumzi nzito)
Isabela: Ni nani yako? (alirudia swali kwa sauti kubwa)
Mimi: Baba aliniambia ni mke wangu.
Isabela: Mke wako?
Mimi: Isabela, nimechanganyikiwa, sijui nifanyeje.
Isabela: Imekuwaje? Mke wako kivipi?
Mimi: Leo wazazi walikuja kutoka kijijini, wamemleta yule mwanamke, wameniambia ni mke wangu, niishi naye kwani baba aliniolea kijijini.
Isabela: Uongo, Denis unanidanganya.