Niliua kwa Kukusudia--24-
ILIPOISHIA:
Jioni ya siku hiyo, tulikuwa kwenye Ufukwe wa Coco.
"Sikukuita huku kwa bahati mbaya, kuna jambo nataka nikuambie," alisema bosi na kusimama.
SASA ENDELEA…
KITENDO cha bosi kusimama baada ya kuniambia kuwa kuna jambo alitaka kunieleza, kilinishtua na kunifanya nibaki kimya huku nikimtazama kwa macho ya woga. Sikuwa na hisia juu ya nini alitaka kunieleza.
"Kama kuna mahali nitakukosea, basi nitaomba msamaha wako lakini nadhani nitakuwa sahihi," alisema bosi na kuendelea kuzungukazunguka mahali alipokuwa amesimama.
Muda kidogo, aliketi na kuendelea na mazungumzo yake.
"Kwanza kabla ya kuendelea, ngoja tuagize vinywaji kwani huwa unapendelea kinywaji gani?"
"Maji yanatosha sana," nikamjibu kwa mkato.
"Tunu bwana, yaani nyumbani unywe maji, hata sehemu kama hizi?"
"Basi ngoja ninywe juisi bosi," nikamjibu na kumwangalia usoni.
"Kuna kinywaji kinaitwa Redd's, hakika kitakufaa."
"Lakini sikifahamu bosi, kwani siyo pombe?"
"Hakina kilevi, ila kinachangamsha tu," alinijibu na kuachia tabasamu.
"Sawa," nikakubali kwa haraka. Sijui ni nini? Maana nilikuwa namuamini sana bosi kwa kila jambo aliloniambia kiasi kwamba sikuwa na uwezo wa kupinga jambo lolote aliloniambia.
Mhudumu aliitwa na kuagizwa vinywaji vyote. Baada ya kurejea, alikuwa amebeba kisado kilichojaa. Akaweka chupa tatu za Redd's kwa upande wangu na kwa bosi. Kinywaji cha bosi kilikuwa tofauti kabisa na cha kwangu.
Kwanza chupa zangu zilikuwa za kopo zikiwa na rangi nyekundu na maandishi ubavuni. Lakini kinywaji cha bosi kilikuwa ni chupa ndefu ambayo ubavuni ilikuwa imeandikwa Grants.
"Naomba utuitie mtu wa jikoni tafadhali," bosi alimuagiza yule mhudumu na kutuacha tukiendelea na mazungumzo yetu. Moyoni nilikuwa na hamu na shauku kubwa ya kujua ni kitu gani hasa ambacho bosi alikuwa amepanga kuzungumza na mimi hadi kuamua kunitoa kwa matembezi ya jioni ikiwemo kuninunulia chakula cha usiku.
Bosi alinifungulia chupa yangu na kunitaka nionje ili nione ladha yake.
Taratibu nilichukua Redd's iliyokuwa imefunguliwa na kuanza kuimimina taratibu kinywani. Hakika ilikuwa nzuri, nilifurahia ladha yake yenye utamu wa kuburudisha mdomoni.
Sasa nikawa nakunywa bila uoga wowote huku mazungumzo yakizidi kunoga.
"Huo ndiyo ukweli wa moyo wangu Tunu, nakupenda nakukuhitaji sana, sawa?"
"Hapana bosi, hakika siwezi kuwa na uhusiano na wewe, lakini pia siyo wewe tu, umri wangu wa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume yeyote bado haujafika," niliendelea kutoa kauli zenye upinzani hali iliyosababisha kuanza kumkera bosi Elhakimu kwani alianza kubadilika kuanzia machoni, sura na hata mazungumzo yake kwani alianza kutoa maneno kwa ukali na kejeli kidogo.
Wakati namalizia chupa ya kwanza, ghafla nilianza kuhisi hali ambayo sikuwahi kuwa nayo. Nikawa naona vitu kwa taswira mbilimbili. Kuna wakati nikawa namuona bosi kama mtu wa kawaida tu. Uwezo wa kuzungumza ukawa unaongezeka na kuanza kucheka hata pale ambapo hapakuhitajika kufanya hivyo.
Licha ya kusikia hali hiyo lakini sikuwa tayari kukubaliana na ombi la bosi kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mimi. Moyoni nilijiapiza kuweka msimamo usiotetereka.
"Au labda unaona kama sikufai?" alihoji bosi Elhakimu huku akipeleka kinywani kwa fujo chupa yake ya Grants.
Tukiwa tunaendelea na mazungumzo, mhudumu wa jikoni alikuja na vyakula alivyokuwa ameagizwa ambavyo ilikuwa ni mbuzi wa kukaangwa na ugali sahani mbili, kachumbari pembeni na pilipili kwa mbali. Kabla ya kuweka mezani, harufu ya mbuzi ilitawala na kutufanya sote tuwe na hamasa ya kuikabili ipasavyo.
Mhudumu alitunawisha na kutukaribisha kwa heshima na taratibu zote ambazo mteja husitahili kupewa wakati wa kupewa huduma. Tukaanza kula huku bosi akiendelea na ajenda yake ya kunishawishi nikubali kuingia naye kwenye uhusiano wa kimapenzi jambo ambalo sikuwa tayari hata kidogo kukubaliana nalo.
Tulipomaliza kula, tayari nilikuwa nimeshabadilika, nilikuwa nazungumza bila kupumzika, maneno yakatawala.
Baadaye macho yalianza kuwa mazito. Usingizi ukaanza kuninyemelea na kujikuta nikiinamia kwenye mapaja yangu na kuanza kusinzia.
Nilishtuka baaada ya kuguswa na kitu kisichokuwa cha kawaida mwilini mwangu. Nikafumbua macho kwa tabu. Sikuamini nilichokishuhudia. Ghafla ulevi ukaniisha.
Je, Tunu ameshuhudia nini? Usikose kufuatilia leo jioni......