Ilikuwa mwaka 1988 wakati huo nikiwa nafanya kazi jijini Tanga katika ofisi ya mkuu wa mkoa baada ya kupata kazi katika ule mpango wa
direct employment. Nilifanya kazi mkoani Tanga kwa mwaka mmoja na mwaka uliofuata yaani mwaka 1989 nilipata kazi jijini Dar katika wizara fulani inayohusika na mambo ya maliasili. Hiyo ni baada ya kuona nafasi za kazi katika gazeti la serikali na kutuma maombi yangu.
Nilifika Dar na kufikia kwa ndugu yangu na kuripoti hapo wizarani wiki iliyofuata ambapo nilipokelewa na afisa utumishi ambaye ndiye aliyekuwa bosi wangu kwa sababu nilikuwa nimeajiriwa katika idara hiyo ya ofisi ya utumishi hapo wizarani. Nilikabidhiwa kwa mfanyakazi mwenzangu kwa ajili ya kuelezwa taratibu za kazi. Ilinichukua wiki nzima kupatiwa maelekezo ya taratibu za kazi na niliambiwa wiki inayofuata ndiyo nitakutana na afisa utumishi kwa ajili ya kukabidhiwa nyenzo za kazi na maelekezo ya ziada ndipo nianze kazi rasmi.
Nakumbuka siku ya Jumapili nikiwa nyumbani nimejipumzisha nilianza kuumwa na kichwa kwa upande wa mbele, niliwahi kuambiwa kwamba ugonjwa huo unaitwa kipanda uso. Ukweli ni kwamba nilikuwa na tatizo hilo la kuumwa na kichwa kwa upande wa mbele kwa muda mrefu sana na nilikuwa nimetumia dawa za kila aina zikiwemo za miti shamba lakini nilikuwa napata nafuu ya muda tu. Nilitoka na kumuomba mtoto wa mwenye nyumba ninapoishi akaninunulie aspro ili kutuliza maumivu ya kichwa. Mwenye nyumba nilipokuwa nikiishi aliniona nikiwa nimejiinamia hapo nje ikabidi aniulize kilichonisibu. Nilimweleza juu ya tatizo langu.
Alinieleza kwamba, kuna duka moja Kariakoo linauza dawa za miti shamba, ambapo pia wanazo dawa za kutibu hicho kipanda uso. Alinipa ushuhuda wa mdogo wake aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo la Kipanda uso na kutibiwa kwa dawa za mitishamba walizonunua katika hilo duka hapo kariakoo na mpaka leo hajawahi kupata tatizo hilo. Alinielekeza lilipo hilo duka na nikapanga siku inayofuata yaani Jumatatu nikitoka kazini nipitie hapo Kariakoo kununua hizo dawa. Siku iliyofuata yaani Jumatatu nilifika kazini asubuhi na mapema kwani ndiyo siku ambayo nilitakiwa kuonana na afisa utumishi kwa ajili ya kupatiwa nyenzo za kufanyia kazi.
Afisa utumishi alipofika alinijulisha kwamba ana kikao, hivyo zoezi letu litafanyika mchana. Hata hivyo niliendelea kumsaidia mwenzangu kazi zake pale ofisini. Ilipofika mchana muda wa kula nilikata shauri kutumia muda wangu wa kula kwenda kariakoo kununua dawa za kipanda uso kama nilivyoelekezwa na mwenye nyumba. Nilikwenda kariakoo na kulipata hilo duka kirahisi kama nilivyoelekezwa, nilimweleza yule mzee niliyemkuta pale dukani kuhusu tatizo langu akanipatia dawa za mavumba za kufukiza kichwani na magome fulani ya kuchemsha na kunywa ambapo alinitaka nitumie dawa hizo kwa siku saba asubuhi na jioni ndipo nitudi kumpa mlisho nyuma. Nilitoka pale na furushi langu la dawa na kurudi ofisini. Nilipofika niliambiwa nahitajika ofisini kwa afisa utumishi. Nilipitiliza na bahasha yangu iliyokuwa na mitishamba hadi ofisini kwa afisa utumishi.
Huyo afisa utumishi alikuwa ni mtu mzima na alikuwa ni mtu anayeongea taratibu huku akirudia rudia maneno kama vile anamuelekeza mtoto mdogo. Mazungumzo yetu yalichukua muda mrefu sana takriban masaa matatu akirudia rudia sentensi mpaka nikawa nimeboreka. Mpaka tunamaliza kikao muda wa kazi ulikuwa umeshakwisha hivyo nilikurupuka na kuondoka zangu kurudi nyumbani. Nilipofika nyumbani nikakumbuka kwamba nilikuwa nimesahau ile bahasha yangu ya miti shamba ofisini kwa afisa utumishi. Hata hivyo sikuwa na wasiwasi maana nilijua nitakuta dawa zangu siku inayofuata.
Siku iliyofuata nilipofika ofisini karibu wafanyakazi wenzangu wote niliokuwa napishana nao hapo ofisini kwetu walikuwa wakinikwepa na kunikodolea macho, hata nilipokuwa nikiwasalimia wengine walikuwa hawaitiki zaidi ya kunitumbulia macho. Nilishikwa na wasiwasi kwamba, kumetokea nini. Kabla sijakaa kwenye dawati langu, niliambiwa naitwa kwa mkurugenzi. Nilipofika ofisini kwa mkurugenzi nilimkuta yule afisa utumishi na wafanyakazi wenzangu wa idara ya utumishi wakiwa wamekaa wakinisubiri. Niliona dhahiri jinsi macho yao yalivyokuwa yakinitazama kwa hofu, mpaka na mimi nikaingiwa na hofu, maana sijui hata kumetokea jambo gani. Pale mezani kwa mkurugenzi kulikuwa na ile bahasha yangu iliyokuwa na ile mitishamba ya kutibu kipanda uso, lakini sikuweza kutabiri chochote. Yule mkurugenzi alinitaka nikae na baada ya kukaa alikohoa kidogo kabla ya kuanza kuongea.
Ndugu zanguni nimewaita hapa kutokana na huyu mtumishi mwenzetu mgeni aliyejiunga nasi hivi karibuni akitokea mkoani Tanga. Alisema yule mkurugenzi, kisha akaendelea
Huyu mwenzetu amekuja kwa kasi ya ajabu, yaani hata kabla ya kuwa mwenyeji ameshaanza kutuonyesha makucha yake kwamba yeye ni gwiji hasa wa mambo ya kishirikiana, na jana akiwa ofisini kwa afisa utumishi kwa ajili ya kupewa maelekezo ya kazi alimtegeshea bosi wake uchawi, sasa haijulikani ni ili amdhuru au achukue cheo chake
..
Muda wote wakati mkurugenzi akiongeaa nilikuwa nimeshikwa na butwaa nisijue cha kusema. Nikiwa bado nimeduwaa yule mkurugenzi alinitupia swali
Hebu tueleze mwenzetu, lengo lako lilikuwa ni nini, kumdhuru bosi wako au unataka kuchukua cheo chake?
Nilijaribu kujitetea lakini sikupewa nafasi kwani nilianza kushambuliwa na yule afisa utumishi pamoja na wafanyakazi wenzangu kiasi kwamba nililazimika kukaa kimya. Yule mkurugenzi alinitaka nitoke ili wajadili swala langu faragha yeye na afisa utumishi.
Baadaye niliitwa na kupewa nafasi ya kujieleza nikiwa na mkurugenzi peke yetu, baada ya kumweleza ukweli kuhusu tatizo langu na mahali niliponunua zile dawa alinitaka nimpeleke ili akajiridhishe, nilimpeleka na akazungumza na yule mzee aliyeniuzia zile dawa na baada ya kupewa maelezo ambayo yalifananana na ya kwangu aliridhika na tuliporudi ofisini alimuita bosi wangu na wafanyakazi wenzangu na kuwapa ufafanuzi kuhusu ile miti shamba.
Ikumbukwe kwamba miaka hiyo ya 80. Mkoa wa Tanga ulikuwa unavuma kwa ushirikina, hivyo kwa sababu nilikuwa nimetokea mkoani Tanga, ilitosha kabisa kuthibitisha kwamba ule ulikuwa ni uchawi.
Nilirudishiwa dawa zangu na nikaendelea na kazi. Hata hivyo zile taarifa zilikuwa zimesambaa pale wizarani nikawa nakwepwa na kila mtu wakiwemo mabinti, na hata pale nilipokuwa nikijaribu kuwaomba mabinti mtoko walikuwa wananishusha na kunipandisha huku wakinijibu kifedhuli kwamba hawako tayari kuwa na mahusiano na mwanaume mlozi.
Nilikosa amani ikanilazimu kuacha kazi na kwenda zangu chuoni kusoma.