SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limesema Rais Jakaya Kikwete hana ubavu wala mamlaka ya kubatilisha au kuhalalisha mgomo ulioitishwa na shirikisho hilo.
Akitoa tamko la shirikisho hilo kwa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Nicholaus Mgaya, alisema chombo pekee chenye mamlaka ya kusitisha mgomo huo ni Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi tu.
Leo (jana) tumeona ni vizuri tukajibu baadhi ya hoja za Rais Kikwete alizozitoa kwenye mkutano wake na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, tunapenda kumwambia hana mamlaka ya kusitisha mgomo huu isipokuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi tu, alisema Mgaya.
Alisema TUCTA imesikitishwa na kauli ya Rais Kikwete kutangaza kusitisha mgomo huo kwa vile kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya ajira na mahusiano namba 6 ya mwaka 2004.
Alisema shirikisho hilo limeshangazwa na kauli ya Rais Kikwete kuwa mgomo huo uliitishwa katikati ya majadiliano kwani haina ukweli wowote.
Sasa tunashangaa kuona Rais Kikwete anasema mgomo huu umeitishwa katikati ya mazungumzo, jambo hili halina ukweli wowote hata kidogo, kwani tulitangaza kabla ya kurudi kwenye meza ya mazungumzo, alisema Mgaya.
Alikanusha kuwa mgomo huo ulikuwa ni ajenda ya viongozi wa shirikisho hilo, bali makubaliano yalifikiwa katika kikao cha mkutano mkuu ambacho kilitoa maagizo ya kusitisha mgomo.
Agizo la kuitisha mgomo shinikizi lake lilitolewa na Baraza Kuu kwa wafanyakazi nchi nzima, haukuwa uamuzi wa viongozi bali ni utekelezaji wa maagizo ya mkutano mkuu, sasa tunashangaa kuambiwa sisi waongo na wanafiki! alisema Mgaya.
Alisema jambo pekee ambalo Rais Kikwete alitakiwa kulifanya ni kutoa majibu ambayo yangeweza kutatua matatizo sugu ya wafanyakazi ambayo hayakuanza sasa kuliko kutoa vitisho.
Akifafanua kauli ya Rais Kikwete ya kuwafukuza kazi wafanyakazi watakaoshiriki mgomo na kuhimiza waajiri wafanye hivyo, ni kinyume cha kifungu cha 83 (1), (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na 6 ya mwaka 2004.
Alisema akiwa kiongozi na mjumbe wa Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO) hakuwahi kuhudhuria kikao chochote cha baraza hilo kikiwemo wa Aprili 14 mwaka huu wala kutia saini katika viwango vipya vya mishahara kama ilivyoelezwa na Rais katika hotuba yake.
Alisema kitendo cha Rais kudai hata wafanyakazi wakigoma miaka nane hawatalipwa ni ya kushtua na ya kukatisha tamaa kwa vile inaonyesha jinsi serikali isivyo na mipango wala mikakati madhubuti ya kuongeza pato la taifa.
Alisema kauli ya Kikwete, imekuwa ikikinzana na matamshi yake kutokana na ukweli kuwa anaposafiri nje ya nchi huwahimiza Watanzania walioko huko warudi nchini kujenga taifa lao wakati anasisitiza serikali haina uwezo wa kulipa mishahara!
Wiki iliyopita, Rais Kikwete aliwaita wazee wa mkoa wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Daimond Jubilee na kuwatuhumu viongozi wa TUCTA kuwa ni waongo, wanafiki na wazandaki kwa kuwapotosha wafanyakazi nchini ili wagome.