Ni vigumu kwa Marekani kutimiza lengo la kuongeza biashara na Afrika kwa kuilenga China

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG41172372825.jpg


Katika siku za karibuni Marekani imekuwa ikiendelea na juhudi zake za kukabiliana na kile inachoita ushawishi wa China barani Afrika, na kutafuta kila njia inayoona kuwa inaweza kusaidia kufanikisha lengo hilo. Hivi karibuni moja kati ya mambo ambayo Marekani imekuwa ikiyataja na kuhimiza kwa nguvu ni utekelezaji wa sheria yake namba S.1022 inayoitwa “kuongeza nafasi za ajira kwa Marekani kwa kuongeza uuzaji wa bidhaa barani Afrika 2021”

Sheria hii iliyopelekwa kwenye baraza la seneti la bunge la Marekani mwaka 2021, ina lengo la kuongeza thamani ya uuzaji wa bidhaa za Marekani barani Afrika kwa asilimia 200 ndani ya miaka 10, pamoja na malengo mengine, inataja wazi kuwa lengo lake ni kupambana na China. Kwenye ibara ya pili A, sehemu ya 4, 5 na 8, sheria hiyo imeitaja wazi jina la China, na kwamba lengo la mwisho la sheria hiyo ni kunufaisha makampuni ya Marekani madogo na yenye ukubwa wa kati, na kupambana na China barani Afrika.

Tukiangalia takwimu za biashara kati ya China na Afrika na kati ya Marekani na Afrika, tunaweza kuona mwaka 2000 mauzo ya nje ya Marekani yalichukua asilimia 14 ya soko la Afrika, huku ya China yakiwa asilimia 4, mwaka 2010 Marekani ilichukua asilimia 11 na China ilichukua asilimia 12, mabadiliko makubwa yalionekana mwaka jana ambapo Marekani ilikuwa na zaidi ya asilimia 5 huku China ikiwa na zaidi ya asilimia 20. Lakini mbali na takwimu hizi, benki ya EXIM ya Marekani imetaja kuwa fedha zilizowekezwa na China barani Afrika ni zaidi kuliko zilizowekezwa na nchi zote za G7 kwa pamoja.

Mara zote China imekuwa ikisema ushirikiano kati yake na nchi za Afrika haulengi upande wa tatu, kwani China siku zote imekuwa inapenda kuona bara la Afrika linapata maendeleo. Kwa hiyo sio bara la Afrika tu linalokaribisha hatua ya Marekani kuongeza biashara kati yake na nchi za Afrika, China pia imesema mara kwa mara hilo ni jambo zuri kama lengo lake ni maendeleo ya bara la Afrika.

Ni vema tukikumbuka kuwa biashara kati ya China na Afrika imepevuka katika vipindi mbalimbali. Ikiwa na msingi wa uhusiano mzuri wa kisiasa, biashara kati ya China na Afrika ilianza kati ya serikali na mashirika ya kiserikali ya pande mbili, na sasa imefika hadi ngazi ya watu wa kawaida kati ya pande mbili kwa hiyo msingi wake ni mkubwa sana.

Licha ya wazalishaji wa bidhaa za China kuzalisha bidhaa kwa mahitaji halisi na uwezo wa kiuchumi wa watu wa Afrika, undani wake umefikia hatua ya watu wa Afrika kuwasiliana moja kwa moja na wazalishaji wa bidhaa hata kuamua wataka bidhaa za namna gani.

Hata hivyo ni vema tukikumbuka kuwa kama kuna nchi ambayo ni vigumu kuamini sera na kauli zake kwa Afrika, basi ni Marekani. Sera za Rais Joe Biden kwa Afrika zinatia moyo, lakini ni miaka michache tu wakati wa utawala wa Rais Donald Trump sio tu bara la Afrika liliwekwa pembezoni kabisa kwenye sera za kidiplomasia za Marekani, bali yeye mwenyewe Donald Trump alifikia hatua ya kutumia lugha ya matusi kuhusu Afrika. Kutokana na mwenendo wa siasa za Marekani kuna uwezekano wa Donald Trump kuwa rais wa Marekani tena, na hilo likitokea sera na hata sheria ya “kuongeza nafasi za ajira kwa Marekani kwa kuongeza uuzaji wa bidhaa barani Afrika 2021” inaweza kuwekwa kapuni.

Kwa upande mwingine tukiangalia sera ya kidiplomasia ya China kwa Afrika, tunaona imekuwa ni tulivu na haibadiliki kuendana na mabadiliko ya uongozi wa rais au serikali ya China. Kama kukiwa na mabadiliko yoyote, ni mabadiliko yanayofanywa kwa pande mbili kukaa na kujadili, na ni mabadiliko yanayolenga kuboresha, kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana na sio kuulenga upande wa tatu.
 
Back
Top Bottom