NEMC yaagizwa kupunguza ada za vibali vya chuma chakavu

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupunguza ada za vibali vya chuma chakavu ili kuhamasisha wafanyabiashara wengi kushiriki katika biashara hiyo ambayo amesema inasaidia kuondoa taka za vyuma katika mazingira.

Alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa wadau wa biashara ya chuma chakavu, watendaji wa wizara yake, NEMC na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa kujadili changamoto zinazoikabili biashara hiyo na kupendekeza namna ya kuiboresha.

“Ada inayozotozwa sasa kwa wafanyabiashara wakubwa ya jumla ya Sh milioni 15 ili kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha chuma chakavu ni kubwa. Vilevile ada ya Sh milioni 1.5 ya mfanyabishara mdogo nayo ni kubwa kulinganisha na mazingira ya ufanyaji biashara yenyewe hapa nchini,” alisema.

Vibali hivyo hutolewa kila mwaka kwa wafanyabiashara hali ambayo inaongeza gharama kwa wafanyabiashara na kupunguza ushiriki wa wadau wengi katika biashara hiyo.

“Biashara hii imekuwa mkombozi mkubwa katika kutunza na kuhifadhi mazingira. Isitoshe taka hizo zinarejelezwa na kuwa malighafi za viwanda vya ndani au kusafirishwa nje ya nchi. Kuna kila sababu ya kupunguza tozo hizi ili biashara hii ifanyike vizuri,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka alisema mapendekezo yaliyotolewa na wadau pamoja na maagizo ya waziri yatafanyiwa kazi ili kuwapo kwa mazingira wezeshi katika ufanyaji wa bishara ya chuma chakavu nchini.

“Tutazipitia kanuni zetu na kurekebisha ada za vibali ili ziwe rafiki kwa wafanyabiashara jambo litakalochochea ukuaji wa biashara hii na kuifanya nchi kupiga hatua kiuchumi,” alisema.

Alisema biashara hiyo ikiratibiwa vizuri italeta matokeo chanya katika kutunza, kuhifadhi mazingira na pia kukuza kipato cha wananchi wanaojihusisha na biashara hiyo na pia pato la taifa litaongezeka kupitia kodi.

Mdau wa chuma Chakavu, Robert Yohana alisema hatua zinazochukuliwa na serikali zina manufaa kwa wadau wa biashara hiyo na nchi kwa ujumla.
 
Back
Top Bottom