NEMC na JMAT wawaelewesha Viongozi wa Dini juu ya Sauti zilizozidi. Waziri Mkuu Majaliwa atoa Maagizo 8

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) leo 12 Juni 2023 wameendesha Kongamano la Kitaifa la Kujengewa uelewa kwa viongozi wa Dini na Kimila juu ya Athari za Sauti zilizozidi Viwango Katika Nyumba za Ibada kwenye Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre(JNICC) Mkoani Dar Es Salaam.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ndiye aliyekuwa Mgeni rasmi na ametumia Wasaa kuwaeleza Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara, wakae na Mabaraza ya Biashara na Wamiliki wa kumbi za Starehe katika mikoa yao kwa madhumuni ya kutafuta muafaka wa pamoja katika utekelezaji wa sheria, kanuni, mwongozo kuhusu udhibiti wa athari zitokanazo na sauti zilizozidi viwango.

Waziri Mkuu amezielekeza Idara za Mipangomiji katika halmashauri za wilaya zote nchini zitenge maeneo ya ujenzi wa nyumba za ibada kama wanavyotenga maeneo ya taasisi nyingine.

Amesema ipo miongozo inayosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayohusu masuala ya usimamizi wa mipango miji. “Nasisitiza toeni miongozo mahsusi ya mipango ya matumizi ya ardhi .”

“Kwa upande wa udhibiti wa sauti zilizozidi, kila mamlaka iliyotoa vibali au leseni ya shughuli au biashara, zifuatilie mwenendo wa matumizi ya leseni hizo. Nasisitiza kuwa kila mamlaka itimize wajibu wake kulingana na maelekezo yaliyimo katika Mwongozo wa Uthibiti wa Uchafuzi wa Mazingira Utokanao na Kelele na Mitetemo uliotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.”

“Leo kuna kongamano la kitaifa linaloratibiwa na JMAT, NEMC wekeni mpango wa kufanya makongamano kama haya hadi katika ngazi ya mikoa ili jamii iwe na uelewa wa pamoja kuhusu athari za viwango vya sauti vinavyozidi. Aidha, toeni elimu kwa umma ili wajue viwango halisi vya sauti vinavyostahili wakati wa mchana na wakati wa usiku.”

Akizungumzia kuhusu wamiliki wa majengo, Waziri Mkuu amewataka wafanye tathmini ya athari ya mazingira kwa watu wanaotumia majengo hayo pamoja na wakazi wa jirani na majengo hayo kwa lengo la kubaini madhara kwa watumiaji wa majengo hayo na jamii inayozunguka.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa dini, wanaoshiriki katika kongamano hilo waendelee kuwa vielelezo na mabalozi wazuri wa kufikisha yale mambo mazuri yanayowasilishwa katika kongamano hilo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema madhumuni ya kongamano hilo ni kuwakutanisha pamoja viongozi wa dini na mila ili kutoa elimu ya athari za sauti zilizozidi viwango kutoka kwenye nyumba za ibada na jamii.

Amesema kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015 zimeainisha viwango vinavyoruhusiwa katika maeneo ya makazi, nyumba za ibada, biashara, viwanda na hospitali kwa ajili ya jamii, mfano viwango vya sauti vinavyoruhusiwa katika nyumba za ibada zilizopo maeneo ya makazi ni dBA 60 wakati wa mchana na usiku dBA 40.

Amesema sauti zinazozidi viwango katika nyumba za ibada zinaweza kuathiri afya za waumini waliopo kwenye nyumba za ibada na maeneo ya jirani na kusababisha matatizo ya kusikia, usingizi na kuathiri uwezo wa kufanya kazi pamoja na kusababisha migogoro kati ya wakazi na viongozi au waumini.

Dkt. Gwamaka amesema NEMC itaendelea kusimamia kwa ukamilifu uzingatiaji na utekelezaji wa sheria na kanuni zake kwa kuandaa semina, warsha na mikutano ili kujenga uelewa mpana zaidi kwa jamii na wadau kadiri inavyohitajika. “Nitoe wito kwa viongozi wa dini tushirikiane katika utekelezaji wa sheria hizi ili kuboresha ustawi wa mazingira yetu.”
IMG-20230612-WA0009.jpg
IMG-20230612-WA0006.jpg
IMG-20230612-WA0020.jpg
IMG-20230612-WA0015.jpg
IMG-20230612-WA0017.jpg
IMG-20230612-WA0022.jpg
IMG-20230612-WA0018.jpg
IMG-20230612-WA0023.jpg
IMG-20230612-WA0016.jpg
IMG-20230612-WA0014.jpg
IMG-20230612-WA0007.jpg
 
NEMC hakika wamejipanga kuhusu kelele za Makanisani na Misikitini. Mungu awabariki. Viongozi wa dini wanataka eti mambo ya dini tusiseme kelele wala Sauti chafuzi bali tuseme sauti zilizozidi viwango. Sasa watu wa dini acheni zidisha Viwango
 
Back
Top Bottom