Hii inaweza kuwa miongoni mwa mada nzuri sana kuletwa hapa jukwaani, wiki hii. Kwa kweli ukitafakari kwa makini unaweza kubaini kuwa migogoro na matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu yanasababishwa na wasomi. Magufuli juzi amesema wazee ndio wameifikisha hapa nchi hii, lakini bila shaka wazee hao aliowalenga sio wale mbumbumbu, ni wazee wasomi. Yeye JPM anaona suluhisho linaweza kuwa vijana, na anasema ndio maana katika awamu yake ameamua awape nafasi vijana wasomi.
Nina wasiwasi na mtazamo wa JPM. Leo ukifanya utafiti kidogo tu katika vyuo vikuu vyetu unaweza kubaini jambo moja kubwa-vijana wanaharibiwa akili wakiwa bado wakiwa vyuoni, na wanapotoka huko hawana tena mawazo na mitazamo ya kizalendo, bali wanakuwa wabinafsi wanaojiangalia wao wenyewe. Hali hii ni matokeo ya vijana hao kuingizwa katika mifumo ya 'kihalifu' ya kutumikia vyama vya kisiasa badala ya kutumikia nchi.
Wapo vijana wazuri tu, wanatoka vijijini wakiwa na uchungu wa kubadilisha jamii zao pindi wakimaliza masomo yao, lakini wanapofika vyuoni wanakutana na hadaa; wanaanza kushawishiwa kujiunga na makundi ya siasa za kihalifu kwa ahadi ya pesa na ajira nzuri baada ya masomo. Nani asiyefahamu tatizo la ajira hapa nchini? Mifumo yenyewe ya maisha vyuoni inawafanya washawishike kwa urahisi na kubadilisha ndoto zao. Wakati awali walikuwa wakiitazama jamii yao, ghafla wanaanza kujitazama wao wenyewe!
Tatizo ni kubwa sana, mfumo wa elimu yetu nao unatufanya tusiwe rahisi kukwepa mbinu za uhalifu unaofanywa kupitia siasa za vyama. Hivi unaweza kuzungumziaje pale kijana msomi aliyehitimu chuo kikuu anapokuja hapa JF, kwa mfano, kutetea ufisadi wa Lugumi vs polisi au ufisadi mwingine katika taifa, kwa sababu tu yeye yuko katika foleni ya kusubiri ahadi ya ajira? Tunaona hapa jinsi vijana wasomi wanavyojitoa akili kutetea hata mambo ya kijinga yanayofanywa na vyama wanavyovishabikia!
Leo mijadala mingi, rasmi na isiyo rasmi, imepoteza sura ya uzalendo na badala yake inabeba sura ya vyama. Tuliona kwenye Bunge la Katiba jinsi wasomi wa kiwango cha madaktari walivyokuwa wajitoa akili wakawa wanajadili mambo kwa maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya taifa. Baada ya Bunge hilo inafahamika nini kilitokea kwa wasomi waliokuwa wanatetea upuuzi!
Ni vigumu kujinasua katika hali hiii. Na ugumu unazidi kuongezeka unapoona hata viongozi wa dini wanaingizwa katika mifumo ya "kihalifu" ya kisiasa. Kinachobakia ni kuwa na nchi ya unafiki, unafiki, unafiki kila mahali...