Stories of Change - 2023 Competition

Calvin Mmari

New Member
Jun 1, 2023
2
3
Usichomoe! "Nimekwambia usichomoe kabla haijafika mwisho, aya irudishe alafu upunguze sauti kidogo saivi ni usiku tusisumbue majirani"

Muda wote huo baba kwani huchoki?
"Hapana hadi ifike mwisho ndo nitakuruhusu uichomoe"

Hayo yalikua ni mazungumzo kati ya baba na mwanae wakizozana baada ya mtoto kuchomoa flashi kwenye redio ambayo baba yake alikua akisikiliza kila ilipofika jioni.

Nakumbuka nikiwa mdogo nilikua na jirani yangu ambaye alikua pia ni rafiki yangu wa karibu sana ambaye aliitwa Kevi, muda mwingi nilikua nashinda kwao tukicheza mziki siku za mwisho wa wiki na jioni tukitoka shule. Baba yake Kevi alikua anapenda sana siasa na alikua pia ni mwenyekiti wa kijiji chetu. Jioni akitoka kazini alikua anapenda sana kusikiliza redio, alikua ana flashi yake ambayo alikua ameijaza hotuba zilizorekodiwa za Mwalimu Nyerere. Wakati mwingine tulikua tunakereka sana baba Kevi akirudi nyumbani maana alikua anatunyang'anya redio na kuweka flashi yake na kusikiliza kwa muda mrefu. Tulikua tunakasirika sana lakini alikua akitulazimisha na sisi kusikiliza hizo hotuba akidai kwamba anatufundisha somo la uraia kwa vitendo. Alikua akisikiliza hotuba zote hadi mwisho bila kuacha neno hata moja. Hotuba nyingi za Mwalimu nyerere alizokua akisikiliza zilihusu Wajibu wa viongozi na Wananchi kwa ujumla. Mwalimu Nyerere alikua akihimiza umuhimu wa uwajibikaji kwa manufaa ya taifa kwa ujumla, hotuba zake zilikua zikidadavua zaidi uhusiano uliopo kati ya uwajibikaji na maendeleo.

Baada ya hotuba ya kwanza kuisha uvumilivu ulinishinda nikaamua kuondoka kwa hasira nirudi nyumbani, lakini ghafla mama Kevi akatoka jikoni akaniita na kuniambia

"usiondoke subiri kidogo ule, alafu baba kevi
atakusindikiza nyumbani"

Kwa ile harufu iliyokuwa ikitoka pale jikoni ilinijulisha kwamba mama Kevi leo kapika pilau, na nilivyokua napenda pilau basi taratibu nikarudi ndani kusubiri huku nikiendelea kusikiliza hotuba ya Mwalimu Nyerere. Nilipofika ndani nikakuta hotuba ya pili ndo inaanza ambapo mwalimu Nyerere alikua akielezea misingi ya maendeleo na umuhimu wa uwajibikaji kwa maendeleo ya taifa. Aliwahusia watanzania kuwa uwajibikaji ndo msingi wa utawala bora na kusisitiza zaidi kila kiongozi atimize wajibu wake ipasavyo na kila mwananchi awajibike kwa nafasi yake huku akishikilia zaidi kuwa hakuna maendeleo pasipo uwajibikaji na hakuna utawala ulio bora usiozingatia na kufatilia uwajibikaji wa viongozi na wananchi kwa ujumla. Mwisho alimaliza kwa kusema "Ufisadi ni adui wa haki, maendeleo na utawala bora"

Siku iliyofuata baada ya kutoka shule tukawahi mapema tukachukua redio tukaihamishia nyumbani kwetu, na flashi tukaenda kuijaza nyimbo za Matonya na Lady jay dee ikawa kila siku tunaitumia kusikilizia miziki, tukamdanganya baba kevi hatujachukua redio, lakini baba Kevi alikua mtaratibu na mwenye busara, akatambua kabisa tulichokifanya, akatikisa kichwa akasema "mkumbuke kusoma pia" basi baba Kevi akawa anatumia simu yake kusikilizia redio, zaidi alikua anasikiliza TBC Taifa kusikiliza nukuu na hotuba za Baba wa Taifa kila ilipofika saa tatu usiku.

Baada ya kukua, nikatambua zaidi kuhusu wajibu wangu mimi kama mwananchi na wajibu wa viongozi pia.
Na sasa natambua yakuwa uwajibikaji ni hali ya viongozi, wananchi na taasisi mbalimbali kutimiza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria zote za nchi. Pia kiongozi anapaswa kuwa tayari kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamana aliyopewa.

Ni wazi kuwa uwajibikaji ni nguzo muhimu ya utawala bora na kila kiongozi anapaswa kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu, na pia kuweka mifumo ya ukaguzi na uwajibikaji, na kuchukua hatua stahiki dhidi ya ufisadi pamoja na ubadhirifu wa mali za umma kila inapotokea.

Hivyo basi, redio ya jirani ilinifunza mengi na kunipa utambuzi wa mambo mbalimbali na kutambua yakuwa ili kuwepo na utawala bora pamoja na uwajibikaji kuna mambo muhimu yanatakiwa kufanyika na kutekelezwa, mambo hayo ni kama yafuatayo;

Kwanza, Uwazi ni nguzo muhimu sana inayochochea utawala bora, serikali pamoja na taasisi za umma zinapaswa kuhakikisha kuwa wananchi wanafahamu kila kitu kinachoendelea nchini hususani katika suala zima la matumizi ya rasilimali za umma, wananchi wanatakiwa kupata hati za bajeti, taarifa za mapato na matumizi ili kuhakikisha mali ya umma imetumika ipasavyo na kurahisa ufutiliaji wa ubadhirifu wa mali ya umma, mfano ufisadi.

Pili, Uhuru wa vyombo vya habari una nafasi kubwa kwenye suala zima la kuhakikiasha uwajibikaji na utawala bora unakuwepo ndani ya nchi. Uhuru wa vyombo vya habari unasaidia kufichua na kuripoti vitendo visivyo vya haki, upindishaji wa sheria, kutowajibika kwa viongozi na pia ubadhirifu wa rasilimali za umma.

Tatu, Kuhakikisha ushirikishwaji wa wananchi katika kufanya maamuzi. Shughuli za kisiasa na kuimarisha mifumo ya kidemokrasia. Utawala bora unaenda sambamba na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za kisiasa na kimaendeleo, pia nchi inapaswa kuunda mifumo maridhawa ya kisiasa mfano uchaguzi ulio huru na wa haki.

Nne, Kuhakikisha uongozi unaundwa na viongozi wenye sifa stahiki, wazalendendo na wajibikaji. Uongozi sio suala dogo hivyo basi, ili kuhakikisha kuna utawala bora na uwajibikaji ni wajibu wa wananchi kuchagua viongozi wenye uwezo na sifa zote na pia teuzi zizingatie vigezo ili kuchochea utawala bora na uwajibikaji.

Tano, Kuunda sheria mathubuti zinazopinga rushwa na ubadhirifu wa rasilimali za umma, serikali inapaswa kutekeleza kikamilifu sheria hizo ili kutokomeza rushwa na matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali za umma. Kuwepo kwa sheria madhubuti zitasaidia kuchochea uwajibikaji wa viongozi na hatimaye utawala bora.

Sita, Kutetea na kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa ipasavyo na kufuatilia vitendo vyote vinavyoashiria kuwepo kwa uvunjifu wa haki za binadamu.

Saba, Ushirikiano na muingiliano wa kimataifa pia una mchango mkubwa sana kwenye kuhakikisha kunakuwepo na utawala bora ndani ya nchi. Nchi inapaswa kushirikiana na taasisi za kimataifa, kubadilishana uzoefu, na kusaidiana katika kuimarisha mifumo ya utawala. Ushirikiano wa kimataifa ni nyenzo muhimu kwenye kukuza maendeleo na kuimarisha mifumo ya kiutawala na kuinua demokrasia ndani ya nchi.

Mwisho, Elimu ya umma inapaswa kuhamasishwa ili kujenga uelewa kuhusu utawala bora na uwajibikaji ili kuchochea maendeleo na kujenga jamii imara, wananchi wanapokuwa na uelewa wa kutosha juu ya haki zao, wajibu wao, na jinsi ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo ikiwemo shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi inarahisisha ujenzi wa nchi yenye maendeleo na utawala bora. "Kama viongozi wote wangekua na mimi utotoni basi tungejifunza kwa pamoja yote hayo, na mengine mengi kuhusu uwajibikaji.

Ila bado muda upo ni vyema kila kiongozi na mwananchi akatimiza wajibu wake ili kuchochea utawala bora.

 
Back
Top Bottom