Tanzania Daima
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, amesema kukithiri kwa rushwa na ufisadi serikalini kunatokana na kuwa na viongozi waliosoma, lakini hawakuelimika.
Mwinyi alitoa kauli hiyo jana wakati wa sherehe za mahafali ya kidato cha nne na sita kwa wanafunzi wa Shule ya Kiislamu ya Markaz, iliyopo Chang'ombe, Dar es salaam.
"Kuna matatizo makubwa ya uongozi katika nchi yetu. Tumevamiwa na maovu mengi, ujambazi wa kutumia nguvu, uongo, ulaghai na ujanja. Karibu kila sekta ya maendeleo ya jamii inakabiliwa na tatizo la kukosa viongozi waadilifu. Kuna matatizo ya uongozi katika mpira, taasisi mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
"Na haya tunayoyasoma na kuyasikia kwenye vyombo vya habari kuhusu kukithiri kwa maovu serikalini, yanatokana na kuwa na viongozi ambao wamesoma lakini hawakuelimika. Wangeelimika wasingelitenda haya tunayoyashuhudia na kuyasikia leo," alisema.
Alisema viongozi waliosoma na kuelimika ni waadilifu kwa sababu elimu ni nguvu ya ajabu ambayo mtu yeyote anayeipata humwingia ndani ya moyo wake na kumbadilisha kitabia.
"Viongozi walioelimika ni waadilifu, wana msimamo, huruma, ubinadamu, wenye upendo kwa wanaowaongoza kama wanavyojipenda wao," alibainisha mzee Mwinyi.
Kutokana na hali hiyo, Mwinyi aliwasihi wahitimu hao kuongeza bidii katika masomo yao ya juu ili waweze kuelimika vizuri na kuziba pengo la uongozi lililopo sasa nchini kwa kulitumikia taifa kwa uadilifu mkubwa.
Akizungumzia umuhimu na faida za elimu, Mwinyi alisema elimu humsaidia mtu aliyeipata kumudu mambo ambayo awali hakuyaweza na hivyo kuweza kuboresha maisha yake.
Alibainisha kuwa ujinga ni adui namba moja wa kila jamii, kwani maadui wengine kama umaskini na maradhi hutokana kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa elimu.
"Tuna maadui watatu nchini - ujinga, umaskini na maradhi. Hata hivyo, mimi naamini ujinga ndiyo adui mkubwa na naweza kusema kuwa ni mama wa adui wengine wote, lazima tupigane vita vya jihadi kumtokomeza adui ujinga," alisema.
Alisema elimu ni safari ndefu ambayo mtu huianza mara tu anapozaliwa na inakoma pale anapofariki dunia.
Mwinyi aliwashauri wahitimu kusoma kwa bidii elimu zote, elimu ya duniani na ile ya dini na kutoitelekeza elimu ya dunia kwa sababu elimu hiyo ni muhimu mno kwa maisha ya bora ya duniani.
Kauli ya Mwinyi kuhusu viongozi wa umma kukosa uadilifu, imekuja wakati viongozi wengi serikalini wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali za ulaji rushwa na ufisadi, wakati baadhi yao wamelazimika kujiuzulu uongozi.
My Take:
Kwanini Mzee Mwinyi naye asipate nafasi kama aliyopata Mwalimu Mei Mosi Mbeya ya kuhutubia Taifa? Hakuna kasherehe kakitaifa ambako Mzee wetu angeweza kuzungumzia masuala muhimu yanayolikabili Taifa hadi tumsikie anazungumzie pembezoni? Kama kuna mtu anahutuba yake hiyo ni vizuri tungeipata.
NB: Kuchomekea kizenji: NI kutuma ujumbe mzito kwa kucheza na lugha kama alivyo fanya mzee Mwinyi "kusoma na kuelemika". M.M. Original