Mbowe achangia mil. 10/- KKKT
na Rodrick Mushi, Siha
MBUNGE wa Hai, Freeman Mbowe, amechanga sh milioni 10 kwenye harambee ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Usharika wa Sanya Juu, kwa ajili ya kununulia gari la kutoa huduma za neno la Mungu kwa kikundi cha Uamsho.
Akizungumza wakati wa harambee hiyo, Mbowe alisema inapaswa ifike mahali wananchi wasitoe nafasi kwa kazi za kibinadamu zikachafua kazi ya Mungu na kuongeza kuwa shida imewafanya watu wengi kufanya matendo yasiyompendeza Mungu kwa ajili ya kujitafutia kipato.
Alisema vitendo vya ushirikina vimekithiri nchini huku viongozi wakubwa wa nchi wanaotegemewa wakitegemea kuongozwa na vitendo vya kishirikina, hususan wabunge.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa alisema zaidi ya asilimia 80 ya wabunge nchini wanategemea vitendo vya kishirikina na wengi wanatoka vyama mbalimbali vya siasa.
Shida imewafanya wananchi kujiingiza katika vitendo viovu ikiwamo kuanzisha makanisa, ili kujipatia vipato, viongozi wa dini tunawategemea katika mambo mengi ya nchi hii ikiwamo kusaidia kupatikana kwa viongozi wanaoweza kuiongoza nchi hii, alisema Mbowe.
Zaidi ya sh milioni 14 zilipatikana kwa ajili ya ununuzi wa gari hilo, ambapo lengo lilikuwa ni kukusanya sh milioni 50.
Mbowe achangia mil. 10/- KKKT