Mchungaji amekaa na kutafakari sana, anzia enzi za Mzee Sawaya, akaja sijui Sarakikya, Mzena, Kitine, Mahiga, Kombe, Apson na sasa Othman. Angalia mafunzo tuliyopata kutoka kwa CIA, FBI, MI5, MI6, KGB, Surete, Mossad, Shin Bet, BOSS, MSS, DGI-Cuba, Mukhabarat, ISI na kwingineko.
Leo miaka karibu 50 tangu tujitawale, TISS ni kama kichwa cha mwendawazimu, ni Taasisi inayoonyesha ama ni kuchanganyikiwa kwa hali ya juu au imeingiliwa kwa hali ya juu kiasi kuwa hata zile hekaya za kusema walikuwa wakiwabana Makaburu zinaonekana kichekesho!
Nasikitika kusema kuwa katika historia yenu, jambo la maana mlilowahi kufanya na kulipa Taifa letu sifa ni mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika pekee, mengine yote mliyoyafanya ni batili, tupu na bure!
Kama kweli mngekuwa ni chombo makini, basi leo hii Tanzania ingekuwa Taifa kubwa linalojitegemea, lenye uwezo wa kujitosheleza, lenye viongozi wanaojiamini na Watanzania wenye kujiamini, kujituma na Uzalendo wa kweli kwa Taifa!
Mnachekesha sana mnapokazana kutafuta nani kasema nini kuhusu Kiongozi fulani au kuanza kusaili viongozi na wanasiasa nia zao za kuanzisha vyama au kuwa ndani ya siasa. Zaidi mmechekesha pale mlipoanza kuhoji nia ya Watanzania kuchangishana na kuwasaidia waliopata maafa huko Kilosa!
Lakini tatizo langu na nyie si huku kufuatanafuatana kama wajinga na kutaka kujua Mchungaji anakaa wapi au anafananaje.
Tatizo langu ni kuwa nyinyi kama Taasisi pekee iliyokuwa na uwezo mkubwa kuliko nyingine Tanzania kifedha, kiufanisi, kiutendaji na uwezo wa kuwa na nyenzo nyingi, mmeshindwa kulisaidia Taifa letu likaweza kupiga hatua mbele, na badala yake mnafurahia karaha na watu kutaabika.
Je ni vipande vingapi vya fedha mmenunuliwa?
Iweje wakati wa vita vya ukombozzi mliweza kufuatilia kila aina ya uhujumu ambao ulipangwa na Kaburu na Mkowezi Ian Smith, lakini leo mnaifagilia Richmond, EPA, Rites. Rada na hata kina Barrick?
NI vipi leo Taifa letu kila mara linakutwa mguu pande katika mambo mengi ya maana ya kijamii, kisiasa na kiuchumi lakini mlikuwa tayari kupeleka timu nzima Uingereza kumkamata Ze Utamu au kukasirika mliposikia tetesi eti kuna mtu ana picha za Rais akiwa Uchi?
Utaalamu na Ukali wenu mbona ni butu pale Taifa letu linapoendelea kunyonywa na kunyanyaswa na Ukoloni mamboleo na Ubepari Uchwara?
Je nanyi mko njia panda baada ya Azimio la Zanzibar na Mageuzi kuwa hamjui wajibu wenu au ni upande gani muelekee?
Je mnahitaji watu na damu mpya ya kuwapa mawazo mapya na mipango mipya na kufanya msukwe upya ili Tanzania iweze kupiga hatua mbele?
Ikiwa leo hii, kila mtu anaogopa TISS, kisa watakufanyia kitu mbaya au utasota milele, je kweli nyinyi wajibu wenu ni Kumlinda na Kumtumikia Mtanzania au ni chombo cha kuwanyanyasa Watanzania?
Mmejisahau vipi baada ya kuvunjika kwa vita baridi kuwa mpaka leo mmeshindwa kufanya mapinduzi ya ndani na kuleta mabadiliko hata katia mfumo wetu uchwara wa kibepari?
Mchezo wa kufuatilia watu kisa wameongea jambo fulani ambalo hamlipendi ni kitu cha kizamani. Mambo ya kutisha watu, tena wa nchi yenu yamepitwa na wakati!
Tanzania ya leo inahitaji kuwa na chombo kama TISS kinachojua wajibu wake kwa manufaa ya Taifa na si Chama au mtu mmoja. Kiapo chenu (niliwahi kuwauliza mwaka jana au juzi mnaapaje) ni kwa ajili ya Katiba ya Tanzania na si Chama, Kabila, Jinsia, Dini au tabaka la kimapato.
Siogopi wala sijiumiumi nitawaambia ukweli, nyinyi ndio chimbuko la Matatizo ya Tanzania na Kikwazo cha Maendeleo ya Taifa letu.
Mkitaka majadiliano, tuendelee nitumieni maswali yenu rev.kishoka@jamiiforums.com au yaulizeni hapa nitayajibu na kuwapasha namna mpya ya kujifua na kuweza kubadilisha sura ya Taifa letu, tukarudi kwenye ile hadhi tuliyokuwa nayo wakati wa Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Kabla hamjaharibu sana, jiulizeni ni kitu gani mnachfanya ambacho kimemfanya Mchungaji aanze kuwaongelea tena!