Kwa nini mnaendelea kuwa walaghai, wadanganyifu, wajeuri na wenye kiburi?
Hivi mnafikiri mnamdanganya nani? Labda mnajidanganya wenyewe kuamini kuwa mnachokifanya na kutamka, basi ni heri ili kutuziba midomo na kutupofusha.
Mlaaniwe kwa Uongo wenu. Mlaaniwe kwa Kiburi na Majivuno yenu. Laana hizi zikae hata na vizazi vyenu vinne, kama laana za Mungu alizoacha kwa vizazi vinne.
Nyinyi mnaendelea kutufanya na kutufikiria sisi ni mabwege? Ni lipi tulilowakosea mpaka mtudharau kiasi hicho?
Hasira zetu na gadhabu yetu, italipwa na Mungu.
Mnakasirika mnaposikia tukiwadai mtupe ukweli, mnatutafuta si kutushukuru, bali kututakia mabaya na maovu, eti tunawaharibia.
Ni nani kati yetu sisi na nyie waliomharibia mwenziwe?
Laiti mngelijua kuwa kama mngekuwa wanyenyekevu, wasikivu na wenye kujirudi, basi mngekuja mbele zetu na kukiri makosa yenu ya Uzembe na Tamaa, na sisi kama Taifa, Watanzania ambao tunasifika kwa Amani, Mshikamano na Utulivu, tungewasikiliza na kama kawaida ya Watanzania tungewasamehe mliyotukosea.
Lakini mnajikuza na kujitweza kuwa nyinyi ni Miungu, msio na makosa, na kila mlichofanya na mnachoendelea kukifanya ni sahihi na halali, zaidi ni halali yenu kuendelea kuwa wagereshaji, waongo, wazembe, wasaliti, wapenda makuu na msio na hata soni au haya mkaona aibu kwa mambo mliyoyafanya, mnayoyafanya na mnayotarajia kuyafanya.
Nashangaa sana, na tena sana kusikia mwaendelea kumtafuta Mchungaji.
Kosa lake ni lipi? mbona wale ambao ni wahalifu au waliotuhumiwa kuwa wahalifu bado "wanapeta" na kila siku mnatupiga "kiswahili" kuwa "jambo kubwa sana, ushahidi hautoshi"?
Mnatuambia kwa kujikanganya kuwa Hazina yetu pale Benki Kuu imekuwa ikichunwa tangu mwaka 1997 au mapema. Ni miaka kumi sasa bado hamjapata ushahidi wa kutosha kujua kilichotokea na waliohusika?
Mwatamka kuwa Meremeta ni mambo ya Usalama wa Nchi na Jeshi, hata Kagoda nayo mlitamka ni masuala ya Usalama wa Taifa.
Najiuliza, ni lini tulikuwa na hali ya hatari ambayo ilisababisha Jeshi na Usalama kujipatia pesa za uendeshaji kinyemela bila kuhusisha mamlaka husika kama Bunge?
Je anayehatarisha Usalama wa Taifa letu mpaka mkachotewa pesa hovyo bila viambatanishi vya ushahidi, na stakabadhi ni nani? Kama Usalama wa Taifa uko mashakani, mbona hamtuambii ili nasi tuanze kujifunga kibwebwe kujiandaa na hata kujitolea kulilinda Taifa letu kwa umakini zaidi?
Ni lini mlitangaza hali ya hatari?
Je nyie wote hamkuwapo dunia hii siku ile mwaka 1977 wakati Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (naona nywele zinawasiamama mkisikia hili jina) alipotutangazia Taifa la Tanzania na Dunia nzima rasmi kuwa tunaingia vitani, kwenda kupigana na Nduli Iddi Amini ili tukomboe nchi yetu?
Alisema "uwezo tunao, nia tunayo, sababu tunayo" mbona hakufanya siri kama nyinyi mnavyotuzuga kila mara kuwa kuna "Unyeti"?
Mkatuletea miradi hewa ya nishati, rada ya hongo, ndege ya raisi mchoko, mmeuza Shirika la Reli kwa Baniani mbaya, mmekodisha dege kubwa mbalo mnalilipia huku halina mabawa, kisa hadhi ya Taifa.
Ni hadhi gani hiyo na majigambo yenye manufaa gani ikiwa Wananchi bado wako uchi, wanakufa njaa na magonjwa ni kila siku?
Ni hadhi gani, tununuliwe Chandarua na Rais mgeni aliyekuja tutembelea? je tumekosa kabisa mipango na hata fungu kupigana na maradhi?
Siri ya mafanikio yenu tunaijua.
Ni Uroho wa kupindukia kutumia migongo yetu na kuendelea kutudhalilisha kwa kutufanya wote tuonekane omba omba, saidia masikini!
Mmeimarisha misingi ya Unyonge na Umasikini wa Mtanzania kwa kuendelea kuwa omba omba, kuwa na sheria mbovu, mikataba ya kianaharamu na wageni wakazi-wawekezaji, kukosa upeo wa kweli na dhamira ya kweli kutuleta maendeleo kwa kutumia dhamana na hatamu tulizowapa.
Hatuwezi kuendelea kumlaumu Mkoloni au Mwekezaji wakati mla nchi ni wewe, yeye na yule, nyinyi, akina nyie!
Ni nyinyi ambao mnadai mna mwamsho wa kutetea maslahi yetu, lakini ni matumbo, mapaja na matako yenu ambayo yanaendelea kunona mpaka mnashindwa kupumua, huku sisi tukikondeana na kupangusa nzi na mbu, tukifukuzana na mbwa kugombea makombo!
Hamna aibu miaka yote ya Uongozi na Uwakilishi kuwa Asilimia 31% ya Watanzania watu wazima hawajui kusoma na kuandika?
Hamuoni haya Mtanzania kwa wastani anaishi kwa chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku?
Haliwasumbui kuwa Asilimia 52% ya Watanzania wanaishi katika Umasikini wa kutupa na hata hawana uhakika wa kesho, licha ya kujua watamalizaje leo na kushangaa waliwezaje jana?
Mmelitia Taifa letu aibu sana, mnatufadhaisha kwa ujasiri wenu kiburi na uchimvi.
Tunapowapigia kelele, au wengine wenu wanaoamka kutoka kwenye limbwata la Utamu na kuhoji kilichootokea, mnapenyeza maneno na kutumia makuwadi wenu kutunyamazisha na kudai eti ni masuala ya Kikundi chenu mkiwa upenuni mmejificha kujadili machungu ya uzazi wetu!
Ndimi zenu, zitawafunga, kama mnavyoendelea kujikanganya kila siku kwa hata kukosa umoja na kutoa kauli moja.
Nimewaasa, hasira zetu zimefika masikioni kwa aliyetupa hii ardhi na maliasili iliyomo.
Endeleeni kutupuuza na kutudanganya, mwisho wa mnayoyatenda hauko mbali sana, kama Usiku wa Kiza, mtashtukia siku moja mkiwa uchi wa mnyama kuwa kilio chetu kimesikika. Ni siku hiyo ambao macho, masikio na midomo yenu viyafunguka na kung'amua siku zote mmekuwa si waadilifu, ni waongo, waroho, wadhalimu wahujumu, wazembe na mafisadi.
Maonyo yetu na hata wema wetu hautakuwa na maana tena saa hiyo itakapowadia. Kaeni chonjo, saa mbaya inakuja, tubuni makosa yenu, tutawasamehe na kuwakaribisha tuanze kulijenga upya Taifa letu na kurutubisha sifa na hadhi ya kweli.
Yaliyowakuta Mobutu, Marcos, Pinochet, Bokassa, Amin, Noriega, Pol Pot, Ceausescu, Saddam, Marie Antoinette na wengine ambao walikuwa ni watawala kama nyinyi, yatawakuta, tena yanaweza kuwa mabaya mno, ombeni Mungu awachukue, kabla ya ghadhabu za Walalahoi, kuamka mithili ya vita vya Maji Maji, Mau Mau na kwingine kote kung'oa wakoloni.
Mnegro mmoja Gil Scott- Heron alisema " Revolution will not be Televised" hamjui siku, wala saa yatakapowafikia, mapinduzi kuondokana na uharamia wenu yanakuja, tunaanza kwa sala na maneno, mkitupuuza, tutafuatia Demokrasia.
Saa ya Ukombozi na Kuokoka ni Sasa, endeleeni kunitafuta, nipo nimejaa tele kama pishi la Mchele!