Muuaji Shoga Aliyepukutisha Wenzake...! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Muuaji Shoga Aliyepukutisha Wenzake...!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Jan 20, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Jan 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280

  imgGianni%20Versace4.jpg
  Gianni Versace

  8How+many+supermodels+can+you+spot+Gianni+Versace+feels+the+love+of+the+worlds+most+beautiful+wo.jpg
  Akiwa na wanamitindo Maarufu

  imgGianni%20Versace3.jpg
  Hayati Princess Diana Na Sir Elton John walimlilia

  HBm3juvT_Pxgen_r_467xA.jpg
  Akiwa na Naomi Campbell na Cindy Crawford

  andrew cunanan.jpg
  Muuaji Andrew Cunanan katika mionekano tofauti

  W
  akati mbunifu maarufu wa mavazi duniani, Gianni Versace alipouawa kwa kupigwa risasi nje ya mlango wa nyumba yake katika jiji la Miami, nchini Marekani, polisi walituhumu moja kwa moja kwamba ni mauaji ya kupangwa. Lakini hata hivyo baadaye waliachana na nadharia hiyo na kumgeukia mtuhumiwa mmoja, aliyekuwa akiendesha mauaji ya watu mbalimbali katika majimbo kadhaa nchini Marekani.

  Ilikuwa ni asubuhi ya Julai 15, 1997, kama kawaida yake, Gianni Versace alitoka kwenye jumba lake la kifahari, lililopo ufukweni na kuelekea kwenye mghahawa uliopo karibu na hapo kwake. Alipofika pale alinunua magazeti na baadae alikunywa kahawa na kisha kurejea nyumbani kwake. Wakati anapandisha ngazi za nyumbani kwake majira ya saa 3 asubuhi, ndipo muuaji alipomtokea kwa nyuma akiwa na bastola na kumpiga risasi mbili kichwani na kisha kutoweka, bila hata kuonekana. Versace alikimbizwa hospitalini na jirani zake waliomwona akigaagaa pale chini huku damu zikimtoka, lakini madaktari wa hospitali ya Jackson Memorial hawakufanikiwa kuokoa maisha yake. Alifariki dunia.

  Kwa wale wasiomjua Gianni Versace, labda niwaelezee kwa kifupi kwamba yeye ni nani? Kama wewe ni mfuatiliaji wa wabunifu wa mavazi, naamini kabisa ushawahi kukutana na pafyum, mikoba ya kike, suruali za dangrizi, maarufu kama Jeans, pochi na hata nguo za ndani zenye lebo ya Gianni Versace.Huyu alikuwa ni miongoni mwa wabunifu wa mavazi, waliojizolea umaarufu kwa kubuni mitindo ya mavazi ya watu maarufu, kama hayati Princess Diana, Elton John, pamoja na waigizaji wa filamu huko Hollywood.

  Akiwa na umri wa miaka 50, Gianni Versace alikuwa katika kilele cha mafanikio na utajiri wake alikadiriwa kufikia zaidi ya dola million 500 {kama shilingi za Tanzania bilioni 600}, pamoja na majumba yake ya kifahari yaliopo, Miami, mahali alipouawa, New York na Milan, nchini Italia alikozaliwa. Kifo chake kiliwashtua watu wengi maarufu hasa Princess Diana, Elton John na Gloria Estafan ambao inasemekana waliwahi kumshauri Gianni Versace ajiwekee walinzi kwa ajili ya usalama wake, lakini alikataa kwa madai kwamba, hataki kuingiliwa uhuru wake.

  Ukweli ni kwamba Gianni Versace alikuwa ni shoga na hata katika mojawapo ya mahojiano yake na jarida la Vague alikiri kwamba yeye ni shoga na kumtambulisha mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Antonio D'Amato kama mpenzi wake wa muda mrefu, mtu ambae gazeti mmoja la udaku nchini Marekani liliwahi kumtuhumu kwamba alikuwa pia ni bwana-ake dada yake Gianni Versace, aitwaye Donatela Versace, kabla hajaanza uhusiano na Gianni Versace. Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba, mauaji ya Gianni Versace yalihusishwa na mauaji ya kupangwa, msemaji wa polisi wa Miami, Richard Barreto alidai kwamba ushahidi wote wa awali uliokusanywa kutoka kwenye eneo la tukio ulionyesha kwamba mauaji yale yalipangwa kwa umakini wa hali ya juu. Ilionekana wazi katika upelelezi wa awali kwamba, Versace aliuawa na mtaalamu wa mauaji ya kupangwa anayejua ni nini anachokifanya.

  Na polisi waliamini hivyo kwa sababu, kuna wakati Versace alituhumiwa kuhusika na genge la maharamia, wanaoendesha uharamia katika biashara ya ubunifu wa mavazi, na hata kuna wakati waliwahusisha wazazi wa Versace ambao ni matajiri wanaomiliki viwanda vya nguo nchini Italia kwamba wanashirikiana na mtoto wao kuvusha dawa za kulevya. Kwa ujumla biashara ya ubunifu wa mavazi ulihusishwa na biashara ya dawa za kulevya, hivyo haikuwa ajabu kwa Versace kutuhumiwa kuhusika na magenge hayo. Versace mwenyewe aliwahi kuzikanusha tuhuma hizo. ‘watu wanasema mimi ni ‘mafioso' hii inaniumiza sana, na inaiumiza hata familia yangu pia.' Alisema.

  Lakini, Polisi hawakusita kulitazama hilo kwa sababu wakati wa mauaji yake alikuwa anachunguzwa na polisi kutokana na tuhuma za kukwepa kodi.Wapelelezi wa Miami walijua kwamba kama mauaji yale yalikuwa ni ya kupangwa, basi kulikuwa na kazi kubwa ya kumkamata muuaji, kwani kwa mujibu wa takwimu za Florida, jimbo ambalo ndipo mji Miami ulipo, kuna kesi zipatazo 300 za mauaji ya kupangwa, na karibu nusu yake watuhumiwa hawajakamatwa, na hii inatokana na kwamba wauaji wanatokea katika majimbo ya mbali ambapo huingia jimboni Florida, kuuwa na kisha kutoweka kabisa bila kuacha ushahidi wa kuwatia mbaroni.

  Majira ya mchana siku yalipotokea mauaji ya Versace, polisi waliokota nguo ambazo kwa mujibu wa watu wanaoishi jirani na Versace, walikiri kumwona mtu aliye kuwa amevaa nguo zinazofanana na zile zilizookotwa, akisalimiana na Versace, mtu ambaye polisi walianza kumhisi kuwa ndiye muuaji. Lakini nadharia hiyo iliwashangaza polisi kwamba iweje muuaji makini aache nguo zake kwenye eneo la tukio? Je atakuwa ni mzembe kiasi gani? Hapo tena wakaanza kujenga wasiwasi mwingine kwamba, huenda Versace ameuawa na mmojawapo wa wapenzi wake.

  Hadi kufikia usiku wa siku mauaji yalipotokea, FBI walishajenga hoja nyingine kwamba huenda Versace akawa ameuawa na na muuaji shoga aitwae Andrew Cunanan, anayeendesha mauaji nchini Marekani akiwa amewalenga mashoga wenzie na mpaka kufikia siku Versace anauawa alikuwa ameshauwa watu wanne katika maeneo ya Minnesota, Illinois na New Jersey. Alikuwa amewekwa kwenye orodha ya watu muhimu kumi wanaotafutwa nchini Marekani na FBI. Cunanan aliyetambuliwa kama kijana mwenye umri wa miaka 27 wakati huo, akiwa na urefu wa futi 5 na inchi 10, alihusishwa na mauaji ya Versace moja kwa moja.

  Na hii ilitokana na kwamba, huenda alikuwa na chuki kwa mashoga wenzie baada ya kupimwa na kuonekana ni muathirika wa Ukimwi, kwani watu wote aliotuhumiwa kuwauwa akiwemo Versace walikuwa ni mashoga. Kutokana na kuwa mtu muhimu anayetafutwa, FBI ilitangaza dau la dola 40,000 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwake. FBI walitawanya picha zake tofauti tofauti zikiwemo zile ambazo alivaa mavazi ya kike kwenye majimbo yote ya Marekani. Siku mbili baadae tangu mauaji ya Versace, Cunanan alionekana kushambulia tena Miami. Polisi walipata taarifa za kuonekana mtu anayefanana naye akikimbia kutoka kwenye jumba la kifahari lililokuwa umbali wa kama kilomita 16 kutoka nyumbani kwa Versace.

  Polisi walivamia katika jumba hilo na kukuta mwili wa mtu aliyekuja kujulikana kama Silvio Alfonso aliyekuwa na umri wa miaka 44, daktari mhamiaji kutoka nchini Cuba. Mwili wake ulikutwa ukiwa nusu uchi sakafuni kama ilivyotokea kwa Versace ambaye na yeye alikuwa ni shoga wa waziwazi aliuawa kwa kupigwa risasi mbili kisogoni. Wapelelezi waliamini kwamba kuna uwezekano mkubwa Dk. Alfonso alimchukua Cunanan katika baa moja ya mashoga iliyopo katika viunga vya Miami na kwenda naye kwake kwa nia ya kufanya naye mapenzi na hivyo kuuawa baada ya kuwa wameshafanya mapenzi.

  Labda nikujulishe tu wewe msomaji kwamba kwa nchini Marekani mtu anayejihusisha na mapenzi ya jinsia moja kwa upande wa wanaume awe anaingilia au anaingiliwa kinyume na maumbile, wote hujulikana kama mashoga. Pia miongoni mwao wapo wanaoingilia na kuingiliwa kinyume na maumbile. Habari za kuuawa kwa Dk. Alfonso zilisambaa kwa haraka sana jijini Miami na kuleta hofu miongoni mwa jamii ya mashoga nchini Marekani, na kusababisha jamii hiyo kuituhumu FBI na Polisi wa Florida kwamba hawafanyi juhudi zozote za kumtafuta muuaji na kumtia mbaroni kwa sababu tu wanaouawa ni jamii ya mashoga.

  Wakati msako wa muuaji Cunanan ukiendelea, majivu ya Gianni Versace yalisafirishwa kwandege ya kukodi kwenda nchini Italia kwa mazishi ya kifamilia ambapo kabla ya mazishi kulifanyika misa maalum katika kanisa la Milan, huku kukiwa na wahudhuriaji wengi maarufu akiwemo hayati Princess Diana na Elton John. Wakati matajiri na watu maarufu wakiomboleza kifo cha Gianni Versace, lakini vyombo vya Habari vya nchini Marekani viliweka kipaumbele katika kumzungumzia muuaji Andrew Cunanan kuliko Gianni Versace.

  Je huyu Andrew Cunanan ni nani? Je, alikuwa na uhusiano gani na na Gianni Versace mpaka kufikia kumuuwa? Je, ni kitu gani hasa kilichosababisha awe anauwa watu hovyo tena Mashoga? Maswali yote hayo yalikuwa yakiulizwa na jamii ya Wamarekani, kwani kwa muda mfupi mno muuaji Andrew Cunanan alikuwa maarufu nchini Marekani. Akielezewa na mama yake wa kumzaa, Andrew Cunanan alikuwa ni shoga Malaya aliyejipachika hadhi ya ya utajiri asiokuwa nao wakati alikuwa ni mtoto wa dalali mmoja aitwae Modesto aishiye Manila, nchini Philipine.

  Mtu huyu alijipachika majina na nyadhifa nzito-nzito katika jamii ya mashoga ili kuwafanya mashoga wenzie wamheshimu na kumhofia, na hii ilitokana na kutaka kuchukuliwa na mashoga matajiri na wenye hadhi. Kuna wakati alijitambulisha kama Andrew De Silver mfanyabiashara na mmiliki wa viwanda kutoka nchini Mexico na wakati mwingine, akijiita Luteni Kamanda Cunnings kutoka jeshi la wanamaji la Marekani au mwigizaji kutoka Hollywood, ama mtoto wa tajiri mmoja maarufuu kutoka Ufilipino.

  Kwa ujumla Cunanan alikuwa anajiweka kulingana na mazingira anayojitambulisha nayo kwani alikuwa na uwezo wa kucheza na sura yake kwa kujiremba kwa jinsi anavyotaka kwa sababu alikuwa ni mzuri kwa sura na alikuwa na haiba ya kuvutia hasa. Alikuwa ni shabiki mkubwa wa mavazi yaliyobuniwa na Gianni Versace kwani mavazi yake mengi yalikuwa na lebo ya Gianni Versace zikiwemo hata chupi zake. Kufikia mwaka 1997 maisha ya Cunanan yalianza kuporomoka na kupoteza ule muonekano wake wa awali aliokuwa akiuringia.

  Sura yake ilioneksana kuchakaa na hiyo ilichangiwa na ulevi wake wa pombe kali kupindukia. Mabadiliko hayo yalimshushia hadhi aliyojipachika na kumshusha thamani kiasi cha kuwa shoga rahisi mno aliyekuwa akiuuza mwili wake kwa bei rahisi ili mradi apate hela ya kujikimu pamoja na ya kunywea pombe na kununulia dawa za kulevya ambazo alikuwa akizitumia kwa fujo.Rafikie aitwae Mike Scott alieleza kwamba, mnamo April 1997, Cunanan alikwenda kituo kimoja kupima Ukimwi kilichopo San Diego na kugundulika kwamba ni muathirika wa Ukimwi. Baada ya kupewa majibu hayo, Cunanan alichanganyikiwa na kuondoka Miami kuelekea Los Angeles, ambapo alikaa kwa siku moja na kisha alirejea na kwenda katika viunga vya Santa Monica Boulevard, mashariki mwa Hollywood na kuwa shoga Malaya wa mtaani akijiuza waziwazi.

  Kuna wakati aliwahi kumweleza rafiki yake huyo kwamba alikuwa akichukuliwa na na watu maarufu wa Hollywood ambao alifanyanao mapenzi bila kutumia kinga ndani ya magari yao na alikuwa akijisifu kwamba atakuwa amewaambukiza Ukimwi sawia. Katika kipindi hicho, Cunanan alikuwa ameishiwa hasa, kwani alifikia hatua ya kukopa nauli ili anunue tiketi ya ndege ili aende Minnesota baada ya kumkumbuka mpenzi wake wa zamani aitwae David Madson aliyekuwa na umri wa miaka 33. Alipofika Minnesota kwa mujibu wa habari za kipolisi, inaaminika kwamba David Madson alikwenda kumpokea Cunanan kwenye uwanja wa ndege na kwenda naye moja kwa moja hadi nyumbani kwake ambapo baadae walitoka kwenda kula chakula cha usiku,
  wakijumuika na mmoja wa rafiki zake David Madson.

  Walionekana wakitoka pamoja kurudi nyumbani. Siku mbili baadae Cunanan alimwalika mtu mmoja aitwae Jeff Trail nyumbani kwa mpenzi wake Madson wakati huo Madson alikuwa hayupo. Jeff Trail alikuwa ni mwanafunzi kutoka Chuo cha Kijeshi, ambaye alipata kuwa mpenzi wake Cunanan wakati akijiuza kwenye viunga vya San Diego, lakini hawakudumu kutokana na tabia ya Cunanan ya kutumia dawa za kulevya kupita kiasi. Trial aliyekuwa na umri wa miaka 28 wakati huo, inasemekana alitoroka jeshini na kukimbilia Minnesota.

  Mnamo majira ya saa nne usiku, siku ambayo Cunanan alimualika rafikie Trail nyumbani kwa Madson, mtu mmoja aishiye jirani na nyumba ya Madson alisikia mabishano ya wanaume wakitukanana nyumbani kwa Madson.Siku mbili baadae Polisi waligundua mwili wa Jeff Trail ukiwa umeviringishwa na zulia nyumbani kwa Madson na ilionesha kwamba Jef Trail aliuawa kwa kupigwa na nyundo kichwani na uso wake ulikuwa umepondwa pondwa kwa nyundo. Polisi waliamini kwamba Madson hakuwepo nyumbani wakati mauaji yanapotokea, na aliporudi alishikiliwa na ndani ya nyumba yake kama mateka kwa siku mbili huku mwili wa Trail ukiendelea kuharibika pale ndani. Baadaye Cunanan alimchukua Madson na kumpakia ndani ya gari aina ya Cherokee Jeep, linalomilikiwa na Madson mwenyewe, kisha aliendesha gari hilo umbali wa kilometa 48, Magharibi mwa jiji la Minnesota, ambapo alimpiga risasi mbili kichwani na kuutupa mwili wake ndani ya ziwa na kutoroka na gari la Madson.

  Baadaye mwili wa Madson uliokotwa na wavuvi, ambao waliwajulisha polisi. Kupatikana kwa mwili wa Madson kulipelekea polisi kwenda nyumbani kwake ambapo waliukuta mwili wa Trail na mkoba wa Nailoni wenye jina la Cunanan. Walipokwenda kuchunguza nyumbani kwa Trail walikuta ujumbe kwenye mashine maalumu ya simu za mezani inayotumika kuacha ujumbe kama muhusika hayupo. Ujumbe huo uliachwa na Cunnan, ukimualika Trail nyumbani kwa Madson. Hiyo ilidhihirisha kwamba Cunanan hakuchukua tahadhari kuficha uhusika katika mauaji yale. Mnamo Mei 4,1997,siku tano baada ya kutokea mauaji ya Trail, mtu mwingine aliye julikana kwa jina la Lee Miglin aliyekuwa na umri wa miaka 72, milionea mmiliki wa majumba, alikutwa na mke wake akiwa ameuwawa ndani ya gereji ya gari, katika mtaa wanaoishi matajiri huko Chicago. Mwili wake ulikutwa umeviringishwa ndani ya plastiki huku ukiwa umekatwa shingoni na kitu chenye ncha kali na mdomo ulifungwa kwa plasta.

  Inawezekana ni ili asipige kelele. Pia macho yake yalikuwa yameng'olewa na alikuwa na majeraha ya kuchomwa sana na kitu chenye ncha kali. Hiyo, iliwadhihirishia polisi kwamba kabla ya kuuawa kwake Miglin alikuwa ameteswa sana. Walipochunguza zaidi ndani ya nyumba waligundua kuwa muuaji alijitengenezea mkate wa nyama na kunyoa ndevu zake, kabla ya kuiba mavazi ya thamani ya Miglin na fedha zipatazo dola 2,000 na kutoweka na gari la Miglin aina ya Lexus. Gari la Madson aina ya Cherocee Jeep lilikutwa likiwa limetekelezwa nje ya eneo la tukio, kwa mara nyingine tena, Cunanan hakuficha kuhusika kwake na mauaji yale. Mke wa Miglin, mama Margareth ambaye hakuwepo wakati mauaji ya mumewe yanatokea, alikanusha kwamba mumewe alikuwa shoga na kuwa alikuwa akifahamiana na Cunanan.

  Siku tano baadaye Cunanan aliibukia Pennsville, New Jersey. Mnamo mei 9,1997, mwili wa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la William Reese aliyekuwa na umri wa miaka 45, mtunza makaburi katika eneo la Finn's Point, ulikutwa katika eneo hilo ukiwa na majeraha ya risasi kichwani, na aina ya silaha ikiwa ni ileile iliyotumika katika matukio ya mauaji ya Madson. Kwa mara nyingine tena makosa ya awali ya muuaji yalijirudia ya kuacha ushahidi wa dhahiri. Gari la Miglin aina ya Lexus liliachwa katika eneo la tukio na gari la Reese aina ya Chevrolet lilikuwa halipo, na hiyo ilionesha kwamba Cunanan alihusika na mauaji yale.

  Wakati mwili wa Reese ukigunduliwa, Cunanan alielekea Miami akitumia gari la Reese. Pamoja na kwamba alikuwa anatafutwa na FBI, na alikuwa kwenye orodha ya watu muhimu wanaotafutwa lakini alikuwa hafichi mwonekano wake. Alipofika Miami alifikia kwenye Hoteli ijulikanayo kama Normandy Plaza ambapo alikaa kwa miezi miwili huku akijichanganya kwenye klabu za mashoga na kujitambulisha katika jamii ya mashoga wa Miami. Mnamo Julai 6, 1997, siku tisa kabla ya Cunanan hajamuua Giani Versace, alitumia sarafu adimu ya dhahabu aliyoiiba nyumbani kwa Miglin na kuiweka rehani kwenye maduka maalum ya kuwekesha rehani, ambapo aliandikisha jina lake kamili na anuani ya hoteli aliyofikia.

  Kwa kawaida Wamarekani hutumia sarafu maalum za dhahabu kukopea fedha kwenye maduka maalum ya kuweka rehani {Pawn Shop} Kwa mujibu wa sheria ya jimbo la Florida, taarifa za muweka rehani hutakiwa kupelekwa polisi ndani ya masaa 24 tangu muweka rehani kuchukuwa fedha, lakini pamoja na taarifa hizo kufikishwa polisi, hazikufanyika juhudi zozote kuchunguza taarifa za mmiliki wa sarafu ile. Ilipofika julai 15, 1997 ndipo Cunanan alipoitikisa jamii ya wafanyabiashara wa mitindo ya mavazi kwa kumuua Giani Versace.

  Ndani ya wiki moja tangu Giani Versace kuuawa FBI wakishirikiana na polisi walianza msako mkali wa kumtafuta muuaji na ndipo Julai 23, 1997 saa kumi jioni, polisi walipopigiwa simu na mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina Fernando Curreira. Mlinzi wa boti za starehe zilizopo pembezoni mwa bahari, akiwajulisha kwamba amemwona mtu mmoja anayefanana na Cunanan akiingia kwenye boti moja inayotumika kama makazi, na alipojaribu kumsimamisha alimrushia risasi na kuingia ndani ya boti hiyo.Baadaye polisi walifika wakiwa na kikosi maalum maarufu kama SWAT, wakiwa na mbwa na kuizingira boti hiyo huku kukiwa na helikopta inayoranda angani.


  Polisi walikuwa wakitoa matangazo kupitia kwenye spika zao wakimtaka mtuhumiwa ajisalimishe, lakini Cunanan hakufanya hivyo na aliendelea kubaki kimya ndani ya boti.Ilipofika saa 2 usiku, polisi walisikia mlio wa risasi kutoka ndani ya boti hiyo na kufuatiwa na ukimya. Baadaye polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na kuvamia boti hiyo ambapo walikuta mwili wa mtu akiwa amejipiga risasi kupitia mdomoni mwake na kuharibu uso wake wote kiasi cha kutotambuliwa. Pembeni mwa mwili ule ilikutwa bastola ambayo ilitumika katika mauaji ya David Madson na William Reese. Mwili ule ulikuja kujulikana kwamba ni wa Andrew Cunanan baada ya alama zake za dole gumba kufanana kabisa na alama alizoacha katika duka la kuweka rehani.

  Msemaji wa polisi, Baretto alisema, sura yake iliharibika vibaya baada ya kujipiga risasi kiasi cha kutotambulika, lakini baada ya uchunguzi wa alama za vidole, imekuja kujulikana kwamba mwili ule ulikuwa ni wa Andrew Cunanan. Baretto aliendelea kusema kwamba ingawa yapo maswali mengi ambayo hayajapata majibu juu ya mauaji aliyokuwa akiyaendesha Cunanan, lakini, wakati umefika wa watu kupumua baada ya jinamizi lile kuondoka.

  Alipoulizwa kwamba, haoni kama polisi walichelewa kumkamata mtuhumiwa wakati alikuwa akijibainisha dhahiri kila anapofanya mauaji. Baretto alisema, 'sidhani kama polisi walizembea, kwani walichukua hatua madhubuti katika kumsaka mtuhumiwa, naamini hawapaswi kulaumiwa kwani walifanya kazi nzuri.'Mtu mmoja alijitambulisha kwa jina la Nicole-Murray mwandishi wa makala za jamii katika magazeti na rafiki wa zamani wa Cunanan alisema kwamba polisi waliichukulia kesi ya Cunanan kwa wepesi mno, mpaka alipouawa mtu aliyegusa jamii ya watu maarufu duniani katika biashara ya ubunifu wa mavazi ndipo wakashtuka na kuchukua hatua zinaostahili, kwa wao polisi ilikuwa kama,'Eh Nguruwe mwingine ameuwawa huko!', lakini alipouwawa Gianni Versace ndiyo wakashtuka kwamba yupo mtu anayeendesha mauaji.
   
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  Jan 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Ni ndefu, lakini ni nzuri kama ukiisoma weekend ukiwa nyumbani umejipumzisha...............
   
 3. Abdulhalim

  Abdulhalim JF-Expert Member

  #3
  Jan 20, 2012
  Joined: Jul 20, 2007
  Messages: 16,472
  Likes Received: 125
  Trophy Points: 160
  Pawn shop.
   
 4. Nyani Ngabu

  Nyani Ngabu Platinum Member

  #4
  Jan 20, 2012
  Joined: May 15, 2006
  Messages: 73,651
  Likes Received: 35,407
  Trophy Points: 280
  Daah naikumbuka hii mwaka 1997!
   
 5. BADILI TABIA

  BADILI TABIA JF-Expert Member

  #5
  Jan 20, 2012
  Joined: Jun 13, 2011
  Messages: 30,866
  Likes Received: 6,217
  Trophy Points: 280
  thanx 4 masimulizi haya
   
 6. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #6
  Jan 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Hii kesi iliwatoa jasho sana Makachero wa Marekani, pamoja na muuaji kutokuwa makini lakini walishindwa kujua nyendo zake kitu ambacho kilimshangaza karibu kila mtu nchini humo. labda kama Gianni Versace asingeuliwa huenda wangeuawa mashoga wengi sana. Lakini kwa sababu Versace ana jina kubwa, hilo liliwaamsha usingizini makachero hao na kuanza msako mkali wa kumsaka muuaji hadi walipomkuta akiwa amejiuwa kwenye Boti.
   
 7. Mshiiri

  Mshiiri JF-Expert Member

  #7
  Jan 20, 2012
  Joined: Jun 16, 2008
  Messages: 1,893
  Likes Received: 66
  Trophy Points: 145
  Hii ni kanuni popote pale hadi ulimwengu wa kwanza. Watu wa kawaida pengine 1000 ni kama mtu mmoja mashuhuri. Pengine mbaya zaidi kwa ulimwengu wa kwanza. Tanzania hii ni tofauti kabisa. Mtu mmoja mashuhuri ni kama mtu mmoja wa kawaida. Simulizi ni ndefu lakini inavuta sana kuisoma. Nimeisoma yote kwa umakini. Mwandishi ni mzuri sana. Asante.
   
 8. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #8
  Jan 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Ahsante Mshiiri kwa maoni yako mazuri, labda kitu kimoja ambacho wengi hawakijui ni kwamba habari hii nimeitafsiri kutoka vyanzo mbalimbali vya mtandao wa internet.
   
 9. Jestina

  Jestina JF-Expert Member

  #9
  Jan 21, 2012
  Joined: Jan 6, 2011
  Messages: 4,806
  Likes Received: 120
  Trophy Points: 160
  nice,mie nilitaka wamkamate bwana....
   
 10. Kombo

  Kombo JF-Expert Member

  #10
  Jan 21, 2012
  Joined: Oct 29, 2010
  Messages: 1,819
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  Kumbe Polisi wana tabia inayofanana ya kuchagua matukio ya kushughulikia kwa haraka? Hovyo kabisa!
   
 11. Horseshoe Arch

  Horseshoe Arch JF-Expert Member

  #11
  Jan 21, 2012
  Joined: Aug 10, 2009
  Messages: 11,228
  Likes Received: 4,945
  Trophy Points: 280
  Nimeimaliza hatimaye
   
 12. Kongosho

  Kongosho JF-Expert Member

  #12
  Jan 21, 2012
  Joined: Mar 21, 2011
  Messages: 36,126
  Likes Received: 301
  Trophy Points: 160
  Neema bana, unanichekesha
  kwani hii ni movie? Ni ukweli

  ila hata mie nilitaka wamkamate

   
 13. Maundumula

  Maundumula JF-Expert Member

  #13
  Jan 21, 2012
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 7,055
  Likes Received: 74
  Trophy Points: 145
  Nimeisoma yote imetulia , ahsante ndugu mwandishi
   
 14. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #14
  Jan 21, 2012
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,632
  Trophy Points: 280
  Mtambuzi asante nimeisoma yote bila kuruka neno hata moja.Ubarikiwe.
   
 15. Raia Fulani

  Raia Fulani JF-Expert Member

  #15
  Jan 21, 2012
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 10,220
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  ni kweli. Nimepumzika hapa nikaisoma yote. Kuna maisha mengi sana humu duniani. Utadhani simulizi za Chase
   
 16. Easymutant

  Easymutant JF-Expert Member

  #16
  Jan 21, 2012
  Joined: Jun 3, 2010
  Messages: 2,569
  Likes Received: 569
  Trophy Points: 280
  Walah! Shigongo akiituta hii anaandaa kitabu!
   
 17. T

  TumainiEl JF-Expert Member

  #17
  Jan 21, 2012
  Joined: Jan 13, 2010
  Messages: 2,891
  Likes Received: 1,644
  Trophy Points: 280
  Mshara wa dhambi ni mauti. Hata ukiwa Trilionea, bado dhambi inaleta mauti. Ila karama za Mungu uzima wa milele. Nadhan nimejifunza juu story hii.
   
 18. T

  TumainiEl JF-Expert Member

  #18
  Jan 21, 2012
  Joined: Jan 13, 2010
  Messages: 2,891
  Likes Received: 1,644
  Trophy Points: 280
  pown shop!
   
 19. B

  Bulesi JF-Expert Member

  #19
  Jan 21, 2012
  Joined: May 14, 2008
  Messages: 6,447
  Likes Received: 414
  Trophy Points: 180
  Furaha ya maisha hailetwi na utajili!!
   
 20. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #20
  Jan 21, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  huwa nikiona hisi sread zako lazima nizimalize hata kama ndefu
   
Loading...