Tusiulize pesa yake imetoka wapi. Tusiulize dhamira yake ni nini? Tusihoji anachotarajia kupata toka kwetu kwani hatumjui na yeye hatujui. Sijanufaika na huo mgao, lakini walionufaika wamshukuru Mungu.
Pamoja na majanga yote yaliyopo duniani, anapotokea mtu wa ajabu kama huyu, hatuna budi kumshukuru Mungu, kwani haya ni matendo yake.
Labda mtu huyu alichuma sana duniani. Labda ameambiwa amebakiza muda mfupi wa kuishi duniani. Kauza mali zake alizochuma, kahakikisha ndugu zake wanaotamani mali zake (alizochuma kwa shida) ili wafaidi atakapoaga dunia. Wako matajiri wangapi ambapo katika siku zao za mwisho waliteseka sana, kisha wakaaga dunia pasipo kujisafishia njia yao huko waendako?
Kama ulichuma, halafu hutoi sadaka kwa Mungu, unatarajia utakapoondoka duniani, utakuwa mgeni wa nani? Nyumba yako ya baadaye itakuwaje? Hata huko kaburini, utahitaji vitu vya kuishibisha roho yako. Kuna chakula cha roho - nenda ukasali. Kuna mwanga wa roho - hujawanunulia watu mishumaa. Fedha hazina matumizi huko, ila katoe sadaka kwa yatima, wajane, maskini, wagonjwa.
Huyu kaenda kuwalipia wagonjwa bili zao. Hakujali kama wana uwezo wa kulipa ama la. Kalipa.
Kawalipia watu nauli. Hakuwauliza kama wanaweza kulipa au hawawezi.
Kawajazia wajasiriamali wa bajaj mafuta. Kawapunguzia gharama za kuendesha biashara yao hiyo ngumu.
TUNAMTAKIA UBAYA MTU MWEMA HUYU WA MUNGU ILI IWEJE?
Badala ya kumwunga mkono, nye wengine mnasema "Watanzania mjihadhari..." Tujihadhari na mtu anayetuletea sinia la dhahabu limesheheni kila aina ya vito vya thamani kisha yu aenda zake bila kusema neno lolote?
Wahenga walisema: Hakuna cha bure.
Lakini huyu ni Mtoa Sadaka. Alijisahau, sasa kaamua kumrudia Mungu. Wewe unayeona boriti machoni mwake, hujaona vibanzi vilivyopo machoni mwako?
Mrudie Mungu, muda bado unao. Hujui utaondoka lini. Hata mimi sina mkataba na Mungu! Sijui nitaondoka lini. Lakini kila fursa ninayoipata ya kumtumikia Mungu, NAITUMIA!