Kwa mtizamo wangu,nadhani pengine mtu HAJIITI msomi bali HUITWA msomi,na wanaomuita hivyo wana sababu zao za msingi (mara nyingi ni wana fani wenzie).Jamii ina uhuru wa kukubaliana na kikundi hicho cha wana fani au kukipuuza.Uluteni,kwa mfano, una mantiki zaidi jeshini kuliko uraiani ambako sanasana wanaofahamu kidogo watasema ni cheo cha nyota mbili.Lakini kijeshi uluteni ni zaidi ya hayo "mawe mawili",kuna uongozi wa moja ya vikundi vya kivita (platuni,kama sijakosea),nk.
Nadhani pia vyeti sio lazima vimaanishe usomi.Lakini again,wanaofahamu zaidi ni wale waliotunuku vyeti hivyo.Jumuiya ya wahadhiri inapoafikiana na kumteua mmoja wao kuwa profesa,kwa mfano,ina mantiki zaidi katika mazingira yao kuliko nje ya ulingo huo.Jinsi ya uprofesa huo utavyotumika ni suala jingine,na jamii ina uhuru wa kuuponda au kuuenzi uprofesa huo.
Na kuhusu vigezo gani vinavyoweza kufanya mtu aitwe msomi,nadhani pia majibu yanaweza kutofautiana kati ya walio ndani ya fani flani na walio nje ya fani hiyo.
Pia naomba nitofautiane kidogo nawe dada yangu katika hoja yako kwamba msomi lazima awe amebuni kitu.Nadhani usomi na ubunifu ni vitu viwili tofauti japo inatarajiwa msomi awe mbunifu ingawa si lazima awe mbunifu.Lakini pia kama unapozungumzia ubunifu unamaanisha kuja na kanuni (theory) mpya,then kuna mahala flani kitaaluma ni lazima uje na aidha theory mpya au uifanyie maboresho kwa iliyopo.Nje ya uwanja wa kitaaluma,huo unaweza usiitwe ubunifu lakini ndani ya ulingo huo,huo nao ni ubunifu.
Pia naomba kutoafikiana nae kwamba kile unachokuja nacho wakati unaingia chuo kikuu kinaondolewa na KUWEKEWA UNACHOTAKIWA KUAMINI...Nani anayekutaka kuamini?Labda kwa wenzetu wa sayansi ambao nyakati nyingine X ni lazima iwe X,lakini mara nyingi (japo si mara zote)huko kwenye "ungwini" ni namna mwanafunzi anavyoweza kucheza na hoja zake.Iwapo kuna mahala mwanafunzi analazimishwa kutetea hoja isiyo yake pasipo kuhoji basi hapo kuna kasoro.
Kuhusu kukutana (naomba kukunukuu)"watu wengi ambao nawafahamu, ambao wamekariri sana elimu ya darasani, wanayo madigrii lakini ukizungumza nao, utafikiri umekutana na mtu ambaye hajawahi kutia mguu darasani hata siku moja" hudhani kwamba tatizo linaweza kuwa mnahukumiana ndivyo sivyo?Yawezekana wao wanaamini mnaelewana katika mnachoongea lakini kumbe sivyo.Hudhani pia kwamba unaweza kuwa huwatendei haki kwa "kujipa mamlaka" (samahani kwa neno hilo) ya kuwahukumu?Au haiwezekani kwamba kwa vile hoja zao hazikuendana na matarajio yako ndio maana ukazihukumu kuwa ni kama za mtaani?
Mwisho,nadhani "makaratasi" (kwa maana ya vyeti) yataendelea kubaki na umuhimu wake hususan miongoni mwa wanafani husika.Kuwepo kwa vyeti feki hakuwezi kuondoa umuhimu wa vyeti halali just like kuwepo kwa noti feki kusivyoweza kuondoa umuhimu wa noti halisi.Jamii hailazimishwi kuthamini au kupuuza vyeti hivyo.Elimu itaendelea kupatikana mtaani,madarasani,kwenye karakana,semina,nk...ni kutoka katika mazingira hayo ndio wahusika watampachika mwenzao/wenzao joho la usomi,umahiri,ujuzi,ubobeaji,ujanja,nk.Watakaotuzwa joho hilo nao hawawezi kuilazimisha jamii iwathamini/iwakubali,bali matokeo ya kazi zao yanaweza kufanya hivyo.