SoC03 Mpango wa kuandaa vijana wenye ubora na uwezo wa kusaidia kuleta maendeleo katika kiwango cha timu ya taifa ya Tanzania katika mpira wa miguu

Stories of Change - 2023 Competition

_pirate

New Member
Jul 16, 2021
4
11
1. TATIZO LINALOIKUMBA TIMU YA TAIFA YA MPIRA WA MIGUU TANZANIA.

Kiujumla timu ya taifa ya Tanzania imekuwa na muendelezo wa kiwango kibovu ambapo kizazi cha kuanzia miaka ya 1990 hakijawahi kuishuhudia timu hii ya Taifa katika kiwango bora hasa katika mechi za mashindano. Timu hiyo ya Taifa haina taji lolote la kiushindani, imefanikiwa kufuzu kucheza michuano ya Afrika (AFCON) mara mbili tu katika historia (1980 na 2019) mara zote ikiondolewa katika hatua ya makundi tena bila ya kupata alama yoyote. Lakini pia timu hiyo haijawahi kufuzu kucheza fainali zozote za kombe la dunia. Rekodi hizo chache zinatosha kuonesha ubovu wa timu ya Taifa ya Tanzania katika mpira wa miguu.


2. MALENGO YA KUFIKIWA ENDAPO MPANGO HUU UTAFANIKIWA.

Yafuatayo ni malengo yanayopaswa kufikiwa endapo mpango huu utafanikiwa:- *Timu ya taifa ya Tanzania kushiriki katika fainali za kombe la dunia. *Kuwa na muendelezo wa ushiriki katika michuano ya Afrika. Suala la timu ya taifa ya Tanzania kushiriki michuano ya Afrika (AFCON) linapaswa kuwa la kawaida sana na endelevu. *Kuzalisha vijana wengi wenye ubora wa kucheza soka kwa uwezo mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Tanzania inahitaji kuwa na vijana wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya, hii itasaidia sana katika kuinua kiwango cha timu ya taifa. *Kuinua maisha ya vijana kupitia mpira wa miguu.

3. CHANGAMOTO KATIKA UZALISHAJI WA WACHEZAJI WENYE UBORA NA UWEZO WA KUISAIDIA TIMU YA TAIFA YA MPIRA WA MIGUU.

i. Uwekezaji mdogo katika mpira wa miguu Tanzania. Hali hii inapelekea kuwa na ligi ya ndani yenye ubora mdogo kiushindani. Kwenye ligi kuu ya Tanzania kumekuwa na ubovu wa miundombinu kama viwanja vya michezo na pia changamoto katika malipo ya waamuzi, hali inayopelekea wakati mwingine baadhi ya waamuzi kufanya maamuzi ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaegemea upande Fulani.

ii. Upungufu wa vituo vya malezi ya soka (football academy) nchini. Ni vituo viwili tu ambavyo angalau vinasaidia kuzalisha wachezaji wazuri nchini ambavyo ni kituo cha Mtibwa Sugar Morogoro, na kituo cha Azam jijini Dar es Salaam.

iii. Michezo kutopewa kipaumbele mashuleni. Kwa mfano kipindi cha mashindano ya mpira wa miguu kwa vyuo vikuu, vijana ambao ni wachezaji hutakiwa kusafiri kwaajili ya kuhudhuria matukio mbali mbali ya kimichezo, lakini wakati huohuo vyuoni masomo huendelea na pia ratiba za mitihani kama kawaida bila kujali kwamba baadhi ya vijana hawapo, hali hii inawavunja mioyo vijana hao na kuamua kusalia masomoni na kuacha kushiriki michezo.


iv. Ukosefu wa elimu kwa wazazi kuhusu namna mchezo wa mpira wa miguu unavyolipa na kuweza kubadilisha maisha ya mchezaji husika. Wazazi wengi wamekua wakiwasisitiza vijana wadogo kukazana na masomo na kuachana na michezo wakiamini kuwa elimu pekee ndio njia sahihi ya wao kufanikiwa. Hii imekuwa ikipelekea vijana wengi wadogo kukatazwa kabisa kushiriki michezo ili wakazane na masomo.


v. Uwekezaji mdogo na pia kuyanyima heshima mashindano ya michezo mashuleni (UMISETA na UMISHUMITA). Haya ni mashindano ambayo yakitumiwa vizuri yatasaidia sana kuzalisha vijana wadogo wengi na kuibua vipaji vingi vya michezo kutoka mashuleni.


4. NJIA ZINAZOWEZA KUSAIDIA KUSULUHISHA TATIZO.

Mambo yafuatayo yatasaidia kupunguza au kumaliza changamoto tajwa hapo juu:-

i. Kuongeza uwekezaji kiujumla katika mpira wa miguu nchini. Hii itasaidia kuongeza hadhi na ubora wa ligi ya ndani. Hii ni kuhakikisha maboresho ya miundombinu kama viwanja, na pia kuhakikisha watumishi wa soka wanaboreshewa maslahi yao ili kutenda haki katika utendaji wao.

ii. Michezo kupewa kipaumbele mashuleni. Hii itasaidia kuhamasisha vijana wadogo kujituma na kujitoa katika michezo. Ratiba za masomo zisiingiliane na ratiba za michezo.

iii. Uanzishwaji wa vituo vingi vya kulea wachezaji (football academy). Angalau kila kanda iwe na vituo vya michezo vya uhakika visivopungua viwili ili kuhakikisha vipaji vya vijana wadogo kutoka kila kona vinainuliwa.

iv. Wazazi wabadilishe mitazamo yao hasi juu ya michezo kwa kuwaunga mkono watoto wao wanapokua na utayari wa kujihusisha na mchezo huu, hii ni kwa kuwatengea muda wa kushiriki michezo na pia kuwanunulia vifaa vya michezo kama jezi na viatu vya michezo.

v. Uwekezaji mkubwa uwekwe katika mashindano ya michezo mashuleni. Mashuleni kuna vipaji vingi sana vya vijana wadogo ambapo vikiwekewa mpango thabiti vinaweza kuleta matunda mazuri katika soka la nchini.


5. NJIA TEULE INAYOWEZA KUSULUHISHA TATIZO.

*Uwekezaji mkubwa kwenye mashindano ya michezo mashuleni (UMISETA kwa shule za sekondari, na UMISHUMITA kwa shule za msingi). Kutokana na upungufu wa vituo vya malezi vya wachezaji, njia hii ni sahihi na rahisi zaidi kuitimiza kwasababu ipo ndani ya uwezo wa serikali na pia itawezesha kufikia vijana wengi zaidi kila kona ya nchi kuliko njia nyingine yoyote.


6. MPANGO KAZI KATIKA KUTEKELEZA ZOEZI LA KUANDAA VIJANA WENYE UBORA NA UWEZO WA KUISAIDIA TIMU YA TAIFA YA TANZANIA.

Mambo yafuatayo yanahitajika ili kufanikisha utendaji wa mpango kazi huu:-

i. Wakuu wa shule na uongozi kiujumla kuipa kipaumbele michezo mashuleni. Hii ni kwa kutenga muda mzuri kwa wanafunzi kufanya mazoezi ya michezo angalau kila siku. Shule nyingi nchini ratiba za michezo ni mara moja kwa wiki, jambo ambalo linadhoofisha viwango vya vijana hao na kuwafanya wasione kama michezo ni muhimu sana katika maisha yao.


ii. Kuboresha miundombinu ya michezo mashuleni. Hii ni kwa kuhakikisha kunakuwa na vifaa vya kutosha vya michezo kama vile jezi na mipira ya kutosha. Pia kuhakikisha shule zinakua na viwanja vizuri vya michezo.

iii. Serikali kuandaa namna nzuri ya ufanyikaji wa michuano hio ya michezo mashuleni na kuweka mipango itakayosaidia kuvuna vipaji.

iv. Baada ya hapo sasa serikali iwekeze pesa ya kutosha katika utendekaji wa mashindano hayo ya michezo mashuleni.

v. Shirikisho la soka nchini lijenge kituo cha kulea wachezaji (football academy) kitakachoendeshwa na shirikisho hilo. Tayari shirikisho la soka la Tanzania linaendelea na ujenzi wa kituo Cha michezo katika manispaa ya kigamboni jijini Dar-es-salaam.

Yafuatayo ni mapendekezo ya namna mashindano haya yafanyike ili kuibua vipaji vya vijana wadogo mashuleni:-

i. Michuano ianze kufanyika kama kawaida kwenye kila kata, kupanda ngazi ya wilaya , ngazi ya mkoa mpaka ngazi ya kanda. Kiujumla Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ina jumla ya mikoa 31, zikiwa ndani ya kanda sita (kaskazini, kati, kusini, pwani, ziwa na Zanzibar). Mashindano hayo yafanyike ndani ya kila kanda na kuhakikisha kila kanda inatoa timu mbili za mwisho. Hapo nafasi zaidi zitolewe kwa kanda mbili, kwamfano kanda ya pwani miongoni mwa mikoa iliyomo ni Dar es Salaam na Morogoro ambayo ina idadi ya watu wasiopungua milioni tatu kwa kila mkoa,pia kwenye kanda ya kati mikoa ya Dodoma na Tabora ina idadi kubwa ya watu.

Kanda hizo mbili zinaweza kugawanishwa mara mbili kila moja, hii itapelekea kuwa na kanda nane kiujumla, ambapo kila kanda ikitoa timu mbili kutakua na jumla ya timu 16 zilizosalia kwenye michuano.

Timu hizo 16 ziwekwe kambi katika eneo moja na zipangwe katika makundi manne (4), ambapo kila kundi zitafuzu timu mbili, hivyo kubakiwa na timu 8 zitakazofuzu hatua za mitoano, mtoano uendelee mpaka apatikane bingwa mmoja.

ii. Katika michuano hiyo kuwe na wataalamu ambao wanaangalia maendeleo ya wachezaji ambapo mwisho wa mashindano angalau kichaguliwe kikosi kisichopungua wachezaji 25 kwa kila msimu.

iii. Wachezaji hao wachukuliwe na kupelekwa katika kituo cha malezi ya wachezaji (football academy) kinachomolikiwa na shirikisho la soka nchini na kuendelea kuwafua na kuwapa mafunzo ya kitaalamu ya mchezo wa mpira wa miguu.

iv. Kwahiyo wachezaji hao watakua wanamilikiwa na shirikisho la soka la Tanzania, hivyo shirikisho liajiri mawakala malumu kwaajili ya kuwatafutia soko la ndani na la kimataifa wachezaji hawa, ambapo kitakua ni chanzo cha kipato kwa shirikisho kutokana na mauzo ya wachezaji hao, Wachezaji watakaobaki basi watatumikia timu za Taifa za vijana nchini.

v. Hii itawezesha kuwatengenezea vijana njia nzuri na urahisi wa wao kwenda kucheza soka la kulipwa nchi za nje mpaka ulaya, ambapo vijana hao watakuja kuwa msaada mkubwa katika timu ya Taifa ya Tanzania. Na pia itasaidia kubadilisha maisha ya vijana hawa pamoja na familia zao. Zoezi hilo la kuchukua vipaji liwe endelevu kwa kila mwaka.

NB: Mchakato huu ukizingatiwa utaleta mapinduzi makubwa katika soka la Tanzania ndani ya kipindi cha miaka kumi (10) tu.

Pichani ni viongozi mbalimbali wa vilabu vya soka nchini wakifuafilia mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 katika kituo Cha michezo Cha TFF. Kituo hiki endapo kitaendelezwa vizuri na kutumika ipasavyo kitaleta matunda mengi katika kuendeleza vipaji vya vijana wadogo nchini.

FwBPaSyWwAESZnL.jpg
 
Back
Top Bottom