Moshi mweupe kesi ya Sabaya

Corticopontine

JF-Expert Member
Sep 20, 2019
664
1,272
Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya na wenzake wawili leo wamefutiwa mashtaka katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha kisha kufunguliwa tena mashtaka hayo kosa moja likiongezeka.

Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka aliileza mahakama hiyo kuwa licha ya kesi kupangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa leo Ijumaa Julai 16, 2021 kwa upande wa Jamhuri kupeleka mashahidi Jamhuri inaomba kuondoa shauri hilo.

Amesema wanaomba kuondoa shauri hilo chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

"Mheshimiwa Hakimu baada ya kuliondoa shauri lililopo Mahakama ya wilaya ya Arusha, tunaiomba mahakama hii kufungua upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,"amesema

Baada ya hoja hiyo Hakimu mkazi mwandamizi, Odira Amworo ambaye ameletwa Arusha maalum kusikiliza kesi hiyo akitoka Mkoa wa Geita aliutaka upande wa utetezi kutoa hoja kama wanayo juu ya maombi hayo ambapo Wakili Dancon Oola alieleza kuwa hawana pingamizi kwa kuwa ni haki yao iko ndani ya sheria.

"Hatuwezi kuwa na pingamizi kwa sababu ni haki yao na iko ndani ya sheria kufanya hivyo,"alieleza Wakili huyo.

Hakimu aliridhia ombi hilo na kuliondoa shauri hilo la awali chini ya kifungu hicho namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Hata hivyo, baada ya kufutwa, Wakili mwandamizi wa serikali Abdallah Chavula aliwasomea upya mashitaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha Sabaya na wenzake.

Katika mashtaka hayo, Sabaya na wenzake, Sylivester Nyegu na Daniel Mbura wanashitakiwa kosa la kwanza unyang'anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh2.7 milioni mali ya Mohamed Saad .

Wakili Chavula amesema kosa hilo likitokea Februari 9 mwaka huu katika duka la Saad Mohamed mtaa wa bondeni jijini Arusha.

Amesema kosa la pili ni la wizi wa kutumia silaha ambapo Februari 9, Sabaya na wenzake wawili wakiiba fedha Sh390, 000 Mali ya Bakari Msangi ambaye ni diwani wa CCM Kata ya Sombetini baada ya kumtishia kwa silaha ya bunduki.

Shitaka la tatu Sabaya na wenzake wanatuhumiwa kuiba Sh35, 000 na simu aina ya techno mali ya Ramadhani Rashid baada ya kumtishia kwa silaha na kumfunga pingu Februari 9 mtaa wa bondeni katika duka Hilo la Mohamed Saad.

Sabaya na wenzake wanaotetewa na mawakili, Oola, Moses Mahuna, Silivester Mahumbuga na Heston Justine walikana mashitaka hayo.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Jumatatu wiki ijayo na kesi nyingine ya uhujumu uchumi inayomkabili Sabaya na wawenzake iliahirishwa Hadi Julai 30 mwaka huu.

Watuhumiwa hao wamepelekwa gereza kuu la Kisongo kwa kuwa makosa yao hayana dhamana. Maelezo zaidi ya kesi ya Sabaya na mwenendo kwa kesi fuailia gazeti Mwananchi kesho.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom