[h=3]Mohammed Mursi raisi mpya wa Misri[/h]
Rais mpya wa Misri Mohammed Mursi
Mgombea wa Udugu wa Kiislamu nchini Misri, Mohammed Mursi, ameshinda urais wa nchi hiyo. Muda mchache uliopita, Tume ya Uchaguzi imemtangaza Mursi kuwa rais wa kwanza wa kuchaguliwa wa taifa hilo la Afrika ya Kaskazini, akishinda kwa asilimia 51.7 ya kura zote.
Maelfu ya wafuasi wake wanaendelea kushangiria kwenye uwanja maarufu wa Tahrir, ambako wamekusanyika tangu juzi kushinikiza kutangazwa kwa matokeo.
Mursi, mhadhiri wa chuo kikuu amemshinda waziri mkuu wa zamani wa enzi za Hosni Mubarak, Ahmed Shafiq, ambaye hapo Alhamis wafuasi wake walitangaza kuwa ndiye mshindi. Mursi sasa anakabiliwa na kazi ngumu ya kupatanisha tafauti za kimtazamo na kimadaraka kati ya vyama vinavyofuata siasa za Kiislamu, jeshi na makundi mengine nchini Misri.
Wafuasi wa chama cha Muslim brotherhood wakishangilia matokeo ya urais
Vikosi vya usalama vimeongezwa katika miji na maeneo muhimu ya nchi, huku wakipewa maagizo ya kuchukuwa hatua kali dhidi ya wavunja amani na sheria. Msemaji wa timu ya kampeni ya Mursi, Jihad al-Haddad, amekiambia kituo cha televisheni cha al-Jazeera, kwamba Mursi atalihutubia taifa muda wowote kuanzia sasa kuelezea mpango wake wa uongozi.
Posted by
Roy Snr. at
00:52