Mdogo wangu Mnyika, nakuonya mimi Lukolo kama kaka yako, kwamba wewe ndiye mbunge bora wa Tanzania. Wewe ndiye uliyetoa hoja nyingi zaidi kuliko wabunge wote nchini, wewe ndiye uliyeuliza maswali mengi sana sambamba na Tundu Lissu. Zitto Kabwe, hakuwemo hata katika orodha ya wabunge kumi bora wa nchi hii katika bunge la 2010 - 2015. Kwa viwango ulivyovifikia Mhe. Mnyika, hupaswi hata kidogo kujishushia heshima kwa kufanya malumbano na watu wa kawaida kabisa kwenye mitandao, wenye nia ya kutaka kukutoa kwenye mstari.
Mnyika hebu komaa kidogo kisiasa mdogo wangu, majibu yako kwa Zitto yanakushushia hadhi na kumpa umaarufu usio wa lazima Zitto. Hebu fanya kazi ya kujenga chama chako cha CHADEMA, na achana kabisa na hizi story za Zitto. Wanasiasa waliokomaa hupinga maandishi ya kwenye gazeti kwa kumshitaki mhariri na si kumjibu mchangiaji wa habari kwenye gazeti. Wanasiasa waliokomaa hawapotezi muda kujibu tuhuma za kitoto za kwenye mitandao.
Mnyika komaa kisiasa! Hivi sasa wewe ni naibu katika mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini, si mtu mdogo hata kidogo. Hupaswi kuweweseka kama mtoto kila unapoguswa. Kuna mengine ambayo unaweza kuyajibu kwa kuitisha press conference iwapo yataonekana yanataka kuleta madhara kwako na kwa chama, na kuna mengine ambayo unapaswa ku-ignore. Lakini kuna yale ya kawaida ya kila siku yanayojitokeza, muache msemaji wa chama ajibu. Ni kujidharirisha sana, kukesha kwenye mitandao kujibu kila hoja ya kipuuzi inayorushwa humo. Usipoteze muda wako mhimu kushughulika na watu wasio kuwa na madhara kwako.
Nimekuonya na kukushauri kama kaka yako, ukishupaza shingo, usinililie itakapovunjika.