IJUE SHERIA
Member
- Dec 11, 2017
- 11
- 146
NA MWANASHERIA WETU
Mara nyingi nimekuwa nikiandika kuhusu masuala muhimu kuhusu ardhi hasa namna ya kuandika mikataba mtu anapokuwa ananunua nyumba/kiwanja, hadhi ya mikataba hiyo kisheria, na ubora wake.
Pia nimeandika mambo mbalmbali kuhusu namna ya kununua nyumba au kiwanja kwa usalama ili watu wasitapeliwe. Nikasema suala si tu kununua kile unachokipenda na kuondoka isipokuwa ni kununua na kuwa salama na ulichonunua bila hatari ya kukumbana na mgogoro mbeleni.
Lengo la haya yote ni katika kuhakikisha watu hawatapeliwi na hivyo kupoteza fedha walizochuma kwa jasho.Lengo lingine ni kuwaepusha wanunuzi na hatari ya kuingia mahakamani ambako kuna usumbufu mkubwa na panapoteza fedha na muda sana tena sana, naongea hili kwa uzoefu.
Leo pia nasisitiza tena kuwa ili ununue kiwanja au nyumba na uepuke kabisa kupata mgogoro hakikisha unafuata taratibu zote za msingi na za kisheria ikiwemo kuhakikisha unaandaa mkataba wenye hadhi ambao hata likitokea tatizo basi mkataba uwe ndio mlinzi wako.
Aidha leo naongelea tatizo lingine tena katika masuala hayahaya ya manunuzi ya viwanja na nyumba. Naongelea fedha ambayo serikali za mitaa wamekuwa wakiichukua kutoka kwa watu wanaouziana ardhi.
1 . SERIKALI ZA MITAA KUCHUKUA ASILIMIA KUMI WAKATI WA MANUNUZI YA KIWANJA/NYUMBA
Hatua hii ya serikali za mitaa kuchukua fedha kutoka kwa wanaouziana viwanja au nyumba limekuwa la kawaida sana.
Watu wanauziana kiwanja au nyumba serikali za mitaa wanawaambia kuwa mnatakiwa kulipa asilimia kumi kama ada ya mauziano .
Asilimia kumi ni hela nyingi sana kwakuwa kama nyumba imeuzwa milioni mianne asilimia kumi ni sawa na milioni arobaini.
Zipo serikali za mitaa nyingine ambazo wakati mwingine hudai chini ya hizo lakini mara kwa mara asilimia kumi ndio huwa inaombwa. Kinachouma zaidi hawa jamaa wa serikali za mitaa huwa wanalazimisha kutolewa kwa fedha hizo.
Hufikia hadi hatua ya kutoa vitisho na ikitokea kuwa mtu ameuza bila kuwa taarifu ili wachukue hela basi wanamjengea uadui na hata yule aliyenunua naye anajengewa uadui.
2 .ASILIMIA KUMI YA SERIKALI ZA MITAA HAIPO KISHERIA
Hakuna sheria yoyote katika nchi hii ambayo inatambua hiyo asilimia kumi. Hili ni jambo la kuzuka tu na limeanzishwa kwa matamanio(tamaa) ya watu.
Narudia tena hakuna katika sheria yoyote ya nchi hii inayosema kuwa watu wanapouziana kiwanja au nymba inatakiwa muuzaji au mnunuzi alipe asilimia kumi serikali za mitaa.Asilimia kumi ni mradi wa watu tu ambao wameamua kujipatia kipato kwa njia hiyo.
Natoa changamoto( challenge) ukimuona kiongozi yoyote wa serikali za mitaa kwa nia njema tu muulize asilimia kumi wanayotoza au gharama yoyote ile wanayotoza wakati wa mauzo ya viwanja na nyumba inapatikana katika sheria ipi.
Niseme tu kuwa Sura ya 113, sheria namba 4 ya ardhi pamoja na sura ya 334 sheria ya usajili wa ardhi zinachosisitiza ni kuwa mkataba wa ununuzi wa ardhi ni lazima uwe katika maandishi.
Sambamba na sheria hizo, kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba kimesema mkataba unaokubalika kisheria ni ule uliofanywa kwa hiari huru,wahusika wenye sifa, malipo halali na mali halali.
Sheria hizi ndizo zinazosimamia mauzo ya ardhi.
Hakuna asilimia 10 humu pote. Pia humu pote hamna mahali kuwa usipolipa asilimia 10 ununuzi wako sio halali. Hakuna kabisa .
Kadhalika hakuna sheria nyingine yoyote nje ya nilizotaja hapa juu imeruhusu jambo hilo.
3 . JE IPI HADHI YA ASILIMIA KUMI?
Jibu ni rahisi kuwa asilimia kumi au malipo yoyote unayoyatoa serikali za mitaa wakati wa ununuzi wa nyumba/kiwanja ni rushwa. Ni rushwa na ni ufisadi.
Ifahamike wazi kuwa viongozi wa serikali za mitaa ni watumishi wa serikali. Fedha yoyote ambayo hulipwa serikalini ni lazima iwe imeainishwa katika sheria fulani.
Hakuna malipo yoyote kwa serikali ambayo hutolewa bila ya kuwa yameainishwa pahala fulani.
Pili fedha yoyote halali inayolipwa kihalali katika mamlaka yoyote ya serikali ni lazima itolewe risiti ya serikali. Inatolewa risiti ya serikali ikiwa na maana kuwa inatambuliwa na serikali , itakwenda serikalini na matumizi yake yatakaguliwa na serikali.
Fedha yoyote inayotolewa kwa serikali bila aliyetoa kupewa risiti ni fedha ambayo ina ufisadi ndani yake.
Na katika maana hiyo ni kuwa unapolipa fedha serikali za mitaa kwasababu yoyote ile kuhusu kufanyika kwa mkataba wa manunuzi ya kiwanja/nyumba unakuwa umetoa rushwa ndugu na kama utachukuliwa hatua utatakiwa kujibu mashtaka ya kutoa rushwa.
Kiongozi wa serikali za mitaa anayeomba na kupokea fedha hizo anakuwa ameomba na kupokea rushwa. Na ndio maana fedha hizi hazitolewi risiti.
Na ukipata bahati ukapewa risiti haitakuwa EFD bali zile za vitabu vyao vya kutengeza ambavyo kimsingi ni zuga tu.
4 . UWEPO WA SERIKALI ZA MITAA UNAPONUNUA ARDHI
Kisheria unaponunua kiwanja au nyumba pahala fulani suala la kuwashirikisha serikali za mitaa ni hiari yako.
Katu mkataba wa ununuzi haubatiliki kwakuwa hakukuwa na serikali za mitaa. Serikali za mitaa tunawahitaji kwa ajili ya kuainisha mipaka na kuepuka kuuziwa kiwanja mara mbili japo hizi dili nazo wamekuwa wakizicheza wao zaidi.
Kwahiyo wewe utaamua uwashirikishe au usiwashirikishe.
Narudia tena mkataba wa ununuzi wa ardhi kisheria haubatiliki ati kwasababu serikali za mitaa hawakushirishwa.
KWA MAPENDEKO YA MADA AMBAYO UNGEPENDA IJADILIWE 0784482959.