Nasikitika sana kuwaambia ndugu zangu wote kwamba siku ya Jumanne tarehe 7 mwezi huu mwaka 2017 nilipotelewa na ndugu zangu wanne ambao ni Mke wangu Sayuni Nsoro, mdogo wangu Denis Rulangaranga, shemeji yangu Renatha Simon pamoja na kijana Sabinian Stefano (cousin)... Ndugu hawa walitekwa na watu wasiofahamika ambao walikuwa na gari aina ya Noah yenye rangi ya Silver (kwa maelezo ya mashuhuda)
Je Ilikuwaje?
Mnamo tarehe 07 mwezi huu (Novemba) 2017 majira ya kati ya saa nne na nusu usiku na saa tano nilimpigia mke wangu simu baada ya kutomkuta nyumbani.
Alipokea na kunijibu kwamba yupo na mdogo wangu wamesimama mara moja kwenye Pub yetu inayoitwa Seblen Pub lakini kuna watu wanaojiita maaskari ni kama wanataka kuwakamata.. nikamuuliza wanawakamata kwa kosa gani? Ndipo nikasikia sauti ya kiume ikimuuliza mke wangu kwa ukali kwamba nani kamruhusu kuongea na simu? Simu ikakatika na kuanzia hapo nikawa nikipiga haipokelewi..
Ilibidi niende haraka sana kwenye hiyo Pub ya Seblen alipokuwepo mke wangu wakati akinipigia simu ili nijue kuna tatizo gani.. ilinichukua takriban dakika 15 lakini nilipofika sikuwakuta.. Nikauliza vijana niliowakuta hapo mke wangu na mdogo wangu wako wapi? Nikaambiwa wamechukuliwa na Maaskari kwenye NOAH ya Silver... Pamoja nao wamechukuliwa ndugu zangu wengine wawili.
waliochukuliwa/waliotekwa ni kina nani ?
1. Sayuni Nsoro - Ambaye ni mke wangu.
2. Denis Rulangaranga -Ambaye ni mdogo wangu
3. Renatha Simon - Ambaye ni shemeji yangu wa kike (Ndiye msimamizi wa Seblen Pub)
4. Sabinian Stefano - Cousin wangu ambaye ni mpishi pale Seblen Pub
Baada ya hapo nilikimbia kwenda kituo cha polisi Kijitonyama (Mabatini). Nikijua kwa vyovyote watakuwa wamepelekwa hapo... Hata hivyo sikuwakuta. Nikashauriwa niende kuangalia Kituo cha Polisi Urafiki ambako pia sikuwakuta.. nikaenda vituo vingine kadhaa vya polisi usiku huo vikiwemo Oysterbay, Simu 2000 (kilikuwa kimefungwa saa sita hiyo), Chuo Kikuu UDSM, Mtambani, Garden, Mwinjuma, Magomeni, Ubungo Terminal kisha nikarudi tena Mabatini... baada ya mzunguko wote huo nilifika pale Mabatini majira ya saa kumi na mbili na nusu asubuhi nikiwa sijapumzika usiku kucha hadi muda huo.
Niliporudi Mabatini nikaandikisha taarifa ya ndugu zangu kutekwa na nikapewa RB namba KJN/RB/10786/2017.. Baada ya hapo nikashauriwa niende Oysterbay Polisi kwa Mkuu wa Upelelezi wa mkoa Kinondoni ambapo nilienda asubuhi hiyo hiyo
Oysterbay Polisi
Nilifanikiwa kumuona Mkuu wa Upelelezi wa mkoa ambaye alinipa ushirikiano mzuri sana! Alinipa maaskari watatu akiwemo mmoja wa mambo ya mitandao. Mapokezi yao yalinifariji sana kwani tulifanikiwa kuhoji mshuhuda wa tukio na pia tulifanikiwa kufuatilia simu zao ambazo zilikuwa bado zikiita hadi maeneo ya Mikocheni "karibu na nyumba za mawaziri" ambapo polisi wanaendelea na uchunguzi wa eneo hilo
Leo ni siku ya 5 toka tukio hilo la kusikitisha litokee lakini kama ndugu hatujatafutwa na hao watekaji kuombwa chochote na wala hatujapewa taarifa rasmi zozote za walipo ndugu zetu.
Hii imeleta sintofahamu ya hali ya juu katika familia na hivi ninavyoandika wanafamilia hawajafahamu kwa nini hawa vijana wametekwa na hakuna taarifa rasmi tulizonazo
ujumbe huu unataka nini?
1. Mtu yeyote mwenye taarifa za hao watu wanne tunamuomba afikishe taarifa hizo kwenye kituo chochote cha polisi.
2. Tunaiomba serikali iingilie kati na iwasaidie polisi ambao mpaka sasa wanafanya kazi nzuri katika kumaliza hili jambo.. pamoja na kazi nzuri ya polisi, sisi kama familia tunaisihi serikali iviruhusu vyombo vyake vingine vya usalama viisaidie polisi ili ndugu zetu warudishwe wakiwa hai na wakiwa salama.
3. Utekaji ule ni wa kinyama na tunomba serikali itusaidie ili kututoa hofu..
C&P from Deo Rulangaranga