Pinda atangaza mali zake
Asema akaunti zake zote hazizidi sh milioni 25
na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametangaza mali zake. Aliwaambia wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jana ofisini mwake, Dar es Salaam, kuwa anamiliki nyumba tatu, na yuko katika pilikapilika za kujenga nyumba ya nne.
Pinda, ambaye ni kiongozi wa kwanza wa serikali ya awamu ya nne kutangaza mali zake hadharani, alisema kwamba ana akaunti kadhaa ambazo zikijumuishwa pamoja, zina kiasi cha pesa kisichozidi sh milioni 25.
Alisema ana nyumba moja Dodoma, ambayo aliijenga kwa mkopo wa serikali; nyingine iko nyumbani kwao Mpanda na nyingine, ambayo aliiita kijumba iko Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa nyumbani kwa baba yake, ambaye yeye alimuita babu, anayeishi Kibaoni, Wilaya ya Mpanda, hana nyumba bali chumba kimoja ambacho amekuwa akikitumia hadi alipokuwa waziri mkuu.
Alisema kuwa hakuwa na shida na chumba hicho, lakini katika mazingira ya sasa ya nafasi aliyonayo amelazimika kupaboresha.
Sasa tunajenga pale, alisema huku akiwatania walinzi na wasaidizi wake kwamba kama si wao, yeye asingepata shida kufikia pale kama ilivyokuwa zamani.
Pinda alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa kuhusu tetesi kwamba yeye ni waziri mkuu maskini akilinganishwa na vigogo waliomtangulia na wengine waliomo serikalini.
Katika kujivunia umaskini huo, Pinda alisema: Najiona kama nina bahati, namshukuru Mungu kunifikisha hapa nilipo.
Alisisitiza pia kuwa hana hisa katika kampuni yoyote, halafu akasema kwa utani, inawezekana ni ujinga tu wa waziri mkuu huyu wa sasa
Alisema kwa nafasi aliyonayo analipwa pensheni kila mwezi, kwa sababu serikali imeweka utaratibu mzuri wa kumhudumia kwa kila kitu, hivyo anaweza kutumia mapato yake ya kila mwezi kufanyia mambo ya msingi au kuweka akiba.
Ukisha-retire (ukishastaafu) serikali inakujali hadi kifo. What more do you want (Unataka nini zaidi)? alisema.
Mara ya mwisho kwa kiongozi wa kitaifa kutangaza rasmi mali zake ilikuwa mwaka 1995. Wakati huo, Rais Benjamin Mkapa, katika mwanzo wa utawala wake, alitangaza kuwa ana nyumba mbili; moja Dar es Salaam, nyingine kwao Lupaso.
Alipostaafu, licha ya wananchi kudai atangaze mali alizonazo, Mkapa hakusema ana mali kiasi gani. Lakini inajulikana kuwa idadi ya nyumba zake ilikuwa imeongezeka, na alikuwa amejiingiza katika uwekezaji ambao baadhi ya wakosoaji wake wamekuwa wakiulalamikia kwa misingi ya kisiasa.
Hatua ya Pinda kutangaza mali zake ni changamoto kubwa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye amekuwa bubu kuhusu nyumba na mali zake anazomiliki.
Kikomo cha ubunge
Katika mazungumo ya jana, Pinda alipendekeza wabunge wawekewe kikomo cha muda wao wa utumishi.
Tuweke kipindi maalumu cha uongozi. Itakuwa suluhu (suluhisho) nzuri ya kuondokana na vijimaneno na kukamatana uchawi
Miaka 15 kwa mfano, inatosha kwa mbunge, na watu watakuwa wanajua kuwa muda wako unaisha, alisema.
Alisisitiza kwamba Tanzania ina watu wengi wenye uwezo, na kwamba kuweka vipindi maalumu kungesaidia kujenga mazingira ya kuwaandaa wengine kupokeana nafasi za uongozi.
Alikuwa akijenga hoja kuhusu rai inayotolewa na baadhi ya wananchi kwamba wazee waachie ngazi, akasema hoja si umri bali muda ambao mtu anakuwa amekaa katika nafasi hiyo.
Hata hivyo, alionya kuwa viongozi wenyewe walio madarakani hawawezi kujipimia. Akasisitiza kuwa ni vema viongozi kuiga mfano wa hayati Rashid Mfaume Kawawa wa kuachia ngazi kwa hiari.
Katika kusisitiza hayumo miongoni mwa wanaopaswa kungatuka sasa, alisema yeye si mzee, lakini akadokeza kwamba iwapo atapata tena fursa ya kuchaguliwa kuwa mbunge miaka 15 inamtosha.
Kasi ndogo ya serikali
Pinda alikataa kukiri kwamba utendaji wa serikali ya awamu ya nne umekuwa wa kasi ndogo.
Alisema swali hilo ni gumu kwake, kwani yeye ni msimamizi wa shughuli za serikali, na kwamba inafanya kazi kupitia Baraza la Mawaziri, na kila waziri ana majukumu ya kutekeleza.
Kila waziri ana potifolio (wizara) yake, lazima aisimamie. Tunakwenda vizuri kiutendaji. Jitihada zimefanyika, alisema.
Kiswahili lugha ya kufundishia
Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia ili kukuza maarifa na ujuzi wa watoto wa Kitanzania, kwa kuzingatia kuwa wanafunzi na watoto wengi hawajui Kiingereza vizuri.
Tutumie lugha inayoeleweka. Mfano China, Ufaransa, Ujerumani na kwingineko wanatumia lugha zao kufundishia, alisema.
Alisema ni ajabu kwamba hata sheria ndogo ndogo za halmashauri zetu, na hata sheria zinazotungwa bungeni zinaandikwa kwa Kiingereza, ilhali wanaozipitisha wanazijadili kwa Kiswahili, na wanaozitekeleza wanajua Kiswahili.
Akasisitiza: itabidi tufike mahali tusema hapana.
Sheria ya Uhuru wa Habari
Pinda alikataa kueleza sababu za serikali kuchelewesha muswada wa sheria ya uhuru wa habari ambao umekuwa unapigiwa kelele na wananchi kwa miaka mitatu mfululizo sasa, na ambao harakati zake zimeanza wakati wa serikali ya awamu ya tatu.
Muswada huo ambao ukipitishwa utasaidia kurekebisha na kufuta baadhi ya sheria mbaya na katili zilizopo, uko mikononi mwa serikali baada ya wadau kukataa toleo la awali ambalo serikali ilitaka kulipitisha kwa kasi. Wadau waligundua kasoro kubwa, wakaomba upitiwe na kurekebishwa upya.
Miongoni mwa sheria zinazotarajiwa kufutwa au kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na muswada huo ni Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ambayo serikali imekuwa ikiitumia vibaya kuyafungia magazeti yanayoikosoa.
Alipoombwa ataje tarehe ya kupelekewa muswada huo bungeni ili ujadiliwe na kuwa sheria, Pinda alitoa matumaini yasiyokamilika, akisema: Haitawezekana kwa Januari, labda Aprili. Kama tutashindwa yote sawa sawa, atakayekuja atalisukuma.
Chanzo: Tanzania Daima