Missed call ya shemeji

Missed call ya shemeji

MH! MISSED CALL YA SHEMEJI!-16

ILIPOISHIA
Kwa mbali dada mtu huyo akaanza kuwaza kuhusu ndoa yake maana tangu amepigwa chini na mumewe hakuwaambia wazazi wake…
"Mimi mama sijafanya kwa nia mbaya."
"Hapana, ulipoona shemejiyo kakwambia hivyo na umemshauri mdogo wako hataki, ungetuletea habari sisi."
"Nisamehe mimi mama."
Mara mlango ukafunguliwa, Aisha akatoka huku akimwaga machozi.
JIACHIE MWENYEWE…"

Nini wewe?" aliuliza mama mtu huyo.
"Mama mimi nasafiri usiku huuhuu."
"Kwenda wapi?"
"Kurudi kwangu."

"Nini kimetokea, mbona unalia?"
"Nimekumbuka mengi mama. Ni kweli nilikuwa nakosea kumkatalia unyumba mume wangu…amekuwa akinisema sana kuhusu hilo sikuwa namsikia, sasa najuta mama."
"Huwezi kupata gari muda huu! Nadhani unajua."
"Hata malori nitapanda mama."

Mara, baba mtu naye akatoka baada ya kumsikia Aisha akitangaza kuondoka usiku huohuo kurudi kwa mume wake, Dar es Salaam…
"Kama amelijua kosa lake na kuamua aende sawa tu, nenda. Ukipata gari wasalimie, ukikosa rudi ulale kesho uondoke," alisema baba mtu huyo huku akirudi ndani. Sauti yake haikuonesha uzembe wakati wa kuzungumza.

***
Asubuhi Aisha aliwaaga wazazi wake kurudi Dar kwa mume wake baada ya jana yake kukosa usafiri.
"Sisi wazazi wako Aisha tunakutaka ukaishi kwa mumeo ukijua yeye ndiye kichwa cha nyumbani kwako. Kama utataka kujifanya mko sawa hamtafika mbali, ukweli tunakwambia."
"Sawa mama, mimi nimeelewa lakini pia naamini mnajua nilivyotendewa na dada yangu," alisema Aisha huku akimwangalia dada yake kwa jicho baya!

"Tunajua, hilo tuachie sisi tutajua jinsi ya kufanya, wewe nenda salama na uwe na amani. Yote yatoe moyoni mwako ili uishi kwa amani."

***
Ilikuwa jioni baada ya Aisha kuondoka, baba yao alipokuwa amerudi kutoka kwenye mihangaiko yao, alimwita mkewe na kumwambia wamuweke chini dada wa Aisha na kumuuliza kuna nini nyumbani kwake mpaka akaenda Dar kuishi kwa mdogo wake yakatokea ya kutokea…
"Tumekuita hapa Ime, tunataka kujua na wewe nyumbani kwako kuna nini mpaka ukaenda kuishi kwa mdogo wako Dar es Salaam?" aliuliza baba mtu kwa sauti isiyotaka utani wale kucheleweshewa majibu…

"Mimi nimeachika!"
"Umeachika! Ime, unasema kweli unanitania?" alidakia mama mtu huku akikaa sawasawa.
"Nimeachika mama," alisema dada mtu huyo huku akianza kulia.
"Nyamaza! Umeachika kwa sababu gani?" baba mtu alikuja juu…

"Mume wangu alisema amechoka tu kuishi na mimi, akanipa nauli niondoke."
"Siyo kweli, mimi si mtoto wa kunidanganya Ime," alikataa baba mtu. Mama naye akasema…
"Au ulifanya umapepe wako huko?"
"Hapana mama."

Baba mtu huyo alichukua simu yake na kumpigia mkwewe lakini huku naye akishangaa kwamba kama ni kweli kwa nini mkwewe huyo hajamwambia?
"Hujambo baba?"
"Sijambo baba shikamoo?"
"Marhaba, mzima?"

"Mimi mzima kiasi, habari za hapo nyumbani?"
"Njema. Tumeona kimya, nikasema ngoja nikupigie."
"Nipo baba."
"Sasa eti huyu mwenzako alipatwa na nini? Maana kaja hapa tunamuuliza kwa mumeo vipi anasema umemwacha."

"Baba kwani hajawapa barua yangu?"
"Barua! Wala hajatupa, ulimpa barua?"
"Nilimpa barua yenye maelezo ya kutosha kabisa, akasema anaanzia Dar kwa Aisha halafu anakuja huko. Nikajua ni kweli, jana tu nikasikia kaharibu Dar, nikashangaa kugundua kumbe alikuwa bado Dar muda wote huo."

"Mh! Baba mimi nashukuru sana. Kwa sababu umesema kuna barua ngoja nimwambie anipe niisome kwanza halafu nitawasiliana na wewe baba."
"Sawa baba."

Baba mtu alimgeukia binti yake…
"Eti barua yangu iko wapi?"
"Ilipotea baba."

Mzee huyo alisimama na kumfuata mwanaye ili amchape makofi, lakini mama mtu akajitahidi kumzuia asifanye hivyo.
"Mjinga sana huyu mtoto. Kenge mkubwa kasoro mkia wewe. Unataka kutufanya sisi watoto wadogo? Barua haikupotea bali umeipoteza wewe makusudi ili tusijue kilichoandikwa ndani yake, mimi nampigia mumeo aniambie kisa," alisema baba huyo kwa sauti yenye ukali.

***
Aisha alifika nyumbani kwake lakini hakumkuta mume wake, Beka. Akachukua funguo mahali na kuzama ndani bila kumwambia kwamba amerudi.
Beka siku hiyo alikuwa kwa demu wake mpya ambaye alianza kuwa na uhusiano naye siku mbili kabla ya fumanizi lake na shemejiye. Kwa hiyo alikuwa nyumbani kwa demu huyo ambapo si mbali sana kutokea kwake.

"Baby, kwa hiyo ni kweli kabisa mkeo anaweza kukunyima unyumba?"
"Si anaweza, ananinyimaga sana tu."
"Daa! Anakosea sweet," alisema demu huyo anayeitwa Faidha huku akimlalia kifuani Beka na kumkumbatia kwa staili ya mahaba mazito.

"Basi kwangu umefika, hata akikunyima mwaka mzima, mimi nipo dear," alisema Faidha huku akifungu vifungo vya shati la Beka.
 
MH! MISSED CALL YA SHEMEJI!-17

ILIPOISHIA
"Basi baby kwangu umefika, hata akikunyima mwaka mzima, mimi nipo dear," alisema Faidha huku akifungua vifungo vya shati la Beka. Songa nayo...

eka alikuwa akipumua kwa nguvu, kila alipokuwa akimwangalia demu wake mpya, Faidha alivyokuwa akifungua vifungo vya shati lake, akabaki akitweta tu.
"Yule mwanamke alinikera sana," alisema Beka.

"Achana naye bwana, hajui jinsi ya kumuhendo mwanaume, ngoja nimuonyeshe," alisema Faidha, alijua fika kwamba alikuwa mwizi, hivyo alitaka kufanya vitu kwa nguvu zote ili aweze kumchukua Beka jumla.
Kwa sababu alisoma alama zote za nyakati hasa kile kilichokuwa kikitaka kutokea mahali hapo, Beka akachukua simu yake na kuizima kabisa, hakutaka kusumbuliwa kwani aliona muda mchache baadaye angekuwa bize.

"Una kifua kizuri, yaani nashangaa alikuachaje miezi yote hiyo jamani, hana hata huruma," alisema Faidha."We acha tu, hebu endelea kwanza, yule mjinga sitaki hata kumsikia."

Faidha alitumia ujuzi wake wote, mara aukandekande mgongo wa Beka, mara ampeleke huku na kule, yaani kila kitu alichokuwa akikifanya mahali hapo kilikuwa ni kumfanya Beka amuone kuwa bora zaidi, alijua kwamba yeye ni mwizi, hivyo alihakikisha kwamba wizi wake unafanikiwa.

* * *
Aisha alitulia chumbani, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alikuwa akijuta juu ya kile alichokuwa amekifanya cha kumnyima unyumba mume wake kwa muda mrefu.
"Mimi mwanamke kwa nini nimefanya vile? Hivi kama ningefanyiwa mimi ingekuwaje?" alijiuliza Aisha.
Wakati huo, hakujua kwamba mume wake alikuwa kwa demu wake mpya baada ya kuona kwamba mke wake huyo alikuwa akimletea mapozi. Aisha aliendelea kumsubiri mume wake arudi ili akae naye chini na kuyazungumza.

"Kwanza yupo wapi? Mbona anachelewa hivyo? Au kapata demu mwingine?" alijiuliza Aisha lakini hakutaka kukubaliana na mawazo yake, alijua kwamba mumewe ni mwaminifu sana japokuwa alimsaliti kwa dada yake, Ime.

***
Baba Aisha hakutaka kukubali, alijua kwamba Ime alipoteza barua ile kwa ajili ya kupoteza ushahidi juu ya kile kilichokuwa kimeandikwa, hivyo alitaka kumpigia mume wa Ime ili amwambie ukweli.
"Niambie baba."

"Huyu mkeo kapoteza barua, hebu niambie ilikuwaje."
"Unaona baba, nilijua tu hataifikisha, huyo mwanamke mpumbavu sana."

"
Hebu niambie ilikuwaje."
"Ime si mwaminifu kabisaaa, yaani japokuwa nilimuoa, alikuwa akitoka nje ya ndoa bila mimi kujua."
"Unasema kweli?"

"Ndiyo, wewe si umeona hata ule ujinga alioufanya kwa mdogo wake, umekuwa gumzo jiji zima."
"Aiseeee, yaani kumbe ndiyo aliyokuwa akiyafanya?"
"Ndiyo baba. Wakati mwingine anachelewa kurudi, nimemfumania mara kibao tu, akawa ananipiga saundi kwamba alikuwa kwa marafiki zake."
"Kumbeeeee."

"Ndiyo, huyo hafai kuwa mke wangu. Na ndiyo maana hata hiyo barua hakutaka kuileta kwenu."
"Sawa, tutaongea zaidi."
Baba Aisha akakata simu na kuanza kumwangalia Ime, kwa jinsi alivyoonekana tu, alikuwa na hasira tele.

* * *
Mlango ukafunguliwa, Beka akaingia chumbani, macho yake hayakuonyesha mshtuko wala tabasamu, kitendo alichofanyiwa na mke wake, Aisha kilimuuma, sasa alikuwa amefika hapo wayamalize.
"Karibu mume wangu."
"Asante," alisema Beka huku akikaa kitandani, bado alionekana kuwa na kitu moyoni.
"Naomba unisamehe."

"Nikusamehe! Umefanya nini?"
Aisha akanyamaza kwa muda.
"Nilikuwa nakunyima unyumba."
"Kwa hiyo leo ndiyo umeamua kuniomba msamaha baada ya kugundua kwamba lile lilikuwa kosa?"
"Hapana, siyo hivyo, naomba unisamehe tu."

Aisha akaona hiyo haitoshi, alichokifanya ni kumsogelea Beka na kuanza kumshikashika mgongoni, Beka mwenyewe wala hakutaka kushoboka, kila kitu alikimalizia kwa demu mpya, Faidha.
"Sawa, tutaangalia."

"
Jamani, sasa tutaangalia nini baby?"
Beka hakutaka kuongea sana, kile alichokisema kilitosha kabisa, akasimama na kulifuata kabati, akavua nguo, akavaa nyingine na kutulia kitandani.
"Naomba unisamehe mpenzi."
"Mbona yameshakwisha, si umeamua kurudi, yameshakwisha kitambo tu."
"Sawa. Nashukuru."

Wala Beka hakuwa na mawazo na huyo mke wake, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Faidha tu, kwake, kipya kilikuwa kinyemi, hivyo demu huyo alionekana kuwa na nguvu kuliko Aisha.

***
"
Haya sasa endelea kutudanganya, yote yashawekwa kweupeeeee, nimeshayajua," alisema baba Aisha huku akimwangalia Ime.
"Amesemaje?" aliuliza mama.

"Kumbe alikuwa akimsaliti mwenzake, hakuwa akitulia, keshazoea ule mchezo na ndiyo maana akaenda kuurudia hata kwa shemeji yake, yaani hata aibu haoni."
"Nisameheni," alisema Ime huku akijitahidi kuyatafuta machozi.
"Wewe si umejifanya mjanja kupoteza barua, kiko wapi sasa, tumeshajua ujinga wako. Unapata mume wa kuishi naye, unafanya ujinga, hujui kama kuolea dili."

"Nisameheni."
"Kwani umetukosea sisi? Nenda kamwambie mumeo kwamba ulimkosea."

* * *

Mapenzi ya Faidha yalimchanganya Beka, japokuwa alimpiga kalenda mke wake kwamba angemwambia kama alimsamehe au la, lakini bado naye alikuwa na mchepuko wake uliokuwa ukimliwaza.

Beka akabadilika kabisa, akawa anakaa sana kwa mchepuko wake Faidha huku wakati mwingine akilala hukohuko kwa kisingizio cha kazi nyingi.

Aisha akavumilia, hakuwa na jinsi, hakuweza kuondoka nyumbani hapo, ila pamoja na yote hayo, makosa yalikuwa kwake, alilikoroga weee, sasa alitakiwa kulinywa.
"Jamani mume wangu unanitesa."
"Nakutesa?"

"Ndiyo. Kila siku unachelewa kurudi."
"Kazi zimekuwa nyingi mno."
"Sasa mbona hauniambiagi?"
Beka hakutaka kuendelea kujibu maswali zaidi kwani yalimchosha. Alikuwa radhi kukaa kimya na kuanza kuufikiria mchepuko wake kuliko kumjibu Aisha ambaye kwake alionekana muuaji, miezi miwili hadi mitatu bila unyumba, ilikuwa ni shiiiiiida.
 
MH! MISSED CALL YA SHEMEJI!-18

Mwezi mmoja ulikatika tangu Aisha aliporejea kwake kutoka kijijini kwao na kutaka yaishe kwa mumewe lakini mumewe alishakolea kwa Feidha…

"Hivi, huyu mwanamke anayemsumbua mume wangu yukoje kwanza? Anaweza kufanana na mimi au kachangudoa tu?" alijiuliza Aisha na kuamua kufanya mkakati wa kumjua.Siku moja mumewe akiwa anaoga, yeye aliichukua simu yake kwa siri na kuanza kusoma meseji akiamini kuwa, atakutana na meseji ambayo itamjulisha kwamba ni ya mwanamke wa Beka…

"Oyaa! Leo vipi, wapi? Mi nikitoka job nakwenda Migomigo kwenye ile baa ya jana."
Meseji hiyo aliipuuza Aisha, akajua ni ya mwanaume…

"Bro vipi ule mzigo, nikuletee lini sasa?"

Meseji hiyo pia aliipuuza Aisha, akaona ni walewale. Aliendelea kuskroo mpaka akakutana na meseji yenye namba iliyoseviwa kwa jina la ‘Material' akahisi ni yenyewe baada ya kusikiasikia maneno kutoka kwa wanaume yakisema ‘wife material.' Akaifungua…

"Sweet, ile suti uliyosema nimeipata kwenye duka moja mjini, ni shilingi laki mbili na nusu, nimekununulia hivyohivyo maana napenda sana siku moja uvae tukiwa wote."
Aisha alishusha pumzi kwa nguvu, akavuta picha na kumwona mwanamke huyo mbele yake, kwamba ni mzuri kuliko yeye na pia ana kazi nzuri kuliko yake…

"Mpaka amemnunulia mume wangu suti ya laki mbili ina maana yuko vizuri? Mh! Sasa nitamwonaje?" alijiuliza Aisha akapata wazo, akachukua ile namba ya simu na kuisevu kwenye simu yake, akaiandika;

NIKIKUKAMATA!
Beka alipotoka kuoga alimkuta mkewe amebadilika sura lakini hakumuuliza kitu kwani alishaamua kutowasiliana naye kwa undani.

Alijiandaa, akaondoka zake kwenda kazini. Nyuma, Aisha alituma pesa kupitia namba za simu alizochukua kwenye simu ya mumewe, akaambiwa athibitishe anakotuma pesa kabla ya kuingiza password ambapo lilitokea jina la Faidha…

"Mh! Jina zuri lakini," alisema moyoni, akamtumia meseji akisema…
"Mambo Feidha?"

Feidha hakuijibu meseji hiyo, ndani ya nusu saa, akapiga simu. Aisha akahangaika apokee au la! Mwishowe akakaa kimya mpaka simu ikakata, ikaingia meseji ikiuliza…
"Samahani nani mwenzangu? Nilipoteza simu."
"Mimi naitwa Suzy, nataka kukutana na wewe Feidha."

"Samahani sana Suzy, Suzy wa wapi na kukutana kuhusu nini anti yangu? Samahani lakini."
Aisha alianza kupata picha ya aina ya mtu anayechati naye kwamba, kwanza si mshari, mstaarabu na mwenye akili zake timamu…
"Suzy wa Kinondoni, nilipewa namba yako na dada mmoja anaitwa Jane, akaniambia unaweza kunisaidia jambo."

Kutoka moyoni mwake, Feidha alikuwa ana rafiki anaitwa Jane, akampigia kwanza simu ikawa haipo hewani. Alitaka kumuuliza ili ajue kama kuna ukweli kuhusu madai ya Suzy huyo feki.
"Oke. Uko wapi Suzy?"
"Nipo Posta kwa sasa."

"Na mimi nipo kazini hukuhuku Posta, nafanyia CRDB Makao Makuu hapa, njoo."
"Mh!" aliguna Aisha baada ya kusoma meseji hiyo, akajiuliza.
"CRDB Makao Makuu, anafagia ofisi, anahudumia wateja au bosi? Lakini kufagia ofisi asingeweza kumnunulia mume wangu suti, atakuwa ana nafasi fulani hivi."
"Oke, nakuja. Nikifika nikuulizie nani?"

Feidha aliishangaa sana meseji hiyo kwani wakati anaanza kumuuliza alisema mambo Feidha iweje aseme akifika amuulize kwa jina gani?
"Ulizia Feidha tu."
Aisha alijua amechemka kwenye hilo, akaumia sana. Alichanganya miguu hadi benki hiyo na kumuulizia Feidha..

Mhudumu alimuuliza kama ana ahadi naye…
"Ndiyo."
Alipelekwa kwenye ofisi ya Feidha ambako kulikuwa na wadada watatu…
"Haa, Ummy…" alishangaa Aisha…
"Haa, Aisha ni wewe?" alisema msichana huyo akiwa amesimama kumlaki Aisha. Walikumbatiana kwa furaha yote.

"Karibu ukae Aisha," Aisha alikaribishwa kisha huyo Ummy akamgeukia mhudumu …
"Anti, halafu kuna mgeni wangu akija mwambie anisubiri hapo kwenye benchi."
"Sawa bosi."
Aisha alibaki na mawazo ya kasi kichwani mwake …
"Enhe, za siku Ummy?"
"Poa tu. Karibu sana."
"Asante."

Wasichana wengine wawili walikuwa wazuri sana, lakini aliyempokea Aisha, yaani Ummy alikuwa mzuri zaidi kuliko wote. Aisha aliamini kwamba katika wasichana wale wawili mmoja wao ni Feidha.
"Niambie, umejuaje niko hapa?" aliuliza Ummy…
"Ummy wala sijajua kama wewe uko hapa, mi nimemfuata anti mmoja," alisema Aisha akiwa amemsogelea Ummy kwa karibu sana…
"Nani?"

"Kwani hao kuna nani na nani?"
"Mmoja anaitwa Salma, mwingine Magreth."
 
MH! MISSED CALL YA SHEMEJI!-19

ILIPOISHIA
"Niambie, umejuaje niko hapa?" aliuliza Ummy…
"Ummy wala sijajua kama wewe uko hapa, mi nimemfuata anti mmoja," alisema Aisha akiwa amemsogelea Ummy kwa karibu sana…
"Nani?"
"Kwani hapo kuna nani na nani?"
"Mmoja anaitwa Salma, mwingine Magreth."
JILEGEZE NAYO MWENYEWE…


Mh! Kweli? Basi niliyemfuata mimi hapa hayupo," alisema Aisha akiwaangalia wale akina dada, yaani Salma na Magreth.
"We kwani umemfuata nani?" aliuliza kwa shauku Ummy…

"Hebu twende nje nikakwambie," alisema Aisha huku akimwangalia Ummy kwa macho ya kutaka kujua atafanyaje baada ya kumwambia waende nje.
Ummy alisimama, wakatoka huku akiwaaga wenzake…
"Jamani niko mgahawani na mgeni wangu."
"Sawa," alisema Salma.

Baada ya kuondoka, Magreth alianzisha mazungumzo…
"Unajua nimeshangaa sana!"
"Umeshangazwa na nini?"
"Kumbe Faidha anaitwa Ummy?"
"Ee, kweli bwana, hata mimi nilishangaa pia."
"Haya majina haya, usikute Faidha Ally ni mtu mwingine kabisa, ila Ummy kaliibukia jina lake kwenye cheti cha chuo."

"Hilo mbona lipo sana tu."
"Teh! Teh! Teh! Teh! The," walicheka na kuendelea na shughuli zao.

* * *
"Aisha naona unapendeza tu mwenzangu!" alisema Ummy wakiwa wameshatoka nje.
"Wewe je? Mi nilidhani mzungu bwana, kumbe mbantu halisi…"
Walicheka wote huku wakiwa wanaingia kwenye mgahawa mmoja jirani.
Mhudumu alifika, akawasikiliza. Alipoondoka, Ummy akashtuka kwa simu yake kuita…
"Sorry Aisha, napokea simu mara moja."
"Oke."

"Haloo baby…poaaa…niko sawa sijui wewe baby wangu! Vipi mamaa hajambo? Bado anaendelea na mambo yake yale? Ha! Ha! Ha! Nipo job…oke…oke sweet..eee…jamani B…oke baadaye," alimaliza Ummy, akamgeukia Aisha ambaye alionekana anataka kusema neno…
"Naona unaongea na shemeji!"
"Mwenzangu, lazima kubembeleza ndoa kwanza, si unajua tena."
"Kwani ulishafunga ndoa Ummy?"

"Nifunge wapi? Wanaume wenyewe hawanioni, nimejikuta nimeangukia kwenye ndoa ya mume wa mtu."
"Kweli Ummy?"
"Sasa n'tafanyaje Aisha?"

"Mh! Kazi unayo, ungekuwa wewe vipi?" aliuliza Aisha huku akimkodolea macho mwenzake…
"Ningekuwa vipi kivipi?"
"Mume wako akichukuliwa na mwanamke mwingine?"

"Weee! Ningeua mtu Aisha. Mimi nilivyo na wivu, sijui ingekuwaje hakyamungu."
"Kumbe mkuki kwa nguruwe siyo? Basi uache na wewe kuiba waume za watu"
"Tatizo si mimi, ila mwanaume mwenyewe ana bifu na mke wake ndiyo maana nimeibuka mimi kumpa faraja. Lakini anyway, tuyaache hayo shoga yangu, lete habari," alisema Ummy huku akionekana kuwa siriasi sasa kwa kumsikiliza Aisha…

"Ummy, mimi nina matatizo, kuna mwanamke ameingilia ndoa yangu, anafanya kazi hapa benki…" alianza kusema Aisha…
"Benki hii?"
"Ndiyo, benki hii. Nimeongea naye akaniambia yuko kazini ndiyo nikaja."
"Kama ni kweli na amekuona si atakuwa amekimbia!"

"Si rahisi maana nimetumia mbinu nyingine."
"Anaitwa nani?"
"Anaitwa Faidha."
"Faidha?" aliuliza kwa mshutuko Ummy…
"Ndiyo, unamjua?"
Ummy alinyamaza kimya kwa muda kwani yeye ndiye Faidha mwenyewe.

Ummy aliingia chuo akitumia jina la Faidha Ally na ndilo aliloajiriwa nalo kwenye benki hiyo. Hata pale Aisha alipoingia ofisini na kumlaki kwa kumwita jina la Ummy, wenzake, Salma na Magreth walishtuka, wakagundua kumbe Faidha ana jina lingine…
"Kwani vipi Ummy, unamjua?" aliuliza Aisha…
"Hapana, simjui, huyo mume wako anaitwa nani?"
"Beka."

"Mh! Ni mumeo kabisa?"
"Ee, kwani vipi Ummy, unamjua huyo Faidha?"
"Simjui," alisema Ummy akionekana kukosa raha kabisa.
"Ngoja nikuoneshe namba zake za simu, huenda ukamjua," alisema Aisha huku akibofyabofya simu yake. Hilo halikumsumbua Ummy kwani alijua jina lake aliloandikishia kwenye usajili wa laini anayoitumia ni kwa jina la Ummy.

"Namba yake hii hapa," alisema Aisha akimwonesha namba hiyo Ummy.
"Oke…oke! Sasa atakuwa nani?" aliuliza Ummy, akaongeza…
"Mi tangu nimeanza kazi humu ndani huu mwaka wa pili sasa sijawahi kumsikia mtu anaitwa Faidha."
Aisha alishangaa unyonge wa ghafla wa Ummy. Aliamini hayupo sawa kama alivyomkuta kwani uso wake ulionesha waziwazi kwamba ana kitu moyoni mwake.

Aisha, bila kumwambia Ummy aliipiga ile simu ikaita. Aliiweka sikioni huku akisema…

"Nampigia."
Ummy alitaka kushtuka lakini akakumbuka kwamba simu yake aliiacha mezani kwake ndani kwa hiyo hakuna mtu ambaye angepokea.
"Hapokei?" aliuliza Ummy kwa sauti ya chini kidogo kwani bado alikuwa hana raha.
"Hapokei," alijibu Aisha, akapiga tena…

Mara Salma alitokea akiwa kasi ameshika simu ya Ummy…
"Simu yako inaita bosi," alisema Salma huku akimkabidhi.
 
hahahaaaaa huyu mume wa ime mbona anaongea kisela sana na mkwewe looo nimecheka sana
 
MH! MISSED CALL YA SHEMEJI!-20

LIPOISHIA
"Hapokei?" aliuliza Ummy kwa sauti ya chini kidogo kwani bado alikuwa hana raha.
"Hapokei," alijibu Aisha, akapiga tena…
Mara Salma alitokea akiwa kasi ameshika simu ya Ummy…
"Simu yako inaita bosi," alisema Salma huku akimkabidhi.
JIRUSHE MWENYEWE…

Ummy aliiweka simu aliyotoka nayo ndani kwenye mapaja, akaipokea aliyoletewa na Salma ambayo ilikuwa ikipigwa na Aisha wakiwa wote pale.Ummy alihisi kuumbuka kwani simu aliyoletewa ndiyo aliyokuwa akichati na Aisha.

Alijifanya anaipokea, lakini akaikata huku akiendelea kuongea…
"Haloo, niambie mama Eliza, hajambo Eliza? Sisi tupo bwana, tunaendelea na kazi tu, sijui wewe. Haya…sawa nimekuelewa mama Eliza."

Alipomaliza alimwangalia Aisha na kumuuliza…
"Vipi, umempata?"
"Mh! Mtu mwenyewe amekata simu bwana," alisema Aisha huku akimwangalia Ummy kwa macho yenye kuomba msaada.

"Atakuwa amekuona hapo nje akaingia mitini, si ajabu alitaka kutumia jina la benki yetu kufanya utapeli kwamba anafanyia hapa, sisi hatuna mfanyakazi huyo," alisema Ummy.
Baada ya kuongea hayo, ulipita ukimya mkubwa, hakuna aliyekuwa akiongea na mwenzake, si Aisha si Ummy. Walipomaliza vinywaji, Aisha aliaga kuondoka ambapo muda mrefu Ummy alitamani aondoke ili ajue moja.

"Basi sawa, mimi naondoka Ummy."
"Sawa, lini upo nyumbani nije kukutembelea?"
"Mmmh! Wikienda huwa sitokagi, karibu sana."
"Oke, basi nitakupigia kwanza kabla sijaja."
"Sawa."

Ummy akiwa anarudi ofisini alimpigia simu Beka…
"Baby…"
"Yes baby," aliitika Beka akiwa hajui hili wala lile…
"Unajua mkeo leo alikuja ofisini kwangu…"
"Mke wangu alikuja ofisini kwako?"
"Ndiyo baby."

"Kufanya nini na umemjuaje kuwa ni yeye?"
"Mh! We acha tu! Ni stori ndefu sana."
Ummy alimsimulia kila kitu Beka. Beka naye akaanza kuumiza kichwa kwamba, mkewe aliipata wapi namba ya simu ya Faidha. Pia Beka mwenyewe alikuwa hajui kama Faidha ana jina jingine la Ummy.
"Mh! Labda alichukuwa namba yako kwenye simu yangu asubuhi."
"Labda, mimi nilishindwa kumuuliza namba yangu aliipata wapi!"

* * *
Aisha naye aliendelea kuumiza kichwa kuhusu huyo Faidha, kwamba ni kweli alikuwa akimtapeli kufanya kazi pale benki au yupo lakini kafichwa?
Alipofika nyumbani jioni alikaa sebuleni, akachukuwa laptop yake na kuingia kwenye Facebook, akaandika jina Faidha.

"Mh!" aliguna Aisha kwani picha iliyojitokeza hapo ni ya Ummy…
"Mungu wangu, naona kweli au nipo usingizini naota? Faidha ni Ummy?" alisema Aisha.
Akaendelea kupekuwa Facebook hiyo ambapo pia Faidha alijiandika kwamba hana mume jambo ambalo Aisha alilikubali maana alimwambia anatoka na mume wa mtu, aliandika pia anafanya kazi kwenye benki hiyo.

"Ni yeye," alisema akikiri moyoni mwenyewe. Aliendelea kuangalia mambo mbalimbali kwenye Facebook hiyo ambapo alikutana na mambo yaliyompa ushahidi wa moja kwa moja kwamba, kweli yule ni Faidha ana uhusiano na mume wake, mfano alikutana na posti ya Ummy ikiwa imeandikwa hivi:
"Kama unajitambua kuwa ni mke, mpe haki yake mumeo na mheshimu sana ukimtii kwa kila jambo, ukilegea hapo unaweza kunyang'anywa ukabaki na kilio kama akina f'lani."
Pia alikutana na posti nyingine ikiwa na maneno haya…

"Ni aibu kweli, mke anamkatalia mumewe tendo la ndoa, akitoka nje mume watampapatikia, we ulie tu."

"Huyu ni yeye, haya maneno pia yamenilenga mimi, lazima," alisema moyoni Aisha akiumia. Aliangalia juu kwa muda akifikiri cha kufanya, akapata wazo la kumpigia simu Ummy kumweleza uovu wake…
"Haloo Ummy," aliita Aisha baada ya Ummy kupokea…
"Niambie Aisha, upo nyumbani?"

"Nipo, Ummy namshukuru sana Mungu nimemjua Faidha ni nani!"
"Ni nani?" Ummy aliuliza kwa haraka sana.
"Si wewe."
"Mimi?"
"Ni wewe ndiyo."
"Kivipi?"

"Nipo Facebook hapa, naona picha yako, tena umeweka wazi unakofanyia kazi ndiyo hapo nilipokuja ukasema humjui, loo! Ummy, yaani unanichukulia mume hivihivi naona?"
"Khaa! Aisha, mbona sikuelewi?"
"Umeshanielewa, acha hizo bwana."

Ummy alichoona mbele yake ni kukata simu haraka sana kisha akaizima kabisa huku akisonya chini kwa chini lakini moyoni alisema...
"Du! Nimeumbuka. Kweli picha ya kwenye Facebook imeniumbua, hilo halina ubishi hata kidogo. Sasa?" alikosa majibu.

Kwa upande wake, Aisha baada ya kukatiwa simu na Ummy au Faidha, alimwandikia meseji…
"Kata simu, kataa niliyosema lakini ukweli ni kwamba wewe Faidha unatembea na mume wangu, Beka."
Akaituma akisubiri idelive wakati wowote.

* * *
Faidha alichukuwa simu nyingine na kumpigia simu Beka…
"Dear mambo yamemwagika huku…"
"Yamemwagikaje?"
"Mkeo si nilikwambia mpaka pale tulipoachana?"
"Ndiyo. Imekuaje?"
 
MH! MISSED CALL YA SHEMEJI!-21

Kanipigia sasa hivi, kasema amejua Feidha ni mimi, akanilaumu kwa nini namchukulia mume wake, wewe Beka. Da! Nimeumia sana darling ila nimejikaza tu. Yaani, nilipoona anazidi kuchanganya shutuma zake kwangu nikamkatia simu na kuizima kabisa."

"Daa! Kweli kimenuka, sasa?" alihoji Beka kwa sauti ya kukatakata.
"Hata sijui mimi. Unajua alipokuja na kunitambua ni Ummy wakati anaondoka nikampa namba za simu ile nyingine maana aliniomba lakini mimi sikuchukua ya kwanza, alipopiga sikumjua ila sauti nikajua maana si nilitoka kuzungumza naye."
"Kwani we uko wapi?"
"Nyumbani, njoo."

"Mh! Kwani hukumwambia unaishi naye jirani?"
"Hilo sikumwambia na kama Mungu vile, unajua kabla mambo hayajaharibika tulikubaliana niende kwake wikiendi hii kumtembelea."
"Daa! Hapa Feidha nimechangayikiwa sana, yaani hata sijui nini kifanyike ili kumaliza hili soo."
"Baby, mbona sikuelewi?"
"Kivipi?"

"Kwani si tulisema tutaishi pamoja, sasa unaogopa nini mke kujua? Mimi nimeogopa kwa sababu kumbe tunajuana."
"Hebu niache kwanza dear, nitakwambia kitu baadaye lakini.

***
Beka alifika nyumbani kwake gizagiza linaingia, akafikia sebuleni ambapo alikutana na laptop kwenye kochi, mkewe akiwa jikoni.Aliisogelea laptop hiyo baada ya kuona picha ya mwanamke juu akiwa katika mapozi. Alipoifikia, ilikuwa picha ya Feidha akiwa amepozi kwenye makochi sebuleni, nyumbani kwake.
"Mh! Hatari," alisema Beka moyo ukamlipuka lip!

Aisha alitoka jikoni baada ya kusikia mlango unafunguliwa, alipomwona ni mume wake akarudi jikoni huku akimuuliza habari za kazi…
"Poa tu," Beka aliitika kwa mkato na kuzama chumbani. Moyoni alinuia kufanya jambo la tofauti.
Baada ya kumaliza kupika, Aisha alimwita Beka kula lakini akakataa kwa kigezo kwamba ameshiba.
"Mh! Umekula wapi?"
"Hotelini."

"Umeanza lini?"
"Siku yoyote ikitokea."
"Mh! Haya," alisema Aisha na kutoka chumbani kwenda kula. Chakula hakikupanda kivile! Aliacha!

Alikaa sebuleni akiangalia tivii, mwisho alihisi anapata tabu tu, akaenda chumbani kwa mumewe…
"Beka," aliita Aisha.
"Nini?" Beka aliitika.
"He! Ndiyo kuitika gani huko?"
"Unataka kuongea na mimi au?" Alihoji Beka.
"Ndiyo."

"Ongea basi."
"Nataka kuuliza."
"Uliza."
"Feidha au Ummy ndiyo nani?"
"Ni mwanamke wangu nilipanga kumuoa awe mke wa pili maana dini inaniruhusu."
"Unasemaje Beka?"

"Ina maana hujanisikia au?"
"Kwa hiyo unataka kuoa mke wa pili?"
"Ndiyo maana yake."
"Kisa nini?"

"Kisa cha kufanya nini?"
"Wewe kuoa mke wa pili?"
"Si unakijua."
"Sikijui."

"Nataka mke ambaye hawezi kuamua kuninyima unyumba akiwa anajua mimi ni mume wake. Ndiyo kisa!"
Aisha aliishiwa nguvu kwani ukweli uliobaki ndani ya moyo wake aliujua kwamba, ni kweli amekuwa akimnyima unyumba mume wake na hata katika kikao cha wazazi wake walionesha kukerwa sana na hilo.
"Mimi nadhani badala ya kuoa mke wa pili, niandikie talaka yangu umuoe yeye awe mke wako mmoja ndani ya nyumba," Aisha alitingisha kiberiti.

"Oke, kama limetoka moyoni mwako nafurahi sana, unaitaka saa hivi?"
"Nini?"
"Hiyo talaka."
"Hapa haachwi mtu nakwambia Beka."
"Kwani aliyesema anaacha mtu nani, si umetaka mwenyewe?"
Aisha alitoka, akaenda kukaa sebuleni. Alianza kumtumia meseji za vitisho Feidha…
"Kama lengo lako ni kuniondoa kwenye ndoa yangu, huwezi na utaondoka wewe."
Meseji ilideliva kwa Feidha, akajibiwa…

"Mimi nadhani ungetengeneza kwako kwanza ndiyo unigeukie mimi. Mwenyewe nimeumia sana kuona nimetembea na mume wa rafiki yangu, ndiyo maana ulipokuja kazini nilikuyeyusha maana pale si sehemu salama kuzungumzia masuala binafsi, lakini sasa niko tayari."
"Umeanza lini na mume wangu?" aliuliza Aisha.
"Hilo swali hata ukimuuliza yeye atakujibu, si amesharudi uko naye!"
"Kwa hiyo unanijibu utumbo siyo Ummy?"

"Umetaka mwenyewe Aisha. Ungekuwa mpole ukapewa ushirikiano, lakini meseji yako moja umenitumia kali sana. "Mume wako nampenda sana na siwezi kumwacha kwa sababu wewe ni mburula tu."
 
Itaendelea saaaa mbiliiiiii hapa hapaaaa!!!!!!!!!!!!!!!
 
umeona me nilisema aisha yupo kama zuzu vile yani hashirikishi ubongo mburula kweli kweli
 
Itaendelea saaaa mbiliiiiii hapa hapaaaa!!!!!!!!!!!!!!!

Halafu daudi eehh unaonaje kama hii story nikiibeba mie halafu niiongezee utamu kisha nitoe kitabu hicho? Naimani kitatumika sana mashuleni ni tamthiriya inayoaskisi maisha ya ukweli kabisa ya leo hapa bongo!
 
Back
Top Bottom