SoC01 Misingi ya Utawala Bora na Uwajibikaji

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Jun 3, 2021
544
558
Ili kuendana na dunia ya sasa inayopiga hatua katika ukuaji wa sayansi na teknolojia, suala la uwajibikaji wa viongozi wetu na wale waliopewa mamlaka kuhakikisha wanatawala kwa kufuata misingi ya haki na usawa ni katika mambo ya msingi sana na muhimu katika jamii yetu. Sawasawa wawe viongozi wa serikali au viongozi katika sekta au mashirika binafsi.

Kuwajibika ni mtu kutekeleza kile anachopaswa kufanya katika wakati husika. Dhana ya uwajibikaji inapozingatiwa kwa viongozi wetu hufanya uongozi na utawala wao kuwa bora. Kwani katika kuwajibika kunalazimu mhusika kufuata taratibu na miiko ambayo kwa kuichunga haki na usawa hupatikana.

Hivyo kwa ufupi naweza kusema utawala bora pamoja na viambata vingine, unategemea uwajibikaji wa viongozi katika tawala au nafasi zao.

Katika jamii yetu, serikali inapambana sana katika kuhakikisha watendaji wake wanakua na weledi wa kazi, maadili ya kazi, lakini pia wanawajibika ili kuhakikisha utawala bora, na ndio maana kupitia sheria zilizowekwa serikali ikaanzisha wizara/kitengo maalumu kwa ajili ya kuhakikisha kinasimamia masuala ya utawala bora na uwajibikaji wa watendaji wa serikali. Aidha kwa upande wa sekta binafsi nako kuna vitengo maalumu vya kupima maadili na uwajibikaji wa wafanyakazi, vitengo ambavyo taasisi husika huunda ndani yake au ni taasisi za nje maalumu zinazojishugulisha na suala hilo.

Kiongozi kuwajibika sio wito bali akidi inamuhitaji awe hivyo. Kiongozi muwajibikiaji ndio kiongozi mwenye sifa ya kuwasimamia wananchi mambo yao. kiongozi anaposhindwa kuwajibika huo ndio wakati sasa wananchi wanawajibika wamuwajibishe kiongozi wao. Sambamba na mambo mengine, uwajibikaji wa kiongozi kwa anaowaongoza huleta natija katika mustakbali wa jamii husika kama ifuatavyo;-

1) Uwajibikaji ni miongoni mwa vichocheo vya utawala bora

Hapa nitatoa mifano halisi. Tukirudi nyuma kwenye awamu ya nne ya utawala wa serikali hapa Tanzania, tutagundua kuwa awamu hiyo ilikosa uwajibikaji kwa baadhi ya watendaji wake jambo ambalo liliipunguzia serikali viwango vya utawala bora, ijapokuwa viashiria vingine kama vile uhuru wa kidemokrasia, uwazi, na uchungwaji wa haki za binadamu viliifanya serikali ionekane kuwa na utawala wenye misingi ya uwajibikaji hivyo kuonekana bora.

Aidha kwa upande wa awamu ya tano, serikalli ilihakikisha watendaji wake wanawajibika kwa kiwango kikubwa sana jambo lililopelekea kuonekana utawala ule kuwa bora kuliko tawala zingine zote zilizotangulia. Kiasi awamu ya tano ikawa inasifiwa hata kwa mataifa ya nje juu ya uwajibikaji na kuifanya Tanzania ikisemwa kuwa mfano wa utawala bora. Hata hivyo, bado kuna baadhi ya mambo yalitia doa sifa hiyo adhimu. Miongoni mwa mambo hayo ni kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari, kukabwa kwa demokrasia na vyama vya siasa, matumizi mabaya ya nguvu za dola kwenye shuguli za kiraia, na mengine mfano wa haya yaliiharibia nchi yetu ile hadhi na sifa ya kuwa na utawala bora.

2) Uwajibikaji huchochea maendelea kwa kiasi kikubwa

Muda ambao ungetumika kutatua migogoro mbali mbali iliyosababishwa na kukosekana kwa uwajibikaji hutumika katika mambo yenye kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

3) Uwajibikaji huleta haki na usawa na huondosha manung’uniko na lawama kwa viongozi kutoka kwa raia

Kwa kuwa misingi ya sheri huwa ndio dira, kila kitu hufanywa kwa kufuata sheria na kanuni, hivyo haki na usawa huakikishwa na kuondosha upendelea matokeo yake raia huishi bila ya manung’uniko kwa viongozi wao. Jambo litakalopelekea wao kupata muda mwingi wa kujishugulisha kwenye shuguli za kimaendeleo.

4) Uwajibikaji huzuia mianya ya rushwa

Kiongozi akiwajibika hufanya hata anaowaongoza kuwajibika pia. Kila mmoja akiwajibika kazi hufanywa kwa ufanisi na kila mmoja huwa na moyo wa kujituma kiasi mianya ya kumfanya mtu aombe au apokee rushwa hufungwa.

5) Uwajibikaji ni sifa kwa taifa mbele ya mataifa mengine

Nchi yeyote yenye utawala bora husifika mbele ya mataifa na hua mfano wa kuigwa kiasi mataifa mengine yakafanya safari kuja kujifunza katika nchi yenu. Ambapo ukiacha sifa za taifa, lakini hata raia huwa na soko katika soko la ajira la kimataifa kutokana na kusifika kwa uwajibikaji.

MISIGI YA UTAWALA BORA

Haki na usawa

Kiongozi ndiye msimamizi wa haki za anaewaongoza. Ubora wa utawala/uongozi wake utapatikana endapo atahakikisha kila mmoja anapata haki yake na hukumu na mgawanyo wa stahiki unakuwa ni kwa usawa kwa wote.

Mgawanyo wa madaraka na rasilimali zingine uzingatie usawa wa kijinsia, na makundi mengine ya kijamii. Katika hili serikali ya CCM ya awamu ya tano ni mfano mzuri sana katika kuzingatia usawa wa kijinsia hasa katika nyadhifa za juu za utawala. Kwa mara ya kwanza mwaka 2015 CCM ilimpitisha mwanake kuwa mgombea mwenza wa uraisi. Jambo ambalo huko nyuma halikuwahi kutokea.

Utawala bora hauna ubaguzi wa raia kwa mujibu wa rangi, dini, tabaka, kanda, ulemavu, nk. Kila mtu anakua na haki sawa.

Ukweli na uwazi
Uongozi bora unakua na tabia ya kusema kweli hasa juu ya kila kinachowagusa wanaoongozwa. Na mambo yote yanayowahusu waongozwa hufanywa kwa uwazi kuanzia chini kabisa katika ngazi ya utawala mpaka juu kwenye kamati za maamuzi. Ukweli na uwazi unatakiwa uwe katika kufanya maamuzi, kuchagua na kuteua viongozi, kugawana rasilimali, kuwajibisha na kutoa hukumu, mikataba, nk. Uongozi unaogubikwa na usiri agalabu hua na uovu unaofanywa na viongozi husika na ndio maana huficha ili wasifahamike na isifahamike hila zao.

Ushirikishaji
Utawala bora wenye kufuata misingi huwa ni utawala shirikishi. Wale wenye kufanyiwa maamuzi ambao ndio wawajibikaji wa mipango iliyowekwa washirikishwe kwenye kupanga na kuchagua. Kwa mfano, katika nchi yetu wabunge ndio wawakilishi wa wananchi kwenye Bunge tukufu ambalo ndio chombo kikubwa cha kupanga kufanya maamuzi. Kuhakikisha utawala bora, wabunge wanatakiwa kufikisha mawazo ya wananchi katika majimbo yao kwenye Bunge na sio maoni kutoka mfukoni mwake.

Nimpongeze Mbunge wa jimbo fulani kwenye Bunge lililopita hivi karibuni, alipoulizwa juu ya kwa nini yeye hachangii katika ajenda ya Raisi kuongezewa muda wa utawala akajibu hayo siyo aliyotumwa na wananchi wa jimboni kwake hivyo hawezi kuwasemea jambo ambalo hawajamtuma akawasemee. Hili liliashiria juu ya utawala bora na uwajibikaji.

Utawala usioshirikisha wananchi wake katika kupanga na kufanya maamuzi huo sio utawala bora.

Uhuru wa misingi ya kidemokrasia
Kwa mujibu wa demokrasia kila mtu ana uhuru, ana haki na ana wajibu. Utawala bora unachunga uhuru, haki na wajibu wa raia wake. Raia kwa makundi yao tofauti wana uhuru wa kufanya baadhi ya mambo pasi na kuvunja sheria na kanuni zilizowekwa. Utawala bora utoe uhuru kwa kuwaruhusu raia kutoa maoni, kukosoa uongozi na viongozi kwa adabu, kujieleza na kujitetea, kuchagua kiongozi wanayemtaka, nk. Wakosoaji wa kubwa wa serikali iliyopo madarakani ni vyama vingine vya siasa na wanaharakati. Makundi haya muhimu yapewe uhuru wa kusema mabaya (kukosoa) na mazuri (kusifia) ya serikali iliyopo madarakani.

Uongozi unaozuia raia kuwa na uhuru wa kidemokrasia huo sio uongozi bora, hasahasa pale ambapo nchi au taasisi husika inapojinadi ni yenye kufuata mfumo wa demokrasia katika utawala wake.

Kufuata sheria
Sheria hutungwa ili zifuatwe na kila mmoja, sawasawa awe ni kiongozi, mtawala, mtumishi, au raia wa kawaida. Watu wote wapo chini ya sheria na hakuna aliye juu ya sheria. Na katika nchi sheria zote hutungwa kutoka katika chimbuko mama nalo ni katiba.

Hivyo uongozi bora huendesha mambo yake kwa kufuata katiba ambayo ndio chimbuko la sheria zote zilizotungwa. Na pale inapoonekana katiba ina mapungufu fulani aidha kwa kupitwa na wakati au ikashindwa kukidhi mahitaji ya wakati huo basi uongozi bora hutoa nafasi kwa raia kupendekeza mbadala wa kile chenye mapungufu. Na ndioa maana tunasikia baadhi ya nchi wamefanya marekebisho ya katiba yao na kuwa na katiba mpya.

Katika kuhakikisha utawala bora, serikali ya awamu ya nne ya Tanzania iliruhusu mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya baada ya kujiridhisha kuwa katiba iliyopo ina baadhi ya mapungufu. Mapungufu ambayo husababisha baadhi ya viongozi kutowajibika au kutowajibishwa wanaposhindwa kuwajibika.

Kutanguliza maslahi ya wengi
Uongozi ulio bora na wenye kuwajibika hutanguliza mbele maslahi ya wengi kabla ya maslahi ya wachache. Na hii ni matokeo ya ushirikishaji katika kupanga na kufanya maamuzi. Kwa mfano katika taifa, lile jambo ambalo lina tija kwa raia wote kwa ujumla kama taifa moja hilo lipewe kipaumbele na sio jambo ambalo baadhi ya watu wachahe watanufaika kwalo. Na hili lizingatiwe hasa katika kuingia mikataba mikubwa ya kitaifa, katika mikataba hiyo maslahi ya wengi yapewe kipaumbele na si kupitisha mikataba yenye kuwanufaisha wachache.

MADHARA YA KUTOKUWA NA UTAWALA BORA

Madhara makubwa ambayo nchi hukumbwa kwa kukosa utawala bora ni kuongezeka kwa vitendo vya unyayasaji, upendeleo, rushwa, wizi, ubadhilifu wa mali za uma, ongezeko la uhaba wa ajira, ukwepaji wa kodi, uhalifu kwa njia zake zote nk. Ambavyo kwa mjumuiko wake hupelekea taifa kuingia katika umasikini uliotopea.

Nchi kuwa na vurugu zenye kuambatana na maandamano yenye kusababisha nchi kushindwa kutawalika ni miongoni mwa madhara yanayotajwa ya kukosa utawala bora.

Viongozi kuwa na kiburi kwa raia na kufanya vile wanavyotaka. Nchi au taasisi ambayo haina utawala bor mambo huwa shagala bagala, kila mtu anajifanyia mambo yake vile anavyoona yeye inafaa bila kujali anakiuka miiko na kuvunja sheria au la.

NENO LA MWISHO

Ni juu ya viongozi wetu kuhakikisha wanatuongoza kwa kufuata misingi ya utawala bora. Ili kuendana na kasi ya dunia ya sasa ambayo kila kukichwa inapiga hatua kwenda mbele hatuna budi kujizatiti katika nyanja mbalimbali hasa tukianzia katika kuwapiga msasa viongozi wetu ili wawe viongozi bora, kwani kiongozi bora huwa muwajibikaji na hutuelekeza kunako utawala bora.

DustBin
 
Back
Top Bottom