Tuendelee...
SHUSHUSHU WA KISOVIETI NA MWILI WA MTU BAHARINI
Sehemu ya Tano.
Ile ndege ikageuka na, lisaa limoja baadae ikatua Israel, kuashiria mwisho wa operesheni Injinia ( sio jina lake halisi), operesheni hii ikawa ya usiri wa hali ya juu kwa zaidi ya miaka hamsini. Mwaka 1949, ndugu wa tatu wa kiume kutoka familia moja ya kiyahudi huko Bulgaria waliwasili Haifa. Mkubwa wao, Alexander Israel, alikuwa amehitimu katika chuo cha Uinjinia huko Sofia. Akajiandikisha jeshini, akapewa cheo cha ukapteni, na akapangiwa kwenye jeshi la wanamaji wa Israel.
Kapteni Israel alikuwa ni kijana mwenye mvuto na mchangamfu sana. Alithaminiwa na wakubwa zake na akapangwa katika utafiti wenye usiri wa hali ya juu katika vita vya kielektroniki na utengenezaji wa silaha mpya. Akapewa kibali cha usalama cha hali ya juu na aliweza kushuhudia na kuwa karibu na nyaraka na vitu vingine vingi ambavyo ni vya nyeti sana. Akabadili jina lake lakwanza kuwa Avner, jina la kiebrania, na mwaka 1953 akamuoa Matilda Arditi, msichana mrembo mwenye asili ya Uturuki.
Wawili hawa wakaweka makazi huko Haifa, karibu na ngome kubwa zaidi ya Kijeshi ya Israel. Matilda alimpenda sana huyu mume wake mwenye mvuto, ila hakujua mapungufu yaliyokuwa katika utu wake. Hakujua kama alikuwa na rekodi ndefu na mbovu huko polisi. Avner Israel alituhumiwa kwa kukodishia jengo moja la makazi mara kadhaa kwa mpangaji zaidi ya mmoja; kwa kujifanya kama muwakilishi wa kampuni ya kuuza friji na kukusanya malipo ya awali kwa friji ambazo hazikukabidhiwa kwa waliotoa fedha; na dili nyingine kadhaa za sampuli hiyo.
Kesi moja ilifika mahakamani, na akapewa wito wa kufoka mahakamani kwa kesi November 8, 1955. Matilda akiwa amebanwa na majukumu ya mtoto, hakujua chochote juu ya utapeli wa mume wake, wala mahusiano yake na karani mrembo katika ubalozi wa Italia huko Haifa. Avner hata alimchumbia na kuweka nia ya kumuoa, ila huyu msichana wa kiitalia alikubali kwa sharti moja: lazima kwanza abadili dini na kuwa mkatoliki.
Kwa kijana Avner hili halikuwa tatizo hata kidogo. Alishawahi kubadili dini mara moja kabla, huko Bulgaria, wakati alipolazimika kumuoa msichana mwingine wa kikristu ambaye alimtongoza. Familia yake iliyokuwa imekasirishwa ilimtaka - karibu kwa kumtisha na bunduki - kwamba abadili dini na amuoe huyo msichana.
Mara tu baada ya harusi akakimbia Sofia, mke wake akajiua, na kisha akarudi Sofia na kurudia dini yake ya 'Judaism'. Sasa akarudia tena. Alisafiri kwenda Jerusalem akiwa na 'mpango wa kando', akabatizwa kwenye konventi ya Terra Santa, na akabadili jina lake kuwa Ivor. Kwa kutumia nyaraka alizopatiwa na kanisa, kapteni huyu mchangamfu alijisajili na wizara ya mambo ya ndani na akapatiwa passi ya kusafiria kwa jina lake jipya, Alexander Ivor.
Yeye na 'bi mdogo' wa kitaliano wakapanga November 7, 1954, kama tarehe ya harusi yao. Ile kesi kule Haifa ilipangwa kusikilizwa November 8. Avner Israel, aka Alexander Ivor, hakuwa na nia ya kuhudhuria hayo matukio yote. Muda ulikua umewadia kwa yeye kupotea.
Mwishoni mwa October, kapteni Israel alienda kwenye likizo ya wiki mbili. Alikuwa hana Visa ya kutoka ila Alexander Ivor alikuwa nayo, na nyaraka zinazojitosheleza, nyingine halisi, nyingine zakugushi. Akanunua tiketi ya ndege kwenda Rome, na November 4 aka...
Itaendelea....