Misheni kubwa za taasisi ya upelelezi MOSSAD!

Misheni kubwa za taasisi ya upelelezi MOSSAD!

Paul Alex

JF-Expert Member
Joined
Jul 14, 2012
Posts
4,346
Reaction score
9,846
1.MFALME WA VIVULI

Sehemu ya kwanza

Wakuu naomba niwatafsirie kitabu kilichoandikwa na Michael Bar-Zohar na Nissim Mishal 'The greatest mission of the Israel secret service Mossad'.

Natafsiri kitabu hiki kama shukrani kidogo kwa makala nyingi nilizosoma hapa kwenye jamii intelligence... watu wametumia muda wao na vipaji vyao kunipa taarifa na kupanua uwezo wangu wakuona mambo hivyo sioni vibaya kama nami nikijita kuandika kidogo...

Story zinazoelezwa katika kitabu hiki ni za kweli kabisa na hata rais wa Israel - Shimon Peres alisema, 'ni mambo ambayo ulimwengu ulipaswa kuwa umeyajua kwa muda mrefu'.

Moja kwa moja nitaanza na sura ya kwanza- King of the shadows au mfalme wa vivuli kwa kiswahili...

Ilikua ni mwishoni mwa majira ya joto, mwaka 1971, mawimbi makali yakipiga katika ufukwe wa Mediterranean na mawimbi makali zaidi yakionekana kuushinda ufukwe wa Gaza. Kwa busara kabisa wavuvi wadogowadogo wa Kiarabu walikaa mbali na fukwe; hii haikuwa siku nzuri ya kushindana na bahari iliyoonyesha kuchanganyikiwa.

Walitazama kwa mshangao wakati boti moja ilipojitokeza katika mawimbi yaliyokua yakinguruma ilipotua kwanguvu katika mchanga ulioloana maji ufukweni. Wapalestina wachache, nguo zao na shungi zao zikiwa zimeloana maji, waliruka kutoka kwenye boti na kukimbilia ufukweni. Sura zao zilizokua hazijanyolewa ndevu zilionyesha uchovu wa safari ndefu baharini, ila hawakua na muda wa kupumzika, walikua wakikimbia kuokoa maisha yao.

Kutoka kwenye bahari iliyokasirika, boti ya kivita ya Israeli ilitokea, ikiwakimbiza kwa speed kali ikiwa na wanajeshi waliovalia kivita. Iliposogelea ufukwe, wale wanajeshi waliruka kwenye maji madogo na kuanza kumimina risasi kwa uelekeo wa wale wapalestina waliokua wanakimbia. Vijana kadhaa wa Gaza waliokua wakicheza kwenye ufukwe waliwakimbilia wale wapalestina na kuwaelekeza sehemu salama kwenye shamba la matunda; wanajeshi wa kiisrael wakapoteza uelekeo wa wale wapalestina ila wakaendelea kuwatafuta ufukweni.

Baadae kabisa usiku huo kijana wa kipalestina aliyebeba bunduki ya Kalashnikov aliingia kwenye shamba la matunda kuchunguza.
Akawakuta wale wapalestina wamejikusanya pamoja kwenye moja ya kona za shamba."Nyie ni akina nani, ndugu?". Aliuliza.
"Sisi ni wanachama wa chama cha ukombozi wa wapalestina- PFLP" likawa jibu."Kutoka katika kambi ya wakimbizi ya Tyre, Lebanon." "Marhaba, karibuni," yule kijana akasema. "Mnamjua Abu-Seif, kamanda wetu? Alitutuma tukutane na kamanda wenu Beth Lahia (kambi kuu ya magaidi kusini mwa ukanda wa gaza).Tuna hela na silaha, na tunataka kuunganisha oparesheni zetu.”"Nitawasaidia kwa hilo", yule kijana akasema.

Asubuhi iliyofuata, magaidi kadhaa wenye silaha wakawasindikiza wageni kwenye nyumba iliyojitenga pembezoni ndani ya kambi ya wakimbizi ya Jabalia. Wakaongozwa katika chumba kikubwa na wakakaribishwa kukaa mezani. Muda kidogo baadae, kamanda wa popular front waliyetegemea kukutana nae akaingia. Wakabadilishana salamu za upendo na ndugu zao wa Lebanoni, na wakakaa kwa kwa kuangaliana.

"Tunaweza kuanza?" Aliuliza kijana mwenye mwili uliojengeka aliyevalia ushungi mwekundu, ambaye alionekana kuwa kiongozi wa lile kundi la walebanoni.
"Kila mtu yupo?"
"Watu wote wapo!". Yule mlebanoni akanyanyua mkono wake kuangalia saa. Hii ilikua ishara waliyokubaliana kabla. Ghafla, 'wale wageni wa Kilebanoni' wakatoa bastola zao na kuanza kumimina risasi. Ndani ya dakika moja, magaidi wa Beth Lahia walikua wamekufa.

'Walebanoni' wakakimbia kutoka kwenye nyumba, wakapita katika viunga vya kambi ya Jabalia na mitaa iliyojaa watu ya Gaza na muda mfupi wakawa ndani ya ardhi ya Israel. Jioni ile, kijana aliyekua na ushungi mwekundu, kapteni Meir Dagan, kamanda wa IDF (Israel Defense Forces) na kikundi cha siri cha makomando (Rimon Commando unit), Akaripoti kwa jenerali Ariel (Arik) Sharon kuwa operesheni 'kinyonga' imefanikiwa. Viongozi wote wa Popular Front Beth Lahia, kikundi hatari cha kigaidi, wameuawa.

Itaendelea....
 
Uzi mtamu sana nimekaa kitako niusone huku nikisubiria game ya united na arsenane ghafra umeukatisha[emoji30][emoji30]
 
Tuendelee...

MFALME WA VIVULI

Sehemu ya pili

Dagan alikuwa na miaka ishirini na sita tu (26) ila tayari alikuwa mpiganaji aliyetukuka. Aliiplani operesheni yote peke yake: kujifanya gaidi wa Lebanoni, kusafiri na boti ya kizamani kutokea Ashdod, bandari iliyopo Israel, usiku mrefu wa kujificha,kukutana na viongozi wa kigaidi, na njia ya kutorokea baada ya mauaji. Alipangilia pia tukio la kuigiza la kukimbizwa na boti ya kijeshi ya Israel.

Dagan alikua mpiganaji wa mstuni (guerilla) aliyeiva, mbunifu asiyesita, na sio mtu aliyefungwa na kanuni za mapigano. Yitzhak Rabin aliwahi kusema:" Meir ana uwezo wa kipekee wa kubuni operesheni za kupambana na magaidi zinazofanana na sinema za kusisimua".

Danny Yatom (mkurugenzi wa Mossad kwa siku za mbele) anamkumbuka Dagan kama kijana chipukizi mwenye mwili uliojengeka na mwenye nywele za kahawia, ambaye aliomba kujiunga na kikosi kilichotukuka sana cha makomandoo cha Sayeret Matkal,na akamshangaza kila mmoja kwa uwezo wake mkubwa wa kurusha kisu. Kwa kutumia kisu chake kikubwa cha makomandoo aliweza kulenga shabaha yoyote kwa uwezo mkubwa wa kufisha.
Japo alikuwa mlengaji mzuri wa shabaha ila alishindwa mitihani ya Sayeret Matkal hivyo alilazimika kuridhia medali ya shaba ya uaskari wa mwavuli.

Mapema miaka ya sabini alipelekwa ukanda wa Gaza, ambao ulikua umetekwa na Israel mwaka 1967 katika vita ya siku sita (Six-Day war) na baada ya hapa ukawa ni kiota cha operesheni hatari za kigaidi.
Magaidi wa kipalestina walikua wakiwaua waisraeli kila siku katika ukanda wa gaza na ndani ya Israeli kwa mabomu, milipuko, bunduki; Jeshi la Israel (IDF) lilishindwa kabisa kuweka utulivu katika kambi za wakimbizi zilizojaa matukio ya hatari.
Tarehe 2/01/1971, wakati watoto wazuri wa Arroyo, Avigal aliyekua na miaka mitano na Mark aliyekua na miaka nane walipopasuliwa vipande vipande na bomu lililotupwa kwa mkono ndani ya gari yao, jenerali Ariel (Arik) Sharon aliamua kuwa imefika wakati umwagaji wa damu huo wa kikatili ufike mwisho.

Aliamua kuwaingiza kwenye shughuli marafiki zake wachache waliopigana pamoja ujanani pamoja na vijana wachache wenye vipaji vya kipekee. Dagan alikua mmoja wao, kijana mwenye uso wa mviringo, mfupi na ofisa makini aliyetembea kwa kuchechemea- alikanyaga bomu la kutegwa ardhini katika ile vita ya siku sita. Wakati akipata huduma katika hospitali ya Soroka Beer-Sheva, alizama kwenye penzi na nesi aitwaye Bina. Na alipopona wakaoana. Hiki kikosi cha Sharon hakikutambuliwa kiofisi, kilikua hakipo. Misheni yao ilikua kuteketeza vikundi vya kigaidi kwa kutumia mbinu hatari na hata zisizokubalika kimapambano.

Dagan aliweka mazoea ya kutembea ukanda wa gaza akiwa na bakora, mbwa aina ya doberman, bastola kadhaa na aina mbalimbali za bunduki. Kuna wanaosema waliwahi kumuona akiwa amejinadili kama muarabu, akitembea na punda kwa starehe katika viunga hatari ukanda wa Gaza. Tatizo lake la mguu halikuondoa nia yake katika kutekeleza operesheni za hatari. Mtazamo wake ulikua rahisi sana. Hawa ni maadui, waarabu wabaya wanaotaka kutuua, hivyo tunatakiwa kuwaua wao kwanza.

Ndani ya hichi kikosi, Dagan akatengeneza 'Rimon', kikosi cha siri cha kwanza cha makomandoo wa Israel, ambacho kilifanya operesheni katikati ya ngome za maadui kwa kujibadilishabadilisha.
Ili kutembea kwa uhuru katikati ya umati wa waarabu na kufikia shabaha walizozitaka ilibidi wafanye hivyo kwa kujibadilibadili. Walifahamika haraka kama timu ya wauaji ya Arik na uvumi ulisambaa kwamba mara kadhaa waliwakamata magaidi na kuwaua hata kama walikua hawawezi kujitetea. Wakati mwingine inasemekana, waliwapeleka magaidi kwenye viunga vya giza na kuwaambia:"una dakika mbili za kutoroka", walipojaribu, waliwapiga risasi. Wakati mwingine walimuachia gaidi kisu au bunduki, akijaribu kukamata, anauawa papo hapo.

Waandishi wa habari waliandika hivyo kila asubuhi, Dagan alitoke kwenda mashambani, akitumia mkono mmoja kukojoa na mwingine kulengea kopo la koka. Dagan alikuwa akikataa habari hizo. "Hizo ni story za kufikirika tunazoziamini," alisema, "ila baadhi ya yanayoandikwa ni uongo kabisa".
Hiki kikosi kidogo cha makomandoo kilikua kinapigana vita ngumu, vita isiyo na huruma, wakihatarisha maisha yao kila uchwao. Karibu kila siku usiku kikosi cha Dagan kilivaa kama wanawake au wavuvi na kwenda kuwatafuta magaidi wasiojulikana.

Katikati ya mwezi wa kwanza 1971, wakijifanya kama magaidi wa kiarabu, walifanikiwa kuwadanganya wanachama wa Fatah kuingia katika shambulio, na mapambano ya bunduki yalipoanza, wanachama wa Fatah wote wakauawa.
Tarehe 29 januari 1971, wakati huu wakiwa katika sare, Dagan na watu wake walisafiri katika jeep mbili mpaka maeneo ya kambi ya Jabalia ( kambi ya wakimbizi wa Palestina). Njiani waliposhana na texi na Dagan alifanikiwa kumtambua moja kati ya abiria kama gaidi mbaya zaidi Abu Nimer. Akaziamuru geep kusimama na askari wake wakaizunguka ile texi. Dagan akaisogelea texi na wakati huo Abu Nimer alitoka ndani ya tex akiwa ameshikilia bomu la mkononi na kutoa pini yake. "Bomu!" Dagan alipaza sauti, ila badala ya kujificha, alimrukia na kumkamata, akamnyang'anya bomu mkononi.
Kwa kitendo hichi alizawadiwa medali ya ujasiri. Inasemekana kwamba baada ya kulitupa bomu mbali, Dagan alimuua Abu Nimer kwa mikono yake mitupu.

Miaka mingi badae katika mahojiano ya nadra na mwanahabari Ron Leshem, Dagan alisema:"Rimon haikuwa timu ya wauaji.. haikua wildwest, ambapo kila mtu alijisikia raha kupiga risasi. Kamwe hatukuumiza wanawake na watoto.. tulishambulia wauaji katili......


Kesho mchana tuendelee.....
 
Tuendelee....

MFALME WA VIVULI

Sehemu ya tatu.

.... Tuliwaua na wengine tuliwapunguzia uwezo na kuwakatisha tamaa. Kulinda raia, serikali wakati mwingine inahitaji kufanya mambo ambayo yako kinyume na matakwa ya kidemokrasia.

Ni kweli kwamba katika vikosi kama chetu, mipaka ya utendaji inaweza isionekane vizuri. Hii ndio maana unatakiwa kuhakikisha kuwa watu wako ni wa viwango vilivyo tukukuka sana. Matendo machafu zaidi yanapaswa kutekelezwa na watu waungwana sana.

Kwa kutumia mbinu zinazokubalika na zisizokubalika kidemokrasia, Dagan na kikosi chake kwa kiasi kikubwa walimaliza ugaidi Gaza, na kwa miaka mingi mbele eneo hili likawa kimya na amani tele. Ila kuna wanaosema kuwa, kuna wakati Sharon alisema kama nusu hivi kwa utani," Taaluma kubwa ya Meir ni kutenganisha kichwa cha mwarabu kutoka kwenye mwili wake". Ila bado wanaomfahamu Degan wa kweli ni wachache. Alizaliwa akiitwa Meir Huberman, mwaka 1945 ndani ya kiberenge cha treni, nje kidogo ya Herson, Ukraine, wakati familia yake ikikimbia kutoka Siberia kwenda Poland.
Wengi katika wanafamilia wake waliuawa katika mauaji ya kimbari ya halaiki. Meir akahamia Israel na wazazi wake na akakulia katika mtaa maskini wa Lod, mji wa kizamani wa Kiarabu maili 15 kusini mwa Tel Aviv.

Wengi walimjua kama mpiganaji mahiri; wachache walijua matamanio yake ya siri: mpenzi wa kusoma vitabu vya historia,mlaji wa mboga za majani na mtu asiyekula nyama, aliyependa muziki wa kilasiki, upakaji wa rangi na uchongaji vinyago.
Alikua ni mtu aliyewindwa toka utoto na mateso makali iliyopitia familia yake na waisraeli katika mauaji ya halaiki. Alijitolea maisha yake kulilinda taifa jipya la Israel lililozaliwa.

Kwa jinsi alivyokuwa akipanda vyeo jeshini, kitu cha kwanza alichofanya katika kila ofisi mpya aliyopangiwa, ilikuwa ni kutundika ukutani picha ya mzee wa kiisrael aliyejizungushia nguo ya kusalia akiwa amepiga magoti mbele ya maafisa wawili wa SS, mmoja akiwa ameshikilia rungu la kuchezea cricket na mwingine bunduki. "Huyu mzee ni babu yangu", Dagan alikua akiwaambia wageni. "Nikiangalia hii picha, najua kuwa lazima tuwe imara na tujilinde wenyewe ili mauaji ya halaiki yasitokee tena".

Huyo mzee kweli alikuwa babu yake na Dagan, aliitwa Ehrlich Slushni, na aliuawa huko Lukov sekunde chache baada ya hiyo picha kuchukuliwa.
Katika vita ya Yom Kippur, 1973, Dagan alikuwa mmoja wa waisraeli wa kwanza kuvuka mfereji wa Suez katika kikosi cha upelelezi. 1982 katika vita ya Lebanon, aliingia Beirut kama kiongozi wa brigedi ya kivita. Mapema tu akafanywa kuwa kamanda wa kanda ya kusini ya ulinzi Lebanon . Na hapo mpiganaji wa msituni (guerilla fighter) aliibuka kutoka kwenye kanali mwenye sare. Aliziunda upya kanuni za usiri, ukinyonga na za kuhadaa za kipindi akiwa Gaza. Wanajeshi wake walimpatia jina jipya. Walimwita "mfalme wa vivuli". Ndani ya Lebanon kwenye ushirika wa kisiri, usaliti, ukatili, vita za kishetani ndipo moyo wa Dagan ulipopenda zaidi. "Hata kabla ya brigedia ya vifaru kuingia Beirut, tayari nilishalijua eneo hili vizuri". Na baada ya vita ya Lebanon kuisha, hakuacha operesheni zake za siri. Mwaka 1994 alipewa onyo rasmi na kiongozi wake ( Chief of Staff) Moshe Levy kwa kutembea akiwa amevalia kama mwarabu katika makao makuu ya magaidi ya Bahamdoun.

Inaendelea muda mfupi ujao....
Stay tuned.
 
Tuendelee...

MFALME WA VIVULI

Sehemu ya nne na ya mwisho kwa sura
ya kwanza.. baada ya hapa tutaanza
sura ya pili...
MAZISHI NDANI YA TEHRAN

Wakati ule wa uasi wa wapalestina (Intifada), 1987- 1993, wakati alipohamishiwa West Bank kama kama mshauri wa 'Chief of Staff' Ehud Barak, Dagan alirejea tabia zake za zamani na hata akamshawishi Barak kuungana nae.

Wawili hawa walivaa suti maridadi kama wavaavyo wapalestina, akachukua gari nzuri ya bluu aina ya Mercedes yenye namba za Palestina na wakaenda kuzurura maeneo hatari ya Nablus Kasbah.

Wakati wa kurudi waliwatisha na kuwashangaza askari wa lindo makao makuu baada ya wao kumtambua aliyekaa siti ya mbele.

Mwaka 1995, Dagan, sasa akiwa meja jenerali aliachana na jeshi na kufuatana na rafiki yake, Yossi Ben-Hanan katika safari ya miezi 18 kwa kutumia pikipiki katika ukanda wa Asia.

Safari yao ilikatishwa na taarifa za kuuawa kwa Yitzhak Rabin.
Aliporudi Israel, Dagan alikaa kidogo katika makao makuu ya mamlaka ya kupambana na ugaidi, akajaribu kiasi kuingia kwenye ulimwengu wa biashara na baadae akamsaidia Sharon katika harakati za uchaguzi ndani ya chama cha Likud. Mwaka 2002 alistaafu na kurudi nyumbani kwake Galilaya alipofurahia vitabu vyake, muziki na vinyago.

Miaka thelathini (30) baada ya gaza, huyu jenerali aliyestaafu alishaanza kuzoea maisha ya familia- " niliamka kutoka usingizini na kukua watoto wangu wamekua watu wazima tayari" - wakati alipopata simu kutoka kwa rafiki yake wa zamani, kwa sasa waziri mkuu, Arik Sharon." Nakuhitaji katika makao makuu ya Mossad kama kiongozi", Sharon alimwambia rafiki yake huyu wa miaka 57."Nahitaji chief wa Mossad mwenye kisu katikati ya meno yake".

Ilikuwa 2002 na Mossad ilikuwa inakosa uelekeo. Kufeli kwa misheni kadhaa kulishusha sana heshima na hadhi ya Mossad; Tukio likilotangazwa sana kwenye vyombo vya habari la kushindwa kumuua kiongozi wa Hamas ndani ya Amman na kukamatwa kwa wapelelezi wa Israel Switzerland, Cyprus, na New Zealand kuliharibu sana sifa ya Mossad. Kiongozi wa mwisho wa Mossad, Efraim Halevy, hakutenda kama alivyotegemewa. Huyu balozi wa zamani katika jumuiya ya Ulaya, Brussels, alikua mwanadiplomasia mzuri na mchambuzi mzuri wa mambo ila hakuwa kiongozi na wala hakuwa mpiganaji.

Sharon alitaka kuwa na kiongozi wa Mossad asiyesita, mbunifu ambaye angekuwa silaha ya kutumainiwa dhidi ya ugaidi wa kiislam na kinu cha nuclear cha Iran. Dagan hakupokelewa vyema ndani ya Mossad, aloonekana kama mtu asiyejua Mossad inafanya nini, aliyejikita zaidi katika operesheni, ambaye hakujali sana uchambuzi wa taarifa za kiintelijensia, wala makubaliano ya siri ya kidiplomasia. Viongozi kadhaa wa juu wa Mossad walijiuzulu kupingana na Dagan, ila Dagan hakujali saana. Alijenga upya kitengo cha operesheni, akatengeneza uhusiano wa karibu na vyombo vya nchi nyingine vya usalama na akajikita katika tishio la Iran.

Wakati vita mbaya ya pili na Lebanon ilipoanza 2006, Dagan alikua kiongozi pekee wa Israel aliyeponga uvamizi wa kutumia ndege nyingi za kutupa mabomu.
Aliamini katika mashambilio ya ardhini na alionyesha wasiwasi mkubwa kama jeshi la anga lingeweza kushinda vita na baada ya vita mawazo na matendo yake yaling'aa.

Ila bado alipingwa na vyombo vya habari juu ya misimamo yake mikali dhidi ya watu anaowaongoza.
Maafisa wastaafu wa Mossad waliokua na hasira na Dagan walikuwa kila leo wakimpinga kwenye vyombo vya habari na Dagan akawa na hekaheka kila mara. "Dagan ndio nani?" Aliwahi kuandika mwandishi mmoja wa makala.

Na ghafla siku moja mambo yakabadilika, vichwa vya habari navyo vikabadilika. Makala nzurinzuri za kusifia zikaanza kujaza magazeti ya kila siku, zikisifia "Mtu aliyerudisha heshima ya Mossad".
Chini ya uongozi wa Dagan, Mossad iliweza kutekeleza mambo yasiyofikirika yafuatayo: mauaji ya muuaji hatari wa Hezbollah, Imad Mughniyeh ndani ya Damascus, Uharibifu mkubwa wa kinu cha nuclear cha Syria, mauaji ya magaidi wakubwa Lebanon na Syria na lakukumbukwa zaidi, kampeni isiyo na huruma na ya bila kuchoka dhidi ya programu ya silaha za Siri, za nuclear, za Iran.

Huu ndio mwisho wa sura ya kwanza...
Tujiandae na sura ya pili...
MAZISHI TEHRAN...

Usiende mbali..
 
2. MAZISHI NDANI YA TEHRAN

Sehemu ya Kwanza.

Julai 23, 2011, saa kumi na nusu na nusu mchana (4:30 pm), watu wawili wenye bunduki wakiwa na pikipiki walitokea katika mtaa wa Bani Hashem kusini mwa Tehran, wakatoa silaha kutoka katika makoti yao ya 'leather' na kummiminia risasi mtu aliyekuwa katia harakati za kuingia nyumbani kwake. Wakapotelea kusikojulikana baada ya mauaji kitambo kabla ya polisi kufika. Aliyeuawa alikuwa Darioush Rezaei Najad, miaka 35, profesa wa fizikia, na mtu muhimu katika programu ya silaha za siri za nuclear za Iran.
Alikuwa kiongozi katika utengenezaji wa switch za kielektroniki kwaajili ya kuwahia kichwa cha bomu la nuclear.
Rezaei Najad hakuwa mwanasayansi wa kwanza wa Iran kukutana na mwisho mbaya.

Rasmi ilifahamika kuwa, Iran inatengeneza tecknolojia ya nyuklia kwa matumizi salama, na walisema kuwa kinu cha Bushehr, chanzo muhimu cha nishati kilochotengenezwa kwa msaada wa Urusi, ilikuwa ushahidi tosha wa nia yao njema. Ila pamoja na kinu cha Bushehr, vituo vingine visivyo rasmi vinavyojishughulisha na nyuklia vilishagundulika, vyote vikiwa na ulinzi mkali na visivyoweza kufikika kirahisi. Baada ya muda Iran ililazimika kukubali uwepo wa baadhi ya hivi vituo, japo walikataa tuhuma za kutengeneza silaha ndani ya vituo hivi. Ila kufikia hapo, tayari taasisi za kiupelezi kutoka mataifa ya magharibi na taasisi za siri za ndani zilishaweka wazi jinsi baadhi ya wanasayansi katika vyuo vya Iran walivyopewa dili la kutengeneza bomu la kwanza la nyuklia la Iran.


Ndani ya Iran, zile zilizoweza kujulikana tu kama 'taasisi zisizofahamika' ziliendesha vita kali ili kuzuia programu hii ya siri ya silaha za nyuklia.

Tarehe 29 ,mwezi wa kumi na moja, 2010, saa moja na dakika harobaini na tano asubuhi (7:45am), kaskazini mwa Tehran, pikipiki ilitokea nyuma ya gari la Dr. Majid Shahriyari, kiongozi wa kisayansi wa mradi wa nyuklia wa Iran. Wakati akilipita gari, mwendesha pikipiki aliyevalia kofia ngumu aligundisha 'kifaa' katika kioo cha nyuma cha gari. Sekunde chache baadae kile 'kifaa' kililipuka na kumuua yule mwana fizikia wa miaka 45 na kumjeruhi mkewe.

Vivyo hivyo, katika mtaa wa Atashi kusini mwa Tehran, mwendesha pikipiki mwingine alifanya vilevile kwa gari aina ya Peugeot 206 mali ya Dr. Fereydoun Abassi-Davani, mwanasayansi mwingine wa nyuklia. Mlipuko ulimsababishia Abassi-Davani majeraha pamoja na mkewe.
Mara moja serikali ya Iran ikawanyooshea Mossad kidole. Uhusika wa hawa wanasayansi wawili kwenye mradi wa silaha za atomi za Iran ulifahamika kwa siri, ila Ali Akbar Salehi, kiongozi wa mradi, alitangaza kwamba lile shambulio limemfanya Shahriyari kuwa 'shahidi' na limeondoa ua pendwa katika timu yake.
Rais Ahmadinejad, pia, alionyesha shukrani zake kwa hao watu wawili kwa namna ya kipekee kabisa. Mara tu baada ya Abassi-Davani kupona majeraha yake, Ahmadinejad alimteua kama makamu wa rais Iran. Watu walioshambulia hawa wanasayansi hawakuwahi kupatikana.

Januari 12, 2010 saa moja na dakika hamsini asubuhi (7.50am), Profesa Masoud Ali Mohammadi alikuwa akitoka nyumbani kwake katika mtaa wa Shariati, Gheytarihe, kaskazini mwa Tehran. Alikuwa njiani kuelekea kwenye maabara yake katika chuo kikuu cha tecknolojia cha Sharif. Alipojaribu kufungua mlango wa gari yake, mlipuko mkubwa ulitikisa mtaa huu uliotulia. Maafisa wa usalama waliowahi eneo la tukio walikuta gari ya Mohammadi iliyopasuliwapasuliwa na mlipuko na vipande vya mwili wake.
Aliuawa na mlipuko wa bomu lililofichwa katika pikipiki iliyokuwa kando ya gari lake.
Vyombo vya habari vya Iran vilitangaza kuwa Mohammadi aliuawa na Mossad.
Rais Ahmadinejad alitangaza kuwa,"haya mauaji yanatukumbusha mbinu za ki-zayoni".

Profesa Mohammadi, miaka 50, alikua ni mtaalam wa 'quantum physics' na mshauri katika programu ya silaha za nyuklia za Iran. Vyombo vya habari vya ulaya vilitangaza kuwa Mohammadi alikua askari wa jeshi la walinzi wa mapinduzi 'Revolutionary guards', jeshi lililoegemea mrengo wa serikali.
Ila maisha ya Mohammadi, kama tu kifo chake, yalijaa mafumbo na sintofahamu. Baadhi ya marafiki zake walisema kuwa alihusika tu katika tafiti za kinadharia, ila sio katika miradi ya kijeshi; kuna waliosema kuwa aliunga mkono wale wanaoipinga serikali na alishiriki katika maandamano ya kuipinga serikali. Ila ajabu ni kuwa, nusu ya waliohudhuria katika mazishi walikua wanajeshi wa jeshi la ulinzi wa mapinduzi 'revolutionary guards'.
Jeneza lake lilibebwa na maofisa wa 'Revolutionary Guards'. Uchunguzi uliofuata ulionyesha kweli kuwa Mohammad alijihusisha sana kuendeleza matamaanio ya nyuklia ya Iran.

Januari 2007, Dr. Ardashir Hosseinpour, inasemekana aliuawa na mionzi yenye sumu. Habari za mauaji yake ziliandikwa kwenye gazeti la 'Sunday Times' London, likionyesha taarifa zilizopatikana kutoka katika moja 'think tank' iliyopo Texas.
Maafisa wa Iran walizinanga hizo ripoti, wakidai Mossad haikuwa na uwezo wakufanya operesheni kama hiyo ndani ya Iran, na kwamba, "Profesa Hosseinpour alikufa kwa kukosa hewa baada ya kuvuta moshi uliosababishwa na moto kwenye nyumba yake".
Walisisitiza pia kwamba, profesa huyu mwenye miaka 44 alikuwa mtaalam wa kutukuka wa 'electro-magnetic' na hakuhusika na miradi ya nyuklia ya Iran kwa namna yeyote.

Ila ilikuja kufahamika kuwa Hosseinpour alifanya kazi katika kituo cha siri cha Isfahan ambapo uranium ilibadilishwa kuwa gesi. Hii gesi ilitumika kuongezea uranium ubora katika kinu cha Natanz, kilichokuwa mbali chini ya ardhi na chenye ulinzi mkali. Mwaka 2006, Hosseinpour alizawadiwa nishani ya juu kabisa ya sayansi na tecknolojia Iran; miaka miwili kabla, alikua amezawadiwa na nchi yake nishani ya kutukuka katika tafiti za kijeshi.

Itaendelea...
Usikae mbali..
 
Mods naomba mnisaidie kubadilisha neno upelelezi kwenye heading, lisomeke Ujasusi..
 
Back
Top Bottom