PADRI MLA NYAMA ZA WATU - 3
Mara walipotea machoni pangu. Niliwaambia waumini kuwa, wametoweka na nikaonesha mahali walipokuwa wamekaa.
Yule mzee aliyewekwa kati akasema, anachojua yeye ni kwamba, waumini waliokwenda kukaa kulia na kushoto kwake ni wanawake na alitaka kuwauliza kisa cha kukaa upande ule wa wanaume.
Basi, niliendelea na ibada huku kila muumini akionekana hana amani moyoni. Hata pale alipoingia mtu na kuliza mlio wa viatu sakafuni, waumini wote waligeuka kuangalia mpaka ikabidi mimi nisitishe kuendelea na ibada ili waumini wamalize kuangalia.
Ibada ilipokwisha, niliingia kwenye chumba nikavua mavazi ya utumishi, nikabaki na mavazi yangu ya kawaida. Nikiwa natoka nje ya chumba, ghafla nikaona giza nene mbele.
Nikawahi kushika flemu ya mlango huku nikiwa nahakikisha sianguki au kukanyaga sehemu ambayo siyo ardhi. Mpaka hapo nilikuwa siunganishi tatizo la kuona giza na uwepo wa wale waumini wawili wa ajabu ajabu.
"Mtumishi wa Mungu kwema?" Nilisikia sauti ikiniuliza.
"Siyo kwema kabisa."
"Unaona nini mbele?"
"Naona giza."
"Fumba macho."
Nilifumba.
"Haya fumbua sasa."
Nilifumbua.
Nikaendelea kuona kama kawaida, lakini hakukuwepo na mtu yeyote aliyesimama mbele, nyuma, kulia wala kushoto kwangu.
Lakini pamoja na hali hiyo, niliisaka ile sauti akilini mwangu na kuigundua kuwa, ilikuwa ya yule mzee aliyekaa jirani na wale watu wa ajabu.
"Khaa!" Nilijikuta nikishangaa sasa.
Nilitembea kwa mwendo wa haraka hadi kwa waumini waliokuwa wamesimama nje ya kanisa wakiongea, wengine wakisalimiana na kuulizana maisha, kwani waumini wengi huitumia Jumapili kuonana na kuongea mambo yao mbalimbali ya maisha.
Nilizungusha macho kumwangalia yule mzee, nikamwona katikati ya watu akicheka na kupiga soga na wazee wenzake, nikamfuata, lakini huku waumini ninaowapita wakinisalimia, wengine wakionekana kutaka kujua kile kisa cha ndani ya kanisa.
Wakati nakaribia kumfikia, nilijiuliza mwenyewe, je, kweli kwa sauti ile kama angekuwa ni yeye angeshafika katikati ya watu?
"Kama ni hivyo, mbona sasa wakati nafumbua macho sikumwona mbele yangu?"
"Faza pole na majukumu bwana," yule mzee niliyekuwa namfuata alinisalimia na kuwawahi wenzake wote aliosimama nao. Sauti yake niliikumbuka vizuri sana, ndiyo ile iliyonielekeza mpaka nikafumbua macho.
"Nimeshapoa mzee wangu."
Wazee wengine nao pia wakanisalimia huku wakinipa mikono.
"Eti mzee ulikuwa unasemaje?" Nilimuuliza yule mzee.
"Wapi?" Na yeye aliniuliza.
"Hukusimama na mimi pale mlangoni?"
"Mlangoni! Wapi?"
"Kule kwenye chumba?"
"Hata, hapana."
Wazee wengine nao wakaonesha kunishangaa mimi, nikajisikia soni kwa nafasi yangu ya u-Padri.
"Oke, sawa basi."
Nilitembea kwenda kwenye ofisi yangu, lakini nyuma nikamsikia mzee mmoja akisema.
"Kwani mzee Makwaya imekuwaje?"
"Sijui chochote," mzee Makwaya alijibu, hali ya mshangao na minong'ono ya chini kwa chini iliendelea hadi ilipofika mahali nikawa siwasikii.
Kule ofisini nilikuwa peke yangu, nikainamia mezani na kuwaza ile hali mwanzo hadi pale ilipofikia nikaona giza nene mbele yangu.
"Hivi, wale ni akina nani?"
"Ni kwanini walinijia kanisani?"
"Wametumwa au?"
Nikiwa naendelea kuwaza hivyo, mara nikasikia sauti ndani ya ofisi.
"Unaendeleaje mtumishi wa Mungu?"
Ilikuwa ni sauti ya yule yule mzee Makwaya.
Nilishtuka sana, nikaangalia kila kona ya ofisi.
Je, nini kitatokea? Usikose kusoma sehemu ya pili ya mkasa huu wa kweli, Padri Mla Nyama za Watu. Maoni, ushauri meseji 0784 275714 au
osanjelus@yahoo.com.