Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 21

“Leo nimemuona hapa Miladiva,” alisema rafiki yake kwenye simu.
“Yupo?”
“Ndiyo! Ila na familia yake!”
“Nakuja! Nilivyokuwa na hamu naye. Nakuja!” alisema Fareed na kukata simu.
Hakutaka kubaki nyumbani, akaelekea huko na kuonana na mwanaume huyo na kumfanyia kituko cha kumshika katika zipu yake. Godfrey akachanganyikiwa lakini akamwambia kwamba angempigia simu.

Hakutaka kujifanya kuwa na haraka, alijua kwamba mwanaume huyo angekuwa na presha ya kuonana naye, alitaka kuvuta muda mpaka wiki moja iishe ndiyo awasiliane naye.

Wakati akisubiri wiki moja ipite, akaanza kupata madili mengi, akawa mtu wa kuzunguka nchi mbalimbali kufuata wateja kiasi kwamba mpaka miezi yote hiyo inakatika bado alikuwa bize na wateja hao, na aliporudi Tanzania, mtu aliyemjia kichwani mwake alikuwa Godfrey hivyo kumpigia na kuonana naye kisha kufanya kile kilichowafanya wapigiane simu.

“Wewe ni zaidi ya wapenzi wangu wote,” alisema Fareed.
“Kweli?”
“Haki ya Mungu tena. Ninakupenda sana mpenzi! Hakika sijuti kuwa nawe,” alisema Fareed, akachukua mkoba wake, akatoa wanja na kuanza kujipaka vizuri huku akijiangalia kwenye kioo.

“Ninafurahi sana kukutana nawe. Hakika sitokuacha. Nitakuwa radhi kuachana na mke wangu ila si kukuacha wewe,” alisema Godfrey huku akionekana kuchanganyikiwa. Kwa kifupi ni kwamba akatekwa na penzi jipya.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 22

Hali ilibadilika, mapenzi ya Godfrey kwa mkewe yakapungua, hakutaka kuwa naye karibu kama ilivyokuwa siku za nyuma, mapenzi yalikuwa kwa mwanaume tata ambaye alikutana naye ufukweni.
Walikuwa wakiwasiliana kama kawaida, mara kwa mara walikutana na hata alipokuwa akienda safari zake za Ulaya, Marekani na nchi nyingine alikuwa akiongozana naye ambapo huko uchafu wao uliendelea.

Fareed aliendelea kufanya mambo yake kama kawaida, alimpenda sana Godfrey, alimpa kila kitu alichotaka lakini siku zote alitamani kutembea na wanaume wengine. Aliijua dunia, alijua nchi zilizokuwa na wanaume tata wengi, watumiaji wa watu hao na hata alipokwenda huko, wakati mwingine alikuwa akimtoroka Godfrey na kujiunga na wenzake kufanya ufuska.

Siku ziliendelea kukatika, walipokuwa wakirudi nchini Tanzania, halikuwa jambo la ajabu kumuona Godfrey akiondoka nyumbani na kurudi baada ya siku tatu. Kila alipokuwa akiulizwa, alikuwa mkali, aligombana na mkewe kisa tu alihisiwa kulala na wanawake wengine.

Mkewe akaanza kupeleleza, aliamini kwamba kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima kuwe na mwanamke aliyekuwa akimzuzua mume wake hivyo kumfuatilia.
Alifuatilia kwa kuchukua simu yake nyakati za usiku na kuangalia meseji mbalimbali, hakuweza kugundua, hakuacha, aliendelea kufuatilia watu aliokuwa akiwasiliana nao, wengi walikuwa wanaume lakini kulikuwa na mwanaume mmoja ndiye aliyekuwa akiwasiliana naye sana, huyu aliitwa Fareed.

Mara ya kwanza akahisi kwamba alikuwa msichana aliyembadilisha jina, akaangalia katika mtandao wa simu kwenye huduma ya kifedha kugundua kama hilo lilikuwa jina lake au mumewe alimfanyia mchezo, alipoangalia, akakutana na jina hilohilo, Fareed Hassan.

Hakuwa na hofu na mwanaume huyo, aliendelea kutafuta lakini hakumfuma mumewe kuwa na uhusiano wa siri na mwanamke mwingine. Akauachia moyo wake kumwamini mwanaume huyo, akajiondoa hofu, akaona kwamba kila alipokuwa akiambiwa kwamba alikuwa bize na mambo ya biashara, kweli alikuwa bize.
 
Back
Top Bottom