SEHEMU YA 112
Akaingia ndani ya gari hilo, alikuwa na kibegi chake kidogo kilichokuwa na pesa nyingi ambazo alizipata katika kazi yake kubwa aliyokuwa ameifanya kwa kipindi kirefu, kutembea na mabilionea wengi.
Kutoka hapo mpaka Fayad ilikuwa ni zaidi ya kilometa mia moja, hilo halikuwa tatizo, kwa kuwa barabara ilikuwa nzuri, hawakuona kama wangetumia muda mwingi mpaka kufika huko.
Garini, walikuwa wakizungumza kirafiki na Fareed alijitambulisha kama Hamad Al Hamad ambaye alitokea nchini Nigeria na kufika hapo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Iddi ambayo ilimalizika kwa siku tano zilizopita.
“Kwa hiyo umetokea Nigeria?” aliuliza dereva yule.
“Ndiyo! Ninarudi huko keshokutwa, ninakwenda fayad kutoa mawaidha katika msikiti mkuu wa hapo kisha nitarudi Cairo,” alisema Fareed huku akimwangalia mwanaume huyo.
Walizungumza mambo mengi sana, hakukuwa na siku ambayo Fareed alijifanya kuwa mtu wa dini kama siku hiyo. Kila alipokuwa akizungumza sentensi tano, aliingizia jina la Mtume Muhammad, kila alipokuwa akizungumza sentensi tano, alizungumza kuhusu swala, jinsi Muislamu anavyoweza kuingia motoni kama tu hatokuwa akiswali swala tano kwa siku.
“Na uzninifu! Siku hizi watu wanazini sana. Wewe una wanawake wa nje wangapi?” aliuliza Fareed huku akimwangalia dereva huyo aliyeonekana kuwa mtu mzima kidogo.
“Mimi ni mwenye dhambi! Nina mahawala watatu. Allah anisamehe,” alisema dereva huyo, aliumia moyoni mwake, kwa jinsi Fareed alivyokuwa akizungumza, alionekana kuwa mtu wa swala tano.
Safari iliendelea, walikuwa wakizungumza mambo mengi njiani. Magari ya polisi yalikuwa yakiwapita kwa sana kiasi kwamba dereva yule alikuwa akishangaa tu. Muda wote Fareed alipokuwa akiyaona magari hayo, alikuwa akishangaa, aliamini kwamba hao walikuwa wakimtafuta yeye, alipokuwa akiangalia saa yake, ilikuwa ni saa 11:30 alfajiri.
Hawakuchukua muda mrefu wakaanza kuingia katika Mji wa Ismailia. Walipofika hapo, wakakutana na magari kama kumi yaliyokuwa yakikaguliwa na askari waliokuwa mahali hapo.
Dereva yule hakuogopa hata kidogo, hakujua kama msako ule ulikuwa ni kwa ajili ya abaria aliyekuwa ndani ya gari lake.