SEHEMU YA 111
Wakati polisi wakihangaika kumtafuta Fareed, yeye alikuwa akifikiria lake, alitaka kuondoka nchini Misri pasipo kuonekana.
Alijua kwamba endapo angeendelea kubaki humo ilikuwa ni lazima kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Alitakiwa kutoroka haraka iwezekanavyo kitu ambacho kwake hakikuwa na tatizo lolote lile, alichokuwa akihitaji ni kupata usafiri wa haraka wa kuvuka na kuingia Ulaya, sehemu ambayo aliamini ingekuwa nafuu kwake na si kuendelea kubaki Afrika.
“Ni lazima niende Ulaya, siwezi kubaki Afrika kwa sasa,” alisema Fareed.
Hakutaka kutumia ndege, aliamini kwamba katika viwanja vya ndege kulikuwa na ulinzi mkubwa na njia pekee ya kuondoka nchini humo ilikuwa ni moja tu, kwa kutumia ndege, tena si kuelekea katika bandari za Said au Ras el Bar bali alitaka kwenda katika Mji wa Fayed ambapo kulikuwa na ziwa Great Bitter lililounganishwa na mfereji wa Suez, hapo angeomba msaada wa kupanda meli za kwenda Ulaya ambapo angetokomea huko.
Safari hiyo ilitakiwa kufanyika usiku wa siku hiyo, hakutaka kubaki hapo Cairo bali alichokifanya ni kuondoka kuelekea barabarani ambapo akakodi teksi kwa ajili ya kumpeleka Fayed.
“How much?” (kiasi gani?)
“One thousand pound,” (paundi elfu moja) alijibu mwanaume aliyekuwa kwenye taksi.
“Okey!” (sawa)
Si kila mtu aliyekuwa akijua kile kilichokuwa kikiendelea, watu wengine walikuwa bize na kazi zao na si wote walioziona picha za Fareed katika sehemu mbalimbali zilipobandikwa.
Mmoja wa watu ambao hawakuwa wakijua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea alikuwa dereva huyo. Ilikuwa ni vigumu kumfahamu Fareed hata kama angeona tangazo na picha zake mara kwa mara kutokana na jinsi alivyovaa.
Alikuwa na kanzu ndefu nyekundu, kichwani alivalia kiremba kikubwa huku akiwa ameshika Juzuu mkononi. Alionekana kama ustadhi ambaye alikuwa akienda sehemu fulani kutoa mawaidha au Imamu fulani aliyekuwa akiwahi sehemu fulani kuswalisha