Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 108

Akaendelea kuvaa kwa haraka sana, watu waliokuwa nje walipoona hafungui mlango, wakauvunja na kuingia ndani. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuweka chini ya ulinzi. Hakuwajua watu hao kwani wale walioanza kuingia ndani ya chumba kile walivalia nguo za kiraia.

Alipiga kelele kwa kudai kwamba alivamiwa na majambazi. Akanyamazishwa kwa kuambiwa kwamba wao hawakuwa majambazi kama alivyofikiria bali walikuwa polisi na ili kumridhisha wakamtolea vitambulisho vyao.

“Mwenzako yupo wapi?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Nani?”
“Uliyeondoka naye kwenye mapiramidi!” alijibu mwanaume huyo.

“Sijui! Nimetoka bafuni, simuoni. Kwani kuna nini?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Una uhakika!”l

“Ndiyo! Kwani kuna nini?’ aliuliza Maria huku akiwaangalia wanaume hao.
Wakamwambia kilichokuwa kimetokea kwamba mwanaume ambaye alikuwa naye alifanya mauaji ya kutisha katika mapiramidi yale, alimuua bilionea Keith ambaye kwa Maria ndiye alikuwa tegemezi lake, ndiye aliyekuwa akimpa pesa nyingi za matumizi, ndiye ambaye alimfanya kujiona mwanamke wa mjini mwenye kila kitu, cheni ya dhahabu, hereni na vito vingine vingi.

“Keith amekufa?” aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo! Ameuawa na mtu uliyetoka naye ndani ya piramidi lile. Mfungeni pingu tuondoke naye, huyu atakuwa anafahamu kila kitu,” alisema mwanaume mmoja na hapohapo kufungwa pingu.

Maria alikuwa akilia, hakuamini kilichokuwa kikitokea, hakuamini kama ingetokea siku moja ambayo angefungwa pingu kwa ajili ya kupelekwa katika kituo cha polisi.

Moyo wake ulimuuma, aliumia na hakuacha kulia. Mbali na kufungwa pingu, kilichokuwa kikimuumiza ni kifo cha Bilionea Keith, mwanaume huyo alikuwa mtu pekee aliyemjali, aliyemsaidia kwa kila kitu, maisha yake yangekuwaje baada ya kifo cha mwanaume huyo?

“Haiwezekani! Keith hajafa! Haiwezekani!” alisema Maria huku akilia kama mtoto.
“Twende kituo cha polisi! Mengine utayasikia hukohuko!” alisema polisi mmoja.
 
SEHEMU YA 109

Hakujua sababu iliyomfanya Fareed kufanya mauaji hayo, alishangaa, hakuona kama Bilionea Keith aliwahi kuzozana na mwanaume yeyote yule, kwa nini Fareed alimuua? Je, Fareed alijua kwamba polisi walikuwa njiani kufika hotelini hapo mpaka kuamua kumtoroka?

Na kwa nini hakumwambia ili watoroke wote? Kila alichokuwa akijiuliza, alikosa majibu.
**** Kila mtu aliyesikia taarifa juu ya kifo cha Bilionea Keith hakuamini, wengi walijua ni tetesi ambazo ziliandikwa kwenye mitandao ya nchini Misri ili kuishtua dunia, kwao, bilionea kama huyo kuuawa kizembe namna hiyo lilionekana kuwa jambo gumu mno.

Watu waliokuwa na ndugu zao nchini Misri waliwapigia simu, walitaka kufahamu kilichokuwa kimetokea, walitaka kujua ukweli juu ya jambo hilo. Waandishi wa habari wa CNN, BBC na wengineo wakawatuma waandishi wao nchini Misri kufuatilia kile kilichokuwa kikiendelea.

Walipofika katika Hospitali ya Sheikh Mazrui iliyokuwa pembezoni kidogo mwa Jiji la Cairo, wakakutana na madaktari ambao waliwathibitishia kwamba mtu aliyekuwa ameuawa alikuwa Bilionea keith.

CNN walipotoa taarifa hiyo ndiyo kila mtu akaamini kwamba kweli mtu huyo alikuwa ameuawa. Lilikuwa pigo kubwa, watu wengi walihuzunika kwani miongoni mwa mabilionea walipokuwa na roho nzuri duniani alikuwa mwanaume huyo, hakukuwa mtu aliyejua ubaya wake kwani kila alipokuwa katika umati wa watu, alijivisha roho ya kondoo na wakati alikuwa mbwa mwitu.

Kila mtu alitaka kujua kuhusu mtu aliyefanya mauaji, kila mmoja masikio yake yalikuwa kwa polisi wa nchini humo wakitaka kujua ni nani hasa alikuwa amehusika katika mauaji hayo na wakati huo muuaji huyo alikuwa wapi.

Polisi wa nchini Marekani, kupitia kitengo cha Interpool walikuwa wakiwasiliana kwa ajili ya kuufahamu ukweli na kujua mahali muuaji huyo alipokuwa. Kulikuwa na kazi kubwa, walipewa picha zake zilizopigwa kwa kutumia kamera za CCTV ambazo hizohizo ndizo walizokuwa wakizitumia.
 
Back
Top Bottom